PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 20


 


SEHEMU YA 20


ILIPOISHIA


"Jamal.." aliita Lutfiya na kumfanya Jamal ageuke na kukutana na sura ya mwanamke huyo. Ni wazi kwamba amekuja kumueleza kuhusu taarifa hizo hizo za kuolewa kwa Maya. Hii inamaana kwamba endapo atakapoolewa Maya basi swala lao ndio limefeli kabisa na hawataweza kupata nafasi ya kumtumia Maya. Walibaki wametazamana tu wasijue nini wafanye kwa muda ule.


ENDELEA NAYO...... 


Samir alijitupa kitandani baada ya uchovu wa safari. Kikubwa hasa kilichomtia kwenye wakati mgumu ni swala la Maya kuhusu kuolewa kwake na mtoto wa Mfalme Joha. Alitafakari ampe ushauri gani Maya kabla ya muda kuweza kufika. Aliitazama pete yake kwa umakini na kuusogeza mkono ule karibu yake.


"Nimpe ushauri gani Maya aweze kuufuata ukawa ni afadhari kwake?" aliuliza Samir huku akiitazama pete yake.


"Kuna jambo la kufuata kama itawezekekana sababu Maya akiolewa na ukoo wa Joha siku tano mbele Mfalme na Malkia wa Eden watauliwa na watu fulani. Atakayeimiliki Eden ni Maya ambaye ndiye mke wa mtoto wa Joha hivyo Eden itakuwa mikononi mwa ukoo wa Joha na siku za mbeleni watamgeuka Maya na kujimilikisha Eden kuwa yao. Kama utataka hili lisitokee basi mueleze Maya kuwa unampenda na unataka uwe mume kwake. Hili litakuwa zito kwakuwa mtapaswa kuondoka Eden kama atakukubalia. Maana ukoo wowote wa ufalme haupaswi kuwa na mahusiano na mfanyakazi yeyote wa kifalme, lakini ndio njia pekee ya kuzuia Malkia Rayat pamoja na Mfalme Siddik kutouliwa. Hivyo unakazi ya kumshawishi Maya kwa muda mfupi uliobaki." ilisema ile pete na kumfanya hata Samir anyanyuke pale kitandani maana anayoelezwa ni mazito.


"Inamaana huu ugeni sio mwema katika taifa hili?" aliuliza Samir.


"Watakaa hapa kwa muda wa siku nne, na kila siku wanayokaa ndio wanabadilika na kuitamani falme hiyo. Kuna mambo mengi yatatokea na ukizembea unaweza hata kujulikana wewe nani na inaweza kukuweka kwenye matatizo, hivyo yakupasa kuwa  makini katika mambo yako yote." ilisema pete na kumfanya Samir ashushe pumzi kwa hofu. Alijikuta anasimama kutoka pale kitandani na kutaka kwenda kuonana na Maya amueleze hali halisi ili wainusuru Eden pamoja na viongozi wake maana inakwenda kufa. 


Alisimama kwa dakika kadhaa akitafakari ataanzaje kumueleza Maya akamuelewa yale aliyoambiwa na pete yake, alipiga moyo konde akafungua mlango na kuelekea sehemu kwa Maya.


Huku sebuleni maongezi yalipamba moto baina ya pande hizo mbili, ilikuwa ni furaha kubwa sana kwa Mfalme Siddik kukutana na rafiki yake huyo wa muda mrefu Mfalme Joha.


"Naamini urafiki wetu unakaribia kuwa ndugu muda si mrefu, falme zetu zikiwa kitu kimoja hakuna wa kuziingilia wala kuleta matatizo. Hakuna asiyefahamu ukoo wa Joha ulivyojizatiti katika majeshi yenye kutumia silaha za uhakika, dhahabu zilizosheheni kwenye ardhi yangu. Wacha tulifanikishe swala hili la watoto wetu watuunganishe falme hizi mbili, na hii ni zawadi kidogo niliyokuandalia Mfalme Siddik." alisema Mfalme Joha na kumfanya askari wake mmoja asogeze sanduku kubwa lililojaa dhahabu ndani yake na kuliweka mezani. Mfalme Joha akamsogezea sanduka lile karibu yake hali iliyomfanya Mfalme Siddik aachie tabasamu zito huku akilikamata sanduku lile.


