PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 10


 


SEHEMU YA 10


ILIPOISHIA


Dakika chache kupita alishuka pale kitandani na kuelekea kwenye ile meza iliyoandaliwa vyakula. Alisogeza kiti na kukaa pale huku akiweka sahani ili apate kupakuwa chakula.


ENDELEA NAYO..... 


Baada ya dakika kama kumi Lutfiya aliongoza njia kuelekea kwa Maya ili apate kuona kama jambo ambalo amelifanya limeanza kufanya kazi. Moyoni alikuwa mwenye furaha sana akijua kila kitu kinakwenda sawa. Alipita sehemu kwenye koridoo na kuweza kumuona Samir akiwa anatokea njia ya kuelekea sebuleni walipo Mfalme na Malkia wakiwa wanakula, walipishana kama hawajuani huku akimtazama akiwa ameshika kitenga akielekea nje. Alipofika mbele Lutfiya aligeuka kumtazama Samir aliyeonekana hana habari kinachoendelea.


Alimsindikiza kwa kumsonya kuonesha hampendi maana amekuwa akimvurugia mipango yake yote. Aligeuka kuongoza njia hadi alipofika nje ya chumba cha Maya, alitazama huku na kule kuangalia kama kuna mtu maeneo yale.


Alipohakikisha usalama upo alisogea kwenye dirisha na kuchungulia ndani akapata kumuona Maya akiendelea kula. Hapo akapata tumaini la kuona kazi yake imefana. Alishangiria pale dirishani na baada ya kuonesha furaha yake hiyo alisogea mpaka pale mlangoni kisha akagonga hodi na kuingia. 


Alimuona jinsi Maya anavyoendelea kula pale mezani bila kujua kinachoendelea. Taratibu akasogea hadi pale.


"Lutfiya vipi.!" aliongea Maya akionekana kunyanyua kipande cha nyama ya kuku na kukipeleka mdomoni kutafuna.


"Ah samahani binti wa Mafalme, nilikuja kwa ajili ya kuangalia kama umemaliza kula ili nipate kutoa vyombo."


"Bado nakula uje baadae." alisema Maya akiendelea kula.


Lutfiya aligeuka huku akiwa ni mwingi wa furaha akaanza kuondoka mule ndani.


"Halafu, pitia kwa mama yangu umwambie Nashkuru sana kwa chakula chake." alisema Maya na maelezo yale yalimfanya Lutfiya asielewe yanamaana gani.


"Sijakuelewa una maana gani binti wa Mfalme." aliongea Lutfiya akitega masikio yake kumsikiliza Maya.


"Hujasikia au hujaelewa, nenda kwa mama umwambie Maya anasema asante kwa kile chakula alichompa Samir kuniletea, umeelewa..?" aliongea Maya na kumfanya Lutfiya ashtuke kusikia maneno hayo.


Alitengeneza tabasamu usoni mwake na kumuitikia Maya kisha akatoka zake nje.

Alihisi kuvurugwa akili baada ya kutoka nje, alisimama sehemu na kuanza kutafakari maneno ya Maya.


"Inamaana na hili swala Samir ameliingilia? Amejuaje kama nilifanya?" alijiuliza Lutfiya na kubaki njia panda. Alipokumbuka muda ule wakiwa wanapishana na Samir aliweza kuona ameshika kitenga akitoka nacho nje. Hakuweza kufahamu ndani yake kulikuwa na nini. Hapo ndipo akaanza kuhisi huenda kuna jambo Samir amelifanya, haraka akatoka na kuelekea alipoenda Samir kujua alibeba nini mule kwenye kitenga.


Upande wa pili Dalfa alikuwa njiani na vijana wake wawili wanakuja ndani ya mji wa Eden na lengo hasa ni kumtambua mtu ambaye amekuwa akimtilia mashaka. Alifumba macho yake na kuanza kuvuta hisia huku akichanganya na nguvu zake kujua kinachoendelea Eden. Upeo wake wa kufikira ulimfanya aone zile nguvu ambazo anazitilia shaka kwa yule mtu bado zipo Eden hali iliyomfanya afumbue macho haraka baada ya kutambua kile alichokiona huenda kikawa kweli. Akazidi kupata hamasa ya kufika Eden haraka kumpata mtu huyo.


Lutfiya alifika nje na kuzunguka nyuma ya jengo kwenye zizi la farasi na kuweza kumuona Samir akiwa anawatupia kuku pamoja na njiwa wengi sana chakula. Alipotazama kwa makini alipata kuona ni punje za wali Samir akiwa anawapa wale ndege huku wengine wakionekana kulewa na kuishiwa na nguvu kabisa baada ya kula chakula kile. Hapo ndipo Lutfiya akapata kutambua kile chakula alichotia unga ule kwa lengo la kumdhuru Maya  endapo angelikula chakula kile.


