SEHEMU YA 17
ILIPOISHIA
Ndoto mbaya zilianza kumtawala Maya usiku ule huku akianza kutokwa na jasho sana mwilini. Alikuwa mwenye kuweweseka pale kitandani na kuona kama anatishwa na viumbe vya ajabu, alitamani kunyanyuka lakini mwili ulikuwa mzito sana. Alitamani kupiga kelele lakini mdomo haukuwa tayari kuongea, ulikuwa mzito kana kwamba amefungwa kinywa chake kutoweza kutamka lolote. Hakika mateso aliyoyapata yalimfanya atoe tu machozi kwa kilio cha moyoni. Alijikuta akimtaja Samir kama mlinzi wake wa sasa japo sauti haikuweza kusikika ikitoka.
ENDELEA NAYO......
Samir alishtuka kutoka usingizini baada ya kusikia akiitwa kwa sauti ya juu sana iliyomfanya akurupuke pale kitandani. Alitazama huku na kule na kushangaa yupo chumbani kwake Magogoni. Alijua kuna jambo huenda lilitokea na ndio sababu ya kurudishwa huku usiku huo. Aliitazama pete yake na kuiona ipo kidoleni kwake.
"Nini kimetokea mbona nimerudi huku usiku huu?" aliuliza Samir huku akiitazama pete yake.
"Dalfa aliingia kwenye falme usiku huu na akafika mahala ulipolala, lengo ni kuzichukua nguvu zako na ndio maana umerudishwa huku, hali ya Maya sio nzuri tayari amemuweka uchawi wa kumdhuru akijua ameshazichukua nguvu ulizonazo hivyo Maya hataweza kusaidiwa na yeyote, muwahi Maya kabla hakujapambazuka arudi hali yake ya kawaida mtu yeyote asijue kimetokea nini."
Ilisema ile pete na kumfanya Samir atambue sababu za yeye kurudishwa huku, alihisi ile sauti kali iliyomshtua kutoka usingizini bila shaka ni Maya anahitaji msaada. Haraka alinyanyuka kutoka kitandani na kuchutama chini akiongea maneno fulani ghafla akapotea mule ndani.
Alikuja kutokea yupo ndani ya chumba cha Maya na kuweza kushuhudia Maya akiwa anapepesuka pale kitandani huku jasho likimtiririka. Haraka alisogea Samir pale kitandani na kumshika Maya mkono na kujikuta akin'gan'ganiwa na binti huyo wa Mfalme kana kwamba anahitaji msaada. Alipeleka mkono wake kichwani kwa Maya na kuanza kuongea lugha isiyoeleweka. Huku Maya alipata kumuona Samir ndotoni akiwa anapambana na viumbe vya ajabu vilivyotaka kumdhuru Maya ambaye alionekana kujificha sehemu akiangalia vita vile. Viumbe wale walikuwa ni wengi sana lakini mwanaume alijitahidi kupambana nao. Walionekana wakitoa moto mdomoni mwao kumtupia Samir ambaye aliukinga kwa mkono wake hali ilifanya Maya ajionee mwenyewe akishangaa baada ya kuona uwezo ule wa ajabu alionao Samir.
Mwishowe akapata kuona viumbe wale wakiuawa na Samir ambaye alionekana kuchoka hoi baada ya kazi hiyo, Maya alianza kutoka pale alipojificha na kuanza kumsogelea Samir akionekana ameinama huku akihema sana huku wale viumbe wakiwa chini . Taratibu akamshika Samir mkono na muda huo huo Samir pale kitandani kwa Maya alikuwa anahema kweli kwa kazi nzito ya kuutoa uchawi ule kwa Maya, alipata kuona akishikwa mikono yake na Maya aliyekuwa pale kitandani akiwa kwenye usingizi mzito.
"Samir.." aliita Maya akiwa bado amelala.
Samir alimtazama baada ya kuona Maya ameongea japo hakuweza kufumbua macho yake. Samir alitabasamu tu na kumshika Maya shavuni ambaye muda huo huo akalala usingizi mzuri usiokuwa na ndoto za kutisha. Alipohakikisha uzima huo kwa Maya naye akarudi chumbani kwake kupumzika.
