PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 9


 SEHEMU YA 09


ILIPOISHIA


.... kwenye yale mafuta kukawa kunaonesha tukio lililopita pindi Maya alipokuwa kitandani amelala akiwa hajitambui, lengo ni kujua kitu gani kilitokea hadi kuweza kumfanya Maya akaamka.


ENDELEA NAYO....... 


Akizidi kuwa makini kutazama tukio hilo na dakika chache mbele akapata kuona kijana mmoja akiingia mule ndani na kusogea hadi pale kitandani alipo Maya. Alimuona akikaa na kutazama huku na kule kisha akaupeleka mkono wake kichwani kwa Maya na kuonekana kama anaongea maneno fulani kwa mbali na sekunde chache tu akapata kuonekana Maya akitapika damu na kuweza kufumbua macho yake, yule kijana akawa anazifuta damu zile hali iliyomfanya Dalfa ashangae baada ya kuona vile. Ilibidi atumie taaluma yake ya uchawi kumsogeza yule kijana apate kumuona vizuri sura yake. Alihamaki baada ya kumuona kijana yule, aliitambua sura ile yule kijana ambaye alikuja kumzuia Malkia Rayat asisaini ile mikataba ya kuitoa Eden kwa Dalfa. 


"Kumbe yule kijana ndio huyu! Amepataje hizi nguvu zangu,?" aliongea Dalfa kwa hasira kuona kuna mtu mwenye uwezo kama wake ambao anautumia yeye kama kusaidia watu na kupata falme nyingi za watu.


Alianza kuwa na mashaka juu ya kijana huyo na kuona akiendelea kumuacha huko mbele anaweza kubadilika na kuwa mbaya kwake.


"Huyu kijana ni wa kumtafuta ikiwezekana niziibe nguvu zake, Dalfa abaki kuwa Dalfa tu pasitokee mwengine mwenye uwezo huu.!" aliongea Dalfa huku akimtazama Samir kwenye yale mafuta yaliyo kwenye karai akiwa anaongea na Maya mara baada ya kuamka.


Huku upande wa pili  Mfalme Faruk alikuwa mwenye furaha na mwanaye Jamal wakiwa ndani ya falme wamekaa.


"Nilikwambia Jamal haya mambo yanaenda kwa uvumilivu, ona sasa nafasi zinakuja waziwazi namna ya kuwa karibu na Maya. Kwa jinsi ninavyokuamini kwenye mapambano sidhani kama nafasi hii itakwenda kwa mtu mwengine." aliongea Mfalme Faruk.


"Hii nafasi imejileta baba sidhani kama nitaichezea, huu ndio muda wa kulikamilisha lile swala tulilopanga muda mrefu,  nitahakikisha mtu wa kumlinda Maya nitakuwa mimi."


"Hii ndio nafasi yako Jamal, tukishindwa hapa tunaanza tena upya tambua hilo kabisa. Hakikisha hii nafasi huipotezi."


"Ondoa shaka ninajiamini sana." alisema Jamal huku akiwa ameshika kipeperushi kinachoelezea mashindano hayo ya kumpata shababi wa kuweza kumlinda Maya.


Mambo taratibu yakaanza kuandaliwa huku uwanja wa mapambano hayo ukaanza kuwekwa sawa kwaajili ya kusubiri siku husika.


Samir alikuwa akishiriki pia kuhakikisha sehemu ya viongozi na watu watakaowasili siku hiyo inakuwa safi na imeandaliwa vyema.

Watu walio tayari wakaanza kusogea kujiandikisha sehemu maalumu ya kupeleka majina ya mpambanaji ili  wapangwe siku ya pambano. Kwa Jamal naye akaanza safari ya kuelekea Eden kwajili ya kujiandikisha aweze kuingia kwenye mashindano hayo. 


Huku upande wa pili Dalfa kazi ikawa moja tu ya kuanza kutengeneza njama za kumdhibiti Samir kule alipo. Hii ni baada ya kutambua kuwa kijana huyo anaweza kuja kuwa hatari kwa upande wake hivyo anafanya haraka iwezekanavyo kuweza kuziiba zile nguvu alizonazo Samir.


