SEHEMU YA 22
ILIPOISHIA
"Ndio twende huko, mimi naamini Faraj tukimueleza yote atatuelewa na kutupokea." aliyasema hayo huku akimtazama Samir aliyekuwa anamsikiliza. Maneno yalijitosheleza kwa Samir na kumuunga mkono Maya, ilibidi wageuke na kurudi walipotokea ili wakamate njia ya kulekea Gu Ram. Hata walipotoka nje ya msitu ule walitazama huku na kule hawakuweza kuona mtu yeyote eneo lile na haraka wakaanza safari yao. Kwa mbali walionekana watu wakiwa kwenye farasi wao wakiwafuata na bila shaka ni wale askari waliotumwa na Rahim, maana hakutaka kukubali kirahisi kumkosa Maya.
ENDELEA NAYO......
Siku hiyo Dalfa naye ndio alikuwa akiikaribia Eden akitokea katika taifa lake. Hakutaka kuamini kama kile alichokifanya kwa Maya hakikuweza kufanikiwa, alijua bila shaka ni yule mtu aliyekuwa na nguvu kama zake. Njiani alipata kuona askari wa Eden wakionekana kutoka mahala wakirudi Eden, alipowatazama kwa umakini aliweza kumtambua Jamal na kumkumbuka ndiye mtu aliyepambana na Samir siku ile pale uwanjani.
"Wametoka wapi hawa mbona wengi hivi?" alijiuliza Dalfa bila kupata jibu kamili huku akiona msafara ule ukitokomea. Taratibu naye akafuata huku akiwa juu ya farasi wake mweupe.
****
Baada ya kwenda umbali mrefu kwa kasi iliwabidi wawapunguze kasi farasi wao na kuanza kutembea taratibu wakawa wanaongea mambo yao.
"Unajua mpaka sasa siamini kama tumelifanikisha hili, moyo wangu naona umekuwa na amani kwasasa na wala sina mashaka tena." alisema Maya akionesha kutabasamu.
"Nitafurahi kama utaendelea kuwa hivyo muda wote, nipo kwaajili yako Maya." aliongea Samir na kumfanya Maya ajihisi mwenye faraja sana. Wakiwa kwenye furaha hiyo ghafla walipata kusikia vishindo vya farasi wakiwa wanakimbia kwa spidi, walipogeuka nyuma walipata kuona wanakaribiwa na kundi la watu nane wakionekana kushika mapanga yao.
"Tukimbie haraka sio wema hawa." aliongea Samir na kumsukuma farasi wake aongeze mbio, Maya naye akafanya hivyo lakini kwa bahati mbaya kilirushwa kisu kikapenya kwenye nyama za mguu wa farasi wake aliyedondoka chini na kumfanya Maya naye aanguke. Hali ile ikamfanya Samir aliyekuwa ametangulia asimame na kurudi nyuma. Haikuwa rahisi muda huo huo wale watu walifika na kuwazunguka kuwaweka kati huku mapanga yakiwa mikononi. Hakujali silaha zile alishuka na kumsogelea Maya pale alipodonda akamnyanyua.
"Upo salama?" aliuliza Samir bila kujali watu walio wazunguka.
"Samir tupo kwenye hatari, hawa watu watatuua." alisema Maya akionesha kuwa na hofu. Alisuhudia kuona Samir akitoa kitambaa na kukishika.
