SEHEMU YA 14
ILIPOISHIA
"Samir kuwa makini kuna mtu anaitwa Dalfa anakufuatilia. Usioneshe kitu chochote hapo atakujua kuwa wewe ni nani." Ilisikika sauti kwenye ngoma za masikio ya Samir na akapata kujua ni Nadhra ndiye aliyeongea vile.
ENDELEA NAYO......
Ilimbidi yule askari atumie ngumi sasa kumdhibiti Samir lakini haikusaida, bila huruma Samir akamchanachana tumboni na upanga ule kwa haraka sana hadi watu wakashangaa kumuona Samir akiwa mwepesi wa hali ya juu. Alishuhudia yule askari akidondoka chini palepale kupoteza maisha na ushindi ukaenda kwa Samir. Watu wengi hawakuamini kuona askari wa Mfalme ameuliwa na mfanyakazi Samir. Maya alistaajabu kuona vile na kubaki kuduwaa tu haamini.
"Kumbe Samir anajua kupambana kiasi hiki. Hadi sasa ameshinda tena anazidi kwenda mbele." alisema Maya nakumfanya hata Malkia abaki kumshangaa tu Samir na kufanya waonekane washindi watatu waliobaki kwenye uwanja.
Mfalme alinyanyuka kuwapigia makofi akafuatiwa na Mfalme Faruk akionesha kufurahi sana, furaha yake ilikuwa kwa mwanaye kuona hadi muda huo amekuwa akishinda mapambano yote aliyopangiwa.
Watu waliwapongeza kwa hatua hiyo waliyofikia. Aliitwa yule askari wa Eden pekee aliyeshinda na kuungana na wenzake watatu waliobaki na kuikamilisha idadi hiyo ya watu wanne Jamal, Samir, askari huyo pamoja na mwanaume mmoja aliyejazia mwili wake.
Mfalme alisimama tena na kuwatazama wale washiriki waliobakii huku akiwa mwenye tabasamu.
"Japo siamini ila utabaki kuwa hivyo tu kuwa mmejitahidi sana wanne nyie mliobaki hadi sasa. Watu 48 wameshindwa kufika hapa mlipo kwasasa ni wazi kwamba nyinyi ni zaidi. Na sitaki kuwaacha hivi hivi japo mmoja wenu atatakiwa kuwa Mlinzi wa binti yangu lakini natoa ofa moja ya kujiunga na jeshi la kifalme. Nadhani kati yenu kuna askari wangu mmoja hapo hivyo basi kama ataibuka mshindi ni yeye basi atakuwa akimlinda mwanangu na siku zote atabaki kuwa na heshima, ila kama hatafanikiwa basii ataendelea na kazi yake. Na kwa hawa wengine natangaza mbele ya watu mshindi wa pili ataingia kwenye jeshi la kifalme kama muongozaji wa majeshi popote pale inapotolewa oda. Hivyo kati yenu watu wanne wawili ndio watapata bahati hiyo. Mmoja anakuwa askari wa majeshi yangu na mwengine anakuwa mlinzi wa binti yangu. Nadhani nimeeleweka na niwatakie ushindi kwa kila mmoja wenu." alisema Mfalme na kuwafanya watu wampigie makofi kwa kile alichosema na kuona ametoa nafasi nzuri kwa watu hao. Kila mmoja wapo baada ya kusikia vile akatamani kuwa mmoja kati ya ambao watafanikiwa kupata nafasi hiyo. Samir alibaki kumeza mate tu na kuona ndio wanaelekea tamati kujua nani ataibuka kuwa mshindi.
Aligeuka kumtazama Jamal na safari hii alipata kugongana macho na Jamal aliyeachia tabasamu baada ya kumuona Samir.
