SEHEMU YA 12
ILIPOISHIA
Alimtazama yule mtu na kuona dhahiri vile alivyovaa ndio kama vile alivyoota usiku ule na kujikuta akihisi huenda ni kweli kile alichoota kikawa ni maono aliyopewa huku akiyakumbuka yale maneno yakimtaka apambane ili amkomboe Maya, na endapo akishindwa au kukataa basi Maya anakufa kifo kibaya sana hapo mbeleni.
ENDELEA NAYO........
Alishtuka sana pale alipo akiwa amemshikia farasi mmoja huku akiona watu wengi sana wakiingia uwanjani pembeni kidogo na jumba la kifalme, taratibu askari wakaanza kusogea eneo lile kwaajili ya kuweka ulinzi. Moyo wa Samir ukawa na hofu sana juu ya swala hilo na bila kujiuliza alijikuta akipiga hatua kuelekea kwenye kile kibanda. Hata alipofika alipata kuona mtu mmoja akiwa anamalizia kujiandikisha. Yule msajili alipomtazama Samir alimtambua.
"Wewe mfagiaji umefuata nini hapa?" aliongea yule mtu akiwa anamdhihaki Samir.
"Nahitaji kujiandikisha na mimi." alisema Samir akiwa anamaanisha kweli.
Yule jamaa alimtazama Samir kwa sekunde kadhaa kisha akaaza kuangua kicheko. Samir alibaki kumtazama tu yule jamaa hadi alipokata hamu yake ya kucheka. Alimtazama Samir akiwa amesimama pale.
"Wewe... usifanye masihara katika uwanja ule, kama umechoka kuishi useme lakini sio kushiriki haya mashindano, kwanza kwa kipi hasa ulichonacho? kuna yeyote unayemuweza humu?" aliongea yule mtu akimkatisha tamaa Samir.
"Hebu tazama hao wanaopita useme yupi kati yao unaweza kumuangusha chini.!?" alisema yule mtu na Samir akageuka kutazama watu wanaopita. Hakika walikuwa ni watu wa miraba minne walijazia miili yao huku wakiwa wana silaha zao za kuingia uwanjani. Samir alipata hofu baada ya kuwatazama watu wale lakini akikumbuka tukio lile la jana usiku kwenye ndoto na kisha muda mfupi akapata kumuona mtu aliyevaa kama vile alivyo mtu yule aliyeweza kumkata kichwa Maya. Alihisi jambo hilo linaweza kutokea muda wowote, aligeuka kumtazama yule msajili.
"Nahitaji uniandikishe nipo tayari kwa lolote." alisema Samir akiwa amemkazia macho yule mtu hadi akashangaa.
"Samir.. unamaanisha kweli au?" aliuliza mtu yule akiwa haamini kile asemacho Samir muda ule. Alishuhudia Samir akitikisa kichwa kumaanisha kile anachosema anamaanisha kweli.
Alikuwa ana wasiwasi juu ya jambo hilo mtu yule maana mashindano hayo ni makubwa na lolote linaweza kutokea uumizwe vibaya ufe au upone hali hiyo ikamfanya awe na mashaka juu ya Samir ambaye anajulikana fika kuwa ni mzembe siku zote.
Hakuwa na jinsi alimuandika Samir na kumpatia wino akachovya dole gumba na kuagizwa kuweka saini ya kidole hicho kwenye neno lililoandikwa KUISHI au KUFA. Samir alifanya hivyo na alipomaliza tu walikuja waamuzi pale kibandani na kuhitaji ile karatasi ya majina ya washiriki kutoka kwa yule mtu. Aliwapatia na wakaondoka zao kuingia uwanjani huku Samir akielekea chumbani kwake, akiwa na wasiwasi kwa mbali.
Hata alipofika alijikuta akishusha pumzi kutoa hofu ambayo inamkabili na ghafla akatokea Nadhra akiwa amesimama na kumfanya Samir amuone.