"Fumba macho yako Maya." alisema Samir akiwa anatazamana na Maya. Hakuwa na jinsi alifanya vile alivyoambiwa. Haraka Samir akanyanyua kitambaa kile na kuyaziba macho ya Maya kusudi asione kinachoendelea muda ule. Alipohakikisha amelifanya hilo alimuacha pale akiwa amesimama kisha akakamata upanga wake na kugeuka kuwatazama watu wale ambao walionekana kuwa na uchu wa kummaliza Samir. Wakashuka kwenye farasi wao na kuanza kumsogelea mtu wao. Bila kuchelewa wakaanza kumvamia Samir kutaka kummaliza, hakuwa tayari kudhurika na silaha zile za mapanga alipigana kwa umakini wa hali ya juu. Alipoona wanazidi kumuandama hakusita kutumia nguvu zake za ziada pindi aangaliapo pete yake iliyopo kidoleni mwake. Alijikuta anabadilika ghafla na kuwa na kasi ya ajabu kuwadhibiti watu wale, hakuwa na huruma nao hata kidogo alichinja kwa dakika chache tu na kubaki watu wawili ambao walistaajabu kuona vifo vya wenzao pale chini na kushuhudia damu nyingi ikisambaa eneo lile. Hawakuwa tayari kuendelea na zoezi hilo, waliona njia ya haraka kuyanusuru maisha yao ni kukimbia maana mtu waliyemtegea ni zaidi ya shetani anatumia nguvu za ajabu.
Haraka walianza kutoka mbio eneo lile. Samir alipata kuwaona na hakutaka kumuacha hata mmoja akiwa mzima maana walikuja kwa shari, aliokota mapanga mawili pale chini na kuyarusha kwa kasi kwa watu wale yakapata kuzama mgongoni mwao na kuwadondosha chini na kupoteza maisha. Alibaki akihema kwa kazi nzito aliyoifanya kwa dakika chache.
Aliwatazama wale watu pale chini na kushindwa kuwafahamu ni watu wa taifa gani lakini alipoweka umakini wa hilo swala akapata kuhisi jambo. Alimsogelea mmoja pale chini na kuivua nguo yake ya juu na kukuta kuna nguo ya pili amevaa. Alipoitazama aliifahamu kuwa ni sare ya askari wa Mfalme Joha jambo ambalo lilimshangaza.
"Inamaana wametuma watu ili watuue?" alijiuliza Samir bila kupata jibu kamili. Haraka akanyanyuka kugeuka kwa Maya na kujikuta wanatazamana. Alikitoa kile kitambaa na kuonekana kama mtu aliyeshikwa na butwaa. Hali ile ikamfanya Samir ashtuke na kuhisi huenda Maya ameona kila kitu na kumjua Samir yupoje. Walibaki wametazamana kila mtu akiwa kwenye hali ya mshangao.
"Ni wewe Samir..?!" lilikuwa ni swali ambalo lilimfanya Samir ashindwe kujibu kwa haraka. Mwili wote ulipoa baada ya kuona tayari Maya amemtambua kuwa anatumia nguvu za ajabu.
"Umeanza lini kuwa hivi?" aliuliza Maya akiwa anamshangaa Samir pale alipo, alijikaza na kuanza kupiga hatua hadi pale alipo Maya.
"Maya, haya yote nitakueleza pindi tutakapofika Gu Ram, tafadhari tuondoke." alisema Samir na kuanza kuongoza njia lakini alijikuta akishikwa mkono wake na Maya, aligeuka taratibu kumtazama.
"Nijibu swali langu Samir, umeanza lini kuwa hivi?" aliuliza tena Maya swali ambalo lilimfanya Samir atafakari namna ya kumwambia.
Alimsogelea Maya na kumshika shavu huku wakitazamana, hakuona ja ya kumficha tena.
"Siku zote nimekuwa hivi tangu ulipolala kitandani kwa majuma kadhaa na kuwafanya watu wote wa Eden waamini kama hutaweza kuwa hai. Na siku ambayo unaamka mtu wa kwanza uliyepata kumuona ni mimi, na ndio nilifanya uweze kupona pindi nilipojua kwamba uchawi uliotupiwa hakuna ambaye angeweza kuutoa. Na ni mimi ndiye niliyetoka siku ileile kwenda Mashariki na mbali kumzuia Malkia asiandike chochote kwenye mikataba ile ya kuiacha Eden mikononi mwa Dalfa, naomba ufahamu hayo machache kwasasa pindi tukifika nitakueleza tu ila usiniogope mimi sina ubaya kwako Maya, nakupenda naomba ufahamu hilo." aliongea Samir kwa ufupi na kumuacha Maya mdomo wazi haamini kama ni Samir ndiye aliyefanya yale yote. Alimtazama tu Samir na kumuona akigeuka na kumfuata yule farasi wa Maya aliyechomwa kisu mguuni alikuwa amejilaza pale chini akiugulia maumivu. Hata alipomfikia akapiga magoti na kushika ile sehemu iliyozama kisu kile na kuanza kuongea maneno fulani huku taratibu akikichomoa kisu kile. Maya alijikuta akipiga hatua taratibu akishuhudia anachokifanya Samir.
