PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 26


 SEHEMU YA 26


ILIPOISHIA..... 


Huku kwa Amour baada ya muda kwenda aliona ni wakati wao kurejea Gu Ram maana lengo la kurudi kwao ni kumuonesha Maya mahala alipotokea. Ilimbidi amweleze Maya ili wapate kurejea Gu Ram maana tangu waondoka hawakuweza kuwasiliana na mwenyeji wao Faraj.


ENDELEA NAYO...... 


Generali alifanikiwa kuwasili katika kijiji hicho akiwa na askari wake. Watu waliokuwa njiani waliweza kuwaona na kuwatambua kwa mavazi yao kwamba ni askari wa taifa la Eden. Kwa heshma ya taifa hilo wananchi wakawa wanainamisha nyuso zao chini kuwapisha askari hao wapite. Moja kwa moja Generali na watu wake wakaelekea kwenye nyumba ya Kiongozi wa kijiji hicho maana ni miaka mingi hakuweza kufika kijijini hapo. Wananchi nao wakawa wanafuata nyuma kwenda kushuhudia nini sababu za ujio huo wa askari wa Eden. 


Muda wote huo Faraj alikuwa nje ya eneo lake amekaa akiangalia mandhari ya hapo, alishapata kutambua kuwa kuna ugeni uliofika katika kijiji chake na muda mfupi waliwasili pale katika nyumba ya kiongozi wa kijiji hicho. Askari walitanda kila kona ya eneo lile kuweka ulinzi kama waliowafuata wamo ndani wasipate kuwatoroka. Faraj alisimama kutoka pale alipokaa akiwatazama askari wale, Generali alishuka kutoka kwenye farasi wake bada ya kusimama kisha akaanza kumsogelea Faraj pale alipo akiwa hamfahamu. Alisimama kwa sekunde kama ishirini wakitazamana wenyewe bila yeyote kuongea.


"Inamaana hufahamu jeshi hili linatokea Taifa gani hadi usitoe heshima?" aliongea Generali akimtazama Faraj akionekana mtoto bado.


"Laiti angesimama mbele yangu Mfalme wa Eden au Malkia ningefanya hivyo japo kwa kuamua pia." alisema Faraj.


"Hata hivyo unadhani nalingana na wewe?"


"Huenda ukawa na umri mkubwa lakini usipate kubarikiwa upeo na heshima. Huenda umri  wangu ndio ukakufanya uwe na kiburi cha kutosalimia. Wewe ni mgeni katika ardhi yangu unapaswa ujitambulishe baada ya salamu na si mimi nianze kukusalimu." alisema Faraj akiwafanya hata askari waliokuwa pembeni akiwemo Jamal waone ni maneno yenye dharau kwa Generali wao. Wakataka kusogea pale kumkamata lakini Generali akanyanyua mkono kuwataka waache.


Alibaki kutabasamu tu huku akimtazama Faraj.


"Unataka kunambia wewe ndio kiongozi wa hapa?" aliuliza General na jibu alilopata ikabidi astaajabu maana hakumtegemea kama anaweza kuwa kiongozi kwa umri ule. Baada ya kufahamu hilo ilimbidi arudi kwenye kile kilichowaleta.


"Bila shaka unafahamu ujio wa watu wawili katika kijiji chako, binti wa Mfalme pamoja na mlinzi wake wapo humu. Tusingependa sisi tutumie nguvu kulikamilisha hili, tunahitaji kwa busara zako uwaamuru watoke Mfalme Siddik anawahitaji mara moja." alisema Generali na kumfanya Faraj atabasamu kusikia hivyo. Aligeuka kumtazama Jamal pamoja na askari wengine kisha akarudi kumtazama Generali.


"Ninavyofahamu mtu akifukuzwa kwenye mji kamwe hawezi tena kurejea mahala alipofukuzwa, taarifa za kuachwa kwenye msitu watu hao wawili nilizipata  na kujua tayari watu hao wameshaliwa na wanyama wa msituni. Imekuwaje mnawatafuta watu ambao mmewasindikiza hadi msituni mkawaacha huko mkijua watakufa?" alisema Faraj kwa sauti kubwa yenye kujiamini. 


Generali alibaki kumtazama tu kwa kuguswa na maneno yale. Baadhi ya wanakijiji walistaajabu kusikia swala hilo maana hawakuwa wanafahamu sababu za Samir na Maya kurejea katika kijiji chao. 


