SEHEMU YA 16
ILIPOISHIA
Moyoni alijikuta mwenye kufurahi sana maana ni heshima kubwa kula chakula pamoja na Mfalme hivyo akawa anatabasamu tu huku yule mzee akimpaka baadhi ya dawa za asili na kumsafisha kidonda kile.
ENDELEA NAYO......
Siku hiyo Eden nzima ilikuwa ikimzungumzia Samir kwa kuweza kupata nafasi ya kuwa mlinzi wa binti wa Mfalme. Hakuna aliyemtegemea kama angeweza kujitokeza na kushiriki mapambano hadi kuibuka mshindi na kuleta furaha kwa watu wa Eden. Si wote waliofurahia ushindi wa Samir wengine kwao ilikuwa ni maumivu na kuzidi kupata hasira. Lutfia muda huo wa jioni alikuwa na wenzake kwenye nyumba moja wakijadili akiwa pamoja na Mfalme Faruk.
"Tumefeli tena kwa mara nyengine, kijana mdogo yule ametushinda tena na hata sielewi imekuwaje na kwanini amekuwa ni yeye tu anazuia mipango yetu?" alisema Mfalme Faruk akionesha kuchukizwa na ushindi ule wa Samir.
Wote walinyamaza wakimsikiliza Mfalme wao akiporomosha maneno ya hasira sana baada ya kijana wake kushindwa kupata nafasi ile waliyokuwa wakiihitaji.
Muda huo Jamal alikuwa kwenye chumba kimoja ndani ya falme naye akipewa matibabu kadhaa. Alikuwa hana raha kuikosa nafasi ile ambayo wamekuwa wakihakikisha wanaipata ili lengo lao litimie.
Baada ya muda aliingia Generali mkuu wa Eden akiwa na baadhi ya askari na kuwakuta baadhi ya watu wakimtibia Jamal mule ndani.
"Karibu katika falme ya Eden. Mfalme ameniagiza nije kwako kukuangalia maendeleo yako, unajisikiaje kwasasa.?" aliongea yule Generali akimtazama Jamal akiwa amekaa kwenye kiti akipata huduma.
"Niko sawa kwasasa baada ya kupata matibabu." aliongea Jamal akiwa anamtazama yule Generali.
"Naamini utakuwa salama zaidi kwa muda mfupi, Mfalme amenituma nije kukutaarifu kuwa hapo baadae utahitajika kujumuika kwenye chakula cha pamoja ili muweze kukaribishwa katika taifa hili la Eden, umekuwa ni askari wa Eden kuanzia sasa na ni ahadi ambayo aliitoa Mfalme kwa watakaofika hatua ile mliofika hivyo unakaribishwa sana Eden kuanzia sasa." alisema yule Generali kisha akawageukia wale watu waliokuwa wakimtibu Jamal na kuwataka wahakikishe wanamaliza kwa wakati.
Baada ya dakika kadhaa Generali aligeuka na kuondoka mule ndani akiwa na watu wale waliokuwa wakimfuata nyuma.
Jamal alibaki kutafakari swala hilo la kuingizwa moja kwa moja kwenye jeshi la Eden kulitumikia. Ilikuwa ni heshima kubwa kuonekana kama ni mmoja wa askari wa Eden lakini kwa Jamal ilikuwa ni tofauti kabisa, hakuwaza wala kufikiria kama atakuja kuwa hivyo. Yeye ni mtoto wa kifalme na alishiriki mashindano yale ili apate nafasi moja tu, ya kuwa Mlinzi wa Maya lakini mwisho wa siku imekuwa ni tofauti na vile alivyotegemea.
Huku upande wa pili kwa Dalfa aliweza kutafuta mahala pa kuweka kambi na vijana wake, na usiku ulipofika alitoka na kuanza safari ya kuelekea kwenye falme lengo ni kuzipata nguvu za Samir naye aweze kummaliza kabisa pasiwepo na mtu huyo tena katika ulimwengu.
Baada ya muda kupita Samir aliweza kuelekea mahala ambapo ameagizwa kufika jioni ile. Alivaa vyema na kuingia ndani ya falme moja kwa moja akaelekea sebuleni ambapo kulikuwa na ukumbi mkubwa ulioandaliwa vyema kwaajili ya kupata chakula. Hata alipofika mtu wa kwanza kuiona sura yake alikuwa ni Maya akionesha kuwa na tabasamu mwanana lililomfanya hata Samir mwenyewe akumbuke mbali. Alimkumbuka msichana anayempenda sana kule shuleni, Aziza.
"Oh Samir karibu sana japo sio mgeni wa eneo hili karibu Samir sogea hiku." alisema Mfalme Siddik na kuwafanya Malkia Rayyat na Maya wageuke kumtazama Samir aliyeonekana kutabasamu huku mkono wake mmoja ukifungwa bandeji. Taratibu akaanza kusogea pale huku akionesha kuwa na hofu maana si kazi rahisi kuweza kusogea kwenye meza moja na familia ya Mfalme. Baadhi ya askari walibaki kumtazama tu wakiwa wanatabasamu maana hawaamini kama ni yule Samir ambaye kwao hakuwa lolote wakimdharau lakini mwishowe amekuja kujulikana ni zaidi ya watu wenye nguvu zao, kikubwa ni kwamba sasa amekuwa zaidi ya vyeo vyao vya uaskari.