Mitaani huko kila mtu alikuwa akijifua kimazoezi kuhakikisha siku ya mpambano anaibuka kinara . Mfalme na Malkia walikuwa juu ya jengo la kifalme wakitazama foleni ya watu ambao wanahitaji kupambana siku hiyo.


"Umati wote huu wanaihitaji nafasi hii, naamini kutatokea mtu wa kuweza kumlinda binti yangu muda wote akawa kwenye amani." alisema Mfalme akiwa na Malkia aliyekuwa akitabasamu tu kutazama msururu wa watu wakiwa wamepanga foleni sehemu ya kujiandikisha.


"Naona watu wamejiandaa kwa jambo hili kweli maana wamethubutu kujitokeza." alisema Malkia.


"Naamini itakuwa ni burudani pamoja na lile lengo letu hasa la kumpata mshindi." alisema Mfalme na kuendelea kuongea mambo mengi akiwa na mkewe wakiitazama Eden yao.


Baada ya saa kadhaa kupita Jamal aliwasili akiwa kwenye farasi wake wa kawaida huku akiwa amevalia mavazi ya kawaida kama sio mtoto wa Mfalme wa taifa lengine. Moja kwa moja  alielekea sehemu ya foleni ya watu naye akapanga foleni baada kumuweka farasi wake mahala.


Samir baada ya kazi mbalimbali kuzifanya alielekea zake chumbani kwake kupumzika. Alikuwa amechoka sana hivyo hakutaka kusumbuliwa na mtu akaufunga mlango wake kwa komeo la ndani na moja kwa moja  akaelekea kupanda kitandani na taratibu akaanza kuutafuta usingizi jioni ile na muda mchache usingizi ukamchukua.


Baada ya muda kadhaa aliona anaamshwa na mtu pale alipolala, kwa uchovu alionao hakufuatilia jambo hilo akawa anaamka huku akiwa amenuna sana hammadi..... alishangaa kumuona kaka yake ndiye aliyekuwa akimuamsha pale.


"We Amour muda wote unaoitwa huo husikii? kulala gani huko kama umekufa halafu umejifungia mlango kwa ndani mpaka nimeamua kuvunja kitasa." alisema kaka yake Amour huku akionesha kukasirika akimtazama mdogo wake huyo.


Amour alibaki kushangaa tu huku akitazama kila sehemu mule chumbani. Hapo ndipo akili zikamjia kwamba yupo Magogoni kwao.


"Kwani unaumwa au mbona sikuelewi unashangaa shangaa?" aliongea kaka mtu na kumfanya Amour arudi katika hali yake ya awali.


"Dah nahisi kizunguzungu kichwa kizito sana." alisema Amour huku moyo ukiwa na mshtuko maana jambo hilo limekuwa la ghafla sana kujiona amerejea duniani tena.


"Ah tatizo lako ndio hilo weye ukiwa unaumwa husemi unajifungia ndani siku utakuja kufa humu sisi hatuna habari shauri yako. Hebu jitahidi uamke ukale ndio umeze dawa sawa..haya amka amka." alisema kaka mtu na kugeuka kutoka zake nje.


Alibaki anajishangaa na kutazama pale kitandani alipo, tukio hilo la ghafla tu limemshtua sana maana alikuwa Eden kwenye kibanda chake amelala na ghafla tu anajikuta yupo huku kwao. Akitazama kidoleni na kuona ile pete yake ikiwepo bado, haraka akanyanyuka na kwenda mlangoni kutaka kuufunga lakini aliona kweli kitasa kimevunjwa na kumfanya aamini kwamba kweli siku zote alikuwa akionekana bado yupo huku Unguja kwao angali mwenyewe anajua yupo taifa la Eden tena kujulikana kama Samir. 

Ilimbidi arudi pale kitandani na kuitazama ile pete.


"Mbona sielewi hili swala na awali uliniambia kwamba huku atakuwepo mtu kama mimi, sasa imekuwaje nimerudi tena huku?" aliuliza Amour akiwa anaitazama pete ile.