"Amri ya Mfalme ifuatwe popote pale bila kipingamizi, hivyo unapoombwa kwa upole ujue unaepushwa na vurugu katika eneo hili, shida yetu ni hao watu wawili waamue watoke ili mahala hapa pawe salama." alisema Generali akiwa anamaanisha kile anachokisema.


"Sijawakaza kuingia ili muangalie, ila naongea kwa amani tu hao watu hawapo hapa."


"Wamekwenda wapi?"


"Sifahamu hata mimi." jibu hilo halikumfanya aamini kinachozungumzwa pale Generali, alitoa amri ya askari wake waingie mule ndani kupekua na askari wakafanya hivyo huku wengine wakiwa nje kuweka ulinzi. Watu wakabaki kuongea chinichini tu kila mtu akisema la kwake kwa kile kinachoendelea pale. Askari mule ndani walipekua kila sehemu bila mafanikio takribani dakika kumi nzima. Mwishowe walitoka nje na kumueleza Generali kwamba hakuna mtu yeyote ndani. Aligeuka kumtazama tena Faraj aliyekuwa hana shaka. 


"Wameenda wapi wawili hawa?" aliuliza kwa mara nyengine huku safari hii hakuonesha kuwa na furaha hata kidogo.


"Laiti ningelijua walipo basi ningeliwaambia tangu awali, lakini ninachoongea hamkiamini mnachokitaka ni nini kwangu?" alisema Faraj akiwa anamtazama Generali.


"Nadhani hunifahamu ndio maana unanichezea akili... Mkamateni haraka!" alitoa amri hiyo na mara moja askari wawili wakasogea pale na kumkamata  mikono Faraj, hakuwa mwenye kupepesuka wala kuhofia jambo. Alibaki kumtazama tu Generali pale aliposimama.


"Mnafanya makosa kuja katika ardhi yangu na kunifanya hivi mbele ya watu wangu. Mnapoelezwa ukweli jaribuni kuwa waelewa ili mpate kusaidiwa." aliongea Faraj kwa busara na upole.


"Kipi cha ukweli unachokiongea hapa, unataka kusema hawa watu hawakufika hapa?... Eti nyie watu hamkuwaona binti wa Mfalme wa Eden pamoja na mlinzi wake?" aliuliza Generali kwa ukali lakini hakuweza kujibiwa na raia yeyote pale. Kwa hasira alizonazo na kujua kwamba anadharauliwa na watu wote pale, alitoa upanga wake na kumuwekea Faraj shingoni mwake lengo ni kufanya kile alichokusudia. 


Watu walishtuka kuona hivyo na kuwatia hofu huenda kiongozi wao akadhurika. Wakawa wanaanzisha zogo kutaka kiongozi wao aachilie, iliwabidi Jamal na askari wengine wawazuie raia ambao walikuwa wanakuja juu. Faraj alikuwa anatazama tu kinachoendelea hali iliyomfanya ahisi huenda kikamtokea kitu kibaya maana amewekewa upanga shingoni. 


Aliikamata bakora yake vyema ili apate kujitoa mikononi mwa askari wale waliomkamata. 


"Muacheni mara moja!" ilisikika sauti iliyowafanya watu wote wageuke kutazama ilipotokea. Kila moja aliinamisha sura chini baada ya kumuona Malkia Rayat akisogea mahala pale. Ilimlazimu Generali atii kile alichosema Malkia, aliutoa upanga wake na askari wake wakamwacha Faraj alikuwa anataka kujitetea muda ule. Malkia alisogea hadi pale na kuwataka askari warudi nyuma kumuacha Faraj peke yake. Alionekana kuwa mwenye huruma na kujali utu, jambo hilo lilijidhihirisha pale alipoinama kupiga magoti huku akimshika Faraj mkono.


"Bila shaka wewe ndiye unayeongoza watu wa Gu Ram, ni kiongozi wa kijiji hiki." aliongea Malkia huku akionesha tabasamu usoni mwake.

Faraj alitabasamu huku akimtazama Malkia usoni mwake.


"Mimi ndiye, Gu Ram ndio ninayo iongoza kwasasa." alisema Faraj kwa sauti ya upole.


"Samahani kwa hiki ninachotaka kuuliza kwako, ni kweli Maya yuhai?" aliuliza Malkia huku akiwa amemshika mkono Faraj.


"Si Maya tu hata Samir ni mzima pia." maneno yale yakamfanya Malkia afurahi sana, alizidi kumsogelea Faraj.


