SEHEMU YA 23
ILIPOISHIA.....
"Sawa hakikisheni hata Mfalme hafahamu kama huyu amepoteza fahamu. Ah sijui nini kimemkuta Jamal hadi kuwa hivi!" aliongea Generali huku akimtazama Jamal pale kitandani akiwa amelala.
ENDELEA NAYO...
Kule msituni Rahim aliweza kufika na askari wake hadi kwenye ile njia ya kuingia ndani ya msitu. Walibaki kuutazama msitu ule huku milio ya ndege na wanyama mbalimbali ikisikika. Aliwaamuru askari watano waongoze njia ya kuingia msituni. Nao wakatii amri hiyo ya mtoto wa Mfalme wakaingia huku wakina Rahim wakisikilizia kinachoendelea. Haikupita hata dakika mbili walishtuka kusikia kelele za askari walioingia mule wakijaribu kuomba msaada na punde tu kukawa kimya huku sauti ya kuunguruma ya wanyama wakali zikisikika kana kwamba wanagombana. Ilibidi wakina Rahim wasogee pale mahala pa kuingilia na kuona mule ndani ya msitu chui weusi zaidi ya kumi wakiwagombania askari waliokuwa tayari washapoteza maisha pale chini. Walitafunwa kama wanyama wa porini hali iliyowafanya askari wote waliobaki nje waogope, Rahim mwenyewe alishangaa kuona vile na kupata ushahidi huenda hivyo ndivyo ilikuwa pia kwa Samir pamoja na Maya.
Alirudi nyuma akiwa hoi amechoka kwa lile alichokiona ni ushahidi tosha juu ya watu aliohitaji kuwapata. Alijikuta akipiga kelele za hasira maana amemkosa Maya akiwa na malengo naye binafsi. Askari waliinamisha vichwa chini wakimsikia Rahim akiwa analalama kwa kutofanikiwa, alisogea kwenye farari wake na kupanda kuondoka zake huku askari wale nao wakifuata baada ya kujua walichokifuata wamekosa.
Muda wote huo Dalfa alikuwa mahala anawatazama hadi walipokomea, alijua nawao wamewafuata wakina Samir kwa namna yao. Alisogea hadi pale kwenye njia ile na kusikia chui wale wakiunguruma. Alishuka kwenye farasi wake na kuanza kuingia mule ndani bila kuhofia lolote.
Wale chui wakiwa wanamalizia kutafuna miili ya askari wale wakapata kumuona Dalfa akiwa anakuja bila kuonesha woga, walikaa tayari kwaajili ya kumrukia binadamu huyo lakini kadri anavyozidi kusogea ndipo anapobadilika na kuwa kama wao na zaidi ya hapo alikuwa akiwaka macho yake na kuonekana yenye kung'aa. Hali hiyo iliyowafanya chui wale watambue yule ni zaidi yao, walirudi nyuma taratibu na kuanza kukimbia kila mtu njia yake. Dalfa kwa mnyama huyo mkali alitembea taratibu huku akitazama huku na kule kuona wanyama wakali ndani ya msitu huo. Aliangalia chini ya ardhi akinusa harufu ya kwato za farasi akijua huenda wakina Samir walipita hapa. Na kweli alipata kusikia harufu hiyo akazidi kwenda mbele zaidi. Alifika mahali akapata kuona ndio mwisho wa kwato zile za farasi. Alinusa harufu ile bila kutambua muelekeo walipoenda watu wake anaowataka. Akapata kufahamu huenda walifika hapo na kugeuza kurudi walipotoka. Naye aligeuza na kurejea kule nje baada ya kujiridhisha hayo.
Huku upande wa pili Jamal alianza kurejesha fahamu baada ya kufumbua macho yake. Alitazama mahala alipo na kujikuta amelala pale kitandani, alinyanyuka taratibu na kuhisi maumivu mgongoni. Aliangalia kila kona kwenye chumba kile akiwa peke yake na ndipo kumbu kumbu zikamjia mara ya mwisho alipata kumuona msichana wa kazi akiwa mule ndani, na ni yeye ndiye aliyemtupa Jamal kwa nguvu za ajabu kumrusha akadondoka chini na hakujua kilichoendelea.