"Hakika mmependelewa ardhi yenye mali za thamani kama hizi. Nimepokea na nimefurahi kwa zawadi yako hii uliyoandaa." alisema Mfalme Siddik na kumfanya hata mkewe afurahi.


"Hiyo ni zawadi yangu kama baba, ila mhusika mwenyewe naye ameandaa zawadi yako kwako." alisema Mfalme Joha na mwanaye Rahim akasimama kwa heshima. Alimsogelea mlinzi wake na kupokea kiboksi kidogo na kumsogelea Malkia Rayat akamkabidhi. Hata alipofungua alipata furaha kuona vidani na mikufu ya dhahabu ikiwa kwenye kiboksi kile. Hakika aliifurahia zawadi ile na kumshukuru sana Rahim.


Hakuishia hapo kijana huyo lilikuja sanduku la nguo mbalimbali zenye mapambo ya dhahabu na yenye heshima kubwa akampatia Mfalme Siddik, hakika walijua kuziteka furaha za viongozi hao wa Eden ikawa ni furaha zaidi ya maelezo.


Huku kwa Samir alikuwa amesimama kwenye mlango wa chumba cha Maya huku akionekana kuzuiwa na msichana mmoja pale mlangoni.


"Nahitaji kuongea naye dakika mbili tu nawaomba." alisikika Samir akimbembeleza msichana yule.


"Hebu kuwa muelewa basi Samir. Maya yupo anaandaliwa akakutane na wageni hakuna ruhusa ya mtu yeyote kukutana naye kwa wakati huu." alizidi kuweka msimamo msichana yule.


"Nakuomba mfuate Maya mwambie Samir anataka kuongea na wewe, akikataa nitaondoka hapa mlangoni." alisema Samir na kumfanya yule msichana amtazame. Ilibidi afanye hivyo kumfuata Maya alikuwa ndani anapambwa ili akaonane na wakwe zake.


"Binti wa Mfalme, kuna mtu yupo nje anahitaji kuonana na wewe muda huu, nimejar...."


"Ni nani? Samir? Samir ndio anahitaji kuonana na mimi?" aliuliza kwa haraka Maya na kuwafanya hata wale wasichana wote waliokuwa mule ndani washangae. Yule msichana alimuitikia kwa kichwa kuwa ndiye mwenyewe, basi akashuhudia Maya akitoka mbio kuelekea mlangoni huku nyuma akiwaacha midomo wazi wale wafanyakazi wake.

Alijihisi mwenye furaha na kujawa na shauku ya kutaka kujua jambo pindi alipomuona Samir pale mlangoni.


"Niambie sasa Samir, nafanyaje?" aliuliza Maya huku akimkamata mikono Samir kutaka ampe ushauri. Samir alijikuta akimeza funda moja la mate ili amueleze ukweli Maya.


"Maya, hakika niliuficha ukweli ulio moyoni mwangu kwa muda mrefu sana, nimekuwa nikihofia kukwambia toka awali nikihofia kufukuzwa na Mfalme lakini tangu nilipopata kufahamu ukweli kutoka moyoni mwako nimejikuta napata nguvu ya kuongea haya mbele yako... MAYA HAKIKA NAKUPENDA.. na ninaongea kutoka moyoni kwamba nakupenda sana. Umekuwa mtu wangu wa karibu siku zote na ni wewe pekee uliyeniamini na kunifanya kama ndugu kwako. Tafadhari naomba unifanye niwe wako." aliongea Samir huku akimtazama usoni Maya ambaye maneno yalimfanya apoe.


"Samir mbona unazidi kuniweka kwenye wakati mgumu, sielewi ujue hadi sasa!" alisema Maya akionesha kuchanganyikiwa.


"Maya elewa kwamba huu ndio muda sahihi wa kuanza mahusiano baina yetu, kama hutaki kuolewa na ugeni huu  ambao upo hapa kwaajili ya kusubiri ndoa basi ndio muda pekee wa mimi na wewe kufanya jambo ambalo litaweza kuvunja mpango huo wa kuolewa na falme ya Joha."