"Naweza kuwaona hata mara moja?"


"Kiukweli hawapo kwasasa, ila huenda wakarejea hapo baadae maana sifahamu hata walipoelekea." alisema Faraj.


"Ila wanaishi hapa kwenye mji wako?"


"Ndio, na maamini watarejea hapa hapa." alisema Faraj na kushuhudia Malkia akinyanyuka haraka na kugeuka kumtazama Generali.


"Hamtaweza kuwapata kwa muda huu, nimeongea na mwenye mji huu amewataka muondoke mrudi Eden, wakirejea ataongozana nao kuwakabidhisha kwa Mfalme. Hampaswi tena kuendelea kukaa hapa." alisema Malkia kumuamuru Generali aondoke na askari wake.


"Lakini Malkia hii ni amri ya Mfalme ameitoa turudi na hawa watu hataweza kutuelewa tukirejea mikono mitupu." alisema Generali.


"Na mimi ndio nimesema mrudi huyu atawaleta nami nikiwemo, amini hilo." alisema Malkia na kumfanya Generali awe na mashaka katika kuchukua maamuzi. 


Lakini mwishowe akaelewa yaliyoongelewa na Malkia, aliwaamuru askari wake waondoke. Jamal alikuwa na wasiwasi kwa kile alichokiamua Malkia na kuhisi huenda anataka kuwageuka, hata walipofika njiani ilimbidi amueleweshe Generali kuwa wanapaswa kuwa makini katika  swala hilo. Waliamua kurejea Eden kwakuwa Malkia ndiye aliyetamka maneno yale na hawakuweza kumpinga.


Huku nyuma Faraj alimkaribisha Malkia huku wananchi wakianza kuondoka eneo lile baada ya kuona amani imerejea.

Walikaa na kuongea mambo mengi pale nje wakivuta muda kuwasubiri wakina Maya kama watarudi.


"Nimepata faraja kusikia mwanangu na Samir bado wanaishi. Nilikata tamaa na kujua sina tena mtoto katika dunia hii. Sitakubali nimpoteze tena Maya nimejua kuumia pindi alipoondoka Eden." alisema Malkia akionesha kuwa na shauku ya kumwona mwanaye. Faraj alibaki kumtazama tu huku akiwa mwenye kutabasamu.


Muda mchache tu walipata kuonekana Maya na Samir wakiwa wameshikana mikono kwa furaha. Wanakijiji walipata kuwaona wakawa wanawafuata kutaka kufahamu walikuwa wapi muda wote. Hali ile iliwatia mashaka wawili hao na kuhisi huenda kuna jambo limetokea maana si kawaida kwa  watu kuwa na wasiwasi kiasi hicho. Hawakutaka kuongea lolote hadi walipofika kwa Faraj. 


Macho ya Maya yaligongana na ya mama yake na kila mmoja wapo akawa mwenye kushangaa. Alinyanyuka pale alipo Malkia na kuanza kumkimbilia mwanaye ambaye naye alikuwa mwenye furaha sana na kujikuta wakikumbatiana muda ule. Samir alitabasamu huku akitoa heshima kwa Malkia wake.


Iliwabidi watulie mahala waongee Maya pamoja na Malkia huku Faraj akiongozana na Samir kuelekea nje kidogo ya mahala pale.


"Niwie radhi kwa kile kilichotokea sikuweza kukwambia maana ilikuwa ni ghafla tu safari yenyewe. Na sikupanga kama tutakaa muda mrefu huko maana Maya ndio ameniomba tubaki." alisema Samir wakiwa wanatembea.


"Sikuwa na hofu sana baada ya kufahamu Maya yupo mikononi mwako, kama wote ni wazima basi ni jambo jema." alisema Faraj na kumfanya Samir amtazame.


"Nimeonana na Nadhra leo." alisema Samir na maneno yale yakamfanya Faraj asimame. Alimgeukia Samir aliyekuwa naye anamtazama.


"Amekuambia nini dada yngu? Na yupo wapi kwasasa?" ni maswali yaliyomfanya Samir atafute namna ya kujibu.


Upande wa pili Malkia alikuwa anaelezwa na binti yake hali halisi ilivyokuwa pindi walipotupwa kwenye msitu ule hadi sasa wapo hai. Ilimfanya ashtuke kupata ukweli wa mambo baada ya kuambiwa uwezo alionao Samir.


