SEHEMU YA 19
ILIPOISHIA
"Unayosema ni sahihi, na hapa ni sehemu ya heshima na salama kwake. Nahisi atakuwa amepumzika muda huu." alisema Faraj na kumfanya yule askari ashtuke kusikia hivyo.
ENDELEA NAYO.....
"Inamaana wapo ndani?" swali hilo lilimfanya Faraj amtazame yule askari. Kwa kuona ataulizwa kwakile alichosema ilimbidi aipindue mada.
"Inamaana amelala mpaka sasa?" aliuliza tena yule askari.
"Nahisi amelala maana jana walitembea sehemu nyingi sana." alisema Faraj na muda huo huo Samir akatoka ndani akiwa tumbo wazi huku akionekana kufungwa nguo mahala alipopata jeraha. Alipomtazama yule askari alishtuka baada ya kumjua kuwa ni Jamal, wakabaki wametazamana kwa muda kadhaa huku Faraj akiangalia tukio hilo.
Basi baada ya muda aliweza kuamshwa Maya na kuonana na Jamal wakakaa sehemu huku Samir akiwa pemben kwa Maya.
"Mfalme amenituma kuja kukupa habari kwamba unahitajika kurudi haraka leo hii, kuna ugeni unatoka taifa la Kusini kuja Eden, hivyo kama binti pekee wa Mfalme unapaswa uwepo pindi watakapofika." alisema Jamal akiwa anamtazama Maya kwa jicho la aina yake. Samir alikuwa akisikia kinachoongelewa pale .
"Kwanini sikupewa taarifa hiyo mpema na jana tu ndio nimetoka huko, tunaharibiana mambo na utaratibu niliopanga, nitaanzaje kuwaeleza watu kama naondoka leo wakati nimeshawapa tumaini la kukaa takribani siku nne." aliongea Maya akionekana kutopenda taarifa ile.
"Elewa kwamba sio mimi niliyesema haya, Mfalme Siddik ndio kanituma nikuletee taarifa hiyo." alisema Jamal akiwa mwenye kujiamini kwa kile anachokisema.
Ikambidi Maya ageuke kumtazama mlinzi wake Samir ambaye alishusha pumzi na kutikisa kichwa chake akimaanisha amsikilize baba yake anachosema, aligeuka na kumtaza Jamal.
"Sawa nitafuata anachosema baba." alisema Maya na kunyanyuka pale alipokaa na kuingia ndani huku akimwacha Samir akiwa pale nje amesimama karibu na Jamal.
Jamal alistaajabu kuona Maya muda ule alimtazama Samir ili apate ushauri kama akubaliane na kile alichosema kutoka kwa Mfalme. Kikubwa zaidi kilichomstaajabisha muda ule akiwa anaongea na Faraj hadi akashtuka ni pale alipoambiwa Maya amepumzika ndani angali anajua fika walitumwa askari zaidi ya kumi na watatu kuja kummaliza Samir na kumteka Maya hivyo alishtuka kusikia watu hao bado wapo. Alimtazama Samir akionekana kuwa na majeraha mwilini mwake na kuhisi huenda alidhurika wakati anapambana na askari wale waliotumwa na baba yake pamoja na vijana wake wawili.
Kwa Samir alikuwa na mashaka juu ya ujio huu wa Jamal, tangu mwanzo amekuwa na mashaka naye tangu alipoota ndoto ile, hakutaka kuendelea tena kusimama pale alitoka kuelekea kwa Faraj muda huo. Jamal akabaki pale akionesha kukasirika hadi kupiga teke mti uliokuwa pembeni yake.
"Na hili nalo tumeshindwa! Ah mpaka nachoka sasa huyu mtu tumfanyaje!" alisema Jamal baada ya kushuhudia Samir yupo salama japo amemkuta na majeraha akijua fika ni kwasababu ya kupambana askari wale wa baba yake waliotumwa kummaliza Samir na kumchukua Maya.
Samir alielekea moja kwa moja kwa Faraj ambaye muda huo alikuwa amepumzika baada ya kufanya mazoezi ya asubuhi ile. Hata alipomuona Samir alijua kuwa ndio amekuja kuagwa baada ya kupata habari kuwa wanahitajika kurejea Eden.
"Imekuwa ghafla sana safari yenu ila hakuna jinsi inahitajika mrudi kama alivyosema Mfalme Siddik." alisema Faraj akiwa anafuta jasho.
