PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 21


 SEHEMU YA 21


ILIPOISHIA


"Hebu mpe uhuru wa kuongea mtoto, muache aseme alichopanga kutueleza." alisema Mfalme Joha na kumfanya Malkia amuache Maya na kujenga tabasamu la kutengeneza.


Watu wote wakanyamaza kimya huku wakimuangalia Maya wamsikie kitu gani ambacho amepanga kukisema.


ENDELEA NAYO...... 


"Mioyo yenu imekuwa na furaha siku ya leo mkiwa mnasubiri jambo ambalo litawaunganisha kuwa familia moja." alisema Maya na kuwatazama wageni wale huku Mfalme Siddik akiwa mwenye tabasamu.


 "Huenda mkawa na furaha kwa upande wenu lakini katika moyo wangu sina hata chembe ya furaha kwa hilo mnalolitarajia. Moyo wangu haupo tayari kuolewa na falme yeyote ile na kauli hii naisema mbele ya watu wote ili mfahamu hilo." alisema Maya na maneno yake yakawa sumu katika mioyo ya watu hususani Mfalme Siddik ambaye alikasirika ghafla kwa kuyasikia maneno ya binti yake.


"Unaongea upumbavu gani wewe Maya?" alifoka Mfalme na kutaka kunyanyuka lakini Mfalme Joha akamzuia pale alipo.


"Si mara ya kwanza baba kukueleza juu ya hili lakini umekuwa unataka iwe ni lazima jambo ambalo sitalikubali abadani." aliongea Maya na kuzidi kumtia hasira baba yake, aligeuka kumtazama Rahim.


"Siku zote ndoa ni maridhiano baina ya watu wawili waliopendana, mimi na wewe tulikaa lini kwa lengo la kukubaliana kwa maongezi tulifanikishe hili? Mimi nikwambie ukweli ulio moyoni sina upendo wowote na wewe na wala usitegemee ukaja kuwa mume kwangu." alimpa ukweli kutoka moyoni bila kujali wapo watu wengi eneo lile.


"Kila mtu ana uhuru wa kumchagua yule ambaye moyo wake umeridhia kuwa naye, sitakuwa tayari kuwa na mtu ambaye hayupo katika fikra za.."


"Usizidi kunikera Maya, askari mkamateni haraka sana!" alitoa amri hiyo na mara moja Jamal aliharakisha pamoja na askari wawili wakamkamata Maya mikono.


"Sijamaliza, naomba kila mtu afahamu sina mapenzi na Rahim hata chembe, yupo ninayempenda naye anajua hilo." alisema Maya na kuwafanya watu wote wamtazame. Hata Jamal na wale askari walimtazama baada ya kusema hivyo.


Huku kwa Samir alikuwa anamalizia kuandaa farasi wa Maya pamoja na farasi wake ikiwa ni maandalizi endapo wakifukuzwa na Mfalme. Alipohakikisha hilo amelikamilisha alirudi zake chumbani kwake huku akiwa ni mwingi wa mawazo. Akiwa anaukaribia mlango mkuu alishangaa kuona askari wapatao ishirini wakikimbia na kumzunguka pale. 


Hali iliyomfanya asimame na kubaki kwenye mshangao akiwatazama askari wale walioweka mikono yao kwenye mapanga yalioning'inia kiunoni tayari kwa kuyatoa kumkabili Samir endapo ataleta tafarani. Akiwa kwenye mshangao huo alitokea Generali Mkuu akiwa ameweka mikono nyuma, walifungua duara lile akapita kisha na kumsogelea Samir aliyebaki kushangaa tu. 


Ngumi nzito ilituwa shavuni kwa Samir akaenda chini huku akishika shavu lake, alishuhudia damu zinamwagika kutoka mdomoni mwake, aligeuka kumtazama Generali aliyeonekana kuwa na hasira.


"Kupewa nafasi ya kuwa mlinzi wake ndio umeona njia nzuri ya kuanzisha mahusiano naye, sasa utaenda kuishi msituni upambane na wanyama wakali pumbavu wewe! Huwezi kumtia aibu Mfalme kiasi hiki." alifoka Generali na kugeuka.


"Mleteni huku akaongee!" aliamuru akamatwe Samir aingizwe ndani akajibu mbele ya Mfalme. Alikamatwa na kuanza kupelekwa ndani, alijua tayari Maya ameongea kila kitu, alikuwa hana hofu juu ya swala hilo. 


"Huwezi kuongea maneno hayo mbele yangu mimi, umenitia aibu kubwa sana Maya." alisikika Mfalme Siddik akifoka kwa ukali huku akimtazama binti yake.


Malkia Rayat ilibidi awe mpole tu baada ya kuona mumewe amepandisha hasira. Muda huo huo aliingia Generali huku nyuma akifuatwa na askari wake waliomuweka Samir chini ya ulinzi.


