SEHEMU YA 11
ILIPOISHIA
Yote hayo alikuwa akikumbuka Samir muda ule aliokuwa amepewa bilauri lile kupeleka tena kwa Maya. Hata alipofika aliingia na kumpatia Maya kile kinywaji kisha naye akageuka kurudi zake kupumzika akiwa amenyamaza kusema lile swala la Lutfiya.
ENDELEA NAYO......
TUENDELEE...
Lutfiya alikuwa akimtazama Samir muda wote na kufahamu swala lake halikuweza kufikishwa kwa Maya. Alishusha pumzi na kurudi zake kuendelea na kazi yake.
Baadae askari wa Eden walianza kutembea mji mzima wa Eden mitaani kuwatangazia wananchi kuweza kufika siku ya kesho kwaajili ya kutazama mapambano ambayo yanahusisha kumpata shababi wa kuweza kumlinda binti wa kifalme, Maya.
Watu walizidi kujitokeza kujiandikisha ili kujaribu bahati zao kama wataweza kuibuka kuwa washindi. Hadi kufika jioni hiyo uwanja maalumu uliandaliwa kwa siku ya kesho.
Mfalme Siddik alianza kuwaagiza baadhi ya askari wake kupeleka mualiko kwa baadhi ya Mataifa jirani ili kuweza kushuhudia mashindano hayo.
Huku kwa Jamal baada ya kujua kinachoendelea alikuwa amejiandaa kwaajili ya mpambano huo wa kesho Alipata chachu ya kuzidi kutamani ushindi kwa siku ya kesho mara baada ya kutambua ana watu wanaomuunga mkono yeye ili kuweza kumteka Maya kiakili. Wanajua fika wakilifanikisha hilo basi wanauwezo wa kufanya chochote ndani ya Eden kwa maana Maya ndiye mtoto pekee kwa Mfalme Siddik na mkewe Malkia Rayat.
"Ushindi kesho lazima ili tufikie malengo yetu, nimetembea Eden kwenye mitaa na kuona jinsi baadhi ya watu wakijiandaa kwa ajili ya kesho sijaona mtu wa kuweza kupambana nami. Nakuhakikishia baba hii nafasi tuliyokuwa tukiisubiri kwa muda mrefu naamini imewadia." alisema Jamal akiwa mwenye kujiamini. Baba yake alimtazama tu huku akitabasamu kwa furaha akiamini kile asemacho mwanaye. Alimtia moyo sana siku hiyo na baadae Jamal aliingia zake sehemu ya kufanyia mazoezi yake Alisogea mbele na kuvua nguo yake ya juu. Alionekana kutuna kifua huku mkono wake uliojazia ulimfanya ajiamini sana licha ya kuwa ni mtoto wa Mfalme. Alipiga hatua kadhaa na kutoa upanga mrefu uliokuwa pembeni umehifadhiwa kisha akaukamata kwa mikono miwili na kurudi nyuma hatua tatu. Alitoa heshima kwa kuinama chini kidogo kisha akaanza kuonesha ujuzi wake wa kutumia upanga kwa weledi mkubwa sana huku akionekana kuwa mwepesi mwili wake.
Hakika alikuwa fiti kwenye kupambana hali iliyomfanya baba yake aliyekuwa akichungulia nje atabasamu tu na kuona kweli amepata kidume.
Muda huo huo askari mmoja aliingia na kumfanya Mfalme atoke kule aliposimama akimtazama mwaaye akasogea alipo yule askari.
"Vipi kuna tatizo?" aliuliza Mfalme Faruk akiwa anamtazama askari yule.
"Hapana Mfalme, kuna askari wa Eden wamefika wapo nje wanashida na wewe, hivyo nimekuja kukupa taarifa hiyo kuwa wanahitaji kukuona." alisema yule askari.
"Umesema Askari wa Eden?"
"Ndio Mfalme wangu," alisema yule askari na kumfanya Mfalme huyo asitambue nini kilichowaleta askari hao. Alimpa amri yule askari akawakaribishe askari hao kisha naye akaelekea ukumbini kukaa akiwasubiri kujua wamekuja kwa dhumuni gani.
Dakika kadhaa waliingia askari wawili wa Eden na walipofika kwa Mfalme hiyo waliinamisha vichwa chini kumpa heshima yake kisha wakanyanyuka. Mfalme alijenga tabasamu usoni na kuwakaribisha wakae.
"Hapana sisi sio wakaaji Mfalme Faruk, tumekuja hapa kuleta ujumbe kutoka kwa Mfalme wetu Siddik." alisema askari mmoja na kutoa karatasi moja iliyokunjwa na kumpatia Mfalme huyo. Aliipokea huku akiwa na shauku ya kujua kilichoandikwa.