Baada ya muda walirudi kwenye chumba cha kupumzika na kila mmoja alikuwa hoi kwa mapambano waliyotoka kupigana. Yule askari pekee wa Eden aliyebaki kwenye mashindano hayo alimtazama Samir na kubaki kutabasamu tu wakiwa wanaangaliana, alimuonesha dole gumba kumaanisha mambo yataenda sawa tu. Ni wao pekee ndio wanaiwakilisha Eden na hata yeye hakutegemea kama Samir angeweza kufika katika hatua ile.
Tangu awali hakuna aliyemdhania Samir kama anaweza kupambana lakini kwa mashindano hayo yamewafanya watu wote wa Eden wanaomfahamu jinsi alivyo watambue kwamba Samir ni mpambanaji wa muda mrefu ingawa hakuwa mwenye kujionesha. Fikra hiyo pia Mfalme pamoja na familia yake walihisi hivyo na kuona kweli Samir hakutaka kujulikana siku zote kama ana uwezo wa kupambana.
Huku kwa Mfalme Faruk aliona ndio muda muafaka unakaribia kuweza kukamilisha lile swala ambalo wamelipanga na mwanaye. Aliona kuna uwezekano mkubwa kwa mwanaye kuweza kuibuka kuwa mshindi kila akiangalia watu waliosalia hakuona mwenye kumzidi Jamal. Alibaki akisubiri tu mwisho wa yote ili roho yake iibuke na furaha ikiwa muda unazidi kwenda kuelekea Alasiri.
Walipelekewa chakula wapambanaji wale wanne wapate kuongeza nguvu ya kuendelea kupambana huku watu wakiendelea kushangiria tu uwanjani.
Kamati ya kupanga nani apambane na nani ilifanya mchujo huo haraka na wakajiridhisha na uamuzi walio upanga wote kisha wakampa majina hayo mtangazaji kwenda kuyawakilisha pale uwanjani kila mtu atambue.
Baada ya nusu saa kupita aliingia mtangazaji na kuongea mawili matatu kuwaweka watu sawa kisha akawaita washiriki wale wanne waliobaki. Watu wote walikuwa wakimsikiliza na kuanza kuwataja washiriki wale, yule mwanaume mwenye mwili wa mazoezi alipangwa kupambana na Samir huku upande wa Jamal akapangwa na yule askari iliwafanya watu wa Eden wawe na hofu na mashaka kuona watu wao wa Eden wamekwa kwenye wakati mgumu maana watu wanao pambana nao wapo makini sana kwenye kutumia upanga na hata wepesi wa kumdhibiti adui. Wakina Jamal walikuwa wakisikia maelezo hayo ya yule mtangazaji wakiwa wanamalizia kula. Kila mtu alibaki kumtazama mtu anayepambana naye na kujua namna gani atamkabili.
Yule askari alitabasamu tu akiwa anatazamana na Jamal aliyekuwa ameshika mkate akiupeleka mdomoni.
"Aisee Samir, hawa watu sio wa kuwaogopa wala kuwahofia kwa lolote lile. Tunapambana nao mpaka tone la mwisho na hii nafasi inabaki hapa hapa Eden. Haiwezekani binti wa Mfalme wa Eden akalindwa na wahuni tu wa mataifa mengine huko." alisema askari yule na kumfanya yule jamaa anayepambana na Samir apandishe hasira, alinyanyuka kutaka kumfuata yule askari lakini Jamal akamzuia kwa kumshika mkono. Alitikisa kichwa tu kuashiria asimfanye chochote.Yule jamaa aliamua kuachana naye kweli akageuka kurudi kukaa huku yule askari akiwa mwenye kujiamini kwa kuwa ni taifa lake ndio sababu ya kujitapa sana.
