SEHEMU YA 15
ILIPOISHIA
Jamal alipandisha hasira kuona kama ni dharau na maneno ya kashfa kwake, alijikuta akiunyanyua upanga wake kwa nguvu huku kila mtu akipata kuona kinachoendelea pale uwanjani.
TUENDELEE.
Bila kuchelewa Jamal aliushusha upanga ule na kumchana yule askari mgongoni mwake na kumfanya apige kelele sana na watu wote wakashuhudia tukio lile. Tukio ambalo lilimfanya Samir ashangae na kuona ile ndoto ambayo ameiota ilienda tofauti na vile anavyoona pale.
Kila mtu alistaajabu kuona vile hata Mfalme alijikuta akisimama pale alipo baada ya kuona Jamal akifanya shambulio lile kwa askari wake. Baadhi ya watu walionekana kumshangiria Jamal kwa kuona amefanikiwa kushinda pambano hilo akiwemo Lutfiya ambaye aliona ushindi bila shaka unakaribia kwenda kwa Jamal. Mfalme Faruk alifurahi sana na kumpigia makofi mwanawe kwa kufanikiwa kushinda pambano lile. Hakuwa na jinsi Mfalme Siddik aliamua kurudi kukaa japo moyoni anaumia kuona askari wake ameshindwa tena kaumizwa vibaya.
Walikuja watu maalumu wakamchukua yule askari na wengine wakamtoa yule mtu aliyeuliwa na Samir.
Jamal alikitoa kinyago chake na kuanza kutamba sasa pale uwanjani na kujikuta alishangiriwa na watu wakimkubali kwa mapigo yake na kuona anafaa kumlinda Maya muda wote. Samir alibaki kumtazama Jamal kwa yale mambo aliyofanya, alibaki kujiuliza sana kuhusu ndoto ile kama ndio tayari ilipangwa iishe hivi au kuna jambo lengine lazima linamhusi Maya pia!. Hakupata jibu kamili juu ya jambo hilo na kubaki kuushika mkono wake uliojeruhiwa na taratibu wakaanza kutoka mule uwanjani kwenda kupata mapumziko.
Kila mtu akawa anaongelea sasa fainali ya watu wawili waliobaki, hakuna aliyetegemea kama Samir mpaka sasa ameweza kufika katika hatua hii ya sasa.
Kwa Maya aliona ni kama ndio mwisho wa Samir pale na nafasi ile inayogombaniwa itaenda kwa Jamal, hii ni kutokana na kuumia mkono wake Samir. Hali hiyo kila mmoja wapo akiwemo Mfalme Siddik ilimfanya naye awe na hofu hiyo juu ya kijana wake. Kwa jinsi ambavyo ameonekana Jamal akipambana na baadhi ya washiriki waliopita na kufanikiwa kuwaangusha hadi yeye kufika hapo.
Muda huo Samir alikuwa akiuguza mkono wake mule ndani walipofika. Alifunga kitambaa ile sehemu iliyojeruhiwa na kisu na baada ya muda akamtazama Jamal aliyekuwa hana habari.
Alichokifanya ni kuunyanyua ule mkono ulio na pete kisha akashika lile jeraha huku akitamka maneno fulani lengo ni kupata afueni kwenye mkono ule apate kuendelea na mpambono dhidi ya Jamal ambaye muda huo alikuwa amekaa kama kawaida yake huku akiwa ameweka upanga wake mbele. Muda huo huo Samir alipotoa mkono wake alipata kuona jeraha lile limepotea na kurudi kawa awali.
Alitabasamu kuona vile na kupata tumaini la kuendelea, na baada ya muda kadhaa washiriki hao wawili waliitwa uwanjani kuweza kukamilisha kile ambacho kimekuwa kikisubiriwa na kila mtu. Watu wote walishangiria baada ya kuwaona Jamal pamoja na Samir wakisimama katikati ya uwanja huku kila mmoja wao akiwa ameshika upanga wake mkononi. Maya alikuwa mwenye hofu juu ya Samir hasa jinsi anavyoonekana kuwa mwenye jeraha lililofungwa kwa kitambaa. Mfalme Faruk akawa anatabamu tu na kuona ndio muda wa kushuhudia mwanaye akichukua ubingwa huo. Walisogezwa karibu na na kubaki kutazamana huku Jamal akimtazama Samir huku akiwa mwenye kutabasamu, tabasamu la kinafki ndani yake. Yule mtangazaji akaanza kuwapa maelezo ya pambano hilo wanalilotarajia kuanza, na baada ya dakika kadhaa alirudi nyuma na kuacha jukwa limilikiwe na watu wawili.