"Kuna hatari Eden inayokuhusu wewe, Dalfa ameshakutambua kuwa una nguvu kama zake jambo ambalo halitaki litokee, anataka awe yeye pekee mwenye nguvu hizo na leo anahakikisha kuzinyofoa nguvu zako zote ili ubaki mtupu, ndio maana umerudi huku. Hataweza kukutafuta kujua wapi ulipo, utakaa huku hadi siku tutakayokurudisha tena Eden." ilisikika sauti ikitoka kwenye ile pete ikimuelewesha Amour kuhusu hali halisi iliyopelekea yeye kurudi tena kwao. 


Maneno yale yalimchosha na kumfanya ajilaze kitandani kutafakari  baada ya kuona kumbe kuna mitihani kama hiyo na alikuwa akifuatiliwa na Dalfa bila yeye kujua. 


Baada ya dakika kadhaa ilibidi tu akubaliane na matokeo aliyoambiwa, alitoka nje na kuona mandhari ya nyumbani kwao na mtaa wanaoishi akabaki kutabasamu tu. Alizoea kuona jengo kubwa la kifalme huku wananchi wa taifa hilo muda wote wakiwa wenye kuchakarika na kazi mbalimbali kuifanya Eden iwe yenye kusifika. Alielekea zake sebuleni kwenda kupata chakula cha jioni.


Kule Eden baada ya Jamal kuweza kujiandikisha jina lake alipata nafasi ya kuanza kutembea baadhi ya sehemu kwenye mitaa ya Eden. Alipita sehemu ya sokoni akawa ananunua baadhi ya vitu walau aweze kula, aliposimama mahala akinunua matunda alikuja mwanamke mmoja akiwa amejifunga ushungi na kuachia sura yake kidogo ipate kuonekana.


"Wewe ndio Jamal...!?" aliuliza yule mwanamke kwa sauti ndogo na kumfanya Jamal amtazame, akaitikia kwa kutikisa kichwa akikubali kuwa ndio yeye. Basi yule mwanamke alimtazama Jamal kwa sekunde kadhaa kisha akageuka na kuanza kuondoka zake. Kwa akili za haraka tu Jamal akafahamu kuwa huenda anapaswa kumfuata mwanamke yule. Alichukua matunda yake aliyonunua pale na kuanza kumfuata kwa nyuma yule mwanamke aliyekuwa amejifunika ushungi. 


Alifika sehemu yule mwanamke na kuingia kwenye nyumba moja, Jamal alipofika pale nje akatazama kulia na kushoto kama kuna usalama kisha naye akaingia mule ndani. Aliwakuta watu watatu akiwemo na yule mwanamke ambaye aliweza kutoa ule ushungi wake na kuonekana.


Walimkaribisha akae kwenye kiti naye Jamal akatii kukaa huku akiwatazama.


"Nadhani hutufahamu kwa sura ila huenda ukawa unasikia tu. Mimi naitwa Lutfiya ni mmoja wa watu walio na mchango mkubwa kwa Mfalme Faruk, na hawa ni watu ambao baba yako anawatumia kupeleka na kurudisha ujumbe wa mambo yanayoendelea ndani ya Eden. Nimekuwa hapa Edeni miaka saba sasa nikiwa kama mfanyakazi ndani ya Falme hadi leo sijulikani kama mimi ni mtu wa taifa lengine ambalo ndio baba yako anaongoza. Sisi wote tumetoka kwenye taifa moja hivyo swala la wewe kuandaliwa kuja kuwa Mfalme wa hili taifa la Eden wote hapa tunalifahamu. Ndio maana baba yako amekazania na kuona njia rahisi ya kulifanikisha hili ni kumtumia binti wa Mfalme yule Maya, tunaziteka akili zake na anakuwa anakuhusu wewe na hata kutaka umuoe, zoezi hilo likikamilika tu basi swala la wewe kuwa Mfalme wa Eden ni rahisi mno ila kwasasa tunalihangaikia swala hilo kwanza." alisema Lutfiya akimueleza Jamal ukweli halisi wa mambo yanavyokwenda.