"Unataka tufanye jambo gani Samir! Unafahamu fika desturi za Eden hasa katika familia za kifalme kuwa na mahusiano na mfanyakazi  yeyote wa Mfalme. Huoni itakufanya upate adhabu ya kuondolewa uishi mbali na hapa?"


"Hilo ndio kusudio langu, nahitaji mimi na wewe tukaishi mbali na hapa. Kama utakataa kuolewa na kijana wa Mfalme Joha na ukanitaja mimi kuwa ndiye uliyenichagua, haitakuwa na kipingamizi tena na nipo tayari kuondoka Eden lakini na wewe uwe na msimamo wa kuondoka na mimi. Najua itakuwa ni aibu kwa Mfalme na hasira zake lazima atakufukuza na wewe pia." alisema Samir akizidi kumvuta Maya.


"Mh Samir unataka tufukuzwe halafu tukaishi wapi maana nafahamu lazima baba yangu ataweka amri kwa mataifa mbalimbali ili wasitupokee." aliongea Maya akiwa hana raha kabisa.


"Maya ninachokiongea hapa sio kwamba nimetengeneza ili nikusaidie usiolewe laa, ninaongea kutoka moyoni nakupenda na ningependa hapo mbeleni tuje kuwa na familia yetu. Hivyo maswala ya wapi tutaishi ni baada ya moyo wako kuridhia maneno yangu na uwe na utayari wa kuwa na mimi.


Nikwambie tu ukweli nimejitolea kufa uwanjani siku ile kuhakikisha napata nafasi ya kuwa mlinzi wako ili nizidi kuwa karibu nawe, na Mungu amesaidia nimeipata nafasi hiyo na alijua nilifanya kwakuwa nakupenda. Nimejitolea kukulinda katika maisha yako yote, hata tukienda kuishi msituni juwa kwamba mimi nipo kwaajili yako. Nakuomba sana unikubalie Maya." aliongea Samir na maneno yake matam yalimfanya Maya amtazame Samir aliyeonekana kuongea kutoka moyoni.


"Samir, nitafanya kile unachotaka ila naomba uniahidi kwamba utakuwa upande wangu." aliongea Maya akiwa ameishika mikono ya Samir.


"Muda wote katika maisha yako nitakuwa nawe hadi mmoja kati yetu atakapotangulia mbele ya haki, niamini Maya nafanya haya yote kwakuwa nakupenda." alisema Samir na kushuhudia mdomo wa Maya ukitua kwenye kinywa chake. 


Hata yeye alishangaa maana hakuamini kama anaweza kumshawishi binti huyo wa Mfalme. Hakuwa na jinsi naye alishiriki kwenye tendo hilo kikamilifu wakabaki kukumbatiana wawili hao.


Yote hayo yalikuwa yakiendelea pale mlangoni kwa ndani wale wafanyakazi walikuwa wametega masikio yao kusikiliza maongezi yale. Walibaki kushika midomo yao hawaamini kile ambacho wamesikia.


Baada ya muda Maya alirejea mule ndani  kumaliziwa kupambwa baada ya kukubaliana na kupanga mambo na Samir. Wale wasichana wakawa wanampamba huku muda mwingi wakitazamana, hali ile ilimfanya Maya atambue huenda wamesikia kilichoongelewa muda ule. Hakutaka kujali alikuwa mwenye kujiamini na kuona hata wakijua haina tatizo maana muda mfupi atakwenda kuongea mbele ya wazazi wake na watu wa Joha.


Huku kwa Samir alikuwa mwenye kutafakari sana baada ya kuweza kumweleza Maya ukweli. Alibaki kusubiria kitakachotokea pindi Maya atakapoongea ukweli.


"Sina jinsi, nitakubaliana na uamuzi wowote atakaotoa Mfalme kwa kile kitakachokwenda kutokea, sifanyi haya kwaajili ya Maya, nailinda Eden yote hasa Mfalme na Malkia waliokuwa katika wakati mgumu." alisema Samir akiwa ameshika tama akitafakari haya. Hakutaka kuendelea kupoteza muda alitoka kuelekea nje kuandaa usafiri wao endapo wakitaka kuondoka na Maya.