"Jambo uliloliamua ni zito sana Samir, na ushaamua kulifanya yakupasa ulimalizie tu." alisema Nadhra akiwa ameshika kitu kirefu kilichofungwa kwa kitambaa chekundu.
"Jana nimeota ndoto mbaya sana na ndio imenifanya niamue hivi. Hebu niambie kulikuwa na ukweli wowote kuhusu ile ndoto?"
"Ndio, umepewa upeo wa kutambua kitu kibaya kinachojiri hapo mbeleni. Huenda Maya angekufa kama ulivyoota, ila sio kwamba unashiriki haya mashindano hatakufa, atakufa kama ulivyoota endapo hautashinda. Wewe ndio unatakiwa uwe mtu wa kumlinda Maya kama ilivyopangwa kwa mshindi wa mashindano haya." alisema Nadhra huku akisikilizwa kwa makini. Alimpatia kile kitu Samir akapokea kwa mikono miwili.
"Hilo ni panga, ndilo utakalotumia kwenye mapambano yako muda wote lina uwezo mkubwa sana wakufanya kitu chochote kile kwa dakika chache. Ila jitahidi usijulikane kama unatumia nguvu za kichawi katika mapambano maana ukikamatwa utauliwa kama baba yangu na tusifikie malengo ambayo tunataka yatimie hapo baadae." alisema Nadhra na kumfanya Samir akubaliane naye maneno hayo hivyo anapaswa kuwa makini muda wote.
Sekunde chache tu Nadhra alianza kuhisi jambo na kujikuta masikio yake yakicheza huku pua yake ikinusa kwa hisia kali sana, akapotea ghafla mule ndani bila kumuaga Samir.
Muda huo ndio Dalfa alikuwa akiwasili ndani ya Eden na kushangaa kuona mtaani kumetulia sana hakuna hata mtu aliyeonekana kutembea nje muda ule mapema sana.
"Mbona mji umetulia hivi.. au kuna sehemu wameenda watu?" aliuliza mpambe mmoja wa Dalfa wakiongozana na mkubwa wao.
Dalfa alitazama kwa makini na kuangalia kwenye ardhi na kuona nyayo za watu zikiwa zinaelekea mbele kule walipokuwa wakienda. Alitumia nguvu zake za kichwa kutazama kwa makini na kupata kujua idadi kubwa ya watu wameelekea sehemu.
Bila kuchelewa akaongoza njia na kuelekea huko kujua kuna jambo gani linaendelea.
Huku Samir alikuwa akijiandaa kwaajili ya kuelekea kwenye mashindano hayo, hata alipokuwa tayari alisimama na kuutazama mlango wa kutokea huku kwa mbali akisikia makelele ya watu kule uwanjani. Alishusha pumzi ili kutoa hofu iliyokuwa ikimkabili na mwishowe alitoka zake nje na kuelekea mahali husika. Vile alivyokuwa akitembea Dalfa kwahisia kali alipata kusikia vile vishindo vya mtu akiwa anakanyaga ardhi akionesha kuwa ni mwenye nguvu sana. Alitoa macho Dalfa baada ya kujua kile alichokuwa akihisi huenda kikawa kweli, mtu aliyekuwa akimtilia mashaka kuwa ana nguvu kama zake yupo ndani ya Eden. Akawa anafuata zile hatua ambazo amepata kuzisikia zinapoelekea ili kumtambua mtu huyo.
Nadhra alitokea nyuma yao na kuweza kuwaona Dalfa na wenzake wakiwa wanaelekea mbele. Alimtambua Dalfa kuwa ndiye mwenye uwezo mkubwa ambao hata marehemu baba yake alikuwa nao na kuweza kuuacha kwa Samir
"Dalfa..? amekuja kufanya nini huku Eden?" alijiuliza maswali kadhaa bila kufahamu sababu za ujio ule wa Dalfa. Nae Dalfa alihisi wanafuatiliwa ikabidi asimame na kugeuka nyuma kutazama lakini hakuweza kuona mtu, alikuwa na hisia kali sana na kuamua kugeuka kuendelea na safari yao.