"Yule msichana anatumia nguvu za kichawi?" alishangaa Jamal pale alipo na kuhisi huenda ikawa kweli. Hakutaka kuchelewa akashuka pale kitandani na kuvaa nguo zake za uaskari na kukamata upanga wake akatoka nje, lengo ni kwenda kumpasha habari Mfalme kuhusu msichana yule akijua huenda kuna jambo baya amedhamiria kulifanya likaleta matatizo kwenye falme. Hakufika mbali akakutana na Generali akiwa anaelekea kumuona Jamal kule chumbani.
"Jamal umeamka!" aliongea Generali huku wakisogeleana.
"Generali, naelekea kwa Mfalme nikamweleze jambo lililotokea, kuna watu wanatumia uchawi humu kwenye falme na huenda si wema." aliongea Jamal na kumfanya Generali amkamate mkono wakasogea mahala waongee.
"Unamaana gani kusema hivyo Jamal mbona sikuelewi?"
"Kuna mfanyakazi wa kike anatumia nguvu za kichawi, nimemuona akiwa ndani ya chumba kile akiwa anatafuta kitu, na mlango niliufunga kwa kufuli funguo hii hapa ninayo, ameingiaje mule ndani? Na ndio maana nilipomshtua kumuuliza hakuwa na la kujibu nikajikuta narushwa sijui na upepo sijui kimbunga hata sijafahamu na sikujua kiliendelea kitu gani." aliyasema hayo Jamal na kumfanya Generali aelewe sababu za Jamal kukutwa akiwa amezimia.
"Huyo msichana unamfahamu ukimuona?" aliuliza Generali na kuweza kuitikiwa.
"Sasa sikia hili swala tutalifanya bila Mfalme kujua lolote kwanza tupate uhakika na jambo hili, tusikurupuke kumpa taarifa zisiso na uhakika akaja kukubadilikia ukapata adhabu na unaelewa ameshampoteza binti yake hivyo hana huruma kwasasa." alisema Generali na maneno yale Jamal akayaelewa.
"Nahitaji nikuweke kwenye nafasi nzuri hapa Eden, huenda ukaja kuwa nafasi yangu na hata ukafika mbali na hapa ulipo, niliongea na baba yako akanieleza kuhusu wewe kutaka kuwa askari mashuhuri hapa Eden na naamini utafika unapotaka." alisema Generali na Jamal akafahamu kumbe baba yake tayari alisharahisisha kazi mapema. Alimshkuru kwa kuwa naye karibu na kumpa kipaumbele sana katika mambo mengi. Baada ya kuongea hayo walitoka na kuelekea kumtafuta msichana huyo anayedhania kuwa na nguvu za kichawi.
Upande wa pili Rahim akiwa njiani na askari wake akitafakari mambo mengi jinsi alivyopanga endapo angempata Maya na kuwa mkewe basi angekuwa na heshma kubwa ndani ya Eden na ndio njia ya urahisi kwake kuja kuimiliki Eden kama mfalme. Akiwa kwenye fikra hizo alikumbuka wale askari wao waliotumwa kwenye kile kijiji cha Gu Ram na muda huohuo akasimama kuwauliza askari wake kama wanafahamu kijiji ambacho wenzao walitumwa kwenda.
Baadhi yao walipafahamu na ikawa ni heri kwa Rahim aliyeamuru waelekee huko. Alikuwa mwenye hasira za kumkosa Maya hivyo alijiandaa kwa lolote huko wanapoelekea.
Kwa Dalfa alipotoka kwenye msitu ule alirudi kwenye umbo lake la awali huku akionekana kuangaza macho yake kila kona bila mafanikio. Hakupata kutambua wapi walipoelekea wakina Samir maana kitendo cha kutoka nje ya msitu ule hakuna alama yeyote inayoonesha muelekeo wa farasi waliopandwa na wakina Maya.
Alikasirika sana kuona mtu anayemsumbua kiasi hicho ni Samir na aliapa safari hii akimpata lazima ammalize kabisa.
Alichoamua ni kurudi tu Mashariki na kati kutuliza akili kwanza ili ajipange namna ya kumpata Samir maana ndiye mtu pekee anayemnyima usingizi kwakufahamu kwamba anatumia nguvu kama alizonazo yeye.
Baada ya muda kupita Maya pamoja na Samir walitoka na kwenda kutembea sehemu mbalimbali ndani ya kijiji hicho huku maongezi ya hapa na pale yakiendea. Na huo muda muafaka wa Samir kumueleza ukweli Maya kuwa yeye ni nani na ametokea wapi.
