PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 18


 


SEHEMU YA 18


ILIPOISHIA


Muda huo huo wale watu wa Mfalme Faruk ndio walikuwa wanaingia katika kijiji hicho cha Gu Ram lengo ni kummaliza Samir ili wampate Maya kuna jambo wanahitaji kulifanya kwake.


ENDELEA........ 


Walifika sehemu  wakaweka kambi kwenye nyumba moja ambayo walikuwa wameandaa mazingira ya mahala pa kufika. Walipokelewa na  mtu mmoja ambaye alikuwa yupo upande wao.


"Hawa watu wamekuja kwa mara nyengine, Maya amekuwa akipendwa sana na wanakijiji wa hapa hivyo mnapomfuatilia Samir muhakikishe hakuna mtu ambaye ataona tukio hilo. Wanakuwa na matembezi ya kwenda mtoni mida ya jioni hivyo muda huo ndio mzuri kuutumia kukamilisha jambo hilo." alisema mtu huyo ambaye ndio mwenyeji wa watu hao wa Mfalme Faruk. Muda huo huo wale watu waliotumwa  na Jamal ndio walikuwa wanawasili na kufika kwenye nyumba hiyo kuungana na wenzao.


Maelezo waliyopewa wakayaridhia na kuamua kukaa kusubiri jioni ifike. Baadae wakatoka watu wawili na kuongozana na mwenyeji wao huyo kuwapeleka huko mtoni wapajue ili hapo baadae asiweze kuonekana kama alikuwa anashirikiana nao. Huku upande wa pili Jamal aliendelea na kulitumikia jeshi la Eden, kwa uwezo wake wa kutumia upanga kwenye mapambano ulimfanya hata Generali mkuu ahamasike kumpenda sana. Siku hiyo hiyo alimuita na kukaa mahala waongee.


"Nimekuwa nikitazama kipawa na akili unazotumia nimekuona una kitu cha ziada kwenye akili yako, na hii ndio inavyotakiwa hasa kwa askari wa kifalme. Mimi naamini ukiendelea hivi siku utakuja kuwa mkubwa zaidi ya hapa ulipo." alisema Generali akimwagia sifa Jamal alibaki kutabasamu.


"Sawa Generali mkuu nitahakikisha nazidi kukua kiakili siku hadi siku."


"Sawa endelea na kasi hiyo, kesho kwenye mazoezi ya Alfajiri nitakupa nafasi ya kuwaongoza wenzako naamini utalifanya hilo."


"Bila shaka Generali, nitafanya hivyo kesho Alfajiri." alisema Jamal na kuagwa na Generali huyo akaondoka zake. Alijisikia furaha kuona ameanza kuaminiwa na Generali mkuu wa majeshi yote ya Eden.


"Hii ni nafasi mpya imejitokeza sitakubali kuipoteza hata kidogo nihakikishe nafika pale nilipokusudia." alisema Jamal akimtazama Generali akitokomea.


Siku hiyo Maya alikuwa mwenye faraja sana ndani ya kijiji cha Gu Ram. Ilifika muda aliweza kutoka anatembezwa na kiongozi wa kijiji hicho Faraj huku wakifuatwa nyuma na Samir akiwa kama mlinzi wa Maya.


"Hata mimi sikuweza kuamini kama ndio atakuja kuwa mlinzi wangu, ila nimefurahi maana kwasasa amepata kuheshiwa na watu, ameamua kuonesha uwezo wake ndani ya uwanja na hakuna aliyetegemea." alisema Maya akiongea na Faraj.


"Niliwahi kukuambia kuwa siku zote hata kama ukiongoza watu wako usimdharau mtu wa chini yako na kumuona si lolote maana huenda siku moja akakusaidia sehemu ambayo hukuwahi kutegemea. Ilikuwa ni bahati kwa Samir na sasa amekuwa mtu wa kukuangalia na uzuri wake mmekuwa kama ndugu toka awali hivyo hakuna shaka." alisema Faraj wakiwa wanatembea taratibu kuzunguka mji huku kwa mbali jua likionekana kuchomoza baada ya mvua kunyesha kwa muda.


Samir mwenyewe alikuwa akiwasikiliza tu wakiongea kuhusu yeye. Alikuwa akimtazama Faraj vile alivyo. Akikumbuka yale maneno aliyoongea muda ule alibaki kuustaajabu tu.


"Inamaana naye ana nguvu kama nilizonazo mimi?" alijiuliza Samir moyoni mwake akiwa nyuma pembeni ya Maya.