Kisu kile kilitoka bila wasi na wala hakukuwa na maumivu kwa farasi yule. Alipolikamilisha hilo akashika kile kidonda na kuachia, hapakuonekana jeraha lolote kwenye mguu wa farasi yule ambaye muda huo huo akapata kunyanyuka na kutembea kama ilivyo awali. Maya alibaki kustaajabu baada ya kushuhudia tukio hilo na kuamini kweli Samir ananguvu za ajabu.
Hakutaka tena kuficha uwezo wake Samir kwa Maya maana tayari alishamuona akipambana na wale askari wa Joha. Alimuamuru Maya apande kwenye farasi wake waendelee na safari huku akimtoa wasiwasi.
Njia nzima Maya alikuwa kimya huku akimtazama Samir, hakumdhania kama yeye ndio amekuwa msaada kwake na hata kwa Eden nzima kwa kumzuia Malkia Rayat kutoweka saini yake kwenye mikataba ile.
Huku upande wa pili Jamal pamoja na askari wenzake waliwasili Eden na kuripoti kwa mfalme kumueleza kuikamilisha kazi ile kama alivyotaka Mfalme. Aliwaruhusu waendelee na ulinzi baada ya kupokea taarifa hizo. Moyo ulimuuma kama mzazi maana anafahamu jinsi msitu ule ulivyo hatari kwa watu wapitao njia ile. Kuna wanyama wakali wa kila aina hivyo si rahisi Maya na Samir kuweza kuwa hai. Hakuwa na jinsi maana sheria ndio imemhukumu mwanaye kwa kosa la kuwa na mahusiano na mfanyakazi. Malkia Rayat alikuwa anawataza tu askari wale wakiondoka kwa mfalme baada ya kuleta ripoti ya kuikamilisha kazi ile. Alihuzunika sana na kuona ndio mwisho wa kumuona binti yake Maya.
Muda huo Dalfa ndio alikuwa akiwasili Eden, moja kwa moja alisogea katika falme na kupata kuona ulinzi wa askari ukifanya kazi yake. Alitazama pembeni na kuweza kumuona msichana wa kazi akitoka kwenye Falme akiwa ameshika kitenga akielekea sokoni. Akaona njia sahihi na ya kuweza kumfanya akaingia mchana ule bila kujulikana ni kumtumia msichana huyo. Taratibu akaanza kumfuata kule alipokuwa anaelekea.
Huku upande wa pili kwa Rahim hadi muda ule hawakuweza kupata taarifa zozote kwa wale watu aliowatuma kwenda kummaliza Samir na kumchukua Maya. Alianza kuwa na wasiwasi juu ya hilo hivyo akaamua swala hilo kulifuatilia mwenyewe. Aliandaa askari ishirini na kuanza safari za kuelekea kule msituni kunaposadikika ndipo Maya na Samir walipoachwa huko. Yote hayo alikuwa anayafanya Rahim huku baba yake alikuwa akimuangalia tu na kuona kweli mwanaye amedhamiria kumpata Maya mtoto wa Mfalme Siddik.