Alikuwa mwingi wa mawazo na kubaki kutafakari namna pete ile inavyomsaidia sana katika mambo mengi. Alinyanyuka na kukaa akimtafakari Dalfa.
"Huyu mtu ameshafahamu
nipo vipi ndio maana ananifuatilia kiasi hiki. Anamuumiza Maya ili aipate Eden kwanini asimdhuru Mfalme mwenyewe anaumiza watu wasiokuwa na hatia!?" alisema Samir akimjadili Dalfa kwa kile anachokifanya kwa Maya na kuona ni unyanyasaji kwa binti huyo. Alijilaza tena kitandani kuutafuta usingizi akiwa amechoka sana kwa kazi aliyoifanya.
Asubuhi kulipo pambazuka Jamal alipata kuamshwa kwa ajili ya kufanya mazoezi akiwa kama askari wa Eden. Hakuwa na jinsi alitii kile alichoambiwa na kuelekea kwenye uwanja wa mazoezi kujumuika na wenzake. Huku Samir alielekea hadi kwa Maya na kugonga mlango, aliporuhusiwa aliingia na kukuta wasichana wawili wakiwa wanampamba Maya apate kupendeza. Alisogea hadi pale na kumpa heshima binti huyo wa Mfalme.
"Samir umefika! Na ndio nilikuwa nakuulizia hapa." alisema Maya akiwa anawekwa urembo kwenye nywele zake.
"Nimefika binti wa Mfalme, nipo kwa ajili ya kuanza kazi yangu ya kukuwekea ulinzi." alisema Samir na kumfanya Maya atabasamu. Dakika kadhaa alimaliza kuwekwa vizuri kisha akawaruhusu wafanyakazi hao waendelee na kazi zengine.
Taratibu wakaanza kutoka mule ndani wakimuacha Samir akiwa amesimama pale ndani. Muda huo huo Lutfiya alikuwa akipita zake njia ile na kuweza kuwaona wale wasichana wakitoka mule ndani kwa Maya, hakuwa na lakusema naye alipita kuendelea na safari yake lakini alipofika mlangoni pale alipata kusikia sauti ya Samir mule chumbani kwa Maya, alitazama pande zote pale alipo na alipohakikisha hakuna mtu eneo lile alisogea taratibu pale mlangoni akatega sikio apate kusikia yanayozungumzwa ndani.
"Safari gani hiyo unayoizungumzia?" aliuliza Samir akimtazama Maya akiwa amekaa kwenye kiti akikitazama kioo kikubwa kilichopo mbele yake.
"Nahitaji twende tena kule kwenye kile kijiji, si unakumbuka niliwaahidi nitarudi siku moja! Sasa naona muda umekwenda sikutimiza ahadi yangu kwao, hivyo leo nimepanga twende tena na nafurahi safari hii umekuwa na mamlaka ya kunilinda na sio mfanyakazi wa kutumwa kama awali, hivyo naomba ujiandae." alisema Maya akionesha kutabasamu.
"Sawa nimekuelewa binti wa Mfalme, nakwenda kujiandaa." alisema Samir huku akimtazama Maya vile alivyopambwa, hakika alikuwa mwenye kupendeza sana hasa uzuri wa asili aliokuwa nao. Hakuwa anafahamu lolote kuhusu kijiji hicho wala mahala kilipo akahisi huenda ni yule Samir mwenyewe ndiye alioweza kuelekea huko na Maya.
Taratibu Samir akageuka na kuanza kuondoka baada ya kujiridhisha kuwa Maya ni mzima kabisa na hakuna aliyetambua kulitokea nini usiku.
"Halafu Samir..." aliongea Maya na kumfanya Samir ageuke tena kumtazama.
"Endelea kama mwanzo kuniita Maya na sio mtoto wa Mfalme ." alisema Maya na Samir akakubali. Lutfiya kule mlangoni alipopata kusikia hayo haraka akatoka pale mlangoni na kuendelea na safari yake.