"Hapana, nguvu nilizokuwa nazo chache sana kuliko ulizonazo wewe. Ndio maana ulipowasili tu kwenye taifa langu nikakujua mapema kuwa una kitu tena kikubwa sana." Samir aliyasikia maneno hayo masikioni mwake na kumfanya ashangae.


Faraj aligeuka kumtazama huku akitabasamu baada ya kuongea vile kwa hisia bila kutoa sauti. Samir alishangaa kusikia vile na kujua mtoto yule anauwezo wa ajabu na hakutaka kuuonesha kwa watu. Alibaki amenyamaza tu akiwasindikiza huko wanapoenda baada ya kufahamu tayari amejulikana na Faraj.


Siku hiyo walitembea sehemu mbalimbali kwenye kijiji kile wakiangalia vitu mbalimbali vinavopendezesha kijiji hicho hasa mazingira kwa ujumla. Kwa mbali yalionekana maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka milimani, Samir alivutiwa sana na mazingira yale.


"Aisee kunavutia sana yaani hadi raha ukiyaona maji yale yanavyotiririka." alisema Samir na kumfanya Maya atabasamu.


"Wewe unayasifia tu lakini kupiga mbizi muoga kwelikweli." alisema Maya.


"Mimi najua mbona! Nayakata maji kama sina akili nzuri." alisema Samir na kuwafanya Maya na Faraj watazamane.


Wakaanza kucheka wenyewe baada ya kuona Samir anajisifia hali ya kuwa anajulikana kwa jinsi alivyo muoga wa maji. Hata yeye alijishtukia baada ya kujua kuwa anajulikana kama Samir. Faraj akabadilisha mada nyengine huku wakiendelea kuzunguka kijiji hicho. Muda wote huo wale askari wa Mfalme Faruk walikuwa ndani ya nyumba waliyofika wakiangalia muda tu, walikuwa wanahamu ya kumaliza kazi yao mapema waweze kurejea kwa Mfalme kumpa taarifa. 


Maya na wenzake walifika sehemu akaona watoto wakiwa wanacheza hivyo naye akajisogeza na kuanza kucheza nao. Faraj na Samir wakawa wanamtazama tu Maya akiwa anafurahi na wale watoto.


"Anaupendo kwa kila mtu na ndio sababu anayo heshima kubwa hapa kwetu, nakuomba sana umlinde sana katika maisha maana atakuja kuwa tegemezi hapo mbele." alisema Faraj akiwa amekaa sehemu pamoja na Samir wakiwatazama watoto wakiwa wanacheza na Maya kwenye matope.


"Nafahamu hilo ndio maana nimehakikisha napata nafasi ya kuwa mlinzi kwake." alisema Samir na kumfanya Faraj ageuke kumtazama.


"Hebu niambie umetokea taifa gani, na hizi nguvu umezipata vipi?" aliuliza Faraj na kumfanya Samir ashushe pumzi kwanza.


"Nimetokea bara la Afrika, mimi ni Mtanzania na nilipata kukabidhiwa nguvu hizi baada ya pete hii kuingia kidoleni hapa." alisema Samir akimuonesha Faraj kile kidole chenye pete. 


Faraji aliitazama pete ile na kujikuta akiushika mkono ule wa Samir ambaye alibaki kumtazama tu Faraj. Alitumia dakika tano na sekunde kadhaa kuutazama mkono ule na kuichunguza ile pete yenye maandishi madogo madogo ambayo aliweza kuyafahamu. Aliurudisha mkono ule huku akiachia tabasamu.


"Nimeangalia matukio hapa kadhaa yaliyopita, hakika una bahati ya kuipata pete hii. Pete iliyobarikiwa na yenye uwezo mkubwa wa kufanya kitu chochote kwa muda sahihi. Ni PETE YA MFALME WA EDEN. Mfalme wa kwanza kuitawala Eden na ndio alikuwa mwenye nguvu ya kupambana hata na majini ambao walikuwa wakitaka kuigeuza Eden kuwa mji wao. Lakini sasa hivi imekuwa ni tofauti Mfalme wa Eden ndio amekuwa mstari wa mbele kukataza nguvu hizi ndani ya Taifa hilo. Ila fahamu kwamba kuwa na pete hii ni ishara kwamba utakuwa kiongozi wa Eden hapo mbeleni japo utapitia vikwazo vingi ila yakupasa uvumilie." alisema Faraj na kumfanya Samir aelewe hali halisi. 


