SEHEMU YA 27
ILIPOISHIA.....
Ujumbe kupitia njiwa yule uliweza kumfikia Mfalme Faruk na baada ya kuelewa kilichoandikwa ndani yake hakutaka kupoteza muda alitoa amri ya askari wengi sana kuwahi kwenye kijiji kile kabla Mfalme na jeshi lake hawajafika. Huku Jamal naye alijichanganya na askari wenzake wakiongozana na Mfalme kuelekea Gu Ram.
ENDELEA NAYO......
Baada ya muda kadhaa Malkia Rayat alikaa na Samir wakiongea mambo kadhaa. Hapakuwa na siri tena juu ya Samir kwa uwezo alionao na hata jina lake pia. Malkia alihitaji kupata uhakika kutoka kwa Samir kama ni kweli hana nia mbaya na Maya maana amekuwa na mashaka hayo tu moyoni mwake.
Alimtoa hofu hiyo Malkia na kumhakikishia kwamba Maya yupo katika mikono salama. Kauli ile ikamfanya Malkia apate faraja na kuwa na matumaini juu ya mwanaye. Alijikuta anamuamini Samir baada ya kutambua anatumia nguvu za kichawi kwa kusaidia watu na si kudhuru. Maya alikuwa sehemu akiwatazama wakiwa wanaongea, alifurahi sana kuona hata Malkia amekuwa muelewa wa haraka kuhusu Samir.
Hakuonesha kukwazika wala kushangaa sana baada ya kuelezwa kuhusu Samir.
Baada ya muda kadhaa ikambidi Malkia awaweke pamoja Maya pamoja na Samir na kuwaeleza sababu za askari wale kufika hapo Gu Ram.
"Na kwakuwa nimewaamuru waondoke bila kuwapata naamini lazima watatumwa tena maana Mfalme amekuwa ni mtu wa kutopingwa katika jambo lake lolote aliloamua liwe" alisema Malkia huku akimtazama mwanaye.
"Inamaana anataka turudi ili atuue au? Kama adhabu kashatupatia tumetelekezwa ndani ya ule msitu hivyo swala la sisi kuwa hai yeye linamuhusu nini?" aliongea Maya akimshangaa baba yake kwa maamuzi yake.
"Tatizo lililopo ni kwa upande wa Samir, ameanza kumhisi huenda akawa anatumia nguvu za kichawi maana si rahisi kwa mtu wa kawaida kutupwa katika msitu ule kisha akaendelea kuishi. Hivyo anamhisi hivyo na huenda kama wakibaini kuwa ni kweli wakampa adhabu kama ilivyo kawaida kwa mtu mwenye kosa hilo." aliongea Malkia kwa upole na maneno yale yakamtia hofu Maya, aligeuka kumtazama Samir akiwa hana la kuongea baada ya kusikia hivyo, alibaki kumsikiliza tu Malkia.
"Ila naamini hakuna kitakachoharibika wala msiwe na hofu juu ya hilo." aliwapa moyo juu ya hilo akiwa mwenye kujiamini na kuwafanya Samir pamoja na Maya wabaki kutazamana.
Muda ulizidi kwenda mbele na hatimaye Askari wa Mfalme Faruk walifika kijijini hapo. Mkuu wa kikosi hicho alitoa amri moja tu kama walivyoagizwa kufanya.
"Unaingia kila nyumba kuangalia watu tunaowataka kama wapo, yeyote atakayeleta ubishi chinja bila kuhofia jambo." alisema askari huyo na kuwapa mori wenzake wakawa tayari kwa jambo hilo, muda ulipofika walianza kazi hiyo kuingia kwenye kijiji hicho kupekua kila nyumba.
Huku wakiwa hawana habari pale nje wakiongea mambo yao walishangaa kumuona Faraj akitoka ndani haraka na kusimama mlangoni. Hali ile ikamfanya hata Samir ahisi huenda kuna jambo limetokea. Alisimama na kumsogelea Faraj pale aliposimama.
"Vipi kuna tatizo umepata kutambua?" aliuliza Samir akiwa namtazama Faraj.