Maya alibaki kumtazama tu Samir baada ya kukumbuka wale viumbe waliokuwa wakitisha wakipambana na Samir.
"Ile ni ndoto gani mbona ilikuwa inanitisha vile?. Na mbona kama nilimshika kweli Samir mikono yake, mmh ndoto gani hii mbona haijawahi kunitokea.!?" alisema Maya akiwa pekeake mule chumbani kwake.
Huku kwa Lutfiya akiwa anatembea zake alipata kumuona Jamal akiwa ametulia sehemu na wenzake wakiwa wamepumzika, alijisogeza maeneo na Jamal akapata kumuona Lutfiya akiwa amesimama akajua kuna jambo. Taratibu akasimama na kusogea hadi pale.
"Vipi Lutfia!"
"Kuna safari leo Maya anaenda na Samir, kuna kijiji kinaitwa Gu Ram nje ya mji wa Eden, kiongozi wao ni mtoto mdogo na anapendwa sana na kila mtu kutokana na ukarimu na maneno ya busara."
"Kwahiyo tunafanyaje, na mimi ndio nimeshaingia kwenye jeshi la kifalme?" alisema Jamal huku wakiwa makini wasije kusikiwa wanacho kizungumza.
"Jamal hizi ndio nafasi za kufanya jambo kwa Maya na hata huyu Samir, hatuna haja ya kuendelea kukubali kuvurugiwa mipango yetu. Wewe ndio una sauti ya kumfanya lolote Samir maana siamini kama amekushinda nguvu na kupambana ilitokea bahati tu akapata nafasi ile."
"Haya nimekuelewa, na vipi kuhusu Maya? Tunafanyaje kwake.?" aliuliza Jamal na kumfanya Lutfiya aangalie pembeni kwanza kisha akamsogelea Jamal na kuanza kumnon'goneza jambo fulani. Jamal alitabasamu baada ya kusikia ushauri huo alioambiwa na Lutfiya.
"Hapo sawa nimekuelewa, wacha nilifanyie kazi hilo." alisema Jamal .
"Sawa fanya hivyo mimi ngoja nimtumie ujumbe Mfalme Faruk apate kujua kinachoendelea." alisema Lutfiya na Jamal akaliafiki swala hilo kisha akarejea kukaa na askari wenzake.
Mfalme Siddik alikuwa amepumzika juu kabisa ya jengo la kifalme akiwa na mkewe wakiitazama Eden yao asubuhi ile. Walipata kuwaona wananchi wao wakiendelea na kazi mbalimbali ya kujenga Taifa hilo hali iliyomfanya Mfalme afurahi kuona vile.
"Nazidi kupata hamasa ya kulipenda Taifa langu kila siku hasa nikiangalia wananchi wangu wanavyoishi kwa amani na upendo, Eden ndio Taifa pekee lenye mfano wa kuigwa katika kila jambo." alisema Mfalme akiwa anaangalia Taifa lake.
"Mimi bado nipo njia panda sielewi ingekuwaje kwasasa tungekuwa raia wa kawaida huku Taifa hili likiwa mikononi mwa Dalfa."
"Siku zote usifanye maamuzi ya haraka kabla ya kujadili na moyo wako, kama ungeridhia kukubaliana na mikataba ile ya Dalfa tusingekuwa hapa muda huu na jina la mfalme pamoja na Malkia ndio lingeishia siku ile." alisema Mfalme Siddik
"Ila kuna watu wanaonekana ni wa kawaida hawana umuhimu sana lakini kiukweli bila ya Samir basi heshima yetu ingeshuka. Yeye ndio kafanya nisiendelee kumsikiliza Dalfa baada ya kunipa habari kwamba Maya ameamka, na nilipanga kumpa adhabu kali nikijua alinidanganya na wewe ndio umemtuma afanye vile kunifikishia taarifa za uongo, tumshukuru sana Samir." alisema Malkia Rayyat.