Uwanja ulikuwa umefurika watu wengi sana wakiwa wamekaa kwenye majukwaa wakitazama uwanja huo uliokaa kama uwanja wa mpira wa miguu. Juu ya jukwaa kuu Mfalme pamoja na viongozi na watu wengine walioalikwa akiwemo Mfalme Faruk walikuwa makini wakitazama kile kitakachoendelea. Maya na mama yake Malkia Rayyat walikuwa pia kwenye jukwaa hilo wakisubiri mashindano hayo yaanze.
Alifika mtangazaji na kusimama katikati ya uwanja akaanza kuwakaribisha wageni walioalikwa na kueleza dhumuni la mashindano hayo ni kumpata mshindi mmoja tu ambaye ataweza kuwa mlinzi kwa binti wa Mfalme. Baada ya zoezi alianza kuwaita washiriki wote walio jiandikisha wakiwa zaidi ya 40 na wote wakaingia mule kwenye uwanja ili watu wawaone huku wakiwa wamevaa mavazi yao ya kupambana. Mtangazaji akaanza kuwataja majina mmoja mmoja na kusogea mbele kutoa heshima kwa Mfalme.
Kila mmoja alisogea mbele baada ya kutajwa na Mfalme alitabasamu baada ya kupewa heshima yake huku watu wakipiga makofi na kelele za shangwe na makofi kunogesha mashindano hayo. Kila mtu alikuwa na mshiriki wake anayemshangiria siku hiyo. Alisogea Jamal mbele na kumpa heshima Mfalme Siddik ambaye baada kumuona alishangaa na kugeuka kumtazama Mfalme Faruk.
"Hata kijana wako pia yupo?" alishagaa Mfalme Siddik na kumuona Faruk akitabasamu huku akitikisa kichwa.
"Ndio, ameamua kushiriki ili aweze kumuwekea ulinzi binti yako, anamjali sana nami sikuwa na pingamizi nikamruhusu." alisema Mfalme Faruk akimtazama kijana wake akiwa pale uanjani.
Mfalme Siddik alifurahi sana kuona ni kama upendo wa aina yake kijana wa Mfalme wataifa lengine anagombania nafasi ya kumlinda binti wa Mfalme wa Eden. Aligeuka na kumpigia makofi Jamal ambaye alirudi nyuma baada ya kutoa heshima hiyo.
Lutfiya alikuwa kwenye majukwaa na wafanyakazi wengine wakiangalia kinachoendelea. Baada ya wengine kumpa heshima Mfalme na mtu wa mwisho alitajwa Samir ambaye alisogea naye pale mbele kutoa heshima.
Watu wote waliomfahamu walihamaki na kushikwa na mshangao. Mfalme na Malkia wote walistaajabu kumuona Samir pale mbele, wakabaki kutazama bila kuelewa imekuwaje. Maya mwenyewe alishangaa kumuona Samir ndani ya jukwaa lile. Askari wa kifalme walimshangaa Samir na kubaki kumcheka maana ameshiriki mashindano ya kufa. Kila mtu akawa anaongea la kwake mule uwanjani maana Samir anajulikana kuwa ni dhaifu na ndiye mshiriki pekee mwenye mwili mdogo kuliko wote.
Mfalme Faruk alinyanyuka huku akitabasamu na kumpigia makofi Samir na kuwafanya wenzake pembeni wamuangalie.
"Hadi anaamua kushiriki ujue anajiamini sana, safi sana kijana." alisema Mfalme Faruk na kukaa chini, moyoni alijua watu wale ndio wa kwanza kufa kwenye mashindano hayo.
"Samir amejiamini nini mama jamani hadi amechukua uamuzi huu?" aliuliza Maya akiongea na mana yake aliyekuwa pembeni yake.
"Hata mimi nashangaa hadi sielewi" alisema Malkia Rayat, hakuwa na jinsi ikabidi wasubiri kinachoendelea.