Kelele za kushangiria zilisikika pande zote kila mtu akimshangiria yule ambaye amemvutia kwa kupambana kwake.
Kila mmoja wao alikuwa makini sana dhidi ya mwenzake na hata Jamal alipoanza kupeleka mashambulizi kwa Samir mwenzake alikuwa makini pia kuzuia asije kujeruhiwa na upanga mkali wa mtoto wa Mfalme Faruk. Hakika watu walikuwa makini kutazama mpambano wa kumtafuta mtu mmoja aweze kuwa mlinzi wa binti wa Mfalme Maya. Mfalme alikuwa akitazama kuona kijana wake Samir akionesha uwezo ambao hakuna hata mmoja wa watu waliotegemea kama angeweza hata kumpiga mtu mmoja kati ya wale wote waliokutana naye na kuweza kuwashinda.
Hakika alikuwa akipambana na Jamal muda ule bila kuhofia kitu hali iliyowafanya baadhi ya watu washangae maana alionekana kuumia mkono awali. Alileta upinzani mkubwa sana kwa Jamal ambaye muda wote alikuwa akitafuta namna ya kumdhibiti mpinzani wake. Dalfa alikuwa akitazama mpambano wa wawili wale na kuona jinsi ambavyo kila mtu akionesha kuwa makini sana japo lengo lake likiwa kwa Samir.
Jamal alivyoona anazidi kuzuiwa na Samir ikabidi atumie njia mbadala ya kumdhibiti mpinzani wake, alirudi nyuma kujipanga upya kisha akaingiza mkono wake ndani ya nguo aliyovaa kifuani na kuurudisha kama kawaida huku akimtazama Samir akiwa anahema kwa kasi. Alinyanyua upanga wake na kushika kwenye makali kwa mkono ule alioutoa ndani ya nguo yake na kuanza kufuta upanga ule. Jambo lile likamfanya Dalfa kule alipo atambue kuwa Jamal kuna kitu amekipaka kwenye upanga ule japo hakutaka kusema lolote na kubaki kushudia nini kitatokea.
Alikuwa hana habari Samir baada ya kupata kutazamana kwa sekunde kadhaa walijikuta wakisogeleana kila mtu akiwa na moto wa kummaliza mwenzake. Watu walizidi kushangiria tu kiasi cha kumfanya hata Mfalme Siddik apate furaha kuona jinsi mpambano ule ulivyo mkali ambao mpaka dakika hiyo haikujulikana nani atakaeibuka kuwa mshindi.
Samir alijitahidi kadri ya uwezo wake na kwa bahati ya Jamal akapata nafasi ya kumchana kwa upanga ule Samir kwenye ule ule mkono wake ambao awali alipata kujeruhiwa. Maumivu aliyoyasikia yalimfanya arudi nyuma kwanza huku akitazama mkono ule uliochanwa kwa upanga ukibubujika damu. Mfalme Faruk alifurahi sana na kuona huo ndio ushindi kwa mwanaye. Muda ule alipata kumuona mwanaye akifanya tukio lile la kupaka sumu ambayo ni yeye ndiye aliyempatia mwanaye kipindi akiwa anajiandaa kwa ajili ya kuja Eden kwenye mpambano huo.
Hivyo sumu ile ikishagusa tu kwenye damu basi ni dhahiri kwamba haitachukua dakika tano mtu huyo kuweza kupoteza maisha.
Jamal baada ya kulifanikisha zoezi hilo akawa mwenye kujiamini na kusubiri muda maalumu apate kutazama hali ya mpinzani wake inavyobadilika muda hadi muda.
Samir alijikuta anaanza kuona mkono ukiwa mzito sana kana kwamba umekufa ganzi hadi upanga wake wake alioshika ukamdondoka mkononi. Alistaajabu sana kuona tukio hilo likimkuta hali ambayo hakuwahi kuona toka awali. Aliinama chini kushika ule upanga lakini alichokitegemea hakikuweza kutokea. Hakika mkono wake ulikuwa hauna kabisa nguvu ya kuweza kushika chochote.