"Ndio nafahamu  hilo, baba yangu alinieleza kuhusu hilo na nashukuru nimeweza kuwaona na kuwafahamu wenzetu tutakuwa pamoja kulifanikisha hili. Nimekuja kwaajili ya kupambana ili nipate nafasi ya kuwa mtu wa karibu na Maya, nadhani nafasi hiyo ndio itakuwa nzuri zaidi nikiwa karibu naye na ndio itakuwa njia pekee ya kulifanikisha zoezi letu, nimetembea kila sehemu kuangalia hakuna mwenye uwezo wa kupambana na mimi lazima nitapata tu nafasi hiyo." alisema Jamal akiwa mwenye kujiamini sana.


Upande wa pili Amour akiwa darasani akisoma daftari lake, ghafla akasikia amri ya kiongozi ya kusimamisha baada ya kuingia mwalimu, alifunika daftari lake na kusimama naye kutoa heshima na alipotazama mbele kwa Mwalimu huyo alishtuka baada  ya kumuona yule Mwalimu.


Alibaki kumtazama Mwalimu yule ambaye ana siku kadhaa pale shuleni ni mgeni, ilaa kwa Amour ilikuwa tofauti kidogo baada kuitambua sura.


"Mfalme?" alishangaa Amour baada ya kumuona mwalimu yule anafanana vilevile na Mfalme Siddik. Alishudia kuona mwalimu huyo akisogea hadi kwenye meza moja na kuweka vitabu vyake huku mkono mwengine akiwa ameshika bakora zaidi ya tatu. Aligeuka kuwatazama wanafunzi baada ya kuitikia salamu aliyopewa.


"Kaeni chini...Viongozi wa darasa naomba mkusanye madaftari yote, naamini siku tano zimetosha kuifanya kazi ambayo nimewapa, tangu Ijumaa hadi Jumatatu kama wewe hukumaliza kazi yangu basi ni makusudi hayo, kama wewe umefanya hesabu zangu 25 ili tu umalize na nisahihishe nikute umepata hesabu kuanzia 15 kushuka chini ni makusudi hayo. Kama wewe unajua umekopi kwa mwenzako na kuhamishia kwako nikute majibu na njia zinafanana kwa watu kama pia ni makusudi maana umeshindwa  kushirikisha ubongo wako. Na mimi watu wote wanaofanya makosa kwa makusudi katika somo langu lazima niwanyooshe wakae mstari mmoja na wenzao. Hatuwezi kuwa kwenye msafara mmoja lakini wengine fikra zipo nyumbani kwao." alisema yule mwalimu akiwatazama wanafunzi wa darasa hilo.


Amour alibaki kumtazama yule mwalimu vile anavyoogea ni vilevile ambavyo Mfalme Siddik anavyozungumza. Alijikuta akitabasamu tu baada ya kuona ni maajabu hayo anayoyaona mbele yake.

Viongozi wa darasa wakaanza kupita kwa wenzao wakikusanya kazi hiyo. Kuona hivyo Amour aliichukua karatasi ile ya maswali na kuiweka kwenye daftari lake kisha akalifunika na kuliweka pale mezani huku akishika kwa mkono wake ambao amevaa ile pete. Aliomba maneno yake kadhaa huku akiwa amefumba macho na muda huo huo kiongozi akapita pale akihitaji kulikusanya daftari lile. Alifumbua macho na moja kwa moja akalifunua lile daftari na kushuhudia maswali yale yakiwa yamechambuliwa kwa uweledi mkubwa kana kwamba aiyefanya kazi hiyo ni yeye. Hata yeye hakuamini kuona vile na hapo ndipo akaona kweli pete ile ni muhimu sana katika maisha yake. Alikusanya daftari lile na kuendelea kumtazama mwalimu yule.


Alionesha kutokuwa na utani kabisa na wanafunzi, muda wote alikuwa anaonekana kuwa makini na kazi yake hiyo hasa pale alipotaka kufahamu kama kuna ambaye hakufanya kazi hiyo. Alipohakikisha hakuna aliyekua hajafanya kazi, aliagiza viongozi wa darasa hilo kuchukua madaftari yale wapeleke ofisini.