Huku upande wa pili Jamal alielekea kwenye nyumba ambayo wamekuwa wakikutana mara kwa mara kupanga mikakati yao. Hata alipofika aliweza kuwakuta wale wenzake wakiwa na majeraha, ni muda ule walipokwenda kumvamia Samir kutaka kumuua na ndio walionusurika kukimbia pindi wenzao walipouawa. Dakika kadhaa alifika Lutfiya na kuungana na wenzake, lengo hasa ni juu ya taarifa za Maya kutaka kuolewa. Taarifa ambayo kwao ni tofauti hawakupenda swala hilo litokee. Walitaka hapo baadae wamfanye Maya awe na mahusiano na Jamal ili aweze kuolewa. Hivyo ugeni huo wa Falme ya Joha haukuwa mzuri kwao kuona wanawaingilia katika jambo lao.


"Tunafanyaje sasa hapa maana hili swala limezidi kunichanganya akili." alisema Jamal akiwatazama tu wenzake.


"Njia rahisi ya kulizuia hili ni kummaliza huyo mtu anayetaka kumuoa mtoto wa Mfalme wa Eden, nadhani kwa kufanya hili itapelekea kuwa na nafasi tena ya wewe kumpata." alisema mmoja wa wale watu akimtazama Jamal. 


"Nahisi ndio njia peke ya kulizuia hili, akiuliwa yule mtoto wa Mfalme Joha kila kitu walichopanga wao kitavurugika. Watarudi katika taifa na kumuacha Maya kama kawaida." alisema Lutfia akimuunga mkono mwenzake.


"Nani sasa ataifanya kazi hii maana kwasasa nimekuwa nategemewa kwenye jeshi muda mwingi nakuwa nipo kazini." aliongea Jamal.


"Hili swala mmoja kati yenu alifanye, ataingia kwenye falme aikamilishe kazi hii. Nimefanya matukio mengi na nimekua nikihisiwa vibaya na Samir hivyo safari hii tuwatumie nyie muifanye hiyo kazi." alisema Lutfiya akiwatazama wale wenzao. 


Walikaa kimya kwa muda kadhaa na mwishowe mmoja wapo akajitolea kufanya jambo hilo. Jamal alimpa moyo na hamasa ya kulitekeleza swala hilo. Ilibidi wamuandae na kuhakikisha wanashirikiana naye hadi kumuelekeza chumba ambacho Rahim atapataka kupumzika.


Baada ya kupanga hayo Jamal na Lutfiya walirejea kwenye falme kila mtu kwa muda wake maana kila wanapokutana hakuna anayewafahamu kwamba wanalengo gani dhidi ya ufalme wa Eden. 


Furaha ilizidi kushamiri ndani  ya ufalme, pongezi za hapa na pale ziliendelea baada ya kupeana zawadi zile. Ilifika muda walihitaji kumuona binti wa Mfalme maana tangu walipowasili hawakuweza kuona hata sura yake. Malkia Rayat alinyanyuka na kuanza kupiga hatua kuelekea chumbani kwa Maya. Rahim alimtazama baba yake na kuoneshana ishara kwamba mambo yanakwenda sawa kama walivyopanga. 


Maya alikuwa karibu na kioo amekaa huku akijitazama vile alivyopambwa na wasichana wale ambao wamemaliza kazi yao vyema na yote ni kwaajili ya kuolewa na mtoto wa Joha. Aliyakumbuka maneno ya Samir na jinsi walivyopanga kufanya. Alishusha pumzi kidogo maana swala hilo linahitaji kuwa na ujasiri wa aina yake kuongea mbele ya wageni na wazazi wake.


"Litakalokuwa sawa ila nafanya yote kwaajili ya furaha yangu, siwezi kuwafurahisha watu angali moyo wangu unakwenda kupata mateso." alijisemea moyoni Maya na muda huo huo mama yake akaingia akionesha kuwa na furaha moyoni. Alimsogelea binti yake pale alipo na kumbusu shavuni.


"Hakika leo ni siku nzuri na yenye kuleta furaha kwenye ufalme huu, kile tulichokuwa tunakisubiri siku zote hatimaye kimewadia. Familia ya Mfalme Joha imefika muda mrefu na sasa wanahitaji kukuona na hata mumeo mtarajiwa anahamu ya kukuona." aliongea Malkia Rayat akiwa na tabasamu mwanana huku akimtazama binti yake kwenye kioo kikubwa kilichopo mbele yake akionekana kurembwa haswa.


