SEHEMU YA 13
ILIPOISHIA
Kama kumbukumbu yako ipo sawa, basi siku ya Jumamosi tulifikia kumuona Dalfa ameshaingia Eden kwa lengo la kumtafuta Samir na wakati huo huo Samir ameshajiandikisha kwenye mapambano ambayo yameshaanza. Je! Nini kitakachoendelea? Tuwe pamoja katika sehemu hii ya 13.
ENDELEA NAYO.....
Hakukuwa na huruma baina ya mtu na mtu ndani ya uwanja. Kila mtu alikuwa akijitetea upande wake. Damu zilimwagika, panga zilisikika zikipigana vikumbo hali iliyomfanya Samir kule ndani alipo na wenzake aone kwamba kuna kazi ya kutetea uhai wake pindi aingiapo kwenye uwanja ule. Alitazama juu ya jukwaa walipo Mfalme na watu wakubwa na kuona sura ya Maya akiwa anaangalia huku akionesha kuwa na woga.
Hapo ndipo akakumbuka ile ndoto ya jana usiku na muda huo huo akageuka kumtafuta yule mtu ambaye alimuona akiwa amejifunika uso.
Aliangalia huku na kule na kuweza kumuona mtu yule akiwa amekaa chini akiwa amekunja miguu yake kama yupo kwenye maombi huku panga lake likiwa mbele yake. Samir alilitazama lile panga na kulikumbuka panga lile ambalo yule muuaji wa ndotoni alilitumia kumkata kichwa Maya.
Alishtuka sana baada ya kutambua hilo na kuona huyu mtu huenda ndiye yule ambaye alimuona ndotoni na huenda jambo hilo likatokea hapo mbeleni. Ilibidi awe naye makini sana muda wote ili maisha ya Maya yasije kukatishwa kama alivyoona kwenye ndoto.
Watu uwanjani walizidi kupungua tu kila kundi la watu nane wakiingia basi wanne wanaibuka washindi kuendelea na hatua nyengine. Kundi la mwisho liliingia uwanjani na watu wengi wakawa wanamtazama Samir aliyeonekana kuingilia mambo ambayo hana hobi nayo. Jamal alikuwa miongoni mwao na kuweza kupangiwa mtu wa kupambana naye.
Samir alikabidhiwa mtu mrefu mwenye mwili mkubwa sana uliojazia aliyeonekana kuwa na rungu kubwa lenye uzito huku mkono mwengine akiwa ameshika mnyororo. Maya akabaki tu kushika mdomo.
"Jamani mbona wamempa jitu lenye nguvu kiasi kile apambane naye?" aliongea Maya akionesha kuwa na hofu sana.
"Haijalishi awe vipi kama amekubali kushiriki kwenye mashindano haya basi amejiamini, ngoja tusubiri atamuepuka vipi." alisema Malkia Rayat na kugeuka kutazama uwanjani. Mfalme alibaki kusikitika tu baada ya kuona dhahiri kijana wake anaelekea kupambana na mtu mwenye nguvu zake.
Pambano likanza na kila mtu akawa anapambana na mtu wake aliyepangiwa. Samir aliutoa upanga wake na kukaa makini sana kumtazama adui yake ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi. Alimtazama Samir na kubaki kucheka tu maana ni mdogo sana lakini hakuwa na huruma maana lazima apatikane mshindi. Alianza kuuzungusha mnyororo wake kumchapa nao Samir ambaye alionekana kuwa na wepesi wa kukwepa na kuwafanya kidogo watu wawe na tumaini naye kidogo.
Huku Dalfa baada ya kumuona Samir pale uwanjani akipambana aliweza kumtambua kwa sura na kujua ndiye yule mtu ambaye aliweza kumsaidia Maya siku ile hivyo lazima atakuwa na uwezo kama wake. Alibaki kuangalia pambano lile akiwa makini kumuangalia Samir kama atatumia zile nguvu.
Jamal alionekana kuwa makini na mwepesi kwa adui yake na sekunde kadhaa tu akaweza kumbana adui yake na kumchana kwa upanga mgongoni akaenda chini. Watu walimshangiria sana kwa kumaliza pambano lake mapema sana kuliko wenzake.
Mfalme Faruk alibaki kutabasamu tu baada ya kuona mwanaye akionesha umahiri wake hadi kuweza kuibuka mshindi kwenye pambano lake la kwanza.