Maya na Malkia walishangaa kuona Samir akienda chini na kupiga magoti huku akiushika mkono ule aliokatwa na upanga wa Jamal. Hakuna aliyefahamu kwamba kuliwekwa nini kwenye upanga ule huku watu wakijua Samir ameenda chini kwa sababu ya maumivu ya upanga aliyokatwa. Jamal aligeuka na kumtazama baba yake aliyekuwa akitabamu tu pale alipo, alitikisa kichwa chake kumuamuru mwanaye amalize kazi ili nafasi iliyokuwa ikigombewa itue kwake Jamal.
Tararibu akaanza kupiga hatua Jamal kusogea pale alipo Samir akiwa amepiga magoti chini, alimzunguka na kuwa nyuma yake akawa anamtazama tu akitafakari ammalize kwa staili gani.
Watu wengi waliokuwa wakimshangiria Samir walinyamaza kimya na wengine kushika tu midomo yao hawaamini kile ambacho anakwenda kufanyiwa mtu wao.
"Mama Samir anauliwa!" aliongea Maya akionesha kuwa na huruma na Samir. Hata Mfalme Siddik alibaki kumeza mate pale alipo hana jinsi maana ndio sheria ya mchezo huo ulivyo ili apatikane mshindi.
Taratibu Jamal alionekana kunyanyua upanga wake ule ambao aliupaka sumu kali sana inayomtesa Samir muda ule. Hata mdomo wake ukaanza kuonesha kukauka kutokana na sumu ile kuwa kali sana. Alijikuta akiitazama ile pete yake tu na kujitahidi kuongea lakini hakuweza maana hata sauti ilikuwa ngumu kutoka, akabaki kujisemea tu moyoni huku akiitazama pete yake.
"Sitojali kama kuna mtu anaitwa Dalfa ananitazama, nahitaji kushinda hili pambano ili niweze kumuweka salama Maya. Huyu mtu nina wasiwasi naye simuamini tangu nilipomuona ndotoni.. NAHITAJI NIUNYANYUE HUU UPANGA NITUMIE NGUVU ZILIZOPO NDANI YAKE ILI NIMZIDI HUYU MTU.." alisema Samir huku akifanya kwa vitendo, alipeleka mkono wake ule kwenye upanga wake na kujikuta akiukamata barabara na kuunyanyua. Na muda huo huo Jamal ndio alikuwa akilishusha panga lake kumkata mgongoni Samir lakini alishangaa kuona upanga wake unazuiwa pindi ulipofika sehemu aliyokusudia kukata.
Samir alizuia kwa kuliweka panga lake na taratibu akanyanyuka na kuchoropoka pale kwenye hatari. Umati wa watu ulionyamaza ukaanza kupiga shangwe kuona Samir ameinuka tena. Dalfa ndio akapata kuamini kile alichokisubiri muda wote kuwa Samir zile nguvu anazo na sasa anazitumia kulikamilisha swala hilo. Alirudi nyuma na kukaa vizuri Dalfa huku akitabasamu baada ya kubaini hilo. Maya pamoja na Mfalme walijikuta wakifurahi kuona Samir ameinuka tena na kuendelea na mpambano. Mfalme Faruk alibaki kutoa macho haelewi kile ambacho anakiona mbele yake, hata mwanaye pia alibaki kushangaa tu kumuona Samir ameinuka tena pale na kuweza kuukamata upanga wake tena.
Lutfiya aligeuka kumtazama Mfalme Faruk maana walichokipanga kimekwenda tofauti na vile walivyotegemea.
Kwa ujasiri wa kupambana Jamal akasogea kwa Samir na kuanza kupambana naye tena lakini safari hii alikipata cha mtema kuni. Samir akionekana kuwa mwepesi maradufu kila ashambuliwapo anakwepa na kuwa nyuma ya adui wake kisha humchana kidogo kumpa maumivu Jamal.
Alisirika sana kuona kibao kimeanza kumgeukia ghafla, hakutaka kukubali kushindwa alimfuata zaidi kumdhibiti lakini hakuna alichofanikiwa zaidi ya kukatwa na upanga ule wa Samir. Mwisho wa siku hasira zilipozidi kumuandama akajikuta akipambana bila kutumia akili na hapo ndipo Samir akaweza kumvizia kwa kumpiga mtama wa nguvu Jamal akala mweleka hadi chini na alipotaka kunyanyuka alishuhudia upanga ukiwa shingoni mwake kumaanisha amewahiwa hana ujanja. Alitazama na kukutana na sura ya Samir ikiwa inatiririka jasho, bila huruma Samir alinyanyua upanga wake kutaka kutimiza ndoto ile aliyoota isije kutokea hapo mbele na alipotaka kummaliza Jamal alisikia akiamuria aache.