"Unamfahamu Nadhra au marehemu baba yake aliyenyongwa mbele ya Mfalme Siddik?" aliuliza Samir huku akimuangalia Faraj.


"Mimi ndio mtoto wa mwisho wa mzee Jailan, mzee ambaye amenyongwa katika falme ya Siddik, na Nadhra ni dada yangu. Haya yote Maya hayafahamu na sitaki ajue kabisa maana akijuwa kuwa baba yangu ndiye aliyemfanya kuugua nusu ya kufa basi naamini hata upendo wake utabadilika na hata kuleta chuki kwangu." alisema Faraj na kumfanya Samir atambue kumbe Nadhra binti aliyemfanya aijue Eden ndiye dada wa kiongozi huyu mdogo wa Gu Ram.


"Yupo wapi Nadhra sasa?" aliuliza Samir.


"Pia naye ana mji wake kama mimi hapa. Upo mbali sana na anawaongoza watu wenye nguvu kama za kwetu, hii ni baada ya kuona Eden kumekuwa na sheria zinazowaadhibu wakaamua kwenda kuanzisha mji wao huko wanaishi." alisema Faraj akizidi kumueleza Samir mambo mengi sana.


Hata baada ya muda kupita Maya alirejea akiwa amechafuka sana kutokana na kucheza kwenye matope na watoto wale hali iliyomfanya Samir amshangae maana amekuwa kama mtoto. Walibaki kumcheka tu na baada ya muda wakarejea nyumbani kwa Faraj. 


Joni ilipoanza kuingia Maya akamtaka Samir waelekee mtoni kawa ilivyo kawaida yao. Kwa Samir ilikuwa ni mara yake ya kwanza lakini hakutaka kujionesha kama ni mgeni huko waendako. 


Njiani aliongea mambo mengi ya kumuaminisha Maya asiweze kuona utofauti wowote. Hata walipofika Samir alisikia furaha sana pindi alipofika sehemu hiyo. Hakika ilikuwa ni sehemu  yenye kupendeza huku maua mbalimbali yaliyojiotea pembezoni mwa mto huo yakizidi kufanya sehemu hiyo ivutie. Maya alijisogeza kwenye jabali moja na kuanza kupunguza nguo zake hali iliyomfanya Samir abaki kumtazama binti huyo. Hakika Maya alikuwa mwenye umbo lenye mvuto wa aina yake, hii ilijidhihirisha hasa pale alipobaki na nguo nyepesi iliyofunika mwili wake kuanzia kifuani hadi kwenye mapaja yake, na hata aliposogea kwenye maji na kujirusha kuanza kupiga mbizi ilimfanya Samir apatwe na hamu ya kutaka kuyaingia maji yale. Alimuona Maya akiibuka na kufanya nguo ile nyepesi aliyovaa iuchore mwili wake, hali iliyomfanya Samir ashindwe kujizuia. Taratibu akavua viatu vyake na nguo kadhaa akabaki na bukta ya ndani na kusogea karibu na maji.


"Utayanywa haya maji shauri yako!" alisema Maya akifahamu fika Samir hana ujanja kwenye maji. Alibaki kutabasamu mwenyewe na muda huo huo akajitosa majini hali iliyomfanya Maya acheke, ghafla akapata kuona Samir akitapatapa kuyapiga maji kuonesha anahitaji msaada. Maya alitabasamu na kuanza kukata maji kusogea pale alipo Samir. Alishangaa mikono ya Samir inazama chini na kutoweza kuonekana. Ilimbidi azame ndani kumtafuta lakini hakuweza kumwona hali iliyomfanya awe na hofu huku akiibuka juu na kuanza kuangaza huku na kule. Alishangaa kumuona Samir yupo mbali akiwa anachezea maji huku akicheka kumtazama Maya ambaye alipata kustaajabu. Ilimbidi Samir atoke kule huku akipiga mbizi hadi pale alipo Maya na kumuacha akiwa anashangaa haamini.


"Kumbe ulikuwa unanidanganya siku zote kuwa hujui kuogelea!" alisema Maya huku akimtazama Samir aliyekuwa anatabasamu tu na kujirusha akazama ndani ya maji, Maya alifurahi kuona vile ikawa ni mchezo sasa baina yao.