Baada ya muda na wengine wakaweza kufanikisha zoezi hilo na kufanya uwanja mzima abaki yule mtu baunsa pamoja na Samir ambaye alionekana kuzuia sana mashambulizi ya mpinzani wake akizidi kumtia maudhi kuona kijana mdogo anamsumbua mpaka dakika ile.
Hata jukwaa walipo Wafalme walishangaa kuona Samir analeta upinzani mkubwa kwa mtu yule jambo ambalo hawakutegemea ikabidi watu wa Eden waanze kumsapoti mtu wao Samir wakilitaja jina lake kama kumpa mori hadi mwenyewe akashangaa kuona anapewa hamasa ya kushinda.
Yule mtu aliposikia vile aliona kumbe anayepambana naye anajulikana Eden, alizidi kupata hasira kutaka kummaliza kabisa Samir ili awanyamazishe midomo watu wote. Alinyanyua rungu lake kwa nguvu zote na kurusha kwa Samir ambaye kwa wepesi wa hali ya juu akalikwepa. Alishangaa kuona yule mtu anakuja mzima mzima ili ampige kikumbo Samir, kwa weledi wa hali ya juu alipiga msamba kwa chini na kuachia ngumi nzito sehemu za siri za yule mtu ambaye alionekana akienda chini mzima mzima kwa kipigo kile na ukawa ni ushindi kwa Samir. Watu wote walishangaa hawakuamini huku wengine wakimshangiria kwakile alichokifanya.
Maya hakuamini kuona vile akabaki kutabasamu tu na kupiga makofi na mama yake aliyekuwa pembeni yake.
Mfalme alifurahi sana na kubaki kupiga makofi tu kuona kijana wake wa Eden amepata ushindi.
"Nilisema mimi huyu kijana anajiamini sana." alisema Mfalme Faruk akimtazama Mfalme Siddik akionesha kutamasamu tu bila kusema lolote. Samir alitoka pale uwanjani na wengine walioshinda akiwemo Jamal na kurudi kupumzika na awamu hiyo ya kwanza ikamalizika na kuwapata washiriki 24 waliobaki huku 24 wengine wakiwa wameshindwa na baadhi yao kupoteza maisha kabisa.
Watu walipumzika robo saa tu na wale washiriki wa awali wakaingia nane na kila mmoja akapangwa na mtu wa kupambana naye na zoezi likaanza.
Ilikuwa ni zaidi ya mpambano kila mmoja alikuwa akijitahidi apate nafasi ya kwenda mbele zaidi. Hata wale baadhi ya askari wa kifalme walioshiriki kwenye mapambano hayo walikuwa makini sana lengo ni kuipata ile nafasi moja ya mshindi. Na katika pambano hilo waliibuka washindi wanne huku majonzi yakiwa kwa Eden kwa kuweza kuwapoteza askari wawili kwenye mpambano huo na kubaki askari wanne wa Eden pamoja na mfanyakazi mmoja wakuitwa Samir.
Washindi walitoka na kwenda kupumzika huku wale walioshindwa na kupoteza maisha wakitolewa kwenye uwanja kurusu kundi lengine liingie na mpambano ukaendelea kama kawaida.
Shangwe zilisikika kwa raia waliokuwa wakiangalia mapambano hayo wakiwapa moyo askari watatu waliokuwa katika kundi lile. Walikuwa na uchungu sana baada ya wenzao wawili kuwapoteza hivyo walipambana kishujaa kama askari kuhakikisha wanatetea nafasi zao. Na kweli katika kundi hilo askari wote watatu waliweza kushinda pamoja na mtu mwengine na kuwafanya watu wa Eden wafurahi sana.
Kundi la mwisho likawa ni la akina Jamal, Samir na watu wengine ambao miili yao ilionekana imeimarika kimazoezi huku wakiwa na mapanga marefu na makali sana. Kila mtu alipangiwa wa kwake na kwa mara nyengine Samir anapangwa na mtu alionekana kuwa na nguvu na mwili uliojengeka kikamilifu. Hakuwa na jinsi ilibidi akubali kukabiliaana nalo na mpambano ukaendelea.
