PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 28


 SEHEMU YA 28


ILIPOISHIA..... 


Aliitazama familia yake ikiwa pale karibu na Faraj na kupata picha kwamba taifa lake si lolote japo linapendwa na wengi. Kama hata familia yake inakataa kurejea Eden ni wazi kwamba kuna tatizo ambalo anahitajika kulifanyia kazi.

Aliona afanye maamuzi magumu ambayo aliona ndio sahihi kwake na hakutaka kupigwa na yeyote.


ENDELEA NAYO...... 


Alirudi nyuma na kupanda kwenye farasi wake huku watu wakimuangalia.  Alimtazama Malkia akiwa amesimama karibu na Faraj.


"Utaishi hapa kuanzia sasa, ila fahamu bado utabaki kuwa Malkia wa Eden siku zote. Wewe ni mke wangu na siku zote itabaki kuwa hivyo." alisema Mfalme na kuamuru jeshi lote alilokuja nalo ligeuze kurejea Eden. Walitii amri hiyo askari wote huku baadhi yao wakistaajabu kwa uamuzi aliouchukua  Mfalme kwa kumruhusu Malkia kuishi Gu Ram. 


Generali alishangaa sana kwa jambo. Ni wazi kwamba Mfalme ameiacha familia yake pamoja na Samir kuwa huru waishi huru. Generali walifuata na askari wengine kurejea sasa Eden wakiongozwa na Mfalme baada ya kuamuru Malkia na wengine waachwe pale.

Maya alimsogelea mama yake na kumkumbatia baada ya kufahamu wapo huru kwasasa kuishi kijijini hapo. Samir aligeuka kumtazama Faraj aliyekuwa akiangalia majeshi yale ya Eden wakitokomea kabisa kwenye kijiji chao.


Baada ya muda iliwabidi wawape taarifa watu ambao muda wote walikuwa wamejificha ndani ya nyumba zao. Taratibu wakaanza kutoka kwenye makazi yao na kuanza kuzunguka kuhakikisha usalama. Waliona watu wengi wameuawa pale chini wakiwa wanapambana, iliwabidi wawakusanye na kwenda kuwatupa kwenye mto maana hawakutaka kuwazika katika ardhi yao watu ambao walidhamiria kuwaua. 


Kwa umoja wao wakaanza kusaidiana kujenga upya baadhi ya nyumba ambazo zimepatwa kuchomwa moto na watu wale waliovamia. Malkia pamoja na mwanaye walikuwa mstari wa mbele katika kwenda kutafuta miti ya kujengea nyumba za wananchi. Watu waliomfahamu kwa heshima aliyonayo kama Malkia hawakutegemea kama anaweza akafanya kazi hizo na watu wa kawaida jambo ambao yeye binafsi hakutaka litokee. Alikuwa karibu na watu akishirikiana nao katika matatizo hayo yaliyowakumba.


Jioni ya siku Faraj aliwakusanya wananchi wake nje ya nyumba yake na kuanza kuwapa maneno yenye busara na kuwatoa hofu kwa kile kilichotokea siku hiyo. Aliwapa ujasiri wa kutoogopa watu ambao wanaingia katika ardhi yao kwa lengo la kuwadhuru.


Taarifa za kuuawa kwa askari wake aliowatuma katika kijiji kile zilimfikia Mfalme Faruk pindi Lutfiya alipomtumia ujumbe kama ilivyo kawaida yao. Kubwa na lenye kumpandisha hasira ni pale alipoambiwa kuwa mwanaye Jamal amekamatwa kwa kujulikana lengo lao hasa ni kuupindua ufalme wa sasa wa Siddik. 


Alipandwa na hasira zisizo na kipimo akitambua kwa vyovyote mwanaye atapewa adhabu ya kuuawa, alishindwa kukaa mahala pamoja kila akifikiria jambo lililompata mwanaye. Usiku huo aliamua kupanga majeshi yake yote lengo ni kuivamia Eden kuweza kumtoa mwanaye katika kifungo hicho. Askari wote walijiandaa ipasavyo wakiweka silaha zao vyema tayari kwa safari ya kuelekea Eden. Baada ya muda Mfalme alitoka na kusimama mbele ya jeshi lake kuwapa maelekezo.


"Kila mtu afahamu anaenda kupambana lengo ni kumkomboa Jamal, wamemkama baada ya kujua ukweli kwamba tunampango wa kuipata Eden. Hivyo basi kwa hili tunalokwenda kulifanya tukifanikiwa kuwadhibiti jeshi la Eden basi tumefanya kazi moja kwa faida mbili. Nadhani ndio utakuwa usiku wa kuipindua Eden na kuitawala. Itakuwa ni sherehe kubwa kwetu kwa kufanikiwa jambo letu, kila mtu awe na moyo wa ujasiri katika hili, T U N A I N G I A    V I T A N I I I." alisema Mfalme Faruk na askari wote wakapata morari ya kufanya kile walichoambiwa, walipiga kelele za kushangiria kwa kile kilichoelezwa na Mfalme. Bila kuchelewa Mfalme aliongoza safari hiyo na askari wote wakafuata nyuma wakiwa kwenye farasi huku mbalamwezi ikiangaza usiku huo.