Muda huo wale askari ndio walikuwa wakielekea maeneo ya mtoni wakiwa wamejiandaa kikamilifu lengo ni kummaliza kabisa Samir kisha wamchukue Maya. Kule mtoni wakiwa wanaendelea kufurahi Samir aliona pete yake aliyovaa ikiwa inambana kwenye kidole muda ule akiwa ndani ya maji, ilimbidi anyanyuke na kuutazama mkono ule uliokuwa na pete akapata kuona kuna askari kadhaa wanafuata njia ile ya kuelekea mtoni hali iliyomfanya awe na mashaka juu yao.


Alimtazama Maya aliyekuwa hana habari akiendelea kupiga mbizi. Alitoka haraka kwenye maji na kuanza kuvaa nguo zake Maya akashangaa.


"Vipi mbona ghafla hivyo?" aliuliza Maya akiwa anamtazama Samir.


"Toka kwenye maji tuondoke haraka!" aliongea Samir na kumfamya Maya ashangae.


"Kuna nini mbona sikuelewi Samir?"


"Nahisi sehemu hii si salama, njoo uvae nguo haraka tuondoke Maya nisikilize." alisema Samir akionesha kuwa makini na anachoongea. Hata Maya alishangaa kuona hivyo ila kwakuwa ameshakuwa ni mlinzi kwake ikabidi amsikilize na afuate vile mlinzi wake anavyosema kwa usalama zaidi. Haraka alitoka kwenye maji yale na kuanza kuvaa nguo zake huku Samir akiwa anatazama kila sehemu kwa usalama.


Alipohakikisha Maya amemaliza kuvaa nguo zake akamkamata mkono na kuanza kuondoka pale mtoni haraka.

Maya alikuwa akipelekwa tu mkukumkuku huku akimtaza Samir kwa jinsi anavyoonekana kuwa makini na kazi yake. Walifika mahala kasi ile ilimchosha binti huyo wa mfalme na kuamua kuutoa mkono wake mikononi mwa Samir akasimama hali iliyomfanya Samir abaki kumshangaa.


"Hebu niambie umeona nini pale mtoni mbona unanipeleka haraka kiasi hiki?" aliuliza Maya akiwa anahema huku akimtazama Samir.


"Maya.. nimejikuta napatwa na hofu ya ghafla sehemu ile nikahisi huenda kuna kitu kibaya kitatokea pale ndio maana nikaona niepuke na hofu ile iliyojaa ghafla." alisema Samir akiwa hataki kumweleza Maya ukweli kama ameona nini.


Wakiwa kwenye maongezi hayo ghafla wakashangaa wanazingirwa na watu wakiwa juu ya farasi huku nyuso zao zikiwa zimefunikwa na kitambaa wasipate kutambulika. Maya kuona vile alishangaa na haraka akakimbilia nyuma ya Samir na kumshika mkono akionesha kuwa na woga. Samir alikuwa anawatazama jinsi wale watu walivyokuwa wanazunguka pale waliposimama huku wakiwa wameshika mapanga marefu kuashiria wamekuja kwa shari. Mmoja wao alitoka nyuma na kumpiga kikumbo Maya akadondoka chini ili wapata uhuru wa kumshambulia Samir. 


Alishtuka kuona Maya ameangushwa na kufikia uso ukapata jeraha. Alipatwa na hasira Samir kuona vile na muda huo huo akasikia upanga ukimkata mgongoni na kubaki kupiga ukelele wa maumivu huku akienda chini. Alinyanyua macho yake kumtazama Maya na kuona akivuja damu kwenye paji la uso wake, alipatwa na hasira sana na kuamua liwalo na liwe hata kama Maya akimtambua kuwa yeye ni nani. Alitazama chini kutaka kutumia nguvu zake za kichawi ili apate kupambana na watu wale waliodhamiria kummaliza. Alipotaka kubadilika ghafla kikatokea kimbunga kikubwa sana kilichowafanya farasi waliopandwa na watu wale waanza kudodoka kwa upepo ule mkali na watu wale wakadondoshwa huku vumbi likitawala sehemu ile, na dakika chache kukatulia. Wale walitoa macho kushangaa kilichotokea.


Hawakuamini kumuona mtoto mdogo akiwa pale katikati na kuwafanya waamini ndiye alisababisha kutokea kwa kimbunga hicho. Kwa pamoja wakasimama wakiwa wameshika mapanga yako na muda huo huo Samir naye akanyanyuka pale chini akiwa na maumivu mgongoni. Watu wale wakaanza kuwavamia wakina Samir ambaye aliweza kupambana nao bila ya kuonesha uwezo wa nguvu alizonazo. Maya alinyanyuka na kukaa pembeni akitazama na kumuona Faraj anavotumia nguvu zake kuwadhibiti wale watu. Alikuwa akiwaadhibu kama mtu mzima akimwacha Maya astaajabu kuona vile.