Jamal alikuwa akipambana kwa staili ya aina yake, hakika alionesha kuwa yeye ni hodari wa kutumia upanga wake. Kama ilivyo kawaida yake dakika kadhaa tu aliweza kumzidi ujanja mpinzani wake na kukata viungio vya miguu na kumfanya mpinzani wake asiweze kusimama kabisa. Watu walimshangiria sana kwa kujua uwezo wake wa kupambana, Lutfiya kule alipo jukwaani alibaki kutabasamu tu na kuona mtoto wa Mfalme wa taifa lao anazidi kupata ushindi. Kwa Samir naye alijitahidi safari hii baada ya kuzoea kupambana, akifikiria kuwa yote anafanya kwa ajili ya Maya asiweze kufa basi anapata ujasiri zaidi wa kuendelea.
Lakini kwa Dalfa alibaki kushangaa kuona mtu yule tangu anapambana mwanzo hadi pambano hili la pili hakutumia hata zile nguvu ambazo anafikiri anazo. Hakumuelewa mpaka dakika ile na kuzidi kumchunguza zaidi akiamini ataujua tu ukweli.
Huku kwa wengine wakiwepo askari wa kifalme wawili walipambana kwa juhudi zao lakini mmoja wao akazidiwa maarifa na kujikuta akidhibitiwa baada ya kukatwa na upanga tumboni huku mwenzake aliyebaki akipata ushindi.
Samir alizidi kukaza msuli na kwa bahati akapata nafasi ya kupenyeza upanga wake tumboni kwa mpinzani wake aliyekwenda chini na kupoteza maisha papo hapo. Watu wa Eden walishangiria sana kuona watu wao wawili katika kundi hili pia wameondoka na ushindi.
Taratibu Malkia pamoja na Maya wakaanza kumuwekea imani Samir aweze kufika mbali. Mfalme alipiga sana makofi kuwapongeza washindi wote waliofika hatua hiyo wakiwa wamebaki 12 huku Eden ikiwakilishwa na askari wanne pamoja na Samir wakiwa washiriki wote wamesimama mstari mmoja wakipongezwa kwakufika hatua ile.
Samir aligeuka kuwatazama wenzake waliofika hatua ile, lakini alishangaa kuona yule mtu anayejifunika sura yake tangu mwanzo kabla ya mpambano hakuweza kumuona mpaka muda huo. Alivuta kumbukumbu kuangalia wale watu walioshindwa kuendelea na mashindano hayo kama alikuwepo lakini akili yake inakataa, akabaki kutafakari mtu yule ameenda wapi?
Walipewa muda wa kupumzika na kuwaacha watu wakiwa wanahamu kubwa ya kujua ni nani na nani wataweza kufika hatua za mbele zaidi. Washiriki wale 12 walirudi sehemu ya kupumzika na kusubiri baada ya muda waweze kuitwa tena. Wale askari wa Eden walisimama pamoja wakawa wanaongea kama watu wa karibu bila yeyote kujua atapangiwa na nani wa kupambana naye. Samir alikaa sehemu yake akijipumzisha huku akiwa ameshika upanga wake ule. Alitoa kitambaa na kuanza kufuta damu zilizogandia kwenye upanga ule huku akiwaangalia wale askari wakiwa wameweka kikundi chao wakiendelea kuongea.
Alitazama pembeni na kumuona Jamal akiwa amekunja miguu kama anafanya maombi huku panga lake likiwa mbele yake. Tukio lile lilimfanya Samir amkumbuke yule mtu aliejifunga sura yake isionekane na ghafla hakuweza kumuona tena. Alikaa na kuweka upanga wake kama anavyomuona huyu wa sasa. Alipolitazama lile panga kwa umakini hapo ndipo akajiridhisha baada ya kutambua ndio huyu huyu ambaye mwanzo aliweza kumuona pindi akiwa ameificha sura yake. Alijiuliza moyoni kuona imekuwaje sura yake ameificha mara moja tu na pindi alipoingia kwenye mapambano hakuweza kuificha sura yake.
Hakuweza kupata jibu kamili juu ya swala hilo lakini alitambua tu kuwa mtu ambaye alimuota kwenye ndoto ndio yule anayemuona pale mbele. Alibaki kumtazama vizuri Jamal aliyeonekana kuwa makini muda wote akiwa si mwenye sura ya kucheka.
Huku uwanjani watu walikuwa wakisubiri kwa hamu muda ufike mapambano yaendelee. Kila mtu alikuwa na shauku ya kujua nani ataibuka kuwa mshindi siku hiyo. Kila mtu alimtabiria mtu ambaye anaona ndio ataibuka kuwa mshindi na kuweza kupewa nafasi ya kumlinda binti wa kifalme. Muda ulizidi kwenda na baadae waliitwa majina washiriki waingie uwanjani.