Safari yao ilikomeshea kwenye jabali moja kubwa wakapanda na kukaa wakawa wanaongea mambo mengi zaidi.
Alitumia muda mwingi kumuelewesha Maya ambaye alibaki kustaajabu tu baada ya kuelezwa kuwa Samir anayemjua yeye si huyu ambaye anamuona kwasasa. Jambo ambalo awali hakuwa mwenye kuamini kwa haraka maana hakukuwa na utofauti baina ya watu hao wawili.
"Jina langu kamili ni Amour na sio Samir, nilipatwa kuambiwa mwenye jina hili ameshauawa na watu ambao walimpa kazi ya kummaliza Maya. Na baada ya tukio la kupata matatizo binti huyo wa Mfalme, Samir akatumia njia hiyo kuwadanganya kwamba tayari amelifanikisha zoezi hilo, swala likabaki kwenye kulipana na hapo ndipo walipomgeuka na kummaliza wakijua wamesaidiwa kuuawa kwa Maya.
Maelezo hayo yalimshtua Maya na kuona jinsi alivyokuwa akiandamwa na wabaya bila sababu yeyote.
"Hiyo ndio tofauti kubwa kati ya mimi na yeye, nipo kwaajili ya kukulinda na si kukuuza kwa watu wabaya." aliongea Samir akiwa anatazamana na Maya. Alimtoa hofu kwa yale yote mabaya anayofikiria binti huyo wa Mfalme, na kubwa hasa alilofanya Samir ili kumpa furaha Maya ni pale alitaka washikane mikono, Maya hakusita alifanya kama alivyoagizwa na kushuhudia Samir akiitazama pete yake iliyo kidoleni mwake na ghafla wakapotea pale walipokaa.
Walikuja kuibuka wapo chumbani tena kwenye viti karibu na meza ndogo iliyosheheni vitabu na madaftari. Samir aliachia tabasamu tu huku akimtazama Maya aliyekuwa akiangaza macho yake huku na kule asijue yupo wapi.
"Ni wapi hapa mbona sipafahamu?" aliuliza Maya akizidi kushangaa, zilisikika kelele za watoto nje wakicheza hali iliyozidi kumshangaza.
"Hapa ndio chumbani kwangu, tupo Unguja sasa nchini Tanzania." aliongea Amour na kumfanya Maya astaajabu kusikia hivyo. Alinyanyuka haraka na kwenda kufunua pazia la dirishani, mazingira na nyumba za watu jinsi zilivyo zilimshangaza sana na kuona kweli ni tofauti na Eden. Akataka kupiga hatua ili atoke nje kuangalia zaidi mazingira lakini Amour akamzuia.
"Wewe nje hapana, kaka yangu atakuona wakati hafahamu kama wewe upo humu usije kuniletea matatizo hapa." alisema Amour na kushika kitasa cha mlango.
"Kwani atakugombeza kwa lipi? Naomba niruhusu nitoke nione mazingira yalivyo, nakuomba Samir!" alisema Maya akitaka kutoka nje. Ilimbidi Samir aufungue mlango na kuchungulia kwanza nje ahakikishe kama kuna watu pale nje. Bahati nzuri hapakuwa na yeyote eneo lile akarudisha kichwa chake ndani na kumruhusu Maya atoke nje na haraka Maya akafanya hivyo. Aliona mandhari tofauti na aliyozoea huku akiona kwa mbele watoto wakicheza mchezo wa gololi na wengine wakiruka kamba, alijikuta akitabasamu kwa kuona watoto wale wakiwa wenye furaha na taratibu akaanza kujisogeza.
"Jamani mnaondoka kimya kimya?" ilisikika sauti iliyomfanya Maya asimame na kugeuka nyuma sauti ilipotokea. Amour alishtuka kumuona shemeji yake anatoka ndani huku akiwa amebeba sahani iliyokuwa na machungwa kwa kauli yake ile ilimfanya Amour atambue huenda alifahamu kama alikuwa na msichana yule mule chumbani. Maya alibaki kushangaa tu na kumgeukia Amour aliyempa ishara kwamba achangamke.
"Ah samahani nilijua umelala ndio maana nikaona nisikusumbue." aliongea Maya akijenga tabasamu.