Baada ya robo saa walitangaziwa watoke mule ndani waelekee uwanjani kwa ajili ya mpambano. Waliingia uwanjani kwa kutajwa majina yao na askari alianza kutoka na upanga wake baada ya kutajwa akaingia uwanjani na kushudia watu wa Eden wakimshangiria sana mtu wao. Hata Malkia Rayyat alipiga makofi kuona askari wake akiingia huku akiwa mwenye kujiamini. Alitajwa Jamal aweze kuingia uwanjani na safari hii aliamua kuvaa lile vazi lake na kufunika sura akionekana kuwa wa tofauti. Samir alipoona Jamal akiwa amevaa vile moyo ulimdunda kuona yule mtu ambaye alimuota siku ile ndio alivaa hivyo.
Muda huo huo Jamal alianza kupiga hatua kuelekea kwenye kiwanja baada ya kutajwa jina lake. Watu waliompenda kwa upiganaji wake walianza kumshangiria kwa kelele zote, hata Lufiya akiwa kwenye jukwaa aliamua kunyanyua mikono yake na kupiga makofi kumpa hamasa Jamal. Alivua kile kinyago cha usoni na kutoa heshima kwa wafalme waliokuwa sehemu yao wakitazama mapambano hayo akiwepo baba yake Mfalme Faruk ambaye alikuwa akijisikia faraja sana kumuona mwanaye pale katikati ya uwanja.
Aliitwa yule jamaa mwengine aliyeonekana kuwa na misuli huku mwili wake uliojazia ukawafanya watu baadhi wamshangirie sana. Alifuata Samir kuingia mule uwanjani na kuwafanya watu wengi wa Eden wamshangirie, hata Maya pamoja na mama yake walijikuta wakipiga makofi kwa wingi kumpa mori kijana wao. Mfalme Faruk aliwatazama na kubaki kutabasamu tu baada ya kuwa na imani kwa mwanaye Jamal.
Baada ya muda walisimama kila mtu na wake ambaye alipangiwa kupambana muda ule. Samir muda wote alikuwa akimtazama Jamal ambaye alikuwa akitazamana na yule askari ambaye muda mchache watapambana.
Aliyakumbuka maneno ambayo askari yule alikuwa akiyasema mule ndani akionesha kujiamini sana, yalimfanya Jamal akasirike sana maana ilikuwa ni kama dharau kwamba wao hawana uwezo wa kuipata nafasi ile ya kuwa mlinzi wa binti wa Mfalme Siddik hali ya kuwa nafasi hiyo wanaisaka ili wakamilishe mambo yao.
Alilikamata panga lake Jamal na kufunika sura yake kwa kile kinyago hali iliyofanya Samir azidi kuwa na mashaka naye. Muda mchache tu yule mtangazaji alitoa amri mapambano yaanze na bila kuchelewa panga zikasikika zikigongana kwa washiriki hao kila mmoja akiwa makini safari hii akijua akipita kwenye pambano hilo anakwenda kuhitimisha pambano la mwisho. Yule mtu mwenye mwili alikuwa mwepesi sana kwenye kutumia upanga hali iliyomfanya Samir apate wakati mgumu sana wa kuweza kumzuia mtu huyo. Muda wote alikuwa akizuia tu na kuona jinsi mtu huyo akiwa anakuja kwa kasi sana. Ilibidi amvizie na alipoona amejisahau alishuka chini na kupeleka upanga ule kifuani kwa yule mtu akajaribu kukwepa na kufanikiwa kutoruhusu panga lile lizame japo lilimchana kifuani. Alirudi nyuma na kushusha pumzi kwanza na Samir akapata nafasi ya kujipanga tena.
Huku kwa Jamal alidhihirisha kuwa habahatishi katika mapambano, alikuwa akimpelekesha sana yule askari ambaye alikuwa makini sana katika kupambana na Jamal aliyeonekana kutokuwa na wasi hata kidogo. Mfalme alikuwa makini kutazama mpambano huo huku akiwa na kazi ya kuangalia huku na huku maana vijana wake wawili wote wapo kwenye kuitafuta nafasi ya kuwa mlinzi kwa Maya.
