SEHEMU YA 25
ILIPOISHIA.....
"Nakwenda kukutana na Mfalme Siddik, nimueleze ukweli kwamba Maya na yule mlinzi wake wapo kwenye kijiji kile hawajafa. Nadhani kwa kufanya hivyo kutanipa nafasi kwa Mfalme akanifikiria tena, bado sijafeli baba niamini." aliongea Rahim kwa kujiamini sana huku akimtazama baba yake.
ENDELEA NAYO......
Asubuhi ya siku iliyofuata Amour alipata kuamka pale kitandani huku akimtazama Maya aliyelala naye usiku wa jana. Ajabu hakuweza kumuona pale kitandani hali iliyomfanya ashtuke. Alikurupuka pale kitandani na kuanza kutazama huku na kule bila mafanikio. Ilimbidi anyanyuke na kuelekea nje kumtazama.
Moyo wake ulipata kutulia baada ya kumuona Maya akiwa jikoni pamoja na shemeji akimfundisha kumenya viazi. Amour alibaki kutabasamu kwa kuona mara ya kwanza binti wa Mfalme anafanya kazi, aligeuka na kurudi zake ndani na sekunde kadhaa kupita akatokea Nadhra mule chumbani, taratibu akasogea na kukaa kitandani alipo Amour.
"Umekuwa adimu Nadhra siku hizi." aliongea Amour akimtazama Nadhra.
"Kuna jambo lilitokea na nikaamua kulifanya bila ya kukushirikisha, na imepelekea hata kuwa kimya kuja kukutembelea." alisema Nadhra akionekana kun'gaa kwa uzuri alionao.
"Jambo gani limetokea hadi ushindwe kuniambia.?" aliuliza Amour na kuona akishikwa mkono.
"Amour naomba unisamehe kwanza kwa kufanya maamuzi bila kukushirikisha, mimi sio tena Nadhra yule uliyekuwa unamfahamu, nimemfuata baba yangu kule alipokwenda lakini nikijuwa fika kwamba nimekuacha ukitekeleza kile kilichopangwa. Lengo hasa la kupata uwezo ulionao ni kuhakikisha unaivunja mila na desturi za Eden juu ya watu wenye uwezo wa nguvu kama zetu. Wewe ndiye wa kuibadilisha Eden kuwa mpya. Mataifa mengi wanaitamani Eden kwa kitu kimoja tu." alisema Nadhra.
"Kitu gani hicho? Na kwanini watu wengi wanaifuatilia Eden?" aliuliza Amour akimtazama Nadhra.
"Ni Pete ya Mfalme wa Eden. Na endapo akaipata mtu yeyote pete hiyo basi hakuna yeyote wa kumpindua kwa namna yeyote ile, na mtu huyo ndio atakuwa Mfalme wa taifa hilo la Eden." alisema Nadhra na maneno yakamshangaza Amour.
"Inamaana pete hii niliyonayo ni tofauti na hiyo inayosakwa na watu.?"
"Pete hii uliyonayo ni mara kumi ya pete hiyo inayotamaniwa na kila mtu aipate. Inauwezo mkubwa sana na ndio pete iliyojazwa nguvu zote za wafalme wa Eden waliopita." alisema Nadhra na maneno yake yakamuingia Jafari akapata kuelewa.
"Nimejitoa sadaka kwa ajili yako Amour ili ufanye kazi hiyo, mimi naamini utafikia lengo japo kuna changamoto nyingi utakumbana nazo ila yakupasa kuvumilia na kusonga mbele. Pete uliyonayo haina kazi tena kwasasa maana unaingia kwenye mtihani wa kuipata pete ya Mfalme wa Eden, pete hiyo inatafutwa na watu wengi hivyo yakupasa uwe makini katika maisha yako." alisema Nadhra na maneno yake yakamshtua Amour.
"Inamaana... inamaana sitakuwa na uwezo wa kufanya lolote tena? Sasa itakuwaje kama haitafanya kazi angali sisi tupo huku.?"
"Na ndio maana nimekwambia nimejitoa mimi ili kazi hii uifanye wewe maana tayari umetengeneza mazingira ya kujulikana Eden, nitakupa nguvu na uwezo nilionao mimi utakuwa unatumia ukiwa unapigania kuitafuta pete hiyo." alisema Nadhra.