Alipofika sehemu ile alisogea askari mmoja alivuta kiti nyuma ili Samir apate kukaa, hata yeye alistaajabu kuona vile lakini hakujali na kuona kama ni kawaida kwake alisogea kukaa na kuanza kushuhudia meza ile ilivyopendeza kwa vyakula mbalimbali vilivyotanda mezani pale.
"Kuwa huru Samir, haya ndio maisha ambayo umeyapigania kwa jasho lako hadi kuyapata. Halafu umenifanya niamini kwamba watu wapole siku zote wana mambo mazito moyoni kumbe ni mpambanaji mahiri na mwenye uwezo mkubwa sana katika kutumia upanga ndani ya vita! Hakika nimependezwa na upiganaji wako naamini Maya atakuwa kwenye mikono salama." alisema Mfalme Siddik akiwa ameshika glasi ya juisi ya mazabibu.
"Usijali Mfalme wangu, nina imani Maya atakuwa salama siku zote katika uangalizi wangu." alisema Samir na kukamata uma na kisu akaanza kusogeza mnofu kwenye sahani na kuanza kukatakata kuanza kula.
"Mimi umenifurahisha pia kuona nafasi hii imechukuliwa na kijana wa Eden tena ambaye tumemzoea na tunamfahamu kiundani zaidi. Sasa uanze maisha mapya kama mlinzi wa binti yangu na usahau maisha yako ya awali." alisema Malkia Rayyat na kumfanya hata Maya atabasamu, alimtazama Samir akiwa mwenye furaha kuambiwa vile na muda huo huo Jamal aliwasili akiwa na askari wawili waliomuongoza hadi kufika hapo.
Alikaribishwa na yeye na kusogea kwenye meza ile akijenga tabasamu mwanana. Aligongana macho yake na Samir ambaye alionesha tabasamu kwamba wafurahie mualiko ule. Jamal alitabasamu tu lakini moyoni hakuwa na furaha kuhusu Samir, hakutegemea kama anaweza akazidiwa ujanja pale uwanjani na mtu kama huyo. Muda wote pale mezani wakiwa wanakula alikuwa akimtazaka sana Samir haamini kama ndiye mtu aliyemuweka chini na kuchukua ushindi ule. Waliongea mambo mengi na familia hiyo ya kifalme na baada ya muda kila mmoja wao akaenda kupelekwa kwenye makazi yake mpya waweze kupumzika usiku huo. Kwa Samir ilikuwa ni furaha kuona anapatiwa heshima kama hiyo, na ndio ulikuwa mwisho wa kuishi kwenye kibanda chake kuanzia usiku huo. Alipewa chumba kimoja karibu na chumba cha Maya lengo ni kuwa karibu na binti huyo kumuwekea ulinzi.
Maya alibaki kutabasamu tu akiwa chumbani kwake, hakumtegemea Samir kama ndio atakuwa mlinzi wake. Alimzoea sana muda wote hasa akikumbuka akiwa anaongea naye muda mwingi na kumpa ushauri. Kwa upande wake alikuwa ni mshauri wa mambo mengi ambayo alikosa maamuzi, hivyo ushindi wa Samir ulimfanya ajione mwenye faraja sana maana atakuwa karibu na rafiki yake huyo.
Huku kwa Jamal bado alikuwa na kinyongo juu ya ushindi ule wa Samir, alijitupa kitandani na kuanza kutafakari mambo kadhaa ambayo walipanga na wenzake lakini mwishowe mtu mmoja ndio anakuja kuwaharibia.
"Huyu mtu ni wa kumfuatilia nijue kwanini anakuwa kikwazo katika mambo tunayopanga siku zote" alisema Jamal akiwa anatazama paa la nyumba akiwa amejilaza pale kitandani.
Usiku huo ulikuwa mwanana kwa Samir ambaye aliandaliwa sehemu mpya ndani ya falme, alikumbuka jinsi alivyopigania nafasi ya kuwa mlinzi wa Maya na mwishowe amefanikiwa japo amepitia mitihani kadhaa. Alimkumbuka Jamal ambaye ndiye alionekana kuwa ni kikwazo kwake hadi akapata kuota lile tukio kuhusu kukatwa kichwa Maya. Alipolikumbuka hilo moyo wake ukaanza kumfikiria Jamal kwa mambo mengi sana akimuwekea wasiwasi akihisi ujio wake sio wa heri.
"Napaswa kuwa makini sana dhidi ya huyu mtu, mbona moyo wangu unakosa raha pindi niikumbukapo ile ndoto!" aliongea Samir akiwa amejilaza kitandani akitafakari hayo.