Kule kwa Dalfa aliweza kumpata msichana yule baada ya kurejea sokoni na kumchukua kumficha sehemu kisha akajibadili na kuwa kama alivyo msichana yule, alikamata kile kitenga kilichosheheni matunda na mboga mboga akaanza safari ya kuingia kwenye falme. Hakuna aliyemuhisi kuwa yutofauti, alipita kwenye geti kuu kama kawaida akiwa anatazama kwa umakini baadhi ya sehemu kama ataweza kumuona Samir. Alienda hadi ndani na kuanza kupita kila sehemu kumtafuta mtu wake huku akiwa makini kutojulikana anachokitafuta. Alienda moja kwa moja hadi kwenye chumba kile cha Samir. Alipokaribia na chumba hicho alipata kumuona Jamal akiwa anatoka kwenye chumba hicho na kukifunga kwa kufuli kisha akaondoka zake. Hali ile ikamfanya ashangae kuona mtu tofauti ndio anafunga mlango ule kuonesha hakuna mtu ndani.
Hakutaka kuamini hilo taratibu alisogea pale huku akitazama huku na kule kisha akaishika kufuli ile huku akiitazama kwa macho makali ikapata kufunguka.
Huku kwa Jamal alipofika mahala alisimama baada ya kufahamu ameacha upanga wake mule ndani haraka akageuza kurudi kule chumbani.
Dalfa akiwa kwenye umbo na sura ya yule msichana alipoingia hakuweza kumuona yeyote mule ndani, alisogea hadi pale kitandani ambazo siku ile alipokuja usiku ndipo aliposimama akimtoa nguvu zile Samir. Aliushika mto uliopo pale kitandani na kuushika huku akivua hisia kutumia nguvu alizonazo kutambua kuwa mto huo ulilaliwa na mtu tofauti na Samir.
Alichanganyikiwa hapo asijue inakuwaje jambo hilo, haraka akatoka mule ndani baada ya kumkosa Samir kwenye chumba chake. Akawa anatembea akiwa anatazama huku na kule kama ataweza kumpata mtu wake. Alishangaa akishikwa mkono kwa nyuma jambo lililomfanya ageuke haraka na kukutana na sura ya askari mmoja akiwa kwenye tabasamu. Yule askari alimvuta yule msichana kwenye korido huku akitazama huku na kule kuangalia kama kuna watu.
"ah nimekuwa na hamu na wewe tangu jana uliponiahidi tukutane leo, nadhani ndio muda muafaka huu kama tulivoku baliana." alisema yule askari na kuanza kumtomasa msichana yule, huenda ni wapenzi wenye kujuana muda mrefu. Hali ile ikamfanya Dalfa apate ghadhabu ya kushikwashikwa vile akawa anajiondoa mikononi mwa askari yule aliyetegemea kupata ushirikiano kwa mpenzi wake. Alishangaa kuona mwenza wake hayupo tayari kwenye jambo hilo akawa anamtazama.
"Unanini kwani mbona sikuelewi?" aliuliza askari yule na kushuhudia akishikwa bega.
"usijali mpenzi wangu kwasasa nina kazi nitakutafuta baadae." alisema msichana yule na taratibu yule askari akaanza kwenda chini kama mtu aliye na usingizi na kulala kabisa pale. Aligeuka haraka na kuendelea na safari yake hadi alitoka nje na kwenda kujibadilisha mbele ya safari na kurudi kuwa Dalfa.
Alikasirika sana kwa kumkosa Samir ndani ya falme hali iliyomfanya atafute mahala kwanza atulie huku akiona baadhi ya wananchi wakipita kutoka mashambani.
"Nimeamini sheria zinafuatwa hapa Eden, yaani mfalme ameridhia kabisa binti yake akatelekezwe msituni bila kujali kama ni mwanaye!" alisikika mtu mmoja akiongea huku akiwa amebeba mzigo wa majani kwaajili ya mifugo yao.
"Hiyo ndio maana ya uongozi sio kubagua adhabu ya kuwapa watu fulani wengine unawaacha."
"Ila kwakuwa yupo na Samir huenda akawa na msaada kwa binti wa Mfalme."