Waliingia askari wa Eden watatu pamoja na wanaume wengine kukamilisha idadi hiyo ya washiriki sita.
Kila mmoja alipangwa mtu wa kupambana naye, na safari hii askari wawili wa mfalme Siddik waliweza kukutana na kupangiwa kupambana. Waliweka uaskari wao pembeni kila mmoja akipigania nafasi ya kuendelea mbele.
Mpambano ulianza huku Mfalme mwenyewe akiwa mwenye hofu kubwa hasa vijana wake hao ambao mmoja wao lazima ashindwe. Watu walishangiria kuwapa hamasa washiriki huku Dalfa akiwa anatazama tu kinachoendelea, lengo lake likiwa kwa Samir na alisubiri muda tu Samir atumie zile nguvu aweze kufanya kitu.
Samir na baadhi ya wenzake mule ndani wakawa wanachungulia tu kuona wenzao wanavyopimana ubavu. Aligeuka kumtazama yule mtu na kumuona bado amekaa hana hata habari kama kuna kinachoendelea.
"Huyu mtu mbona anajiamini sana hivi?" alijisemea moyoni Samir akiwa anamtazama Jamal aliyeonekana kukaa pale chini huku wenzake wakichungulia mapambano yanavyoendelea.
Hakika hakuna aliyetaka kuzidiwa ndani ya uwanja. Kila mtu alionesha umahiri wake na kufanya meza kuu ya wageni waalikwa pamoja na wafalme wapate hamasa ya kuzidi kuangalia kinachoendelea. Miongoni mwa wale askari waliokuwa wakipambana aliweza kumzidi ujanja adui yake baada ya kupitisha shingoni panga na adui yake akaweza kwenda chini na kupoteza maisha papo hapo. Samir kuona vile akabaki kufumba macho na kuamua kutoka pale waliposimama asiendelee tena kuangalia, alitafuta sehemu kutulia akisikiliza kelele za mashabiki wakiwashangiria watu ndani ya uwanja. Wale washiriki wengine kila mmoja alikuwa imara katika kutumia silaha ya upanga, jambo ambalo lilikuwa gumu kutabiri nani ataibuka kuwa mshindi. Katika harakati za kupambana walijikuta wakiwahiana na kila mmoja akapeleka upanga tumboni kwa mwenzake hali iliyowafanya watu wote washangae tukio lile walishuhudia wote wakienda chini na kupoteza maisha. Tukio hilo liliendana na tukio la wapiganaji wengine ambao na kwa staili tofauti walirushiana visu vifuani na kusababisha asipatikane mshindi baina yao. Uwanja mzima akawa amebaki yule askari wa kifalme aliyeweza kushinda peke yake na wenzake kupoteza nafasi ya kuendelea. Haikuwa na jinsi watu walimshangiria sana kuona anaitetea Eden vyema na baada ya kupokea sifa hizo hata kwa Mfalme akatoka mule uwanjani kwenda kupumzika.
Liliingia kundi la mwisho na kila mmoja akakabidhiwa mtu wa kupambana naye. Maya alipata kustaajabu pale alipomuona Samir amekabidhiwa askari mmoja wa Eden apambane naye. Hawakuwa na ujanja ilibidi wafanye kama ilivyopangwa huku naye Jamal akipewa askari mmoja apambane naye.
Watu wengi sana walianza kumuwekea tumaini Jamal kwa vile anavyopambana kuonesha umahiri wake.
Hali ile ilimpelekea kupata mashabiki wengi wanao muunga mkono hali iliyomfanya Mfalme Faruk atabasamu kuona mwanaye ameweza kukonga nyoyo za watu. Mfalme akawa na hofu juu ya kumpoteza askari wake mwengine maana anapambana na mtu mwenye uwezo mkubwa sana huku upande mwengine akiona Samir akipewa nafasi ya kupambana na askari huyo mmoja wa Eden. Hata mapambano yalipoanza kila mtu alikuwa amemuwekea tumaini mtu wake ambaye anahisi atakuja kuibuka kuwa mshindi. Kila mtu alikuwa makini kupambana na mwenzake huku Samir akiwa anamkwepa tu yule askari.