"Ndio maana nilipopata ushauri kutoka kwa wazee kipindi kile kuwa nimfukuze Samir kutokana na muonekano wake wa kazi sikuwasikiliza. Watu kama hawa wanafaida kubwa sana katika maendeleo, anahaki ya kushkuriwa maana hata sielewi alipitaje njiani hadi kukuwahi wewe kabla ya sisi kufika." alisema Mfalme wakizidi kumsifia Samir. Wakiwa kule juu walipata kumuona binti yao Maya akiwa juu ya farasi huku Samir naye
akipanda kwenye farasi wake ambaye alibebeshwa baadhi ya mizigo kwaajili ya safari.
Maya aligeuka na kuwatazama wazazi wake kule juu huku akiwa mwenye tabasamu mwanana. Aliwapungia mkono wa kuwaaga nao hawakuwa na hiyana, walimruhusu kwenda safari hiyo akiongoza na Samir kuelekea kwenye kijiji cha Gu ram.
Jamal alipata kuwaona wakianza safari hiyo na kuamua kusimama pale alipo na kuelekea nje ya jengo la kifalme akiwasindikiza wakina Maya kwa macho. Alitazama huku na kule na kuona hakuna mtu anayemuona, haraka akatoka pale kuelekea sehemu ambayo walikuwa wakikutana watu wa Taifa lao mara kwa mara.
Wakiwa njiani stori za hapa na pale ziliendelea huku Maya akikumbushia matukio ya nyuma ambayo kwa Samir yalikuwa ni mageni kwake lakini hakutaka kuonesha kwamba hafahamu lolote.
"Kwahiyo tunapoenda huko tunarudi muda gani Maya?" aliuliza Samir akiwa anamtazama Maya huku farasi wao wakitembea mwendo wa taratibu.
"Safari hii tutakaa sana kama siku nne hivi maana nahitaji kuwa nao karibu watu wa Gu Ram, kuna mambo mengi najifunza nikiwa karibu na yule mtoto, tangu upate kushinda pale uwanjani na kuwa mlinzi wangu nimejikuta naamini yale maneno yake kuhusu wewe. Tazama sasa Eden haikutazami kama Samir yule waliyemzoea, una heshima yako Eden kwasasa na huenda ukafika mbali zaidi." alisema Maya na maneno yale yakamfanya Samir awe na shauku ya kumuona mtoto huyo.
Huku kwa Jamal alipofika kwa wenzake akawapa kazi ya kufanya, waelekee kijiji kile cha Gu Ram kuwachunguza kujua kitu gani Maya amefuata huko. Pia wahakikishe wanammaliza Samir asiweze kurudi tena Eden. Baada ya kupatiwa taarifa hiyo haraka wakaanza safari ya kuelekea kwenye kijiji kile kuweka kambi wakiwasubiri watu waliowafuata.
Ujumbe uliweza kufika kwa Mfalme Faruk baada ya Lutfiya kutuma ujumbe kupitia njiwa yule wanayemtumia. Alifurahi baada ya kujua kuna mpango kabambe umeandaliwa na unapaswa ufanyike haraka sana. Alimuita mkuu wa majeshi yake aandae vijana kadhaa kwaajili ya kuifanya kazi hiyo. Waliteuliwa vijana kumi na watatu kwaajili ya kufanya kazi hiyo na bila kuchelewa wakaanza safari ya kuelekea kwenye kijiji cha Gu Ram. Walipanga kufanya jambo la tofauti ili wapate kufanikiwa kile wanachokihitaji. Baada ya mambo yote kwenda sawa Mfalme Faruk alirudisha ujumbe kupitia njiwa yule. Lutfiya alipata kuusoma ujumbe huo na kupata tumaini jipya la uhakika kuona idadi watu waliotumwa kwenda kukamilisha kazi hiyo wanatosha . Alimpasha habari hizo Jamal ambaye alikuwa na furaha kuona hata baba yake anamuunga mkono kwenye hilo. Wakabaki kusubiri kupata taarifa ambazo zitawafanya wafurahi.