"Nadhra, inamaana umejitoa kwaajili yangu?" aliongea Amour kwa sauti ya huruma lakini haikumfanya Nadhra abadili maamuzi yake. Palepale alinyanyuka huku akimtazama Amour, alinyanyua mikono yake kushika kichwa cha Amour huku akiongea maneno ambayo hayakuweza kueleweka kwa haraka. Ghafla tu mwili wake ukaanza kutoa moshi mweusi kila sehemu huku Amour nuru ikianza kummurika kichwani na kujikuta akiyafumba macho akihisi kuna vitu vinaingia mwilini kwa kasi sana na muda huo huo hali ikaanza kubadilika mwilini mwake, kizunguzungu kilianza kumzonga na kushindwa kupata hata nguvu ya kuendelea kukaa pale, taratibu akaanza kuregea mwili na sekunde kadhaa mbele akadondokea kitandani na kupoteza fahamu.
Baada ya muda kupita Rahim ndio alikuwa akiwasili Eden akiwa na askari wawili tu waliomsindikiza moja kwa moja wakaaza kuelekea katika falme ili apate kukutana na Mfalme. Taarifa za kuwasili Rahim ndani ya mji wa Eden zilimfikia Mfalme Siddik pamoja na Malkia wakiwa wanatoka kupata kifungua kinywa. Iliwabidi waelekee ukumbini kukaa kusubiri ugeni huo uweze kufika huku wakiwa na maswali imekuwaje mtoto wa Mfalme aweze kurejea mwenyewe. Muda mfupi Rahim aliweza kuwasili na wale askari waliomsindikiza, alikaribishwa kwa heshma kubwa na kupelekwa hadi pale ukumbini ambapo alipata kuwaona viongozi wa taifa hilo wakiwa wametulia.
Alitoa heshima kama ilivyoada na kufanya viongozi hao wampokee na kumkaribisha akapata kukaa.
Waliongea mambo mengi ya kimaendeleo na mwishowe Rahim ikambidi aeleze kilichomleta.
"Nimeona nije asubuhi na mapema kuja kuwaeleza jambo, nafahamu mmekuwa na shauku za kufahamu kwanini nimerejea tena mapema hivi. Upendo wangu kwa binti yenu hauwezi kufutika japo ameelekeza hisia zake kwa mlinzi wake, hata siku ambayo wanatolewa ndani ya Eden kupelekwa kwenye msitu ule sikuwa nyuma kuhakikisha kama ni kweli Maya niliyempenda anakwenda kuachwa msituni." aliongea Rahim huku akiwatazama wawili hao.
"Ah Rahim, hayo yamepita hatupaswi kuyaongelea tena, ilikuwa ni adhabu ilikuwepo toka enzi na enzi hivyo haitapendeza kukumbushia maana hata sisi inatuuma." alisema Mfalme Siddik kwa sauti ya upole akionesha kweli kuumizwa na jambo lile.
"Askari wenu wameifanya kazi ile kwa ufasaha kuhakikisha wanawaacha kwenye ule msitu, ila walipoondoka huku nyuma haikujulikana imekuwaje ila nimepata taarifa kutoka kwa askari wangu kuwa Maya pamoja na Samir wapo kwenye kijiji cha Gu Ram wanaishi huko." maneno yale yalimshtua Malkia Rayat akajikuta akisimama pale alipo.
"Unasema!!.. Inamaana Maya wangu bado anaishi?" aliuliza Malkia akiwa mwenye kutetemeka baada ya kusikia hivyo.
Upande wa pili Jamal alimfuata Generali mkuu akiwa kwenye ofisi yake. Alimpa heshima kama mkubwa wake wa majeshi akakaribishwa kukaa.
"Hapana mimi si mkaaji sana, nimekuja kwako kukupa taarifa moja tu na nimeamua kutoka moyoni mwangu." alisema Jamal akiwa anajiamini lengo ni kumweleza Generali kuhusu kuacha uaskari na kurudi katika taifa lao.
"Eh jambo gani hilo Jamal ambalo unataka kuniambia?" aliuliza Generali huku akimtazama Jamal, alitazama chini na mwishowe akanyanyua uso wake kuongea.