"Ah wapi ule msitu una wanyama wakali sana huwezi kuwazuia wasikudhuru, ni wengi na wakali."
"Hebu acheni mada hizo tayari wawili hao kama kufa wameshakufa tangu muda walioondoka Eden, itakumbukwa tu kwamba binti wa mfalme alikuwa na mahusiano na mlinzi wake na wamepata adhabu ya kutelekezwa msituni. " aliongea mtu mmoja akiwa na wenzake watatu wakijadili mada hiyo.
Maongezi yao yalimshangaza Dalfa akiwa amekaa mahali akiwatazama wale watu wakitembea huku wakipashana habari hizo.
"Ina maana hawa watu walikuwa na mahusiano? Ndio maana yule kijana amekuwa akimlinda muda wote ." aliongea Dalfa baada ya kuupata ukweli kuhusu Samir na Maya. Alipopata kufahamu kwamba wawili hao wametelekezwa msituni alijuwa fika swala hilo si hatari kwa Samir kama ananguvu kama yeye. Alijua kwa namna yeyote ile watu hao ni wazima na huenda wapo mahala kujihifadhi. Haraka alisogea kwenye farasi wake na kupanda kuelekea kule msituni kupata uhakika wa kile anachokiwaza.
Huku upande wa pili Samir na Maya waliweza kuwasili katika kijiji cha Gu Ram. Walipokelewa kama ilivyokawaida, wanakijiji wengi waliungana nao kuwasindikiza hadi kwa kiongozi wao Faraj. Alipata faraja kuwaona wageni hao kwa mara nyengine na kuweza kuwakaribisha kwa kuwapa baraka kama ilivyoada na zoezi hilo lilipokamilika watu wakarejea kwenye kazi zao na wageni hao wakapata kuingia ndani baada ya kukaribishwa na mwenyeji wao.
Maongezi ya hapa na pale yaliendelea na hata walipomueleza ukweli juu ya kile kilichojiri Eden kwamba wamefukuzwa hawatakiwi tena katika taifa la Mfalme Siddik.
"Huu ni mtihani mmeupata katika maisha, ila sidhani kama kuna kikubwa cha kuogopesha juu ya uamuzi na sheria iliyotolewa dhidi yenu. Hapa ni nyumbani kwenu karibuni na mtaishi hapa siku zote kama Eden wameweka marufuku kwenu kurejea. " aliongea Faraj akiwafariji.
"Hivi ni kweli sitaweza kuonana na mama yangu tena?" aliuliza Maya akiwa anamtazama Faraj.
"Ni rahisi kumuona, ila ni vigumu sana kuonana naye. Kwasasa huesabiwi kama mtoto wa Mfalme kama ilivyo zamani, na wewe ndio mwenye kazi ya kurudisha jina lako pindi utakapohitaji kurejea Eden, ila sio kwasasa yakupasa ukae muda mrefu usionekane ili siku utakayorejea waamini hukuuawa kwenye msitu ule hatari." alisema Faraj na kumfanya Maya apate kuelewa, aligeuka kumtazama Samir aliyekuwa akisikiliza yanayozungumzwa pale. Faraj aligeuka kumtazama Samir pale alipokaa.
"Samir, usiku wa jana nimepata kuota ndoto kuhusu wewe na imekuwa kama bahati mmeweza kuja leo." alionge Faraj na kauli yake ile ikamshtua Samir.
"Ndoto? Ni ndoto gani hiyo?"
"Nimeota unavalishwa pete, ni pete yenye thamani kubwa sana katika mataifa, ni Pete ya Mfalme wa Eden. Mfalme wa kwanza kuitawala Eden hii ambayo kwasasa inatawaliwa na Siddik." alisema Faraj na kumfanya Samir ashangae, aligeuka kumtazama Maya aliyekuwa anamuangalia pia.
"Hiyo ndoto inamaana gani Faraj?"
