PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 24


 


SEHEMU YA 24


ILIPOISHIA..... 


Safari hii hawakutaka kumsikiliza yule mtoto wakatoa mapanga yao na kuruhusu farasi waliwapanda kwenda mbele wammalize kwanza mtoto huyo ili wakavunje nyumba za watu.


ENDELEA NAYO.... 


Faraj aliipiga fimbo yake chini kwa nguvu na kupata kuonekana moto ukitanda kama mpaka ili kuwazuia askari wale wasipite. Askari wote walishangaa kuona moto ule uliowafanya farasi wao wafurukute kurudi nyuma kuhofia kuungua. Rahim alibaki kushangaa pale alipo haelewi imekuwaje.


"Anatumia nguvu za kichawi!" alistaajabu Rahim baada ya kutambua mtoto yule anatumia nguvu za kichawi. Alihamaki kuona moto ule ukianza kutanda kuwazunguka na kujikuta wamewekwa kati na moto ule na kubaki kuhaha. Faraj aliwatazama tu na kuona jinsi ambavyo hawaamini kile wanachokiona.


Hasira zilimpanda Rahim kuona vijana wake wanaanza kuingiwa na woga, ilimbidi awape amri ya kusonga mbele zaidi na askari wale wakapata morali ya kwenda mbele. 


Waliwaamu farasi wao  wasöge mbele kuvuka moto ule, walitoka spidi ya hali ya juu hali iliyofanya Faraj autazame moto ule kwa macho makali sana ule moto ukazidi kuchochea mara mbili yake, hata farasi wale walipofika pale walijikuta wakisimama ghafla kuhofia kuungua na kufanya askari waliokuwa juu yao wadondoke mbele na kuuvaa moto ule askari wote. Wakaanza kupiga mayowe kuhitaji msaada maana nguo zao zimepamba moto. 


Iliwabidi wajitupe chini na kuanza kugaragara moto upate kuzima. Hali ile ilimfanya Rahim asiamini kile anachokiona mbele yake, alibaki ametulia juu ya farasi wake. Faraj alitazama taratibu akaanza kusogea alipo Rahim, aliuvuka moto ule bila hofu na kusogea hadi pale akizidi kumuaminisha Rahim uwezo alionao. Walibaki wakitazamana kwa muda kadhaa na Faraj akapata kumfahamu Rahim.


"Mtoto wa Mfalme Joha, nini kimekuleta pamoja na askari wako katika ardhi yangu?" aliuliza Faraj akimtazama Rahim.


"Nimemfuata Maya, namuhitaji hilo ndilo lengo langu mimi." alisema Rahim.


"Nani amekwambia kama Maya yupo hapa angali yeye ni binti wa Mfalme wa Eden."


"Mimi naamini tu yupo katika makazi haya, yupo... tena yupo na mlinzi wake Samir." aliongea Rahim akiwa anajiamini.


"Sawa hata kama wapo, imekuwaje awali ukawatuma askari wenu wamvamie Samir jioni ile na leo unakuja na askari wengine unasema unamtaka Maya wakati leo mmedhamiria kuwavamia watu kwenye makazi yao." alisema Faraj akiwa mwenye kujiamini sana. Rahim alinyamaza kutafuta la kusema na muda huo huo Maya pamoja na Samir ndio walikuwa wakifika eneo hilo na kukutana na hali ile askari wote wakiwa chini wanaugulia majeraha. 


Walikimbia haraka kusogea pale waliposimama Faraj pamoja na Rahim ambaye kitendo cha kuwaona tu wakina Maya alishtuka akiamini kweli wawili hao ni wazima.


"Faraj, vipi upo salama?" aliuliza Maya akiwa na wasiwasi.


"Mimi ni mzima kabisa, tumetembelewa na mtoto wa Mfalme Joha na amekuja hapa anasema anakuhitaji wewe, kuna mmepanga mkutane?" aliuliza Faraj na kumfanya Maya ageuke kumtazama Rahim, alimsogelea hadi pale alipokaa juu ya farasi wake.


"Nilishatangaza mbele ya wazazi wangu pamoja na wako kwamba sipo tayari kuolewa na wewe, na mtu niliyemchagua ni huyu hapa ambaye tumepewa adhabu ya kutelekezwa kwenye msitu wenye wanyama wakali. Nini kimekuleta tena hapa na umejuaje kama nipo hapa?" aliuliza Maya akionekana kuwa mkali juu ya swala hilo.