Jamal alikuwa akicheza na akili za yule askari vile anavyopambana akizidi kumsoma tu. Alikuwa na hasira naye kwa kile kitendo cha kuongea kauli chafu kule ndani akijihalalishia ushindi kabla ya pambano. Akiwa kwenye akili hiyo alijikuta anawahiwa na kupitishiwa upanga tumboni ukamchana akarudi nyuma. Alipeleka mkono wake tumboni na kuona damu zikimtoka, alishusha pumzi na kujipanga tena upya huku akizidi kupandwa na hasira juu ya askari yule aliyekuwa akishangiriwa na umati wa watu waliokuwa jukwaani.
Hata Mfalme Siddik ile hali aliiona na kupata tumaini juu ya askari wake. Aliona ndio nafasi ya kuzidi kuongeza jitihada zaidi ili apate kumshinda mpinzani wake. Alikamata upanga wake vizuri na kumfuata Jamal kuendelea kupambana.
Huku kwa Samir baada ya kumjeruhi yule mtu alikuwa ana wakati mgumu maana alikuwa amezidisha kumtia hasira yule mtu akawa anakuja kwa spidi ya hali ya juu kiasi cha kufanya hata Dalfa aliyekuwa kwenye jukwaa ashangae.
"Atakufa kizembe huyu anakuwa na hasira kiasi hicho anakuja tu bila kuangalia." alisema Dalfa akiwa amekaa na kijana wake pembeni.
"Mpaka sasa unahisi nani atakuwa mshindi kati hawa wanne Mfalme wangu.?" aliuliza yule kijana akiongea na Dalfa.
"Sina uhakika mpaka sasa kama nani atakuwa mshindi."
"Ina maana hata yule mtu uliyemfuata hana nafasi ya kushinda?"
"Hadi muda huu sijaona akitumia nguvu za ziada na ndio maana sina uhakika kama ataweza kuwa nani mshindi, ila kama wataendelea hivi hivi basi yule aliyevaa kinyago ndio atakuwa bora kati ya wote." alisema Dalfa akiwa anamtabiria Jamal kuwa mshindi na wakawa wanaendelea kuangalia kitakachotokea.
Yule mtu alikuwa mwepesi sana kuchezea upanga wake hali iliyomfanya Samir kuwa makini naye na macho kuwa makini sana. Alikuja kushangaa kuona yule mtu akiruka samasoti na kurusha kisu kidogo ambacho kiliruka na kukita kwenye mkono wa Samir akapiga ukelele wa maumivu. Hali ile ikawafanya watu wengi washike midomo yao kwa mshangao kuona vile. Hata Maya kule alipo alijikuta akisimama bila kujali baada ya kuona Samir akiwa amejeruhiwa vile, Malkia Rayyat alimshika mkono kumvuta chini akae maana haileti taswira nzuri kwa watu.
Yule mtu alisimama vyema baada ya kuona sasa amempunguza makali Samir hatoweza kupambana kama awali kwakuwa mkono mmoja umedhurika. Hakika yalikuwa ni maumivu ya aina yake maana kisu kile kilizama ndani zaidi kwenye nyama za mkono, alikishika kisu kile na kuanza kukivuta kuweze kutoka, Maya kule alipo alihisi kama kinatoka mwilini mwake na kujikuta akifumba macho yake asiangalie kinachoendelea. Kwa hali ile tu Mfalme akapata kuamini kweli Samir ni mtu mwenye roho ya ukakamavu, alijikuta akimkubali kuanzia pale na muda huo huo akakivuta kwa nguvu na kuweza kukitoa kisu kile mkononi. Damu zilianza kuchuruzika mfululizo na bila kupumzika akashangaa kuona yule mtu anasogea kuendelea na mpambano, ilibidi apambane hivyo hivyo bila kuhofia kitu.