Muda huo huo akaingia askari mmoja bila kubisha hodi na moja kwa moja akatoa saluti kwa Generari.
"Generali kuna taarifa imefika kwa Mfalme muda huu kwamba binti wa Mfalme Maya pamoja na Samir bado ni wazima na wamekutwa wakiishi katika kijiji cha Gu Ram." aliongea askari yule na maneno yale yakamsimamisha Generali kwa mshangao. Aligeuka kumtazama Jamal ambaye naye alibaki kushangaa baada ya kusikia taarifa hiyo.
"Unasemaje? Bado wanaishi?" ni maswali mfulilizo yakimtoka kinywani Jamal akiwa haamini kinachoelezwa pale.
"Ndio, na hapa nimeagizwa na Mfalme nimuite Generali." alisema yule askari akaeleweka. Hakutaka kuchelewa Generali akaanza safari ya kuelekea kwa Mfalme kumsikiliza huku nyuma akifuatwa na askari yule.
Jamal alibaki akishangaa baada ya kusikia kama Maya na Samir ni wazima hali ya kuwa waliachwa kwenye msitu ule wa wanyama wakali. Alijikuta akiuziba mdomo kumaanisha kile alichokuwa anataka kumweleza Generali amekifuta baada ya kujua Maya yumzima hivyo nafasi anayohitaji bado ipo. Haraka naye akatoka mule ndani kwenda kusikiliza kinachozungumzwa kwa Mfalme.
"Kama Maya ni mzima basi nami nitaondoka nikaishi naye, nampenda mwanangu sitakubali niwe mbali naye safari hii." alisema Malkia Rayat akiwa amesimama na mwenye shauku ya kutaka kumuona mtoto wake.
"Unamaana gani kusema hivyo?" aliuliza Mfalme akimtazama mkewe.
"Tambua hilo tu kwamba sitaweza kuendelea kumfikiria mwanangu, nimekuwa sina raha kwa kujua tayari nimempoteza mwanangu lakini kama ni mzima sitaweza kukubali niwe mpweke kiasi hiki tena." aliongea Malkia akionesha kuwa na msimamo wa kile alichoamua.
Muda huo huo akafika Generali na kumsogelea Mfalme kwa kumpa heshima na kusimama kumsikiliza.
"Bila shaka taarifa umeipata kuhusu binti yangu."
"Nimeisikia Mfalme japo imenishangaza sana, niombe samahani kwa niaba ya askari wangu nadhani wao ndio wamefanya makosa kutokuwa makini juu ya swala hilo." alisema Generali kwa upole akiwaombea msamaha askari wake.
"Kwa taarifa zilizofika nimepata kutambua askari hawana kosa lolote juu ya swala hilo. Mtu pekee ninayemuhisi ni Samir, huyu naomba achunguzwe kwa umakini sana huenda akawa ana nguvu tofauti na binadamu wengine." alisema Mfalme Siddik na kauli yake ikawashtua watu wote waliopo mahala pale.
"Mh Mfalme, kitu gani kimekufanya uamini hayo unayosema?" aliuliza Generali baada ya kutoamini kile alichokizungumza Mfalme dhidi ya Samir.
"Tangu kuumwa kwa Maya hadi Malkia kuamua kwenda Mashariki na mbali, ni Samir ndiye aliyewahi kufika kule na kuweza kumzuia Malkia, nilikaa nikifikiria alifika muda gani kule angali sisi tumetumia siku mbili bila kulala njiani na ajabu hata hatukufika tumekutana nao njiani wakirejea. Samir siku zote ni mzembe wa kupitiliza amepata wapi ujasiri na nguvu za kupambana uwanjani hadi kuibuka kuwa mshindi. Na tukio hili ndilo linanifanya niamini haya yote kwamba huyu kuna nguvu za kichawi anazitumia." aliongea Mfalme na kila mtu akaanza kuhisi huenda kinacho zungumzwa ni cha kweli.
"Kwahiyo unataka tufanye jambo gani kwa Maya na Samir?" aliuliza Generali huku Rahim akiwa makini kusikiliza.
"Natoa amri kama Mfalme hawa watu waletwe hapa mara moja, ukweli utapatikana hapa hapa na sheria ifuatwe" alisema Mfalme akitoa amri na kuvunja amri ile ya wawili wake kutokanyaga tena Eden.