"In amaana Samir anatumia nguvu za kichawi?" aliuliza Malkia akiwa haamini kile alichosikia.


"Nguvu zake ni sawa na alizonazo Faraj, hawa watu si wabaya na wanatumia uwezo walionao kusaidia watu." alisema Maya akijaribu kuwatetea.


"Umeamini vipi kama ni wema kwako? Huenda wakawa wanakuzunguka wakipanga kukufanyia jambo baya."


"Nawaamini sana na sio watu wabaya kwangu. Mama.. Labda nikwambie tu ukweli usioujua, huyu si Samir unayemfahamu wewe, huyu ni mtu kutoka taifa lengine kabisa na nimepata kwenda huko na ndio tumetoka huko muda huu. Yote aliyonifanyia ndio nimeamini kuwa huyu ni mtu sahihi kwangu, yeye ndio alinisaidia kipindi mnahangaika kwenda kwa Dalfa ili nipate kupona, yeye ndio alikuzuia wewe usikubaliane na mikataba ile ya Dalfa. Hayo tu ni matukio yanayodhihirisha kwamba si wote wenye kutumia nguvu hizi ni wabaya. Ufalme umeshikilia sheria ambazo zinawaumiza hawa watu, unadhani angekuwa mbaya angekukataza kuiuza Eden mikononi mwa Dalfa! Ndio maana nimekuwa na amani ya kuishi hapa Gu Ram najua kuna amani na usalama kwangu, sijafikiria kujuta kuondoka Eden hata mara moja." alisema Maya akionesha kuwa na furaha. Malkia hakuamini kuambiwa kama ni Samir ndiye aliyefanya yote hayo. Alielezwa mengi kuhusu wema wa mtu huyo huku akilazimishwa aamini kwamba si wote walio na nguvu hizo wanatumia uchawi.


Upande wa pili Generali na askari wake waliweza kuwasili Eden, moja kwa moja akaelekea kwa Mfalme ambaye  alikuwa pamoja na Rahim hadi muda huo. Kitendo cha Generaki kuja mikono mitupu kilimshtua Mfalme hadi akanyanyuka pale aliposimama.


"Vipi! Kuna nini kimetokea.?" alikuwa na shauku kubwa ya kufahamu kilichojiri.


"Tumeweza kufika hadi kwenye kijiji kile na tukambana Kiongozi wa pale aweze kunieleza wapi walipo Maya na Samir lakini Malkia akaingilia kati kutaka tumuache. Na ni yeye pekee ndio aliyeongea na yule kiongozi na kuelezwa. Alitoa amri kwamba turudi ili watakaporejea wawili hao atarudi nao hadi kwako wa kukabidhi." alisema Generali kwa upole.


"Akhh.. Malkia  mbona ananiingilia katika maamuzi yangu sana! Inamaana yeye pia amebaki huko?" aliuliza Mfalme na Generali akamjibu sawiya.


Aliyakumbuka maneno ya mkewe huyo kwamba hawezi kunyamaza angali anafahamu mwanaye bado yupo hai. Kauli hiyo ilimpa mashaka na kuona huenda kuondoka kwake ndio safari ya moja kwa moja. Hakutaka yatokee hayo yote kwa kuikosa familia yake yote, alimuamuru Generali waongozane wote pamoja na askari kurudi tena Gu Ram ili apate kurejea nao watu anao wahitaji.  


Muda huo Jamal alikuwa mahali akiwa na Lutfiya akimueleza hali halisi ilivyokuwa. Kidogo wakapata kuona kuna matumaini tena ya kumpata  Maya. Walichofanya ni kumtumia ujumbe Mfalme Faruk  kumueleza hali halisi. Walichukua njiwa na kutuma ujumbe huo mara moja wapate kufanya jambo.


Ujumbe kupitia njiwa yule uliweza kumfikia Mfalme Faruk na baada ya kuelewa kilichoandikwa ndani yake hakutaka kupoteza muda alitoa amri ya askari wengi sana kuwahi kwenye kijiji kile kabla Mfalme na jeshi lake hawajafika. Huku Jamal naye alijichanganya na askari wenzake wakiongozana na Mfalme kuelekea Gu Ram.


ITAENDELEA..... 


Jeshi la Mfalme Faruk lipo njiani kuja kummaliza Samir na kumchukua Maya, na huku Mfalme Siddik yupo njiani kuja kuwachukua Samir, Maya na mkewe. Nini kitakachotokea? Mambo ni 🔥


GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA (27)


Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group