"Nahisi kuna waru wameivamia Gu Ram, nasikia harufu ya damu hapa." alisem Faraj akiwa anazidi kuangalia kila sehemu. Alipoona hali inazidi kubadilika aliingia ndani na punde tu akatoka akiwa ameshika ile bakora yake.
"Ingieni ndani msitoke hadi tutakaporejea." alisema Faraj akiwataka Maya na Malkia waingie ndani. Haraka wakanyanyuka pale walipokaa na kuelekea ndani huku Samir pamoja na Faraj wakienda kuangalia kulikoni.
Hawakuwa na huruma askari wale wa Mfalme Faruk kila mtu aliyeleta kipingamizi kuwazuia walimkita upanga wa tumbo na kupoteza maisha ya watu. Watu walikimbia kwenye nyumba zao wakihofia kuuawa maana askari wale hawakuonesha mchezo kwenye jambo hilo. Samir na Faraj walipokaribia eneo husika walipishana na watu waliokuwa wakikimbia kuelekea walipotoka wao. Baadhi ya askari walipata kumuona Samir hali iliyowafanya wawataarifu na wenzao kwamba mmoja wa wale wanao wahitaji wamepata kumuona. Ikawabidi wasogee pamoja wakimtazama Samir akiwa anakuja bila wasi. Askari wale walitazamana huku wakiachia tabasamu kuona mtu wao anajileta mwenyewe. Wakashuka kwenye farasi wao huku wakiwa wameshika mapanga kila mmoja.
Faraj alitazama pembeni na kuona baadhi ya raia wake wameuawa na askari hawa, alijisikia vibaya sana maana yeye ndio mtu wa kuwalinda watu wake wasipatwe na matatizo lakini ameruhusu waumizwe na hata kupoteza maisha.
"Faraj hawa mimi nawamudu wewe rudi kule ukawaangalie Malkia na Maya kwa usalama zaidi." alisema Samir akiwa anatazama askari waliokuwa mbele yao. Hakuweza kukubaliana na maneno haya ambayo hayakumuingia akilini kabisa. Aliona askari wale wakianza kuja kwa kasi lengo ni kuwavamia pale waliposimama, walipokaribia tu Faraj akanyanyua bakora yake na kuishika kwa mikono miwili ghafla tu ikabadilika na kuwa upanga mkali wenye kumeremeta. Samir alitoa upanga wake na waliposogea wale askari mapanga yakaanza kuchukua nafasi yake.
Faraj pamoja na udogo alionao lakini alikuwa yupo vizuri kwenye kupambana jambo lililowaacha askari wale washangae maana hawakumdhania kama ataweza kuwapa changamoto kama hiyo. Askari hao walikuwa na umoja hasa baada ya kuona wanapambana na watu wanaojua kutumia upanga vizuri. Na muda huo huo Mfalme Siddik ndio alikuwa akiwasili katika kijiji hicho hju akifuatwa na askari wake akiwepo Generali pamoja na Jamal. Walipatwa na mshangao baada ya kuona baadhi ya nyumba za kijiji hicho zikiwaka moto huku kelele za watu zikisikika. Hali hiyo ikamfanya Mfalme ashangae. Iliwabidi wazidi kusogea mbele kujua imekuwaje. Huku Faraj alizidi kuonesha umahiri wake kwa kila anayesogea mbele yake anakata. Alipoona wanazidi kuja kwa wingi akaamua kuzitumia nguvu zake za kichawi kuzidi kuwapunguza askari hao. Alimfanya hata Samir naye afanye hivyo tena kwa uwezo wa hali ya juu. Alimudu kuachia pigo moja lililoweza kuwadondosha askari wanne kwa pamoja huku macho yake pamoja na Faraj yakibadilika na kuwa makali sana. Na muda huo huo Mfalme pamoja na askari wake kwa ujumla wakapata kufika kwenye tukio hilo na kushuhudia kwa macho yao jinsi Samir alivyobadilika na anavyopambana na watu wale. Jamal kuona vile akataka kwenda kutoa msaada kwa Samir ili baadae wapate kumkamata lakini Mfalme akamtuliza ili wapate kuangalia zaidi pindi Samir anapotumia nguvu zile akiwa sambamba na kiongozi mdogo Faraj.