"Leo sitafundisha chochote ila nitakapomaliza kusahihisha kazi hii hata baadae nitakuja na kama nilivyosema wale watu wangu wa makusudi mjiandae." alisema Mwalimu yule na kutoka zake mule darasani baada ya madaftari yale kupelekwa ofisini kwake. Hapo wanafunzi wote wakaanza kushukuru Mungu kwa kuona wamepewa uhuru maana walikuwa wameingiwa na woga.


"Huyu ticha naona amekuja kwa kasi sana hapa shuleni, atapoa tu we subiri hajakutana na wababe, sasa

we mwalimu hata wiki haijaisha tayari wanafunzi wameanza kukuogopa duh!" alisema mwanafunzi mmoja na kuwafanya hata baadhi ya wenzake wamuunge mkono kwa kile alichokisema. Wakawa wanamuongelea mwalimu yule huku Amour akisikiliza tu kinachoendelea huenda akasikia hata jina la mwalimu huyo ili apate kufananisha na mtu anayemjua.


Baada ya muda vipindi vengine viliendelea hadi ulipofika muda wa mapumziko kengele iligongwa na wanafunzi wakaelekea kupata kifungua kinywa. Muda huo ndio Amour aliutumia kupata uhakika juu ya yule mwalimu, alimuona Eliza akiwa anaelekea kwenye chai akamkimbilia kumuwahi wakawa wanatembea wote.


"Baba Azizaaa vipi uko powa." alitania Eliza akionesha kutabasamu.


"Hebu acha ujinga wako bwana, ..hivi Eliza yule mwalimu anaitwa nani maana jina lake nimelisahau kidogo.."


"Mwalimu yupi tena ?"


"Yule mgeni aliyekusanya madaftari."


"Dah halafu umenikumbusha, kumbe ile kazi uliifanya ukawa unanidanganya mshkaji wangu si fresh Amour.." aliongea Eliza akiwa anampa lawama Amour.


"Dah usinifikirie vibaya rafiki yangu nilijua unanitania muda ule ndio maana nikakujibu vile, nisamehe sana." aliongea Amour kwa upole.


"Mimi nilikuwa sijamaliza kweli sio utani, sema fresh nilikopi kwa Fardat ila sasa sijui itakuwaje yule ticha akijua kama tumeibiana majibu,"


"Mimi sidhani kama ataweza kupitia kila daftari kuona kama watu wamekopiana mpaka njia, vile ni vitisho tu, haya hebu nikumbushe jina lake basi."


"Yule si Mwalimu Sadiki na wewe jana tu kalirudia jina lake mara kwa mara."


"Sadiki? Mhh... Sadiki au Siddik?" aliuliza Amour na swali lake hilo likaonekana kumkera Eliza.


"Kwani una matatizo ya masikio siku hizi? Utanikera sasa hivi Amour. Anaitwa Sadiki." alisema Eliza na kumfanya Amour abaki kushangaa. Kwa namna fulani aliona jinsi majina hayo mawili yanavyoshabihiana hali iliyopelekea kuwa na wasiwasi juu ya mwalimu yule.


"Haya shemeji huyo anapita." alisema Eliza na kumfanya Amour ageuke kutazama, alimuona Aziza anapita kuelekea kwenye chai. Akabaki kutabasamu tu huku akiwa anaongozana na Eliza nao wakielekea huko. Muda wote alikuwa akimtazama Aziza kwa umbo na vile alivyo akapata kuona jinsi alivyofanana na Maya kule Eden. Hapo ndipo akapata kujua kweli duniani ni wawili wawili lakini kwa upande wa Mwalimu Sadiki hakuweza kuamini maana aliona hata majina jinsi yalivyo shabihiana na kujipa moyo atalifuatilia swala hilo hapo baadae.


Huku Eden mambo yalizidi kupamba moto kila sehemu. Ilikuwa ikisubiriwa siku ya kesho ambayo ndio mashindano hayo yatarindima kwenye uwanja maalumu kwaajili ya mpambano. Watu walikuwa wakijifua kikamilifu kuhakikisha wanapata ushindi siku hiyo. Kwa Lutfiya yeye bado alikuwa na kazi ya kuhakikisha swala lake linafanikiwa kabla ya siku hiyo. Alihakikisha siku hiyo anatumia njama yeyote ile kuhakikisha anafanya swala lake. Alitoka kwake na kuelekea upande wa jikoni kwanza kuhakikisha kama kuna idadi zaidi ya watu. Kwa bahati alipata kumuona msichana mmoja peke yake akiwa anaandaa chakula muda huo.