"Maya hebu nifikirie mimi japo mara moja, hakika nakupenda na ndio maana wazazi wetu kwa pamoja wamelipitisha na kulibariki swala hilo, hebu tazama maisha unayoishi huku, wewe sio mwanamke wa kuishi huku vijijini una heshima yako Eden. Tafadhari nikubalie turudi Eden nitamshawishi baba yako afute adhabu yako uwe ni mtu wa Eden." alisema Rahim akijaribu kumshawishi Maya.


"Naomba niongee kauli ya mwisho na sitopenda nirudie tena, Sipo tayari kuolewa na wewe , naomba uniache na maisha haya haya ninayoishi kwasasa." alisema Maya na kugeuka nyuma kuwataka waondoke. 


Faraj aligeuka na kuongoza njia huku wenzake wakimfuata.

Walimuacha Rahim aliwa anawatazama tu hadi walipotoweka, alipiga kelele kwa hasira zilizopo moyoni mwake huku moto ule ukianza kutulia taratibu. Aliwatazama askari wake na kuona wakiugulia maumivu huku wengine wakiungua sana mwilini. 


"Huyu mpumbavu Samir ndiye anayemfanya Maya anione si lolote." aliongea Rahim akionesha kuchukizwa na jambo hilo, aliona mtu anayemuwekea kizuwizi ni Samir hivyo lazima ammalize ili lengo lake litimie.

 

Baada ya muda kupita  Maya na wenzake walikaa mahala kujadili juu ya swala lile lililotokea.


"Huyu mtu sidhani kama ndio itakuwa mwisho wa kutufuatilia hapa, maana anaonekana kuwa upande wako Maya." aliongea Samir.


"Hata afanyaje sitaweza kukubaliana naye, siwezi." alikuwa kwenye msimamo mzito Maya.


 "Mimi nadhani anakuhitaji kwa maslahi yake binafsi na si upendo. Asingekuja na askari wote wale ni wazi kwamba alikuja kwa shari." alisema Faraj akimtazama Maya.


"Na taarifa kwamba sisi tupo hapa wamezipata wapi?" aliuliza Samir.


"Hapa mimi nina mashaka itakuwa kuna ambaye anawapa taarifa hizi." aliongea Maya na kuwafanya wenzake wahisi jambo hilo likawa kweli. Waliweka moyoni mwao kwamba kuna mtu anashirikiana na Rahim kwenye jambo hili. Iliwabidi wajitose kumnasa mtu huyo wanayemuhisi hivyo.


Tangu kuondoka kwa Maya ndani ya falme hakukuwa shwari hasa kwa upande wa Mama yake. Muda wote Malkia Rayat alikuwa kwenye mawazo tele juu ya mwanaye. Muda mwengine alidiriki hata kufikiria mbali kujitoa sadaka naye katika msitu ule maana Maya alikuwa ni muhimu sana katika maisha yake. Hali hiyo ya Malkia ilimfanya hata Mfalme Siddik kukosa raha. Aliichukia sheria ya adhabu ile ambayo imemgusa na kutoa furaha katika familia yake. Muda wote amekuwa akimtazama mkewe akiwa mwenye huzuni. Alinyanyuka na kuondoka sehemu hiyo ili asizidi kuumia kwa kile kilichotokea kwa binti yake anayedhaniwa tayari ameuawa kwa wanyama wakali kule msituni.


Kwa Jamal, ilikuwa ni kama amekosa kitu mwilini mwake baada ya kumkosa Maya, alifahamu ndio mwisho wa mipango yao waliyopanga ili kuipata Eden kupitia binti wa Mfalme. Alichoamua ni kutaka kuachana na uaskari ili arudi katika taifa lao kama mtoto wa Mfalme Faruk. Hakuona sababu ya kulitumikia jeshi la Eden wakati  mtu aliyemfanya awe askari hayupo tena na hatambuliki Eden.


Hadi kufika jioni ya siku hiyo kila mtu alionekana kutulia nje ya nyumba yake wakiwa makini kuhofia huenda wakaja majeshi mengi zaidi kuwavamia hivyo kila mmoja hakucheza mbali na kwake. Kwa Samir na Maya haikuwa hivyo na wala hawakuonesha kuwa na hofu hata kidogo. Walitoka ma kwenda mtoni kama ilivyo kawaida yao. 