Hakuna aliyetegemea kumuona Samir akiwa anapambana na askari wale kwa uwezo ule. Jamal alibaki kushangaa kile ambacho anakiona mbele yake. Alikumbuka siku ile ndani ya uwanja akiwa anapambana na Samir na kuanza kuhisi huenda nguvu hizi ndio zimemsaidia Samir hadi kuja kuwa Mlinzi wa binti wa Mfalm. Kwa kujua hilo akataka kujenga mazingira ya kujiaminisha kuwa yeye ndio alistahili kupata nafasi hiyo.
"Huyu mtu anaonekana ni muda mrefu anatumia nguvu hizi, tazama jinsi alivyo mzoefu katika kupambana huku akitumia uchawi." alisikika Generali akiongea na kumfanya Mfalme azidi kuamini kwa kile anachokiona mbele yake. Hawakuwa wanafahamu lolote kama wanaangaliwa muda huo. Walifanya kile wanachokiona kwao kitaleta amani katika kijiji hicho lengo ni kuwamaliza askari wale maana wamekuja kwa nia ya kuua watu.
Muda mfupi tu waliweza kuwamaliza wote huku wakionekana kuchoka kwa kupambana. Wakiwa kwenye hali hiyo makofi yalisikika mfululizo na kuwafanya wageuke kutazama sauti hiyo inapotokea. Walipatwa na mshangao baada ya kumuoni Mfalme akiwa anaendelea kupiga makofi kuashiria amefurahishwa na uwezo walio uonesha wawili hao kwa kuwamaliza askasi zaidi ya ishirini. Waligeuka kutazamana baada ya kufahamu kile walichokifanya kimepatwa kuonekana na watu wengi.
"Safi sana, nimependa mbinu mlizotumia." alisema Mfalme akionesha tabasamu usoni mwake. Dakika chache kupita alibadilika na kuwa na sura ya hasira.
"Siku zote umekuwa mkimya kumbe ulikuwa ni miongoni mwa wanaotumia uchawi! Nilitokea kukuamini sana lakini baada ya kupata wasiwasi juu yako na leo ndio nimeiaminisha nafsi kwa kile nilichokuwa nakifikiria. Binti yangu hawezi kulindwa na mchawi hata siku moja, kufanya hivyo ni sawa na kuruhusu uchawi ndani ya falme yangu.... Lazima uadhibiwe kama sheria ya Eden inavyofuatwa ka yeyote yule aliyejulikana ana nguvu hizo, mkamateni haraka." alitoa amri hiyo Mfalme na haraka askari wakashuka kwenye farasi na mapanga yao wakaharakisha kumsogelea Samir pale aliposimama. Faraj kuona vile alisimama mbele ya Samis kuzuia kile kinachotaka kutokea.
"Mbona unabadilika hivyo Mfalme wa Eden? Huyu mtu pamoja na binti yako si uliwafukuza katika taifa lako wasikanyage tena!? Haitoshi ukawapa adhabu ya kutupwa kwenye msitu wenye wanyama wakali mkijua fika hawataishi hata siku isingeisha wangeliwa na wanyama wa porini. Imekuwa ni bahati leo ni wazima na baada ya kutambua kwamba hawatakiwi Eden wamekuja hapa kuanza maisha yao mapya. Na hadi sasa hawa watu wanajulikana ni wa kijiji changu. Nakuheshimu kwa kuwa ni Mfalme wa Taifa kubwa, waache watu wangu waishi kwa amani, kama uliwakataa ukaona hawastahili kuishi Eden basi huku hawa watu wanaheshimiwa na watu wote hapa kijijini." alisema Faraj kwa kujiamini sana na maneno yake yenye ukweli ndani yake yalianza kumwingia Mfalme na hata Generali aliyeko pembeni anatazama kinachoendelea.
"Unaongea nini wewe mbele ya Mfalme? Unapanga sheria zako mbele ya utawala wa Eden!?" alifoka Jamal na kumfanya hata Mfalme ageuke kumtazama maana alikosa la kusema.