Alitamani atumie nguvu alizonazo lakini akikumbuka maneno ya Nadhra kuwa Dalfa yupo pale kwa ajili yake aliona ajikaze kama yeye. Alirudi nyuma hatua kadhaa huku akishuhudia yule mpinzani wake akija kwa spidi sana na alipomkaribia kutaka kumkata Samir kwa upanga aliona mwenziye akienda chini kumkwepa akawa nyuma yake, haraka Samir alipiga teke lile panga la yule mtu na kumuacha akiwa mikono mitupu na kubaki kushangaa. Bila kuchelewa alimsogelea pale na kuurusha upanga wake kwa nguvu zote ukatua kifuani kwa yule mtu katokeza upande wa pili na papo hapo akadondoka chini kama mzigo. Watu walishangiria kuona ushindi wa pambano lile umeenda kwa Samir.
Mfalme alifurahi sana baada ya kuona mfanyakazi wake amewezaa kushinda kwa mara nyengine tena.
Macho yakawa kwa yule askari wa Eden akiwa anapambana na Jamal ambaye alionesha dhahiri kuzidi kumuandama yule askari hasa baada ya kukatwa na upanga muda ule, alitumia akili nyngi na uzoefu Jamal akawa anamzuga yule askari kupeleka upanga miguuni akijua anataka kukata miguu. Askari yule alipokariri hivyo alikuja kushangaa anachanganywa na Jamal na kushuhudia kifuani, alipokuja kuzuia juu alishangaa tena upanga ukikata mapajani na kwenye mishipa ya mguu na palepale akakosa hata uwezo wa kusimama tena, alienda chini kama mzigo na kubaki kupiga tu magoti.
Taratibu Jamal alimsogelea huku akiwa ameshika upanga wake akionesha kuwa na hasira sana, yule askari akawa anatazama tu mbele na kumuona Samir akiwa ameinama chini hana habari akihema maana amejeruhiwa sana mkono wake. Alinyanyuka taratibu Samir na kumuangalia mwenzake aliyekuwa akipambana na Jamal, alishangaa kumuona yule askari amepiga magoti pale huku akimuangalia. Tukio hilo likamfanya akumbuke sasa ile ndoto ambayo aliitoa usiku ule.
Alimuona Jamal amesogea nyuma ya yule askari na kumuwekea ule upanga wake kichwani kumaanisha anataka kumaliza kazi. Samir kuona vile akawa anapiga hatua kusogea pale. Jamal alimuona Samir anakuja pale aliposimama na kubaki kutabasamu tu na mwishowe akawa anacheka sana.
"Nilikuwa nimenyamaza tu nikisubiri kuona kama ataweza kushinda kama alivyokuwa akijiamini pale awali, sasa mbona amepiga magoti ana maana gani!, Eden inakutegemea bwana amka upambane.!" alisema Jamal na ni wazi kwamba anamdhihaki kwa maneno yale akijua fika askari yule hawezi kuamka pale. Yule askari alinyanyua uso wake na kumtazama Samir.
"Umebeba taifa la Eden kwasasa Samir naomba uelewe hilo, hii nafasi ni muhimu kwa mtu wa Eden kuweza kumlinda binti wa Mfalme wetu na sio atoke mtu wa Taifa jengine, itakuwa ni fedheha kubwa sana endapo tukashindwa wote kuitetea nafasi hii. Nafasi ndio yako Samir ya kuweka heshima ya jina lako na kuiweka Eden izidi kuwa juu siku zote. Hawa hawapaswi kuichukua hii nafasi tambua hilo." alisema yule askari maneno hayo na kumfanya Jamal apandishe hasira kuona kama ni dharau na maneno ya kashfa kwake, alijikuta akiunyanyua upanga wake kwa nguvu huku kila mtu akipata kuona kinachoendelea pale uwanjani.
ITAENDELEA......
Final: Jamal vs Samir, je! Nani atakaefanikiwa kuwa mshindi? Kwahivyo kuna atakaekufa ili mwengine awe ni mshindi? Patamu hapo, tukutane kesho kujua hatma ya mpambano huu.
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA TANO (15)