Baada ya masaa kadhaa safari ya Maya na Samir iliweza kufika tamati baada ya kuwasili kwenye kijiji kile. Watu wengi waliwakimbilia kuweza kuwakaribisha
ndani ya kijiji chao wakiwemo watoto. Maya alishuka kwenye farasi na kujikuta akizingirwa na watoto wengi waliomsogelea pale. Alifurahi sana kwa upokeaji ule na kuamua kuwashika mikono baadhi ya watoto na kuanza kutembea kuelekea kwa kiongozi wa kijiji hicho.
Samir alitabasamu tu kuona umati ule wa watu wakimfuata Maya. Naye alipokelewa baada ya kushuka kwenye farasi wakaja vijana wawili wakamchukua farasi yule na kumpeleka mahala apate kupumzika. Naye akafuata njia aliyoelekea Maya na watoto wale. Walifika kwenye nyumba moja iliyojengwa kwa ubora wake kuliko nyumba zengine na muda huo huo akapata kutokea mtoto mwenye kukadiriwa umri wa miaka saba akiwa ameshika bakora yake fupi akiwa kwenye mavazi ya kifalme akiwatazama wageni hao kwa tabasamu.
Samir alipomtazama yule mtoto alipata kujua huenda ndiye aliyekuwa akizungumziwa na Maya wakiwa safarini. Alishangaa kuona umri wake mdogo na inasadikika ndio anayeongoza kijiji
hicho. Maya alisogea hadi pale alipo mtoto yule na kupiga magoti, yule mtoto alimsogelea na kumshika kwenye paji la uso kama ishara ya kumkaribisha na kumbariki awe mwenye amani. Samir kuona vile naye akasogea hadi pale na kupiga magoti na mtoto yule akasogea kwa Samir na kumshika kwenye paji la uso ghafla akapata kuona mkono wake ukitetemeka pindi alipomshika Samir. Yule mtoto alishtuka na kurudi nyuma hatua mbili kumtazama Samir vizuri. Aliwatazama wanakijiji wake waliozunguka eneo lile kuwatazama wakina Maya.
"Tumepata ugeni leo katika Taifa letu dogo la Gu Ram, ugeni huu umekuja na baraka tele na kuleta kitu kipya ndani ya ardhi yetu na naamini hata mimea na viumbe hai wengine watashangiria siku ya leo." alisema yule kiongozi mtoto na sekunde kadhaa mbele matone ya mvua yakaanza kudondoka kuwafanya watu washangae. Kila mmoja alishangaa kuona mvua inaanza kunyesha na kila mtu akawa anakimbia kwake kwa furaha kadhaa safari ya Maya na Samir iliweza kufika tamati baada ya kuwasili kwenye kijiji kile. Wazee, vijana na watoto waliwakimbilia kuweza kuwakaribisha
kwenda kuyakinga maji hayo, Samir alishangaa kuona hali ile ya ghafla tu na kushuhudia Maya akinyanyuka.
"Tuingieni ndani jamani mvua itanyesha kubwa sana kwa muda." alisema yule kiongozi mtoto na kugeuka nyuma kuongoza njia kuingia ndani akifuatiwa na Maya. Samir aligeuka na kuona jinsi watu wanavyoshangiria mvua ile.
"Inamaana walikuwa hawapati mvua hawa mbona wanafuraha hivyo!" alisema Samir akishuhudia furaha ya wana kijiji baada ya mvua ile. Aligeuka na kupiga hatua naye akaingia ndani. Alibaki kushangaa pindi alipotazama ndani kulivyo, ilikuwa ni nyumba yenye thamani kwa ndani lakini aliyeitazama nje aliiona ni ya kawaida. Mapambo ya kila aina yaliweza kuipendezesha nyumba ile hali iliyofanya Samir abaki kushangaa.
Walikaribishwa na kuweza kusogea kukaa kwenye viti, mwenyeji wao alisogeza kiti chake na kuweza kukaa huku mvua ikizidi kunyesha nje.