Taratibu akaanza kunyemelewa na usingizi na baada ya muda mfupi ukamchukua. Usiku huo ndio Dalfa alikuwa akiwasili karibu na jengo lile la kifalme. Alilitazama na kutafakari kujua wapi aanzie na mlengwa mkuu ni Samir ambaye muda huo alikuwa akiuchapa usingizi. Ulinzi ulishamiri kila kona ya jengo hilo huku askari wakionekana kutembea usiku kucha kuhakikisha usalama. Yote hayo kwa Dalfa hakuweza kutetereka wala kuwa na hofu dhidi ya ulinzi ambao umewekwa.
Bila kuhofia lolote alianza kusogea kwenye geti kubwa lile na kuona walinzi wakiwa wanamtazama tu bila kumzuia muda huo. Alipita pale kwenye ulinzi mkubwa na kuingia ndani ya falme, kitendo hicho kikafanya ile pete aliyovaa Samir ianze kumbana kidole bila yeye kuhisi kama kuna maumivu hayo akiwa kwenye usingizi.
Alifika mahala Dalfa na kuanza kuangaza huku na kule akitafuta kujua alipo Samir, kwa hisia alizonazo akapata kujua yupo chumba gani, taratibu akaanza kuingia kwenye falme huku askari wakiwa wametanda kila kona lakini hawakuweza kumuona. Alizidi kwenda ndani zaidi bila kuwa na wasi hadi alipofika kwenye chumba husika akasogea hadi pale mlangoni akawa anautazama huku macho yake yakiwa yamebadilika na kuwa makali huku akiushika ule mlango na kufanya lile komeo lililofunga kwa ndani kuweza kufunguka.
Aliufungua mlango na kuanza kuingia ndani usiku ule, kulikuwa kumetulia sana huku kelele za maaskari kwa nje zikisikika wakipiga doria kuhakikisha usalama. Alisogea mpaka pale alipolala Samir huku akiwa na macho ya kutisha na kufunua shuka alilojifunika Samir na kuweza kumuona amelala akiwa hana habari. Alitabasamu Dalfa na kuanza kunena maneno kadhaa huku akimuangalia mlengwa wake na kushuhudia miale meupe ikitoka
machoni mwake na kupenya mwilini mwa Samir. Aliendelea kuyatamka maneno ya kichawi lengo ni kuzitoa zile nguvu zote zilizopo kwa Samir kuzihamishia kwake. Zoezi hilo lilimchukua muda hadi kuweza kumaliza na baada ya kujiridhisha kulikamilisha hilo aligeuka zake na kuondoka. Alipofika mlangoni alisita na kugeuka kumtazama Samir, alifikiria ammalize kabisa ili asipate kumsikia mtu huyo akiendelea kuishi lakini alipojiridhisha kuwa tayari kamtoa nguvu zile hakuona haja ya kummaliza. Aliamua kutoka mule ndani na kuelekea kwa Maya ili amjaze tena ule ugonjwa . Na hata alipofika alipofika chumbani kwa Maya alifanya kile alichokusudia usiku huo. Alipomaliza hakutaka kuendelea kukaa tena mule alitoka zake na kurudi mahala walipofikia na watu wake akiwakuta wanamsubiri usiku ule.
"Vipi umefanikiwa?" aliuliza kijana wake mmoja.
"Dalfa hashindwi na kitu hasa kile alichokipanga, hii Eden itakuwa yangu tu muda si mrefu, na safari hii sidhani kama watachelewa kunifuata maana nimeweka uchawi mzito kwenye mwili wa Maya. Hatupaswi kuendelea kukaa tena hapa tunaanza safari ya kurudi Mashariki ya mbali usiku huu tusubiri ugeni wa Mfalme na Malkia wa Eden wakija kunikabidhi Eden." alisema Dalfa na kuwafanya watu wake wafurahi kusikia hivyo.
Haraka wakaanza kukusanya mizigo yao na kuweka kwenye farasi wao usiku uleule wakaanza safari ya kurudi kwao.
Ndoto mbaya zilianza kumtawala Maya usiku ule huku akianza kutokwa na jasho sana mwilini. Alikuwa mwenye kuweweseka pale kitandani na kuona kama anatishwa na viumbe vya ajabu, alitamani kunyanyuka lakini mwili ulikuwa mzito sana. Alitamani kupiga kelele lakini mdomo haukuwa tayari kuongea, ulikuwa mzito kana kwamba amefungwa kinywa chake kutoweza kutamka lolote. Hakika mateso aliyoyapata yalimfanya atoe tu machozi kwa kilio cha moyoni. Alijikuta akimtaja Samir kama mlinzi wake wa sasa japo sauti haikuweza kusikika ikitoka.
ITAENDELEA.....
Dalfa ameshachukua nguvu kwa Samir na hakumaliza kwa hilo tu, bali akampa na ugonjwa mkubwa Maya na ameshaanza kuweweseka huku akilitamka jina Samir lkn sauti ndio haitoki. Unadhani nini kitatokea? Hebu jaribu huenda nikakupa zawadi. 🙈🙈🙈
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA SABA (17)