Faraj alimtazama Jamal akionekana kukereka kwa kile kilichozungumzwa.
Kwa kumtazama tu kwa muda akapata kumtambua vilivyo hata lengo lake.
"Mtoto wa Mfalme Faruk, Mfalme mwenye kutamani siku moja kuupindua utawala wa Eden kisha akumilikishe wewe. Hivi kabisa umeamua kuacha heshima ya kuitwa mtoto wa Mfalme ambaye siku moja utakuja kurithi nafasi ya baba yako lakini ukajitoa kwenda kugombania nafasi ya kuwa mlinzi wa binti wa Mfalme wa Eden. Ulijua utakapofanikiwa kupata nafasi ya kumlinda Maya ndio mtakayemtumia katika kufanikisha mambo yenu." alisema Faraj na maneno yale yalimshtua Mfalme.
Jamal kusikia vile alipata mshtuko baada ya kujua tayari siri yao imevuja tena mbela ya Mfalme Siddik.
"Unaongea kuhusu nini wewe!?" alikuja juu Jamal akitaka kujitetea kwa kile kilichozungumzwa na Faraj.
"Huo ndio ukweli, upo Eden kwa maslahi ya taifa lako wewe na baba yako na kitendo cha Samir kuwa mlinzi wa Maya kiliwauma sana na mmekuwa mnafanya njama za kummaliza Samir, hata walipoadhibiwa kutupwa msituni mlikuwa mnafuatilia kila hatua kujua kinachoendelea.
"Acha mara moja kutupakazia mabaya ili upate kuonekana mwema kwa Mfalme Siddik. Samir amekutwa na uchawi na lazima sheria ya Eden ifuatwe maana huyu ni mti wa Eden tu." aliongea Jamal akizidi kujiwekea mazingira ya kutojukana.
"Ahaa, kama unaongea mbele ya Mfalme uongo wako unadhani nani atakuamini hata siku ukaja kuwa kiongozi wa Eden maana hilo ndilo linalowafanya msilale siku zote, mmewatuma askari wenu kuja kummaliza Samir ili mpate nafasi ya kuonekana bora kwa Mfalme." alisema Faraj na kusogea kwa askari mmoja aliyekuwa chini amekufa kisha akavua nguo yake ya juu, vazi lililopo ndani liliwafanya watu wote wa pale washangae.
Hapo ndipo Jamal akakosa la kusema baada ya kuonekana askari wa taifa lao wakiwa kwene vazi hilo. Walikuja kwa nguo tofauti ili wasipate kujulikana na hatimaye imekuwa tofauti.
Mfalme Siddik alistaajabu kuona tukio hilo mbele ya macho yake, alimgeukia Generali ambaye hakuwa na la kusema akabaki kuwa kimya muda wote.
"Hapana.. Hapana.. Hii ni njama tu na hakuna ukweli wowote. Mfalme na kuhakikishia baba yangu ni rafiki mkubwa sana kwako na hawezi kufanya hivi hawa wametengeneza hili swala amini ninayokwambia." alisema Jamal akiwa mwenye kujitetea muda wote.
Mfalme aliwaamuru askari kadhaa kwenda kuihakiki ile miili ya askari wanaosadikika ni wa Mfalme Faruk. Walisogea hadi pale na kupekuwa baadhi ya alama na hata mavazi yale ukweli ukabaki kuwa pale pale kwamba ni watu wa Mfalme Faruk. Alisikitika sana Mfalme Siddik baada ya kuona hata rafiki yake kumbe anaombea mabaya na kuitamani taifa la Eden. Alikasirika sana kusikia hivyo na muda huo huo akatoa amri Jamal akamatwe mara moja, askari wakafanya hivyo kama alivyotoa amri Mfalme ya kumkamata Jamal. Alizidi kukataa kwamba jambo lile wamelitengeneza Samir na Faraj ili wazigombanishe Falme hizo mbili lakini kwa Mfalme hakuweza kuamini hilo. Muda huo huo walimfunga kamba na kumuweka kwenye farasi askari kadhaa wakaanza kurejea naye Eden wakamuweke selo wasubiri kitakachoamuliwa.