"Wala sikuwa nimelala, mimi nilikuwa nawamenyea machungwa wageni, hebu rudi walau utie baraka kidogo." alisema Shemeji mtu na kumtaka Maya arudi kuchukua chungwa, naye akafanya hivyo na kupokea chungwa hilo huku akitoa shukrani. Ilibidi Amour naye asogea pale kuchukua kipande, baada ya dakika kadhaa kujiridhisha kwamba swala hilo shemeji yake anafahamu akawa anajiamini. Alimkamata mkono Maya na kumuaga shemeji yake kuwa anamsindikiza.
Maya aliaga na kugeuka kuongozana na Amour.
Alianza kumzungusha kwenye mitaa huku Maya akionekana kushangaa tu.
"Halafu mbona najiona mwepesi sana Samir?" aliuliza Maya wakiwa wanatembea pamoja. Samir alitabasamu huku akitazama mbele.
"Labda nywele zako zilikuwa zinakupa uzito." alisema Samir na kumfanya Maya ashike kichwa chake. Alishtuka kuona nywele zake zipo tofauti, ni fupi na zimesukwa kabisa.
"Mungu wangu! Samir nini tena hiki mbona sielewi?" alistaajabu Maya baada ya kuona yupo tofauti.
"Kuna msichana anaitwa Aziza yupo kama wewe ulivyo kasoro yenu ni hizo nywele tu, hivyo ungeonekana wa ajabu kila mtu angeshangaa kuona nywele ndefu zenye kufika mgongoni."
"Inamaana hata mimi kuna mtu nafanana naye?"
"Ndio, anaitwa Aziza. Nasoma naye shule moja." aliongea Amour (kwa jina la Tz 😂) na kumfanya Maya ajue kumbe hata yeye pia kuna aliyefanana naye huku Tanzania.
Wakiwa kwenye maongezi hayo akatokea Eliza akiwa anapita njia ile, alitabasamu tu baada ya kumuona Amour akiwa na mrembo yule. Aliwasalimia kisha akaendelea na safari yake. Amour alitabasamu na kujua Eliza amepata neno la kuongea endapo wakikutana.
Huku upande wa pili Rahim aliweza kuwasili na askari wake katika kijiji cha Gu Ram. Walikuwa wamesimama sehemu wakikitazama kijiji kile huku Rahim akionekana kuwa na hasira sana. Alitoa amri kwa askari wake wavamie kiji kile na kupiga watu ili iwe fundisho na kisasi kwa kile walichofanyiwa askari wake. Muda huo huo akawasili yule mtu wanayemtumia katika mambo yao na kuwaeleza ukweli halisi.
"Wamerudi tena Maya na yule Samir." aliongea yule mtu na kumfanya Rahim ashangae.
"Unachoongea una uhakika?" aliuliza Rahim akiwa haamini.
"Siwezi kumdanganya mtoto wa Mfalme Joha, hawa watu wamekuja leo na nimepata kusikia kwamba wamefukuzwa Eden na sasa watakuwa wakiishi hapa."
"Hawa watu kumbe bado wazima....Safi sana!" alifurahi Rahim na kuwageukia askari wake.
"Namuhitaji Maya akiwa mzima huyo mwengine auawe." alitoa amri hiyo Rahim na askari wake wakaipokea, bila kuchelewa wakaanza kusoga mbele kuikamilisha kazi hiyo.
Huku kwa Amour akiwa anazidi kumzungusha Maya kwenye mita aliona pete yake ikimbana kidoleni na kufahamu huenda kuna jambo. Maya alitazama kumuona Amour akinyanyua mkono wake kuitazama pete ile, alimuona amebadilika ghafla akionesha kukasirika.
"Vipi mbona umebadilika hafla hivyo?"
"Gu Ram kuna matatizo, Rahim na askari wake wameingia kwa shari." alisema Amour na kumfanya Maya ashangae.
"Jamani sasa kwanini wanafanya hivyo! Kwahiyo tunafanyaje.?" aliuliza Maya akionekana mwenye huruma.
Amour alisogea na kumshika mkono Maya alifahamu wanarudi walipotoka. Na kweli sekunde kadhaa walitoweka pale walipo wakaja kuibuka kule walipokuwa juu ya jabali moja. Haraka bila kuchelewa wakaanza kutoka mbio kurudi kijijini ambapo ndipo sehemu inayotarajiwa kuvamiwa.