"Inahusu nini lakini?" aliuliza Mfalme huyo akimtazama yule askari.
"Siku ya kesho kutakuwa na mapambano ya kumtafuta shababi wakuweza kua mlinzi wa binti wa Mfalme katika kiwanja kikubwa cha Eden hivyo kwa heshima yako Mfalme Siddik anakuomba uhudhurie siku hiyo ili kuonesha ujirani wa mataifa haya mawili. Hivyo anakuomba sana ufike siku ya kesho." alisema yule askari na kumfanya Mflame yule aelewe kilichodhamiriwa mule kwenye ile karatasi. Hakuona haja ya kuendelea kuifungua.
"Sawa hakuna tatizo, mwambieni tutakuwa pamoja." alisema Mfalme Faruk na kuwafanya wale askari waombe ruhusa ya kurejea Eden muda huo. Mfalme aliwaruhusu naye akarudi kuelekea kwa Jamal aliyekuwa anaendelea na mazoezi yake jioni ile. Alipomuona baba yake ameingia mule ilibidi asimamishe zoezi lake.
"Kuna taarifa nimepokea hapa kutoka Eden."
"Eden? Taarifa inahusu nini?" aliuliza Jamal akiwa ameshikilia upanga wake huku mwili wake ukitiririka jasho.
"Mfalme Siddik amenialika kwenye mashindano hayo hivyo nami nitakuwa miongoni mwa watu watakaotazama kinachoendelea kwenye kiwanja vile." alisema Mfalme na taarifa zile zilimfurahisha mwanaye na kujikuta wote wakifurahi baada ya kuona wanapata nafasi zaidi.
Usiku huo kwa Mfalme Siddik aliutumia kuelekea kwa binti yake kumuangalia. Alimkuta Maya akiwa anasoma vitabu mule ndani, aligonga mlango na taratibu akaanza kusogea hadi pale alipo binti yake aliyeonekana kuwa makini na kusoma. Alitazama kitabu kile kichokuandikwa EDEN YA MFALME SALEH. Alijikuta akitabasamu tu Mfalme baada ya kutambua mwanaye anamsoma aliyekuwa Mfalme wa Eden miaka ya nyuma.
"Unajua Eden ni Taifa ambalo tangu hapo awali lilikuwa na historia ya kipekee. Viongozi wake walikuwa mashuhuri sana na wenye nguvu huku wakiheshimika kila kona na kila Taifa ambalo lilikuwa na askari wake. Majeshi ya Eden yalikuwa imara sana na kuogopwa na kila Taifa ndio maana vita zao zilikuwa dhidi ya mataifa yenye kuongozwa na viongozi wenye kutumia nguvu za kichawi kwa maana tangu enzi hizo Mfalme wa kwanza wa Eden ambaye ni Saleh alikuwa na nguvu kubwa sana za ajabu hivyo aliweza kuwadhibiti wabaya wake." alisema Mfalme Siddik na kumfanya Maya amtazame.
"Inamaana hata Mfalme Saleh alikuwani mchawi.?" aliuliza Maya.
"Bila shaka, alikuwa ni zaidi ya wengine na uchawi wake haukuwa kama wa wengine. Aliutumia kuwasaidia wananchi wake katika shida na hata vita."
"Sasa kwanini unakataza uchawi Eden baba wakati hata Mfalme mwenzako alikuwa hivyo!?"
"Binti yangu Maya, muda na zama zinabadilika. Uchawi wa Mfalme Saleh haukuwa wa kudhuru tofauti sasa, kila mtu anatumia uchawi kumdhuru au kumkomesha mwenzake. Na ndio maana nilipoliona nikaweka amri ya kuuawa wachawi wote bora tuishi kawaida tu. Tazama hata wewe walivyokufanya, ulifanya kosa gani sasa binti yangu!, ni chuki tu za watu na ndio maana sitaki kusikia uchawi tena hapa Eden." alisema Mfalme na maelezo yake yakamuingia mwanaye. Alikitazama kile kitabu na kupata swala la kumuuliza baba yake.
"Huyu Mfalme Saleh alitokea Bara gani.?"
"Mfalme huyu alikuwa mzawa hapa Eden na Mkewe Zainab alikuwa pia mtu wa Eden na katika mwisho wa maisha yao waliacha vitu vingi ili wafalme wajao waweze kufuata. Kitu pekee ambacho kilikuwa cha tofauti ni pale ambapo ilipatwa kuachwa alama ya kiganja cha mkono iwe kama nembo na ishara ya Mfalme atakayekuja kuitawala Eden na ilisadikika alitokea Bara la Afrika.