"Ni kweli lazima turudi Eden kama alivyoagiza Mfalme." aliongea Samir.
"Ila siku zote uwe karibu na Maya, kuna watu watamuwinda na kutaka kumtumia kusudi wapate urahisi wa kuupindua ufalme wa Siddik ili wamiliki Eden. Japo nipo kwenye kijiji hiki lakini pia ninauchungu na Eden, nimezaliwa huko na daima nitakuwa raia wa Eden japo tumekimbia kuhofia kuuliwa kwakuwa hatutakiwi. Ni mapema sana endapo Maya akakufahamu kuwa wewe ni nani. Hakikisha siku zote Maya hajui lolote kuhusu wewe maana huenda ikaleta matatizo." alisema Faraj na kumfanya Samir amuelewe.
"Sawa nimekuelewa. Nitahakikisha inakuwa siri." alisema Samir na muda huo Maya ndio alikuwa anatoka ndani baada ya kuwa tayari kwa kuianza safari. Jamal alimtazama na kuachia tabasamu baada ya kuona anatazamwa na Maya. Alikuja Samir na kusimama karibu na Maya huku Jamal akiwatazama.
"Upo tayari?"aliuliza Samir huku akimtazama Maya aliyeitikia kwa kichwa na kumfanya Samir atabasamu, alimkamata mkono Maya na kuelekea mahala walipohifadhiwa farasi wao.
Jamal alishangaa kuona vile na kujiuliza imekuwaje hadi Samir kama mlinzi kuweza kumshika mkono binti wa Mfalme. Ikamtia mashaka kuona kama wamefikia hatua ya kushikana hivyo basi ni wazi kwamba kutakuwa na ugumu kwa watu hawa kuweza kuwatenganisha.
Alipanda kwenye farasi wake na kuwafuata, na baada ya muda Maya alimuaga Faraj pamoja na baadhi ya wanakijiji hicho na safari ikaanza kurudi Eden.
Huku upande wa pili Mfalme Faruk alionekana kumzaba kibao askari mmoja aliyekuwa amepiga magoti akiwa na mwenzake. Ni wale askari ambao waliweza kukimbia kifo pindi walipomvamia Samir kule maeneo ya mtoni. Taarifa zile zilikuwa kero na mbaya kwa Mfalme huyo na kuona anazidi kufeli kila mipango ambayo wanaiandaa.
"Huyu mtu auliwe mara moja na binti wa Mfalme apatikane haraka sitaki kusikia lolote zaidi ya hayo." alisema Mfalme Faruk akionesha kukasirika. Ilibidi wale askari waitikie na kutii amri ile kuweza kukamilisha kile anachotaka Kiongozi wao.
Huku Eden kulianza kupambwa kila mahala ndani ya falme baada ya kufahamika kuna ugeni kutoka taifa moja lenye kuheshimika sana. Mfalme pamoja na Malkia Rayat walikuwa wakiwatazama wafanyakazi wao wakiwa wanachakarika siku hiyo ya ugeni huo.
"Hawa sijui watafika salama huku maana nimekuwa na mashaka juu ya maisha ya mwanangu." alisema Malkia akiwa na wasiwasi kwa Maya.
"Mimi sioni sababu ya wewe kuwa na hofu kubwa hivyo maana yupo na Samir pamoja na Jamal watahakikisha wanamrudisha salama hapa wala usijali." alisema Mfalme akimtoa hofu mkewe, wakaendelea kuangalia maandalizi yale.
Hadi siku hiyo Dalfa tangu afike kwenye taifa lake hakuweza kupata wala kusikia habari zozote kuhusu Maya ambaye anajua fika kwa uchawi aliyomuwekea siku ile angepata kuona ugeni wa Mfalme au Malkia wa Eden ukiwasili hapo lakini imekuwa kinyume na matarajio yake. Ilimbidi atoke kuelekea kwenye chumba cha kufanyia maombi yake. Hata alipotaka kukaribia aliona askari wawili wakisogea kwake ikabidi asimame.
"Vipi kuna habari gani mpya?" aliuliza Dalfa huku akiwatazama watu wake hao.
"Tumepata habari kwamba ufalme wa Joha unakwenda Eden kukutana na Mfalme wa Eden, na lengo hasa ni kuzungumza kuhusu ukaribu wao wakitaka watoto wao waoane na kuunganisha mataifa hayo mawili kwa udugu." alisema askari mmoja akimweleza Dalfa ambaye alishangaa kusikia taarifa hiyo mpya.