"Huyu mjinga ndio amekuteka akili hadi unakosa heshima hata kwa mzazi wako!?" alisema Mfalme na kugeuka kumtazama Samir.


"Sikutegemea kama utakuja kufanya jambo hili katika falme yangu, Samir niliyemlea mimi muda wote leo amekuja kunigeuka na kutaka kuchuma mmea wangu nilioupanda mwenyewe. Sitahitaji kusikiliza la mtu nakupa uhuru uondoke hapa Eden ukatafute mji wowote wa kuishi nje ya Taifa langu, ole wako nikuone unakanyaga tena hapa, haraka naomba uondoke!" alisema Mfalme Siddik akiwa amekasirika sana huku Mfalme Joha akimtaza Samir aliyekuwa ameinamisha tu kichwa chini. Rahim alimkata jicho Samir baada ya kujua ndiye mtu aliyemfanya asikubalike kwa Maya.


Hata alipogeuka kutaka kuondoka Maya alimkamata mkono angali naye ameshikwa na wakina Jamal.


"Baba, Samir hawezi kuondoka Eden peke yake kama kupendana ni sisi ndio tumependana hivyo hata kama nitalazimishwa sitakuja kumpenda mtu mnayemtaka nyie, chaguo langu ni moja tu, Samir." aliongea Maya na maneno yake hata mama yake yalimchoma na kujua kweli mwanaye amependa. 


Watu wote walielewa kweli Maya amedhamiria kuwa na Samir. Mfalme Joha alisimama na kupiga makofi kadhaa huku akijenga tabasamu, watu wote wakageuka kumtazama hata Mfalme pia.


Aligeuka kumtazama Mfalme Siddik.

"Siku zote usilazimishe jambo ambalo haliwezekani maana unaweza ukaumia ama likakuchosha. Muache mwanao afanye uamuzi anaotaka." aliongea kwa upole mfalme Joha akijaribu kumtuliza mfalme Siddik aliyeonekana kuwa mkali sana. 


Ilimbidi Mfalme aite baraza la wazee wakaingia mahala kulijadili swala hilo huku kila mtu akiongea la kwake juu ya jambo hilo, Jamal alimtazama Samir akiwa ameshikiliwa na askari pale karibu yao, moyoni alipatwa na hasira baada ya kufahamu kumbe Samir pamoja na Maya walikuwa ni wapenzi, swala hilo lilimfanya hata Lutfiya apate kuhisi ndio sababu ya Samir kuwa karibu kila anapotaka kufanya jambo baya kwa Maya, Malkia alibaki kumtazama tu binti yake huku akisikitika na kuona huenda likaamuliwa lolote na wazee pindi watakapopata muafaka wa swala hilo. 


Mfalme Joha alimsogelea mwanaye na kujadili naye mambo fulani pale walipokaa wakisubiri muafaka utolewe na Mfalme Siddik. Huku Maya alikuwa ameinama tu chini pale alipokamatwa na wakina Jamal, ilisikika tu minon'gono pale ukumbini kila aliyeko eneo hilo alilipokea swala hilo kwa namna yake. 


Baada ya muda Mfalme Siddik alitoka sambamba na wazee wale na kurudi kukaa sehemu zao, kila mtu alitulia kimya huku wakimtazama Mfalme aliyeonekana akiwa amenuna. Maya na Samir walikuwa wenye hofu wakisubiri kitakachoamuliwa na Mfalme.


Alinyanyuka mzee mmoja na kusogea pale mbele akasimama huku watu wakimtazama.


"Baraza la wazee wa Eden likiwa chini ya Mfalme Siddik limekaa na kuchukua uamuzi wa pamoja na kumfikishia Mfalme. Hata yeye ameridhia sheria ifuatwe kama inavyotaka." alisema Mzee yule na kumfanya Malkia Rayat aanze kulia baada ya kufahamu kinachojiri.


"Kuanzia sasa Samir pamoja na Maya hawatatakiwa kuonekana katika Taifa la Eden milele." watu walihamaki baada ya kusikia hivyo, wengine hawakuamini kama itatokea adhabu hiyo.


"Ufalme unasheria zake na ni kosa kubwa Mfanyakazi wa falme kuwa na mahusiano na mtoto wa kiume au binti wa Mfalme na endapo litatokea hilo basi mmoja kati ya hao auliwe na mwengine atupwe msituni lakini Mfalme amekataa kushuhudia kifo cha mmoja kati ya hawa hivyo wote watapelekwa kutupwa msituni na hawataruhusiwa kurudi Eden maisha yao yote." alisema Mzee yule na kumaliza maelezo yake akarudi kukaa. 


Mfalme Joha alitabasamu kusikia vile, kuna namna amefikiria na kuona huo ndio muda pekee wa yeye kufanya kitu.