Hivyo wafalme wote walioweza kuitawala Eden walijua ipo siku Eden itakuja kutawaliwa na mfalme wa aina hiyo." alisema Mfalme Siddik akiwa anamueleza mambi binti yake.
"Ahaaa ndio maana nimesoma kurasa nyingi humu nimeona likitajwa hili Bara la Afrika ambalo ametokea Mfalme huyu anayeitwa Saleh. Kumbe hiki kitabu ni cha Mfalme Saleh aliyetokea Bara la Afrika."
"Ndio, hiki kitabu kinamuhusu yeye. Aliweza kuibadilisha Eden kutoka kwenye ubaguaji wa rangi za watu hadi leo hii tunaishi na watu weusi kama ndugu na wengi wamezaliana ndani ya Eden, tupo nao siku zote." alisema Mfalme Siddik na kumfanya Maya atambue historia fupi ya Mfalme Saleh.
"Kwahiyo hata hawa wakina Samir wametokana na huyu Mfalme Saleh?"
"Sio Samir tu wengi unaoona na ngozi nyeusi wametokana na uzao huo wa Mfalme Saleh." alisema Mfalme na kuzidi kumuelewesha binti yake ambaye hakuona umuhimu wakuendelea kusoma kitabu tena, akawa anasimuliwa mambo mengi sana baba yake.
Taratibu akaanza kuona jinsi watu weusi walivyo na upendo kwa watu na umuhimu pia katika maisha ya wengine.
Mwishowe Mfalme aligusia swala la kesho na kumtaka Maya aweze kua na furaha ya swala hilo maana mtu anayetafutwa ni kwaajili yake ili aweze kumlinda katika maisha yake.
Alimuelewa baba yake na kukubaliana naye kwa jambo hilo ambalo awali hakupendezwa nalo lakini mwisho wa siku aliona muhimu kwake kuweza kuangaliwa kama binti wa kifalme. Baada ya muda waliagana mtu na mwanaye kisha Mfalme akatoka zake na kuelekea kulala na mkewe. Maya alikitazama kile kitabu na kubaki kutabasamu.
Alifurahishwa na jinsi Mfalme huyo alivyoleta mabadiliko katika taifa hilo la Eden na kuona ni mfano wa kuigwa. Alisogea nacho kile kitabu hadi kitandani akapanda na kujilaza, alifungua kurasa kadhaa akaendelea kukisoma huku usingizi ukimnyemelea na muda mfupi akapitiwa na usingizi huku kitabu kile kikiwa kifuani mwake.
Alionekana msichana mmoja akiwa hoi amepiga magoti chini ya ardhi huku sura yake iliyozibwa na nywele zake ikiangalia chini kufanya asiweze kuonekana vizuri, mikono yake ikiwa imefungwa minyororo huku pembeni akionekana mtu mmoja aliyekuwa amejifunika sura yake akiwa nyuma ya msichana huyo akiwa ameshika upanga wenye kung'aa. Kwa mbali alionekana kijana mmoja akiwa anakuja eneo lile akiwa anachechemea huku mkono wake wa kulia uliokuwa umeshika upanga ukiwa unavuja damu. Alikuwa akihema sana kuonesha ametoka kupambana na watu wengi sana.
Alipofika pale alipata kuona yule mtu akipeleka upanga ule shingoni kwa yule msichana pale chini huku akitabasamu.
"Ukitaka kumsaidia huyu pambana na mimi, ukinishinda atakuwa huru umemsaidia. Na endapo nikakushinda au ukakataa kupambana nami basi kichwa cha mtu wako huyu nitakifyeka kwa upanga huu kama hivi..." alisema yule mtu na kunyanyua upanga wake juu, yule msichana taratibu akaanza kunyanyua sura yake kumtazama yule kijana alikekuwa mbele yake akionekana kuvuja damu mkononi akiwa hoi. Kijana yule alipomtazama vizuri yule msichana alishtuka baada ya kuifahamu sura ile na muda huo huo alishuhudia upanga wa yule mtu ukipita shingoni mwa yule msichana kama fyekeo na kukata kichwa. Yule kijana alishangaa kuona tukio lile huku akishikwa na bumbuwazi, hasira zilimpanda na kujikuta akipiga kelele kwa nguvu...
"HAPANAAAAAA......." alishtuka kutoka kitandani baada ya kusema maneno hayo. Alitazama huku na kule na kuona kiza tu kikitawala mule ndani. Alinyanyuka na kuwasha taa ya kandili kwanza kisha akarejea pale kitandani huku akishusha pumzi kwa nguvu.