Alijikuta akikasirika sana baada ya kuona mpango huo tena amefeli. Alimuona Samir akinyanyuka pale alipokaa na kugeuka kumtazama wakabaki wakiangaliana. Samir akapiga hatua na kusogea pale alipo Lutfia ambaye alibaki kuangalia tu pembeni akionesha kukasirika.


"Naomba uniambie leo, kwanini unataka kumdhuru Maya?. Mara ya ngapi hii nimekuwa nakuona ukijaribu kumuwekea vitu vya hatari.?" aliongea Samir huku akimtazama Lutfiya kwa jicho la hasira sana.


"Samir nisikilize.. haya mambo wewe hayakuhusu usitafute matatizo mengine. Kaa mbali na Maya usijaribu kunizuia kwa lolote lile kuanzia sasa, fuata kilichokuleta humu kwenye falme fanyakazi zako." aliongea Lutfiya kwa kujiamini sana baada ya kuona sasa akizidi kumhofia Samir anaweza asifanikiwe kabisa kile alichowaahidi wenzake.


"Wewe.. hunijui sikujui nimekukuta tu humu na kukupa heshima kama mfanyakazi mwenzangu. Siwezi kukaa kimya nikikuona ukijaribu kumdhuru binti wa Mfalme. Yule ni Malkia wetu wa baadae iweje umfanyie visakama hivi, amekukosea nini au kuna watu wanakutuma uje kuharibu hii furaha iliyopo sasa?. Ina maana haufurahia kupona kwake, ulitaka afe si ndio." aliongea Samir akiwa makini na kile asemacho. Lutfiya mwenyewe alishangaa kuona Samir aliyemzoea hivi leo anaongea kwa kujiamini sana.


Mwanaume aligeuka na kuwatazama wale kuku na njiwa wote wakiwa hoi pale chini na wengine wakionekana kufa kabisa.


"Nimekuvumilia kwa mambo uliyokuwa ukifanya nyuma sasa imetosha, ni muda wa kuyaeleza mambo yako kwa mhusika. Ulitaka kumuua Maya kwa sumu hebu ona.. wewe sio binadamu wakuishi kwenye falme hii." alisema Samir akimueleza ukweli Lutfiya aliyebaki kutulia tu hana neno la kusema. Samir alimpushi Lutfiya pale alipisimama na kupita kuelekea zake.


"Sawa endapo ukienda kusema kwa Maya nami naelekea kwa Mfalme kumueleza ulivyotaka kumbaka Maya. Hapo ndipo tutakapojua nani ataondoka kwenye falme hii." alisema Lutfiya na kumfanya Samir asimame ghafla na kushindwa kuendelea mbele na safari. Aligeuka nyuma kumtazama Lutfiya aliyekuwa anamuangalia Samir.


"Unasemaje,? Mimi nilitaka kumbaka Maya,? Wapi na lini." aliuliza maswali kwa mkupuo Samir baada ya swala hilo kutolielewa vyema.


"Lini? Unajifanya kusahau kile ulichotaka kukifanya usiku ule Maya akiwa kitandani?" alisema Lutfiya na kumfanya Samir ashangae habari hizo ambazo kwake ni ngeni. Alijua huenda mwenye jina la Samir ndio alitaka kufanya tukio hili. Taratibu akaanza kukosa ujasiri wa kuendelea na msimamo wake wa kupeleka taarifa zile kuhusu Lutfia.


Alilitafakari swala hilo na mwisho akageuka na kwenda hivyo hivyo ndani. Alimuacha Lutfiya pale nje akiwa ameshika kichwa kuona mambo yamezidi kuwa magumu kwake.


"Kama nitafukuzwa humu basi lazima na yeye atafukuzwa sitakaa kimya." alisem Lutfiya akiwatazama wale kuku wakiwa pale chini wengi wao waionekana kukata roho. Hakujali kuhusu hilo aligeuka naye kuelekea ndani ya falme kujua kinachoendelea kama Samir ataongea kweli.


Samir alifika ndani na kukutana na mfanyakazi mmoja wa ndani.

"Malkia alikuwa anakuhitaji, yupo ukimbini." alisema msichana yule na kugeuka kuondoka zake. Samir aliposikia hivyo haraka akaongoza njia kuelekea ukumbini, alipata kumuona Malkia akiwa amekaa na Mfalme wakiwa wanapata kinywaji.


"Vipi ulifikisha chakula kile?" aliuliza Malkia akimtazama Samir aliyesogea pale na kutoa heshima kwao.


"Ndio nilifikisha Malkia wangu, na amekushukuru kwa kumpatia chakula kile." alisema Samir.


"Sawa chukua na hii umpelekee." alisema Malkia akinyanyua bilauri lenye kinywaji ndani yake, Samir alipokea na kugeuka kuelekea kwa Maya kumpati. 