"Sawa nimesikia." alijibu kwa mkato Maya huku akijitazama kwenye kioo kile.


"Hupaswi kuwa hivyo sasa Maya, tengeneza tabasamu uonekane mwenye furaha au hujafurahia ugeni huu?" alisema Malkia na kumfanya Maya asimame na kutazamana na mama yake.


"Mama, unakumbuka kauli yangu ya mwisho nilisemaje kuhusu kuolewa?"


"Mayaaa, hebu usifanye wazazi wako tuingiwe na aibu, baba yako alikukataza kushikilia msimamo wako huo, bado tu hujaubadilisha moyo wako? Hebu sahau yote ili lifanyike jambo kubwa hapa Eden kwa hizi familia mbili." alisema Malkia na kushuhudia Maya akitikisa kichwa kutokukubaliana naye.


"Siwezi kubadili maamuzi yangu eti nisiwatie aibu! Hivi nawezaje kuwafurahisha nyinyi kwa siku kadhaa halafu nije kuwa na majuto katika maisha yangu yote ya ndoa? Nilishasema sipo tayari kuolewa na falme yeyote ile, na kama huamini ngoja uone kinachokwenda kutokea hivi sasa." alisema Maya na kutoka pale chumbani kuelekea ukumbini walipokaa wageni wote pamoja na Mfalme Siddik. Malkia kusikia hivyo haraka naye akatoka kumkimbilia mwanaye huku akimtaja jina lake. 


Huku chini wakiwa hawana habari walizidi kuongea mambo mbalimbali. Muda huo huo akapata kuonekana Maya akisogea pale walipo huku kila mmoja wapo akimtazama. Rahim alibaki kuachia  tabasamu baada ya kumuona mwanamke ambaye anategemea kuwa mkewe siku za karibuni. Watu wote walimtazama Maya kwa vile alivyopendeza, hakika hata Mfalme Joha alifurahi kuona mwanaye anapata chaguo lililo sahihi. Aliwasili Jamal na kusimama mahala ambapo baadhi ya askari waliochaguliwa kuwepo eneo hilo. Alimtazama Rahim pale alipokaa na kuona ndiyo mtu anayepaswa kuuawa. Alitazama pembeni na kumuona Lutfia naye akiwa amesimama na baadhi ya wafanyakazi. 


"Binti yangu mpendwa, hakika umependeza sana siku ya leo, naamini hata mumeo mtarajiwa anasikia faraja kukuona." alisema Mfalme Siddik huku akiwa mwenye tabasamu. Maya alimtazama baba yake huku sura yake haikuwa yenye furaha, na muda huo huo mama yake ndio alikuwa anakuja akionekana kuharakisha. 


Hata alipofika pale aliwashtua watu kwa mwendo wake wakawa wanamtaza. Maya aligeuka kumtazama mama yake akionesha kuwa na wasiwasi, na kweli alikuwa anahofu mwanaye kuongea maneno mabaya mbele ya umati ule wa watu pale ukumbini walipokaa. 


"Samahani jamani, Maya nakuomba tuongee mara moja." alisema Malkia Rayat akitaka kugeuka kwenda sehemu aongee na binti yake.


"Nitakuja subiri kwanza niyaseme machache mbele ya wageni wangu na baba yangu Mfalme wa Eden." alisema Maya kwa kujiamini na maneno hayo yakamshtua mama yake akageuka kumtazama. Haraka akamsogelea pale alipo akataka kumkamata mkono watoke mahala pale.


"Hebu mpe uhuru wa kuongea mtoto, muache aseme alichopanga kutueleza." alisema Mfalme Joha na kumfanya Malkia amuache Maya na kujenga tabasamu la kutengeneza.


Watu wote wakanyamaza kimya huku wakimuangalia Maya wamsikie kitu gani ambacho amepanga kukisema.


ITAENDELEA..... 


Je! Nini kitakachoendelea baada ya Maya kusema aliyopanga kuyasema au ataghairisha? Mambo ni 🔥🔥 Tukutane kesho kujua utamu wa PETE YA MFALME WA EDEN

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA (21)

Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group