Alikuwa ni Samir muda wote huo alikuwa akiota ndoto hiyo ambayo alijiona dhahiri ni yeye ndiye aliyekuwa akivuja damu mkononi huku akishuhudia msichana yule akikatwa kichwa na mtu ambaye hakuweza kumtambua kutokana na kuificha sura yake. Aliikumbuka ile sura ya yule mwanamke na kubaki kushika mdomo huku akiwa na hofu haamini kile alichokiona ndotoni.
"Hii ni ndoto gani jamani naota?. ndoto ya kutisha...Mmmh hapana.. Huwezi kufa vile Maya angali mimi nipo hii ni ndoto tu wala haina ukweli wowote." alisema Samir akijituliza moyo wake baada ya ile ndoto kutokea. Alipuuza na kuona haina ukweli wowote, alizima ile taa ya kandili na kujilaza kitandani japo hakuweza kuupata usingizi mapema akiifikiria ile ndoto..
Asubuhi ya siku iliyofuata kulipopambazuka watu walianza kufanya kazi zao mapema sana wakijua hapo baadaye kutakuwa na mashindano ya kupimana ubavu kwa wanaume ambao wamejitokeza ili apatikane mmoja mwenye kuweza kupewa nafasi ya kumlinda binti wa Mfalme.
Si raia tu waliokuwa wakiharakisha kazi zao mapema hata wafanyakazi ndani ya falme walikuwa shapu siku hiyo kukamilisha kazi zao mapema wapate muda hapo baadae wa kuhudhuria kitakachojiri uwanjani.
Samir naye alifanya kila linalowezekana kuhakikisha siku hiyo anafanya usafi kila sehemu pamoja na kuwapa chakula mifugo aliyopewa dhamana ya kuiangalia. Taratibu Eden ikaanza kutembelewa na wageni kutoka sehemu mbalimbali huku washiriki wa mpambano huo wakianza kuwasili kutoka mataifa mbalimbali wakiwa na farasi wao kama usafiri.
Hali hiyo ilimfanya Samir azidi kupata kazi ya kuwapokea watu na kuhakikisha farasi wao wanakuwa katika usalama.
"Hii sasa adhabu kila dakika wanakuja watu si nitashindwa hata kuangalia mashindano yenyewe.!" alisema Samir akiwa anamuweka farasi mmoja sehemu na kumfunga.
Baada ya masaa kwenda mbele uwanja ukafunguliwa na taratibu watu wakaanza kuingia uwanjani kwenda kukaa kusubiri muda ufike. Kila dakika walizidi kuingia ndani hali iliyomfanya hata Samir atamani kuacha kazi anayoifanya naye akawahi. Alitazama pembeni na kuona kwenye kibanda kidogo baadhi ya watu siku hiyo wakiwa wanamalizia kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki nao. Aliwaona wakiwa wapo kwenye mavazi maalumu ya kupambana huku wakiwa wameshika mapanga mikononi. Alipotazama kwa makini aliona mmoja wa wale watu waliokuwa wakijiandikisha pale akiwa amejifunika sura yake huku akiwa mwenye mavazi meusi. Alijikuta akiikumbuka ile ndoto ya jana usiku aliyoota na kumuona mtu kama huyo alikuwa amemuwekea upanga Maya shingoni na mwishowe akaweza kukata kichwa chake hali iliyomfanya Samir ashtuke.
Palepale akaanza kuingiwa na hofu baada ya kuona kama ni maono ambayo huenda yakatokea .Alijikuta akijiuliza maswali kichwani kama ndoto ile ni ya kweli inamaana Maya atakufa kwa kukata kichwa? Na yule mtu aliyejifunika sura ni nani ili amtambue. Palepale akaanza kuhisi huenda katika mapambano haya yanayokaribia kuanza kuna jambo litatokea ambalo litaweza kuwa na madhara katika familia ya Mfalme. Kwa kulijua akaona anapaswa kuwa makini sana katika hilo. Alimtazama yule mtu na kuona dhahiri vile alivyovaa ndio kama vile alivyoota usiku ule na kujikuta akihisi huenda ni kweli kile alichoota kikawa ni maono aliyopewa huku akiyakumbuka yale maneno yakimtaka apambane ili amkomboe Maya, na endapo akishindwa au kukataa basi Maya anakufa kifo kibaya sana hapo mbeleni.
JE! KWAHIVYO NI NDOTO YA KWELI AMA? MIE SIJUI, ILA NINACHOKUSHAURI USIKOSE SEHEMU IJAYO ILI TUJUE KAMA NI MAONO YA KWELI, BASI TUTEGEMEE KUONA MAYA AKIUWAWA KIKATILI ðŸ˜ðŸ˜
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA MBILI (12)