"Nimekuwa nikiwakumbuka kila siku tangu nilipoondoka mara ya kwanza, maneno yako yenye ushauri ndani yake nimekuwa nikiyafuata kila siku na siku hizi za karibuni nimekuwa na amani sana moyoni japo nilipatwa na maradhi makubwa ambayo kila mtu Eden aliniombea niweze kupona. Nashkuru kwa ushauri wako Faraj." alisema Maya akimtazama yule mtoto aliyeonekana kusikitika baada ya kupata taarifa hiyo ya maradhi.
"Pole sana Maya, unajua siku zote binadamu tumekuwa watu wa tamaa sana katika maisha yetu, swala la maradhi yako nilipata kusikia na nikatamani kuja Eden kukupa msaada lakini sheria zenu zilinitia hofu nikahofia maisha yangu na huenda baadae ningekusaidia kisha wakanigeuka kwakuwa natumia nguvu za kichawi." alisema mtoto yule aliyefahamika kwa jina la Faraj. Maneno yake yakamfanya Samir ashtuke na kumtazama baada ya kutaja mambo ya nguvu za kichawi.
"Ni kweli sheria ya Eden hairuhusu mtu mchawi na endapo akijulikana huna adhabu yake ni kifo, nilijaribu kumueleza kuwa sio wote wanatumia nguvu hizo kwa ubaya lakini hakuweza kunielewa, mwisho wa siku naumwa mimi wanatafuta watu wenye nguvu za kichawi waweze kunisaidia nirudi katika hali yangu. Na nimesikia walitaka hata kuitoa Eden iwe mikononi kwa yule Mfalme wa mashariki ya mbali, Dalfa. Na sijui nani aliyenisaidia hadi kurudi katika hali yangu hii." alisema Maya huku akisikilizwa na Faraj pamoja na Samir ambaye alikuwa kimya muda wote.
Faraj alinyanyuka pale alipokaa na kumsogelea Maya pale alipo akamshika vidole vyake huku akivibinya taratibu.
"Kuna mtu amejitolea kukusaidia katika maisha yako, yeye ndio amekufanya hadi sasa uitwe Maya tena maana uchawi ule ungekutoa uhai, ulikuwa nusu ya kufa ila yeye ndiye amekusaidia hadi sasa unaishi tena." alisema Faraj na kumfanya Maya ashangae, Samir kusikia vile alishtuka na kujua huenda Faraj aweshamtambua kuwa yeye ndiye aliyetoa msaada ule.
"Unamaana gani kusema hivyo Faraj?" aliuliza Maya akiwa hajapata kuelewa.
"Tambua tu hivyo Maya kuwa yupo ambaye anakuangalia muda wote kwa kukulinda na kuhakikisha usalama wako, tutaongea siku nyengine hiyo mada naona mvua imeacha kuyesha, mimi ngoja niwaache naingia kwenye ibada, karibuni sana Gu Ram maana hapa ni kwenu, Samir karibu sana." alisema Faraj na kumpa heshima Samir kwa kuinamisha uso wake chini kisha akauinua na kuelekea zake kwenye chumba chake cha ibada.
Maya akawa njia panda kwa maneno yale ya Faraj.
"Kumuelewa yataka umakini sana, lakini kadiri ya muda unavozidi huenda ukapata kujua nini anamaanisha mimi nishamzoea maneno yake." alisema Samir akitaka asijulikane kama ni mgeni ndani ya kijiji hicho cha Gu Ram.
"Namuamini Faraj huenda anachosema kipo japo sijapata kujua kiundani zaidi." alisema Maya akiwa mwenye kutafakari. Ilimbidi Samir aanze kubadilisha mada tofauti ili amtoe Maya mawazo hayo ya kufikiri.
Muda huo huo wale watu wa Mfalme Faruk ndio walikuwa wanaingia katika kijiji hicho cha Gu Ram lengo ni kummaliza Samir ili wampate Maya kuna jambo wanahitaji kulifanya kwake.
NINI KITAJIRI NDANI YA KIJIJI HICHO? NA PIA FARAJ AMESHAMJUA SAMIR? MAANA ANAYOYAONGEA NI UKWELI MTUPU.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA NANE(18)