"Na hivi tunavyoongea huenda ugeni huo upo njiani na kuna nafasi kubwa jambo lao likafanikiwa maana falme hizi zimekuwa na urafiki sana." alisema askari mwengine wakimpatia habari hizo Mfalme wao Dalfa.
"Sawa.." alisema Dalfa na kugeuka kuendelea na safari yake akaingia kwenye chumba chake cha maombi. Taarifa zile alizopewa zilimfanya ashindwe kuelewa mambo anayoyasikia.
Anafahamu fika kwamba Maya amemuwekea uchawi ambao asingeweza kuamka kabisa hadi yeye atakapokwenda kutoa uchawi huo kwa Maya. Alifanya hivyo baada ya kujua tayari ameshamtoa nguvu zote Samir usiku ule na ndio maana hadi siku ya leo ameona kimya imemtia mashaka sana, alisogea kwenye chombo chake cha kutazama matukio yanayoendelea na moja kwa moja akapata kuona jinsi falme ya Eden inavyopambwa siku hiyo huku Mfalme Siddik akiwa mwenye tabasamu.
Hali ile ikamfanya Dalfa ashangae, alihisi kuanza kuchanganyikiwa hasa pale alipotaka kufahamu hali ya Maya kwa muda huo. Macho yalimtoka baada ya kuona Maya akiwa juu ya farasi huku Jamal na Samir wakiwa pembeni kwake.
"Nini tena mbona sielewi hapa!" aliongea Dalfa akiwa anatazama kwenye beseni kubwa lililokuwa na maji ndani yake akitazama wakina Maya wakiwa kwenye farasi wakionekana kurudi Eden. Alipatwa na hasira sana Dalfa na kujikuta akipiga teke yale maji na kumwagika pale ndani.
Hasira alizonazo alitamani kurudi tena Eden muda ule baada ya kujua huenda bado Samir anazo nguvu zile. Alitoka mule ndani na moja kwa moja akaelekea zake chumbani kwake kutuliza akili kwanza.
Huku njiani kwa Maya muda wote alikuwa kimya juu ya farasi, Samir alikuwa akimtazama na kuhisi huenda kuna jambo Maya analitafakari.
"Maya.. Unawaza nini muda wote?" aliuliza Samir na kauli yake hiyo ikamfanya Jamal azidi kuamini kwamba Samir amekuwa na ukaribu sana na Maya hadi kumuita kwa jina lake badala ya kumtukuza kama mtoto wa Mfalme.
"Ah kuna jambo linanipa wakati mgumu sana pindi nikilitafakari, na najikuta nakosa jibu lililo sahihi." alisema Maya wakiwa kwenye farasi wamepunguza mwendo.
"Unaweza kunishirikisha pia huenda nikapata ushauri wa kukupa!" alisema Samir na kumfanya Jamal atege sikio kwa makini naye apate kusikia. Maya alimgeukia Jamal kumtazama naye akabaki anamuangalia, akajua huenda hapaswi kusikia maongezi hayo hivyo alimsimamisha farasi wake na kuwaacha Maya na Samir watangulie kidogo mbele naye akafuata nyuma.
"Huu ujinga yaani nimekuwa mlinzi wao huku nyuma, sijui wanataka kuongea nini hawa?" alilalama Jamal mwenyewe akiona wakina Maya mbele yake wakiongea.
"Hao wageni ambao wanakuja wanatoka kwenye taifa moja la falme ya Joha, na dhumuni la ujio wao ni kuja kujadili na baba yangu kuhusu kuunganisha falme hizi mbili ziwe kitu kimoja." alisema Maya na kumfanya Samir amtazame.
"Wasiwasi wako upo wapi hapo? Huwaamini hao watu wa Joha?" aliuliza Samir na kumfanya Maya ageuke kumtazama.
"Sina maana hiyo, wanataka mtoto wa Mfalme aje kunioa mimi niwe mkewe, na swala hilo litafanya falme hizi mbili kuwa kitu kimoja. Hakika moyo wangu umekuwa mzito kukubali swala hili, sihitaji kuolewa kwenye koo ya ufalme wowote na ndio nimepanga kutoka moyoni mwangu." alisema Maya akionesha kuwa na huzuni juu ya swala hilo.