Mfalme alikuwa na hofu ya kumpoteza Samir ambaye ni mfanyakazi wake pia lakini hakuwa na jinsi maana ameamua kushiriki naye. Alijenga tabasamu na kupokea heshima aliyotoa Samir pale kisha akarudi nyuma kijana kusimama na wenzake kwenye mstari.
"Washiriki wetu wote wa leo ndio hawa, wataingia washiriki nane kwenye uwanja na kila mmoja atapangiwa mtu wa kupambana naye hivyo kati ya watu nane hao wanne ndio wataoshinda na wengine wataaga mashidano. Tutaendeleo hivyo hadi washiriki wote 48 waishe hisha tutaanza hatua nyengine tena hadi wabaki wawili ambao ndio tutajua nani kati yao atapata nafasi ya kuwa mlinzi wa binti wa Mfalme." alisema yule mtangazaji kwa sauti na watu wote wakapiga mayowe kushangiria. Bila kupoteza muda washiriki wote walirudishwa ndani na kuchaguliwa watu nane wakaingia uwanjani na kila mmoja akapewa mtu wa kupambana naye, mapambano yakaanza.
Ilikuwa ni kama uwanja wa vita muda ule kila mtu alionekana kuchafukwa na roho kuhakikisha anakuwa mshindi kwa mpinzani wake. Pindi ukizembea unauliwa mara moja maana kila mtu alikuwa na silaha yake kali lengo ni kumdhuru mpinzani wake ili yeye apate kuwa mshindi. Watu walishangiria sana kufanya mapambano hayo yaonekane yenye shamrashamra kubwa sana.
Mfalme pamoja na meza yote ya waalikwa walikuwa makini kuangalia kile kinachoendelea. Maya alibaki kushangaa kuona jinsi watu wanavyotoana roho kwaajili yake. Tangu awali hakupendezwa na kitu hicho lakini ilibidi akubaliane na baba yake ili apate ulinzi katika maisha yale.
Wapambanaji wengine walikuwa ndani ya jengo moja wakichungulia tu jinsi wenzao wanavyopigania nafasi ile. Ndani ya uwanja kila mtu alionesha umahiri wake na mwisho wa pambano waliweza kushinda watu wanne na wengine wakiwa chini wamejeruhiwa vibaya sana huku mmoja akipoteza maisha wakatolewa.
Walitangazwa wale washindi na kumfanya Mfalme na watu wengine wanyanyuke kuwapigia makofi kwa kuwapongeza kwa kile walichokifanya.
Walitoka kwenda kupumzika wasubiri kitakachoendelea.
Baada ya dakika kadhaa walitajwa tena watu nane wakaingia uwanjani na pambano likaendelea kama kawaida.
Huku Dalfa na watu wake walifika pale uwanjani na kuingia mule wakipata kuona umati wa watu wakiwa wanatazama mapambano yale. Nao bila kujiuliza wajipanda kwenye majukwaa na kutafuta sehemu wakakaa kutazama kinachoendelea. Dalfa alitazama kule kwenye jukwaa la wakubwa na kuweza kumuona Mfalme Siddik akiwa mwenye furaha kuangalia mapambo yale. Alimuona Malkia Rayat akiwa pembeni na binti yake wakiwa wapo makini kutazama kinachoendelea. Hapo ndipo akapata kuamini kweli binti wa Mfalme ameweza kupona na jambo la msingi ni kumpata yule mtu aliyemponesha binti huyo. Aliangalia tu mapambano yale yanayoendelea pale kiwanjani.
ITAENDELEA.....
Samir ameshaingia kwenye mpambano na ana majaribio matatu.
1. Lazima ashinde (ataweza?)
2. Afute ndoto ya ajabu.
3. Asalimike na Dalfa.
Nini kitakachojiri? Naona wahusika wetu wakuu wote wapo mashakani, nikimaanisha Tamara na Samir
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA TATU (13)