Haraka Generali akapokea oda ile na kuwaanda askari wake akiongozana na Jamal kuelekea kwenye kijiji cha Gu Ram.
"Nimeamini kweli huna mapenzi na binti yako, pia huna hata shukrani kwa msaada alioutoa Samir dhidi ya Maya. Hata kama anatumia nguvu za kichawi ila katumia kumuokoa binti yako, hivi bila ya Samir wewe si ungekuwa raia wa kawaida tu Eden ingetawaliwa na Dalfa!." alisema Malkia akionesha kukasirika sana kwa maamuzi aliyoyachukua Mfalme.
Hakutaka kuendelea kukaa pale alitoka nje na yeye akapanda kwenye farasi wake kwenda kumuona mwanaye katika kijiji hicho cha Gu Ram. Mfalme alibaki kusimama akishuhudia mkewe akiondoka. Rahim alikuwa pembeni akitabasamu tu na kujua lazima sheria ya Eden itamuadhibu Samir kwa kujulikana kwamba anatumia uchawi, ni wazi kwamba lazima anyongwe mpaka kufa.
Baada ya muda kupita Amour aliweza kufumbua macho yake
pale kitandani. Tangu alipopoteza fahamu muda ule alivyokuja Nadhra hakuweza kuelewa ilikuwaje na nini kilitokea muda ule. Moja kwa moja akatoka mule chumbani na kuelekea sebuleni kutazama kalenda iliyoko ukutani. Alishusha pumzi baada ya kutambua ilikuwa ni bado ni siku ile ile ya Jumapili. Fikra zilimfanya ahisi huenda jambo lile alilofanyiwa na Nadhra limechukua siku kadhaa. Alisogea na kukaa kwenye kiti akitafakari ilivyokuwa. Alitazama vidole vyake na kuona bado pete ile ipo kidoleni. Alinyanyua mkono wake na kutazama ile pete lengo ni kutaka kujua kama kweli haina kazi kwasasa. Punde tu akatokea shemeji akiwa ameshika chupa ya chai.
"Mkeo yupo shapu kweli katika kazi sema anaonekana kwao in mtu wa kupikiwa maana hana hata anachojua kwenye kupika." alisema Shemeji huku akiweka chupa ile mezani. Amour aliachia tabasamu baada ya kuambiwa hivyo. Ni wazi kwamba Maya hakuna anachojua maana ametoka kwenye familia ya kifalme. Kuna muda alitamani amueleze shemeji yake lakini nafsi inasita na kulifanya ni kama siri ya wao pekee.
Huku kwa Faraj tangu siku ya jana alikuwa akiwatafuta Maya pamoja na Samir maana walipotea ghafla tena bila hata kuaga wanapoelekea. Lakini kadiri muda ulipozidi kwenda akapata kutambua huenda Samir amemueleza ukweli Maya wapi alipotokea na ikamfanya amuoneshe ili apate kuamini. Kidogo hofu na mashaka juu yao yakapungua maana alihisi wamepata tatizo ndani ya Gu Ram.
Baada ya muda kupita kikosi cha askari wa Eden kilikuwa kinakaribia katika kijiji cha Gu Ram. Generali alikuwa mstari wa mbele akiwaongoza vijana wake. Pembeni alikuwa Jamal akionekana kuwa makini katika kazi hiyo wanayokwenda kuifanya. Malkia Rayat alikuwa nyuma sana hadi kuweza kuwafikia lengo ni kutaka kumuona binti yake baada ya kupata taarifa kwamba yupo hai. Huku kwa Amour baada ya muda kwenda aliona ni wakati wao kurejea Gu Ram maana lengo la kurudi kwao ni kumuonesha Maya mahala alipotokea. Ilimbidi amweleze Maya ili wapate kurejea Gu Ram maana tangu waondoka hawakuweza kuwasiliana na mwenyeji wao Faraj.
ITAENDELEA.......
General na Jamal ndio wanaingia Gu Ram na wakati huo huo Samir na Maya nao wanajiandaa kurudi Gu Ram. Je! Nini kitakachoendelea wakati lengo la General ni kuja kuwachukua na kuwarejesha Eden ili Samir akanyongwe?
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA (26)