Samir alimtazama na kumuonea huruma baada ya kujua msimamo wa Maya japo ni ngumu kulizuia maana Mfalme ndiye mwenye kuamua hayo yote.
"Nipe ushauri Samir nifanye nini na hapa ndio wanakuja leo hawa watu, na naamini hawataondoka hadi maswala ya ndoa yakamilike hivyo kama nitaolewa basi nitaondoka nao kurudi kwenye falme yao ya Joha." alisema Maya na kumfanya Samir ashangae kusikia hivyo.
"Inanipa wakati mgumu sana kukushauri maana Mfalme Siddik anakupenda sana kama binti yake, na kama ugeni huu una urafiki na falme ya baba yako maana yake hatakubali kupata aibu kwa ugeni huo. Lazima atafanya kile ambacho ataona ni heshima kwake na kwa falme nzima." alisema Samir na kuzidi kumchanganya Maya.
"Sasa unanishauri vipi mbona unazidi kuniweka kwenye wakati mgumu?" aliongea Maya akionesha kuchanganyikiwa na swala hilo. Samir alibaki kutazama chini huku akishusha pumzi kutafakari itakuwaje.
Muda wote Jamal alikuwa nyuma yao kama hatua kumi bila kusikia lolote linalozungumzwa na wawili hao. Alijaribu kutega sikio kwa umakini bila mafanikio hali iliyomfanya achukie sana.
"Maya! Nitakuambia tukifika Eden usijali." alisema Samir.
"Huu ndio muda wa kunieleza Samir ili nijipange nitasemaje mbele yao na hakuna muda mwengine tutakaopata kuonana, tambua kwamba kama nitaolewa basi hata wewe ndio itakuwa mwisho wa kuwa mlinzi kwangu maana kila kitu atakipanga mwanaume huyo." aliongea Maya na kumfanya Samir ashtuke kusikia hayo, alipiga moyo konde.
"Niamini Maya nitakwambia tukifika Eden na lazima nitapata tu nafasi ya kukuona. Nitakapokwambia sasa hivi utakuwa mwenye hofu na kukuzidishia mawazo kama utaweza kulifanya jambo hilo, hivyo muda wa kwenda kuonana na wageni ndio nitautumia kukueleza wazo langu, kwasasa niache nitafakari wazo ninalolifikiria." alisema Samir na kumpiga farasi wake aongeze spidi.
Maya akabaki kumtazama tu Samir akienda mbele zaidi. Jamal akapata muda wa kumsogelea Maya pale mbele alipo.
"Vipi upo salama?" aliuliza Jamal na kumfanya Maya ageuke kumtazama.
"Nipo salama ndio." alijibu Maya naye akapiga farasi wake akaongeza kasi ya kwenda mbele zaidi, Jamal aliwatazama tu bila kuelewa kimetokea nini, ilimbidi naye aongeze kasi kwenda nao sawa.
Baada ya kila kitu kwenda kama kilivyopangwa wakawa wanasubiri ugeni huo uweze kuwasili kwenye falme. Japo Malkia Rayat muda wote alikuwa akimfikiria mwanaye maana ndiye mtu muhimu katika ugeni huo. Akiwa kwenye hali hiyo walifika askari wawili na kuweza kutoa taarifa kwamba wageni waliowasubiri wanaanza kuingia Eden hali iliyowafanya watabasamu japo binti yao hakuweza kufika hadi muda ule. Wananchi walianza kuwashangiria kwa mapokezi makubwa yenye furaha. Mfalme Joha akiwa sambamba na familia yake pamoja na askari wake zaidi ya 30 waliosindikiza ufalme huo. Watu walijipanga njiani kuwakaribisha wageni hao waliokuwa kwenye farasi wao walifika askari wa Eden takribani kumi kuupokea msafara huo na kuanza kuwaongoza kuelekea kwenye falme.
"Hakika watu wa Eden ni wanyenyekevu sana na wanaonekana wakarimu. Mfalme Siddik lazima ajivunie kwa hili." aliongea mtoto wa kiume wa Mfalme Joha aliyejulikana kwa jina la Rahim.
"Pia wana umoja wa hali ya juu na maisha yao ya kawaida, hii inafanya jina la Eden likue siku hadi siku kwakuwa na wananchi wenye umoja wa kufanya kazi." alisema askari mmoja wa Eden akimueleza mtoto huyo wa Mfalme.