"Hii nafasi sipaswi kuichezea tena ni kuongeza umakini tu." alijisemea mwenyewe akiwa anatazama kule jikoni. Muda huo huo alianza kusogea hadi pale jikoni na kumfanya yule msichana amuone Lutfiya.


"Naona unaandaa chakula kwaajili ya Mfalme pamoja na Malkia."


"Ndio, leo nimeona niandae mapema maana kuna kazi zinanisubiri hapo baadae."


"Upo peke yako leo?"


"Ndio, wenzangu wametoka kwenda sokoni kutafuta mboga za kesho." alisema yule msichana huku akiwa shapu kuendelea na kuandaa.


"Dah pole sana, wacha nikusaidie baadhi ya kazi mwenzangu haya vyombo vya kumuwekea Maya chakula viko wapi.?" alisema Lutfiya akisogea kwenye sufuria na yeye, yule msichana aliona ni wema anaofanyiwa kusaidiwa kazi. Alichukua vyombo hivyo na kumpatia Lutfiya aliyepokea na kuanza kuweka chakula huku akimtazama mara kwa mara yule msichana. Dakika kadhaa kupita aliweza kuweka mambo sawa msichana yule na akanyanyua vyakula na kuelekea sebuleni kuandaa mezani. Lutfiya alibaki kumtazama tu aliondoka na kuona ndio muda pekee wa yeye kufanya kile kilichomleta. Aliingiza mkono kifuani na kutoa kikaratasi kidogo kilichokuwa na unga fulani wa rangi.


Akaanza kuchota kwa mkono na kuanza kunyunyizia kwenye chakula kile kilichopaswa kwenda kwa Maya.

Alipolikamilisha zoezi hilo alikirudisha kikaratasi kile na kuendelea na kazi nyengine. Muda huo huo yule msichana alirejea na kumkuta Lutfiya akimsaidia hata kuosha vyombo.


"Jamani nashkuru sana leo kwa kunisaidia hivi maana leo ningezunguka kila kazi ningeifanya mimi."


"Usijali kuhusu hivi, sote tunafanya kazi kwenye falme hivyo kusaidiana ni jambo la kawaida sana. Itafika siku na wewe ukiwa hauna kazi unaweza ukaniona nimebanwa na kazi ukanisaidia pia."


"Ni kweli kabisa usemacho" alisema msichana yule bila kuelewa kilichoendelea.


Baada ya muda alichukua kile chakula na kupeleka kwa Maya. Hapo ndipo Lutfiya akabaki kutabasamu na kuona kazi yake inakwenda kukamilika, alibaki kumtazama tu msichana yule akitembea kuelekea chumbani kwa Maya, naye akaamua kutoka mule jikoni baada ya kumaliza kazi yake iliyomleta akaondoka kuendelea na mambo yake.


Aliweza kuingia mule chumbani na kumkuta Maya amejipumzisha kitandani, taratibu kwa heshima akasogea hadi kwenye meza iliyopo pembeni na kuweka kile chakula. Akaanza kuandaa pale kila kitu na alipokamilisha aliweza kumkaribisha Maya aweze kusogea mezani kupata chakula.


"Sawa nakuja wewe kaendelee na kazi." alisema Maya akiwa amejilaza kitandani. Yule msichana aligeuka na kuondoka zake baada ya kukamilisha kazi yake.


Dakika chache kupita alishuka pale kitandani na kuelekea kwenye ile meza iliyoandaliwa vyakula. Alisogeza kiti na kukaa pale huku akiweka sahani ili apate kupakuwa chakula.


ITAENDELEA..... 


Amour yupo Unguja, na Maya ameshapelekewa chakula kilichotiwa dawa. Je! Nini kitakachojiri? Au kwa leo atafanikiwa? Hebu jaribu utabiri wako Maya ndio anakula huyo 🤣🤣🤣


GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI (10)



Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group