"Inatosha..inatosha.. Hongera kijana kwa kuweza kuwa mshindi wa hili pambano. Ushindi umebaki EEEDEN.." alinyanyuka Mfalme Faruk na kuyasema hayo baada ya kuona angempoteza mwanaye pale. Watu walishangiria sana hata Mfalme na familia yake kwa ujumla walifurahi kwa kuona aliyetoka kwenye falme hiyo ndio ameibuka kuwa mshindi. Walitoka watu kwenye majukwaa na kuingia uwanjani kwenda kumbeba Samir kwa furaha ambayo waliyopata kuona Samir amewainua.
Mfalme, Malkia, Maya na wageni wengine walioalikwa walinyanyuka na kuanza kupiga makofi kumpongeza kijana huyo. Mfalme Faruk alikuwa akipiga makofi kwa unafiki moyoni akiwa na hasira isiyopimika kuona mwanaye amefeli kupata nafasi ya kuwakaribu na Maya binti wa Mfalme, . Lutfiya alikuwa hana raha kabisa na kuamua kuondoka kabisa ndani ya uwanja.
Dalfa alinyanyuka na watu wake akionesha kuridhika na kile kilichotokea.
"Hatimaye nimepata kuona nilichokihitaji, huyu leo nammaliza na kuzichukua nguvu zangu zirudi kwangu hatuwezi kuwa wawili." alisema Dalfa huku akitazama uwanjani akimuangalia Samir akiwa juu amebebwa kwa furaha na watu wa Eden.
Mfalme aliwashukuru wageni wake aliyowaalika kwa kuweza kufika katika swala hilo. Mfalme Faruk alijenga tabasamu zito akiweka utofauti wa kile kilichopo moyoni mwake. Alibaki kutazama tu uwanjani na kuona jinsi Samir anavyoshangiriwa na kupongezwa.
Samir alisogea pembeni na kuanza kuyatazama yale majeraha aliyonayo huku akinyanyua pete yake, ghafla tu yale majeraha yakaanza kupotea na kuwa mzima kabisa.
Baada ya kumalizika hayo alirudi kwenye hali yake ya kawaida huku wengine wakimpungia mikono kwa kama pongezi.
Siku hiyo ikawa ya heshima kwa Samir ambaye alirudi zake kwenye chumba chake na kujilaza akiwa hoi kwa uchovu. Aliutazama ule mkono wake na kuona ghafla ukianza kurudisha yale majeraha ambayo ameyapata akiwa anapambana na kubaki kushangaa wakati yalipotea na mkono ukarudi kama awali.
Sekunde kadhaa kupita mlango wa chumba chake uligongwa na kumfanya haraka ainuke pale kitandani na kwenda kuufungua. Alipata kuona mzee mmoja akiwa na vijana wake wawili wakiwa wameshika vyungu vya udongo.
"Pole sana kwa uchovu na majeraha uliyopata ukiwa kwenye uwanja wa mapambano, pia hongera kwa kuweza kushinda na kuwa Mlinzi wa binti wa Mfalme." alisema mzee yule akiwa mwenye tabasamu.
"Asante sana mzee." alijibu Samir akiwa ameshikilia mlango wake.
"Mfalme ametuagiza tuje kukupa matibabu maana uliumia sana, na baada ya kufanikisha hilo atakuhitaji kwenye chakula cha jioni hivyo ujiandae Samir." alisema yule mzee na kuwageukia vijana wake wakatua vile vyungu. Ilimbidi Samir atoe kiti pale nje na kukaa ili apate kutibiwa na hapo ndio akapata kufahamu kwanini majeraha yale yalirudi tena yenyewe.
Moyoni alijikuta mwenye kufurahi sana maana ni heshima kubwa kula chakula pamoja na Mfalme hivyo akawa anatabasamu tu huku yule mzee akimpaka baadhi ya dawa za asili na kumsafisha kidonda kile.
ITAENDELEA......
Samir amefanikiwa kuwa mshindi wa mapambano, lkn ana mtihani wa pili wa Dalfa ameshasema haondoki mpaka abebe nguvu alizonazo Samir. Je! Nini kitakachojiri?
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA SITA (16)