Stori za hapa na pale ziliendelea hadi walipofika kwenye ufalme ambapo walipokelewa kwa furaha kubwa sana na wenyeji wao. Askari wa mataifa hayo mawili walikaribishana na kuwa pamoja kwa siku hiyo baada ya wafalme wao kuweza kukutana siku hiyo. Walikaribishwa sehemu husika na kuweza kukaa kuongea pande hizo mbili. Muda huohuo wakina Jamal ndio walikuwa wanawasili Eden, njiani walipata kuona jinsi mitaa ilivyopambwa vizuri kwaajili ya ugeni ule. Moyo wa Maya ulimwenda mbio baada ya kuona hali na kujua ugeni wa ufalme wa Eden umeweza kuwasili katika ufalme wao. Aligeuka kumtazama Samir ambaye naye alikuwa akishangaa ile hali.
Hata walipokaribia na jengo la kifalme walipata kuwaona wasichana watano wanaofanya kazi chumbani kwa Maya wakisogea kuwafuata. Hata walipofika walimsimamisha Maya na kumtaka ashuke kwenye farasi wake.
"Kuna nini mbona mnataka ashuke hapa?" aliuliza Jamal akiwa haelewi.
"Tumeagizwa na Malkia kuwa tumchukue Maya tupite naye mlango wa pili ili asionekane na ugeni uliokuja kuwa ni mtu wa kutembea, huyu ni mwari hivyo si vizuri kuwa nje kwa muda huu." alisema mmoja wa wale wasichana na kauli yake ile ilimshtua Jamal kusikia taarifa hiyo. Alimgeukia Maya ambaye baada yakusikia hivyo alimtazama Samir.
"Bado tu unatafakari jambo la kunishauri Samir?" aliuliza Maya na kumfanya Samir amtazame.
"Fuata ulichoambiwa na wahudumu wako kwanza muda sio mrefu nitakueleza." alisema Samir na kuona Maya anashuka kwenye farasi wake akionesha kukata tamaa. Alishikwa mkono na wasichana wale wakaanza kutembea naye kupitia mlango wa pili asipate kuonekana.
Jamal alibaki kutazama tu asijue kitu gani kinaendelea hapa kati. Alimuona Samir anashuka kwenye farasi wake na ilibidi naye ashuke kwenye farasi kumfuata Samir aliyekuwa anakokota farasi wake huku akionekana kuwa kwenye mawazo. Alitangulia mbele na kumzuia Samir asiende mbele.
"Kuna kitu gani kinaendelea kwa Maya mbona sielewi hapa?" aliuliza Jamal huku akimtazama Samir kwa umakini.
"Hebu naomba uniache nahisi kuchanganyikiwa nikitafakari, niache nikapumzike Jamal." alisema Samir na kusogea pembeni aweze kuendelea na safari yake lakini Jamal hakutaka kumruhusu aondoke.
"Tafadhari Samir niambie kuna nini kinaendelea hapa!?" Samir alimtazama Jamal baada ya kuongea vile.
"Unataka ujue kitu gani tena na umesikia pale kwamba Maya ni mwari kwasasa inamaana anataka kuolewa. Sasa kuna kitu gani wataka ujue?" alisema Samir huku akimtazama Jamal.
Maneno yale yalizidi kumchanganya Jamal baada ya kusikia Maya anataka kuolewa, muda huo huo Lutfiya alitokea pale na kukuta Jamal akiwa amesimama na Samir. Ilimbidi asite kusogea pale na dakika chache akamuona Samir akiondoka zake kuelekea chumbani kwake. Haraka akakimbia kumfuata Jamal aliyekuwa mnyonge baada ya kuambiwa vile na Samir.
"Jamal.." aliita Lutfiya na kumfanya Jamal ageuke na kukutana na sura ya mwanamke huyo. Ni wazi kwamba amekuja kumueleza kuhusu taarifa hizo hizo za kuolewa kwa Maya. Hii inamaana kwamba endapo atakapoolewa Maya basi swala lao ndio limefeli kabisa na hawataweza kupata nafasi ya kumtumia Maya. Walibaki wametazamana tu wasijue nini wafanye kwa muda ule.
ITAENDELEA......
Je! Maya ndio ataolewa? Na kama ni hivyo, maisha ya Samir yatakuaje wakati ametakiwa amlinde na watu waovu au safari ya kurudi kwao Zanzibar itakua imewiva? Na vipi kuhusu Jamali.
Masuala ni mengi ila tukutane kesho tupate majibu yake.
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI (20)