Mfalme alikosa hata la kusema baada ya kutambua ukweli kwamba Eden yake inamezewa mate na falme za jirani. Alijitokeza Malkia Rayyat akiwa sambamba na binti yake Maya wakifika katika eneo lile. Mfalme alipomuona binti yake moyo wake ulikumbwa na wimbi la faraja kuamini kweli yuhai. Bila kujali lolote Maya alisogea hadi alipo Samir na kumkamata mkono kuonesha yuko pamoja naye.
"Nimejaribu kumueleza binti yako kuhusu amri yako uliyotoa ya wao kurudishwa Eden lakini imekuwa kinyume kwao. Hivyo sikuweza kuwalazimisha baada ya kuona wanaishi kwa amani. Hakuna haja ya kuwasumbua tena kama umeshaamuru kuwa ni haramu kwao kukanya Eden basi huwezi ukawachukua kuwaadhibu watu uliowatoa sadaka. Nimekaa hapa kwa muda mchache tu lakini najiona mwenye amani pia, uchawi unaotumiwa na watu hawa ni kwa ajili ya kusaidia katika matatizo na kujihami mbele ya adui zako, sijaona sababu ya kuchukia tena jambo hili kama limekuwa na faida kwa watu, nitafurahi sana nikiishi hapa muda mrefu na si kurudi tena Eden, Faraj... Ningetamani kupata ruhusa kutoka kwako ya kunifanya niwe raia wa kijiji hiki, hakika nitashuru kama utanikubalia." alisema Malkia Rayyat na kuwafanya watu wote washangae kwa kauli yake hiyo.
Mfalme Siddik alishtuka kusikia hivyo, hakutaka kabisa swala hilo litokee hata kidogo lakini kwa Malkia alikuwa anamaanisha kweli kile alichoongea, hakuona hamu ya kuendelea kukaa katika taifa ambalo hana furaha angali mwanaye anaishi mbali naye.
"Hapana sitapendezwa na jambo hilo, haitaleta picha nzuri kuona Malkia wa taifa langu anaishi mbali na sehemu yake, tafadhari naomba usifanye hivyo." alisema Mfalme akionesha upendo kwa mkewe.
Mtu wa pekee anayepaswa kuruhusu hilo alikuwa ni Faraj, yeye ndiye mwenye kuamua kumkubalia Malkia aishi Gu Ram au laa. Hata yeye alikuwa kwenye wakati mgumu juu ya swala hilo huku Malkia akionesha msimamo wake wa kuwa upande wa binti yake. Mwisho wa siku ikambidi atumie busara na hekima ili kulifanikisha swala hilo kila mmoja apate kuridhia.
"Nafasi ya Malkia kuishi hapa ni kubwa mno maana ameshapata kutambua mji huu ni wa amani ila ningependa kutaka jambo kwa Mfalme, endapo Malkia akiondoka nawe kwenda Eden basi Maya na Samir sitataka wasumbuliwe tena. Na endapo Malkia akiishi hapa basi sitaruhusu mtu yeyote kutoka kwenu kuja kuleta vurugu kwa hawa watu. Hivyo nakupa nafasi hizo mbili uchague moja wapo." alisema Faraj huku akimtazama Mfalme. Alimtazama Generali akiwa naye anamuangalia Mfalme ili apate kuamua moja kati ya hayo mawili.
Aliitazama familia yake ikiwa pale karibu na Faraj na kupata picha kwamba taifa lake si lolote japo linapendwa na wengi. Kama hata familia yake inakataa kurejea Eden ni wazi kwamba kuna tatizo ambalo anahitajika kulifanyia kazi.
Aliona afanye maamuzi magumu ambayo aliona ndio sahihi kwake na hakutaka kupigwa na yeyote.
ITAENDELEA.....
Ni maamuzi gani atayachukua Mfalme? Huku Samir ameshaonekanwa pawa yake, na kule Jamal ameshajulikanwa njama zake na yupo njiani kupelekwa selo, mambo yanazidi kupamba moto.
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE (28)