Malkia alijikuta akimsogelea mwanaye na kumkumbatia pale huku akionekana kulia maana hatakuja kumuona nae tena. Mfalme Siddik alijikaza kutosikia maumivu kama baba lakini moyoni aliumia sana, hakukuwa na namna ya kulizuia hilo Maya na Samir lazima waondoke Eden. Aliumia sana kwa kuona ameingia aibu kwenye falme ya Joha kwa maneno yale ya binti yake kuonesha kutokuwa tayari kuolewa na ukoo huo. Kubwa na ndio linalobeba adhabu ya kuwafukuza wawili hao ni kuwa na mahusiano baina ya mtoto wa Mfalme na mfanyakazi wa mfalme.


Taratibu Maya alimsogelea baba yake hadi pale alipo na kuinama chini kuishika miguu ya baba yake kama kuchukua baraka. Hata alipomaliza alirejea nyuma na kufanya hivyo kwa mama yake pia ambaye alijikuta akimnyanyua mwanaye na kumkumbatia huku akionekana mwenye majonzi. 


Generali aliwaamuru askari wafanye kazi na mara moja walianza kuwatoa wawili hao huku Malkia Rayat akitolewa mwilini mwa binti yake wakiwa wamekumbatiana. Maya alijihisi huzuni kumuona mama yake akiwa katika hali ile, alishuhudi kuona mama yake akikimbia kuelekea chumbani kwake. Ni wazi kwamba ameshindwa kuvumilia kumuona binti yake huo akitolewa katika taifa alilozaliwa.


Taarifa nje zikapata kusikika na kuwafanya wananchi watoke wote majumbani kwao na kusimama nje.

Hata walipotoka Samir na Maya walipanda kwenye farasi wao kila mmoja na kuanza kusindikizwa na askari kumi waliochaguliwa na Generali akiwemo Jamal. 


Wafanyakazi wa Maya waliokuwa wakimhudumia waliumia sana kuona bosi wao anaondoka ndani ya falme hivyo hawatakuwa na kazi tena katika falme. Lutfiya alibaki kutazama tu msafara ule unavyoondoka pale na kuona mipango yao imekufa bila shaka. 


Wananchi walimpa heshima Maya kwa kuinamisha vichwa chini kuonesha bado wanamheshimu lakini walipewa mgongo wakaanza kumshambulia Samir kwa maneno na hata kumrushia vitu kama mayai na nyanya mbovu. Iliwabidi askari waingilie kati kumkinga Samir asizidi kuchafuliwa, alibaki kuinamisha kichwa chini tu huku akiona kama ni fedheha kwake kufanyiwa vile.


Malkia Rayat alikuwa juu ya chumba chake akitazama dirishani na kuona Maya na Samir wakiiaga Eden. 


"Mungu awatangulie huko muendako naamini mtaishi muda mrefu." alisema Malkia Rayat akiwaombea uzima Maya pamoja na Samir.


Huku nyuma Mfalme Siddik aliwaomba radhi familia yote ya Mfalme Joha kwa kile kilichotokea. Hata yeye hakutegemea kusikia yale ambayo yamemchoma moyoni. Hapakuwa na jinsi waliona hakuna haja ya kulaumiana kwa jambo lile na kuamua kuachana nalo. Hata zawadi zile walizotoa waliamua kumpatia Mfalme Siddik kwa moyo mmoja. 


Waliongea mambo mengi siku hiyo na baadae iliwalazimu waage ili kuweza kurejea kwenye taifa lao. Mfalme Siddik aliwapatia magunia ya vyakula ikiwa kama shukrani yake ili kuweza kusahau yale yaliyotokea. Walipokea mizigo hiyo askari na kuanza safari ya kurudi kwenye ufalme wa Joha. Rahim alibaki kuitazama Eden vile ilivyo, roho ilimuuma sana maana alitegemea kumuoa Maya kungemfanya akaheshimika Eden.


"Nimeagiza vijana kadhaa wawafuatilie wajue wanaachwa kwenye msitu gani, bado nina tumaini la kuja kupata heshima Eden, nitampata tu Maya na yule mpumbavu lazima auliwe." alisema Rahim akionesha kukwazika sana kwa kumkosa Maya. Mfalme Joha alibaki kumtazama tu na kusikia lengo la mwanaye huyo .


Mfalme Siddik alirejea chumbani kwake na kumkuta mkewe akiwa amesimama tu pale dirishani akitazama nje. Alijua bila shaka alikuwa akiwatazama wakina Maya kipindi wakiondoka. Alishusha pumzi kidogo kabla ya kuongea lolote huku akiinamisha kichwa chake. Alifahamu kuwa adhabu ile imemuumiza hata mkewe maana Maya ndiye mtoto wao wa pekee hivyo kuondoka kwake ni sawa na kumfanya Malkia ajione hana mtoto tena.