Walipofika wakatafuta mahala na kuketi wakiongea mambo yao. Maya alipakumbuka nyumbani kwa akina Samir nchini Tanzania na kumtaka jioni ile waende kwa mara nyengine  na ni wazi kwamba amevutiwa na mazingira yale. Samir alitabasamu tu na hakuwa na jinsi akafanya vile alivyotaka Maya. Walikamatana mikono na sekunde chache tu wakapotea kabisa eneo lile. Walikuja kutokea chumbani kwa Amour hali iliyomfanya Maya atabasamu kuona wamerejea tena.


Alifarijika sana Maya kuwa pale, hata alipotazama nywele zake zilibadilika na kuwa fupi zenye kusukwa. Alibaki akicheka tu kicheko ambacho kilimfanya Amour amfumbe mdomo asije kusikika. Alimuacha mule chumbani na kutoka nje kuangalia usalama kwanza.


Alimuona shemeji yake akiwa jikoni anapika muda ule, taratibu akapiga hatua kusogea hadi pale na matani ya hapa na pale yakaendelea.


"Kaka yuko wapi?" aliuliza Amour akiwa amekamata kisu akikatakata nyanya kumsaidia shemeji yake aliyekuwa anakorogea uji wa ugali.


"Kwani amekwambia anarudi leo? Tangu jana si kaondoka kupeleka mzigo wake wa Mahindi Dar na hapa kurudi hadi kesho au keshokutwa si unajua kazi zao wakipata mzigo huko huko wanaunganisha kwenda mkoa mwengine." maneno yale yakamfanya Amour awe na amani baada ya kusikia hivyo kwamba kaka yake hayupo.


"Kwahiyo analala kwako leo?" aliuliza shemeji mtu na swali lake lilimshtua Amour, akajikuta anapatwa na kigugumizi.


"Nani?"


"Si nimemuona amerudi jioni hii akaingia geto kwako." alisema shemeji na kumfanya Amour atambue kumbe Maya anajulikana kufika kwake, alijichekesha tu pale ili jambo lile liishe.


"Ila shemeji angalia mtoto wa watu huyo usimharibu, wote mnasoma msijisahau mkaja kuleta aibu katika familia." aliongea Shemeji maneno ya busara kumweleza Amour. Aliyaelewa maneno yale na kuendelea kusaidiana kupika.


Hata baada ya muda walipoivisha aliandaa chakula na kumpa Amour akale na mwenza wake jambo ambalo lilimfanya Amour apate kufurahi kwa kupata shemeji mwenye upendo kwake. 

Alipoingia chumbani akamkuta Maya kashabadilisha nguo na kujifunga taulo lililopo mule ndani. Taratibu Maya alimsogelea Amour na kumpokea chakula kile akionesha kuwa mchangamfu hata Amour akashangaa. 


Alitabasamu tu na kusogea hadi pale Maya alipoweka chakula kile na baada ya kunawishana mikono wakaanza kula. Hakuwa mwenye kuchagua chakula Maya, alikula chakula kile bila kujali kama ndio kwa mara ya kwanza kula chakula hicho, alijua fika hata siku za mbele atakuwa akija huku hivyo chakula kitakuwa ni hicho. 


"Usiku umeingia huu." aliongea Maya akiwa anapeleka tonge mdomoni.


"Kwahiyo.."


"Hatutaweza kurudi Gu Ram kwa muda huu, tutalala tu hapa hapa." aliongea Maya akiwa mwenye kujiamini, Amour alitabasamu kwa kusikia maneno yale na kwakuwa ni wapenzi hapakuwa na shaka juu ya uamuzi aliouchukua Maya. 


Asubuhi na mapema Rahim alikuwa anaongea na baba yake baada ya kupata kifungua kinywa.


"Sasa umeamua vipi baada ya kutambua hilo?" aliuliza Mfalme Joha akimtazama mwanaye aliyeonekana kutokuwa na furaha usoni mwake.


"Bado naamini nina nafasi ya kuwa naye, hapa ninapoongea nikitoka naenda Eden."


"Eden? Kufanya nini tena Eden?"


"Nakwenda kukutana na Mfalme Siddik, nimueleze ukweli kwamba Maya na yule mlinzi wake wapo kwenye kijiji kile hawajafa. Nadhani kwa kufanya hivyo kutanipa nafasi kwa Mfalme akanifikiria tena, bado sijafeli baba niamini." aliongea Rahim kwa kujiamini sana huku akimtazama baba yake.


ITAENDELEA.... 


Je! Mfalme Siddik atachukua maamuzi gani atakapopata taarifa za uwepo wa mtoto wake ambae alijua tayari ameshafariki? Tukutane kesho.

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO (25)

Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group