"Huenda ukawa Mfalme hapo mbeleni." aliongea Faraj na kuwafanya Samir na Maya washangae kuambiwa vile.
"Inamaana Samir atakuja kuwa Mfalme? Kwenye Taifa gani sasa?" aliuliza maswali kwa mkupuo Maya huku akimtazama Faraj.
"Siwezi tambua ni Taifa gani labda lakini kwa ndoto niliyoota ni kwamba anavalishwa pete ya Eden. Na pete hiyo hadi kuivaa ni kwamba umekubalika uitawale Eden." alisema Faraj na kuwaacha Samir na Maya wakiwa wenye kutafakari swala hilo.
Alinyanyuka na kuwaacha pale yeye akaenda kwenye chumba chake cha kufanyia ibada.
Iliwachukua dakika tatu bila kusemeshana pale ndani na hatimaye Maya akafungua kinywa chake.
"Mimi namuamini Faraj, ndoto zake zimekuwa na ukweli katika maisha yangu na siwezi kupinga kwa hili pia"
"Lakini nitawezaje mimi kuwa Mfalme?" aliongea Samir akijua fika kuwa yeye ni mtanzania hivyo asingeweza kulitawala taifa hilo.
"Huwezi juwa ni sababu zipi zitakufanya ukawa Mfalme hapo mbeleni." aliongea Maya akimuelewesha Samir wakiwa wenyewe pale walipoachwa.
Huku Eden zilianza kusambaa kila kona kuhusu kupatikana kwa mwili mfanyakazi wa kike wa mfalme ukiwa kwenye moja ya njia ya uchochoroni akiwa tayari amekufa. Watu walipatwa na hofu juu ya kifo hicho kisichojulikana mhusika wa tukio hilo ni nani. Taarifa hiyo ilimshtua yule askari ambaye ni mpenzi wake na muda mchache uliopita alikuwa pamoja naye lakini alijikuta haelewi kilichotokea mara baada ya mpenzi wake kumshika begani akapoteza fahamu.
Mfalme Siddik pamoja na Malkia walipatwa na mshangao baada ya kufikishiwa taarifa hiyo, ilibidi waongozane hadi kwenda mahala mwili wa marehemu ulipohifadhiwa.
Walifika na baadhi ya waganga wa jadi na Generali kushuhudi. Waliuchunguza mwili huo lakini hawakuweza kuona jeraha lolote mwilini, ilibidi wazee watumie ujuzi wao kutazama zaidi huku Mfalme akitazama tu na mwisho wa siku wakapata kujua ukweli.
"Kuna mtu amemnyonga kwa kutumia mkono na hakuna silaha yeyote iliyotumika. Mtu huyo ana nguvu sana maana hakuukaza mkono wake shingoni alijua kwa kufanya hivyo kungebaki alama ya vidole vyake." alisema mzee mmoja baada ya kuchunguza maiti ile kwa makini.
Ilibidi Mfalme atoe amri kwa Generali kuwapa kazi askari ya kufanya upelelezi ili abainike mtu huyo aliyefanya mauaji hayo.
Moja kwa moja Generali alitoka hapo na kuelekea kwa Jamal. Inasadikika tangu alipodondoka na kupoteza fahamu hakuweza kuinuka, alifika na kumkuta akiwa amelazwa kitandani huku askari wawili wakiwa pembeni kumuangalia.
"Mmehakikisha hakuna anayefahamu swala hili?aliuliza Generali.
"Ndio hakuna anayefahamu kinachoendelea." alijibu askari mmoja akiwa anamtazama Generali wake..
"Sawa hakikisheni hata Mfalme hafahamu kama huyu amepoteza fahamu. Ah sijui nini kimemkuta Jamal hadi kuwa hivi!" aliongea Generali huku akimtazama Jamal pale kitandani akiwa amelala.
ITAENDELEA....
Jamal nae amekumbana na nini mpaka awe amezimia? Mpaka sasa mie sijui tukutane kesho kupata jawabu.
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU (23)