Taratibu alipiga hatua pale alipo kumsogelea mkewe, akamshisha bega.

"Haikuwa na jinsi, sheria za Eden ndio zinatuongoza." aliongea Mfalme kwa sauti ya upole.


"Nafahamu hilo, nami sina jinsi nitabaki kuwa Malkia tu nisiye na mtoto kwasasa. Sijui huko aendako atakuwa hai kwa muda gani au atakufa lini." aliongea Malkia na maneno yale yalimchoma Mfalme Siddik. Hakuwa na jinsi maana binti yake amehukumiwa kwa sheria zilizowekwa Eden. 


Taarifa za binti wa Mfalme kufukuzwa ndani ya taifa la Eden zilimfikia Mfalme Faruk hali iliyomfanya ataharuki.

"Wameelekea wapi kwasasa?"


"Wanakwenda kutelekezwa kwenye msitu na askari wa Eden." alisema kijana mmoja aliyeileta taarifa hiyo akitokea Eden.


Alichoka Mfalme Faruk maana taarifa hiyo ilimfanya aamini swala la kumtumia Maya katika njama yao ili waipate Eden kwa njama hiyo imegonga mwamba. Alitafakari namna ya kufanya na mwishowe akapata jibu alilohisi litaleta maana.

"Yuko wapi Jamal kwasasa.?" aliuliza swali akitaka afahamu mwanaye alipo.


Safari ilikaribia kuishia ukingoni baada ya kuukaribia msitu ambao unasadikika kuwa na wanyama wakali. Hapo ndipo walipaswa kuachwa Samir pamoja na Maya kama adhabu ilivyotolewa. Walikuwa wakiutazama msitu ule jinsi ulivyo mkubwa na kuwafanya watazamane kuona ni wao ndio wanapaswa kuingia humo. Baada ya dakika kadhaa walifika mwanzo wa msitu huo na kuonekana njia kubwa ambayo ni ya kupita watu na usafiri wao.


"Huu ndio msitu wa mpaka wa Eden unapoingia kwenye msitu huu kuanza kuifuata njia hiyo hautambuliki kuwa upo Eden, hilo ni taifa lengine tena. Hivyo basi hiyo ndio njia yenu ya kupita kuwa nje ya Eden, mkatafute mji wa kuishi huko muendako kama mtafanikiwa kupita salama ndani ya msitu huu. Sisi safari yetu imeishia hapa tutasimama hapa kuhakikisha mmepita hapo ndipo turudi." alisema Kamanda wa kikosi hicho alimtazama Samir aliyekuwa makini kusikiliza. Aligeuka kutazama msitu ule uliokuwa unasikika sauti mbalimbali za wanyama na ndege. Jamal alibaki kuwatazama tu Maya na Samir, taratibu huruma ikaanza kumjia pale akiwa juu ya farasi.


"Nendeni haraka!" alisema askari yule na kumfanya Maya aanze kutangulia. Samir naye akafuata wakinyoosha njia ile kuingia mule ndani huku askari wakishuhudia wakitokomea wawili hao. Walisimama kwa dakika kadhaa pale hadi walipojiridhisha kuwa wamefika mbali na wao wakageuka na kuanza safari ya kurejea Eden. Jamal alibaki kuutazama tu ukubwa wa msitu ule na kuwa na mashaka juu ya maisha ya wawili hao.


Samir na mrembo Maya walifika sehemu wakakuta mifupa na mafuvu ya watu hali iliyomfanya Maya ahofie na kuingiwa na woga.

   

"Samir, kwani tunaenda wapi?" aliuliza Maya na kumfanya Samir amsimamishe farasi wake.


"Umeniwahi kuongea hayo maneno maana tunapokwenda hakujulikani." alisema Samir wakawa wamenyamaza kwa muda wakitafakari.


"Unaonaje tukaelekea Gu Ram?" aliuliza Maya.


"Gu Ram?"


"Ndio twende huko, mimi naamini Faraj tukimueleza yote atatuelewa na kutupokea." aliyasema hayo huku akimtazama Samir aliyekuwa anamsikiliza. Maneno yalijitosheleza kwa Samir na kumuunga mkono Maya, ilibidi wageuke na kurudi walipotokea ili wakamate njia ya kulekea Gu Ram. Hata walipotoka nje ya msitu ule walitazama huku na kule hawakuweza kuona mtu yeyote eneo lile na haraka wakaanza safari yao. Kwa mbali walionekana watu wakiwa kwenye farasi wao wakiwafuata na bila shaka ni wale askari waliotumwa na Rahim, maana hakutaka kukubali kirahisi kumkosa Maya.


ITAENDELEA.....


GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI (22)

Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group