"Maya ameanza kumuamini Samir hadi kumtuma leo chakula angali wafanyakazi wapo." alisema Mfalme akimtazama Samir akitokomea.


"Ni maamuzi yake naona leo kaamua kumtuma Samir." alisema Malkia wakawa wanaendelea kupata kinywaji.


Samir akiwa anaelekea kwa Maya njiani alijikuta akihema baada ya kuona amefanya kazi kubwa sana siku hiyo. Muda ule ambao Lutfiya alikuwa akiandaa kuweka unga wenye madhara kwa Maya kwenye chakula kule jikoni huku upande wapili Amour aliweza kutambua baada ya kuona ile pete yake ikimbana, na alipoitazama aliona tukio lile Lutfiya akiwa ananyunyizia ule unga kwenye chakula cha Maya hali iliyopelekea Amour atoke mbio akiwa zake kwenye mgahawa anakunywa chai na moja kwa moja akaelekea kwenye vyoo vya shule lengo asionekane. Hata alipoingia mule aliitazama pete ile na kuanza kuongea maneno fulani na ghafla akajikuta yupo kwenye choo ndani ya falme. Alitoka haraka na kuumiza kichwa atazuiaje swala lile ili hata yeye asijulikane wala kuulizwa amelijuaje swala hilo. Alielekea kwa Malkia akimkuta yupo mezani anakula pamoja na Mfalme.


"Malkia wangu, Maya ameniagiza kwako anasema angependezwa leo kula chakula ambacho kimeandaliwa kwaajili yenu wazazi wake apate kuonja ladha hiyo." alisema Samir akiwa anamtazama Malkia Rayyat.


Alishangaa kusikia hivyo akageuka kumtazama mumewe wakabaki kutazamana.


"Una uhakika na hicho unachokisema Samir.?" aliuliza Mfalme akiwa anamtazama Samir.


"Bila shaka, ni maneno ya binti yako Mfalme wangu na ndio kaniagiza nifikishe hili kwa mama yake." alisema Samir akionesha kweli anamaanisha. Malkia alianza kuamini kile asemacho Samir. Kwa kuona ni kwa ajili ya afya ya mwanaye wacha atoe kile chakula. Aligawa nusu ya vyakula vilivyokuwepo pale mezani na kumruhusu Samir achukue umpelekea Maya. 


Haraka Samir alifanya zoezi hilo huku akiwaacha Mfalme na Malkia wamtazame tu. Muda ule chumbani Maya alivuta kiti na kukaa, akasogeza sahani na kupakuwa chakula anachotaka kula.


Alipotaka kupeleka kijiko mdomoni aliona mlango ukifunguliwa  na kumuona Samir akiwa ameshika vyakula. Ilimbidi abaki kushangaa tu na kuona Samir anasogea pale.


"Umeshakula hata kijiko kimoja?" aliuliza Samir akiwa anahema sana.


"Umenishtua maana ndio nilikuwa naanza kula Samir, haya mbona umekuja na vyakula hivi.?" aliuliza Maya akiwa haelewi. Bila kuchelewa alianza kutoa kile chakula cha mezani kilichoandaliwa ambacho ndio kiliwekewa ungaunga ule na Lutfiya.


Alipomaliza akamuwekea mezani sasa chakula kile alichopewa na Malkia  kisha akamtazama Maya.


"Nimeagizwa na Malkia nikupatie chakula hichi ambacho amekichagua kwaajili ya mwanaye, hakika anakujali na kukupenda na amenisisitiza ukipokee upate baraka zake." alisema Samir na kumfanya Maya atazame kile chakula, hakika kilikuwa kinavutia sana.


"Una uhakika kweli kama amekuagiza hivyo.?,"


"Bila shaka, nimeagizwa hivyo na Malkia Rayyat." alisema Samir na kumfanya Maya asipoteze muda alisogea vizuri na kuanza kula chakula kile.


"Haya ondoka na hicho chakula chengine sitaweza kula." alisema Maya akiwa anaendelea kula chakula kile akicholeta Samir.


Alikichukua na kuweka kwenye kitenga kisha akatoka nacho nje, hapo moyo wae ukawa umetuliana baada ya kuona ameokoa maisha ya Maya kwa mara nyengine, na muda ule alipotoka ndipo akapishana na Lutfiya njiani na wala hakutaka kumtazama maana alifahamu kuwa anakwenda kupata uhakika wa kazi aliyokuwa ameifanya.


Yote hayo alikuwa akikumbuka Samir muda ule aliokuwa amepewa bilauri lile kupeleka tena kwa Maya. Hata alipofika aliingia na kumpatia Maya kile kinywaji kisha naye akageuka kurudi zake kupumzika akiwa amenyamaza kusema lile swala la Lutfiya.


ITAENDELEA....


GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA MOJA (11)




Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group