Faraj akiwa zake kwenye chumba chake cha maombi alipata kuhisi ishara ya jambo la hatari kuweza kutokea. Haraka akatoka mule chumbani hadi nje na kusimama mlangoni, aliona kuna kila dalili mbaya kutokea. Haraka aliingia ndani na punde tu akatoka akiwa ameshika pembe ndefu iliyojikunja na kuanza kuipuliza kama tarumbeta. Mlio uliotoka pale ulikuwa mkubwa sana uliowafanya wananchi wote wapate kusikia na kujua maana ya mlio huo. Haraka wakaanza kukimbia kila mmoja wao akaingia ndani kwake kufunga milango na kutulia kimya.
Muda mfupi kupita waliwasili jeshi hilo la Rahim wakiwa juu ya farasi wao huku wakitazama kila kona bila kuona yeyote.
Walizunguka kila njia kutafuta kama wataweza kumpata hata mtu mmoja lakini haikuwa rahisi.
"Inamaana walijua kama tunakuja! mbona hakuna hata mtu nje?" aliuliza Rahim akiwa mwenye kushangaa.
"Huenda ikawa hivyo, hapa kilichobaki ni kuvunja milango yao na kuwatoa wapate adabu." aliongea askari mmoja aliyekuwa karibu na Rahim ambaye naye alikuwa na wazo hilo hilo, bila kuchelewa akawaamuru askari wote wavamie kwenye nyumba za watu, lakini ghafla tu wakapata kumuona mtoto mmoja akisogea pale walipo. Mavazi yake ya heshima huku akiwa ameshika bakora kama mzee yaliwashangaza wakina Rahim aliyewasimamisha kwanza watu wake. Alikua ni Faraj aliyesogea pale walipo wakina Rahim.
"Karibuni Gu Ram taifa dogo lenye amani ndani yake." alisema Faraj huku akiachia tabasamu.
"Mtoto, kaa pembeni hatukuja kuongea na rika lenu hivyo kaa mbali kabda sijakubadilikia." alisema Rahim huku akimtazama Faraj, hakumtambua kuwa ni nani kwenye kijiji kile hali iliyomfanya Faraj atabasamu tu huku akitazama askari wote waliokusanyika pale.
Ilibidi Rahim awape ruhusa askari wake waendelee na zoezi lile lakini Faraji aliwazuia kwa kunyoosha mikono yake.
"Nawaomba sana muwaache watu na furaha yao, nimewakaribisha kwa hekima na heshima, siwafahamu nami hamnifahamu ila nimesimama hapa kushikilia amani. Mimi ndiye kiongozi wa taifa hili hivyo lengo la kufika kwenu hapa ni lazima mimi nifahamu maana ninyi ni wageni wangu." alisema Faraj na maneno yake yalimshangaza hata Rahim kuona mtoto mdogo kama huyo anaongea maneno ya kikubwa na yenye tija ndani yake.
"Yaani mtoto wewe ndio wakupe uongozi!unaongelea kuhusu kuwaongoza watu au kuwaongoza watoto wenzako?" aliongea Rahim akimdharau Faraj.
"Watoto pia ni watu ujue, ila kwamimi nawaongoza watoto pamoja na hao watu." alisema Faraj na majibu yake yalimchosha Rahim akawaruhusu askari wake wafanye kilichowaleta.
"Nimesema hakuna mtu kupita hapa, kama hamuwezi kueleza shida yenu geuzeni mrudi mlipotoka, siwezi kuruhusu watu waingie katika ardhi yangu bila kuwafahamu." Faraj alishikilia msimamo wake na safari hii alikuwa mkali sana. Rahim kuona vile akaona ni dharau kwa mtoto mdogo kuwazuia wakati wapo kazini, alitoa amri ya lazima askari wafanye kile alichowaagiza.
Safari hii hawakutaka kumsikiliza yule mtoto wakatoa mapanga yao na kuruhusu farasi waliwapanda kwenda mbele wammalize kwanza mtoto huyo ili wakavunje nyumba za watu.
ITAENDELEA...
Patashika inataka kuanza ndani ya kijiji cha Gu Ram, nini kitakachojiri? Tukutane siku ya Jumatatu baada ya mapumziko ya kesho ili tujue hatma ya mpambano huo.
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE (24)