Huku Samir alifanikiwa kuwamaliza watu kadhaa kwa upanga wake ambao alipata kukabidhiwa na Nadhra kipindi alipokuwa akielekea uwanjani kupambana. Hakuwa na huruma na mtu alikata watu kwa hasira isiyopimika huku damu zikitapakaa mgongoni mwake, hali ile iliyomfanya Maya amuamini Samir na kuona kweli alichokifikiria muda ule kilikuwa sahihi. Watu wale walijikuta wanabaki wanne tu na wenzao wote wameuliwa wakatazamana na kuafikiana bora wakimbie kuyaokoa maisha yao. 


Walipopata upenyo walikimbia na kuacha farasi wao pale, Faraj akabaki kuwatazama tu. Samir alichoka hoi huku akionekana kuwa na majeraha mwilini mwake. Haraka Maya akakimbia hadi alipo Samir huku akionesha kuwa na hofu juu yake na Faraj akasogea pale.


"Nipo sawa tu Maya wala usijali.." aliongea Samir akimuondoa hofu Maya aliyeonekana kuonesha sura ya huruma. 


"Hapana umeumia sana Samir." alisema Maya na kuchana nguo yake kisha akaanza kumfunga Samir mgongoni. Faraj alitazama tukio lile na kuona upendo na huruma alionayo moyoni mwake. Samir mwenyewe alibaki kumtazama tu Maya na kuona jinsi gani alivyo na upendo juu yake. Alitamani aunyanyue mkono wake walau amshike Maya lakini nafsi yake ilisita na kubaki kumeza mate tu.


"Utaweza kutembea au nikubebe?" aliuliza Maya baada ya kumfunga vyema Samir kwenye jeraha lile. Aliposikia swala la kubebwa alishtuka na kupata nguvu ya kusimama.


"Nguvu ninazo natembea vizuri tu ona..!" alisema Samir akiwa mwenye kuchangamka japo maumivu anayasikia sana. Hakutaka kuona anabwebwa na mwanamke na isingeleta picha nzuri kwa watu wanaowatazama njiani. Faraj alilijua hilo na kubaki kutabasamu, alisogea na kumkamata mkono Samir huku akimtazama Maya.


"Nguvu anazo za kutembea hivyo tumuache atembee mwenyewe." alisema Faraj na kugeuka kuanza kuongoza njia ya kurudi nyumbani jioni ile.


Alifuata Samir kutembea naye huku akiugulia maumivu yake hali iliyomfanya Maya apate kumuona akiwa vile, alipiga hatua na kwenda kuukamata mkono wa Samir kuanza kutembea wote pamoja kurudi nyumbani kwa kiongozi wa kijiji hicho, Faraj.


Asubuhi ya siku iliyofuata mapema sana Walifika watu wawili nyumbani kwa Faraj wakimkuta nje amekaa akifanya mazoezi ya viungo. Hata walipofika walimpa heshima yake kama Mfalme wao, alinyanyuka na kupewa taarifa moja iliyomfanya ashtuke kusikia hayo.


"Muda mchache anaweza akafika hapa hivyo uwe tayari kumsikiliza." alisema mmoja wa wale watu na Faraj akapata kuelewa. Hata walipoondoka dakika kadhaa alifika askari mmoja akiwa juu ya farasi, Faraj alipata kumuona alishuka askari yule na akamtambua kwa mavazi yake aliyovaa kuwa anatokea Eden. Alipofika pale alitoa heshima baada ya kujua mtoto huyo ndiye anakiongoza kijiji hicho, Faraj alimkaribisha kwa tabasamu mwanana.


"Bila shaka wewe ndio kiongozi wa Gu Ram, na siku ya jana umepata ugeni ulio na baraka na heshma kubwa, binti wa Mfalme wa Eden amefikia kwenye kijiji chako." alisema yule askari kwa kauli ya upole.


"Unayosema ni sahihi, na hapa ni sehemu ya heshima na salama kwake. Nahisi atakuwa amepumzika muda huu." alisema Faraj na kumfanya yule askari ashtuke kusikia hivyo.


ITAENDELEA... 


Nini kitakachoendelea? Ni nani huyo aliyefika? 

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KUMI NA TISA (19)



Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group