"Sisi sote ni watu wa Eden na ukiona umeshindwa pambano unadondoka chini ili mwenzio asipate kukuumiza." alisema Samir akiwa anamtazama yule askari aliyekuwa akipambana naye.
"Huu ni mchezo wa kufa au kupona, ulikubali kuingia humu uwanjani na ukakubaliana na kila hali italayotokea humu.Fanya kilichokuleta." alisema yule askari na kuupeleka upanga wake akitaka kumkata lakini alilizuia Samir kwa uhodari.
"Fikiria kuhusu wewe pia nitakapo kudhuru na una nafasi katika falme kama askari wa Eden, hebu fikiria hilo." alisema Samir akimsihi yule askari wapambane kawaida na mmoja wapo akizidiwa asidhurike.
"Unaongea ujinga gani Samir... unadhani nikipata nafasi ya kuwa mlinzi wa mtoto wa Mfalme nitaendelea kuwa askari pia. Nitakuwa zaidi ya askari na ndio lengo langu hilo." alisema yule askari na kuendelea kumuandama Samir aliyeonekana kuzuia tu.
Alimtazama Jamal pembeni na kuweza kumuona akiwa amemzidi mpinzani wake aliyeonekana kuwa hoi mapema.
Hali ile Mfalme Siddik aliiona na kujua kuna uwezekano mkubwa wa kumpoteza askari wake. Aligeuka kumtazama Mfalme Faruk ambaye alionekana kutabasamu kuona jinsi mwanaye anavyowadhibiti wenzake. Haikupita dakika mbili Jamal alimpindua yule askari akadondoka chini, alipotaka kufurukuta kujitetea yule askari alishuhudia kuona upanga ukipiga begani ukachana. Alipiga ukelele wa maumivu na kumfanya Jamal aachane naye baada ya kuona amemzidi na kupata ushindi kwa mara nyengine tena.
Watu waliokuwa upande wake wakaanza kumshagiria kwa kelele huku baadhi ya wengine hawakupenda kuona watu wao wa Eden wanapigwa vile. Waligeuza macho yao kwa wengine na kuona hata yule askari aliyebaki akizidi kutetea nafasi yake. Alipambana kadri ya uwezo wake japo alikutana na mtu mwenye uwezo mkubwa sana na mwenye mwili. Aliutumia upanga wake vyema na mwisho akafanikiwa kummaliza yule askari wa kifalme pale na kumfanya Mfalme azidi kupata machungu. Malkia alibaki kusikitika tu pale kuona vijana wa taifa lao wanaisha na wamebaki uwanjani Samir na yule askari mbishi.
Hakutaka kusikia lolote kwa kile anachoelezwa na Samir ambaye mara kadhaa amekuwa akimtazama Mfalme akiwa anawaangalia. Alishuhudia akipigwa ngumi nzito na kwenda chini na hapo ndipo akapata kusikia watu wakimshangiria yule askari ambaye alizidi kufurahi na kujitapa uwanjani pale akitaka kumaliza kazi. Aligeuka kumtazama Samir pale chini akiwa anatokwa na damu mdomoni baada ya konde lile la shavuni.
Alifikiria kile alichoambiwa kuhusu kuipoteza nafasi ile atampoteza Maya hapo akapata hata nguvu ya kusimama na kuwafanya watu wapunguze kelele zile kuona Samir ameamka.
"Nimekwambia toka awali hunisikii basi wacha tugombanie hii nafasi vizuri." alisema Samir na bila woga akamsogelea yule mtu pale pale aliposimama. Alicheka sana kwa dharau na kutaka kunyang'anyia panga lake Samir akalia kwa kulipiga teke likadondokea pembeni. Wakabaki wakiangaliana tu kwa macho yenye chuki ndani yake huku Samir akiwa amekamata ule upanga wake. Hapo Dalfa akawa makini kutazama kuona kama mtu huyo anaweza akafanya lolote kwa yule askari.
"Samir kuwa makini kuna mtu anaitwa Dalfa anakufuatilia. Usioneshe kitu chochote hapo atakujua kuwa wewe ni nani." Ilisikika sauti kwenye ngoma za masikio ya Samir na akapata kujua ni Nadhra ndiye aliyeongea vile.
ITAENDELEA.....
Mpambano unaendelea. Je! Samir atafanya maamuzi gani? Maana hatakiwi kutumia uchawi.
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA NNE (14)