Upande wa pili Mfalme Siddik aliongozana na Generali hadi kwenye selo ambayo Jamal amehifadhiwa. Alikuwa mwenye hasira sana pindi alipotambua kwamba lengo la Jamal kuja Eden ni kuweka mazingira ya kuudidimiza ufalme wa sasa wa Eden. Walimkuta akiwa amefungwa kamba mikononi na kunin'ginizwa juu akionesha kuchoka sana. Mfalme alimsogelea hadi pale akiwa amekunja sura.


Alimpiga ngumi ya shavuni na kumfanya Jamal ayasikie maumivu hayo huku damu zikianza kumtoka. Generali alibaki kushuhudia tu kinachoendelea..


"Inamaana lengo lenu ni kuja kunipora uongozi wangu mjimilikishe! Kwanini hamridhiki na Taifa lenu mkalijenga na kuliendeleza! Kipi kimewafanya hadi muitamani Eden yangu?" aliuliza Mfalme akiongea kwa hasira sana lakini Jamal hakuweza kuongea lolote. Hali hiyo ilimfanya Mfalme azidishe hasira, alishusha ngumi nzito iliyotua tumboni kwa  Jamal aliyeugumia kwa maumivu anayosikia. 


"Nieleze ukweli kitu gani kinawafanya muitamani Eden!?" alifoka Mfalme kwa hasira hadi Generali akafahamu hapa Jamal anaweza kuuliwa kwa hasisa alizo nazo Mfalme. Alitamani kuingilia lakini huwezi kumzuia Mfalme pindi afanyapo jambo lake. Hasira za Mfalme hazikuwa ndogo, alizidi kumpiga Jamal akiwa pale amefungwa kamba  lengo ni kumtaka aseme sababu hasa za kutaka kuivamia Eden.


Huku mashariki na mbali, Dalfa baada ya kufanya mambo yake kwa uwezo alionao akapata wazo la kurejea tena Eden, aliona njia rahisi ya kumpata Samir ni kumfanyia jambo Mfalme Siddik. Alijua kwa kufanya hivyo lazima binti yake Maya ambaye ndio yupo sambamba na mtu wake lazima atataka kwenda kumuona baba yake na itafanya waongozane pamoja na Samir na hapo atapata kufanikisha swala lake. 


Safari hii alichukua nguvu na silaha zake zote akiamua kulivalia kibwaya jambo hilo na hakutaka kufeli tena. Aliingia kwenye mahala pake pa kufanyia ibada na kufanya maombi yake apate kupotea pale alipo atokee karibu na Eden aikamilishe kazi hiyo.


Huku majeshi ya Mfalme Faruk yalizidi kuja kwa kasi huku mwenyewe akionesha kuwa na hasira sana, kila akimfikiria kijana wake na kuhisi huenda anapata mateso makubwa  usiku huu. Alijikuta akizidisha kasi kwa farasi wake kusudi awahi kumkomboa mwanaye.


Huku Eden ulinzi uliendelea kama kawaida wakihakikisha usalama wa raia. Hata ndani ya falme kila kona askari walitanda kuweka ulinzi. Muda huo Mfalme Siddik alikuwa zake chumbani kwake akitafakari mambo yanavyoenda. Mpaka muda huo Jamal hakuweza kusema lolote lile na kumfanya Mfalme awakabidhi askari wake kumuadhibu hadi apate kusema wanamipango gani wa kutaka kumpindua yeye na falme yake. Aliumiza kichwa sana na huku akiwa mwenye hasira kuona rafiki yake Faruk amethubutu kuitaka Eden ajifanye kuwa ni kiongozi. 


"Kamwe sitakubali mtu baki kuja kuichukua Eden hata awe nani, kama Siddik nipo hai hakuna wa kuitawa Eden yangu, hakuna.." aliongea Mfalme akiwa anaweka msisitizo. 


Baada ya muda kupita usiku ukizidi kuwa mkubwa, Lutfiya alichukua chakula na kuanza kuelekea mahala alipohifadhiwa Jamal. Tangu alipokamatwa hakuweza kupata chakula chochote hadi kufika usiku ule. Alinyata huku akiwa makini asije akaonwa na askari mahala anapotaka kwenda. Alifika hadi karibu na selo ile na kupata kuona walinzi wawili wakiwa wamesimama mlangoni macho makavu wakiwa makini kuhakikisha Jamal ndani ya selo hatoki. Aliumiza kichwa afanyaje kuwatoa askari wale lakini hakupata njia sahii ya kufanya. Ghafla alishangaa anazibwa mdomo na mtu nyuma yake na kugeuzwa, alishtuka kumuona ni Generali aliyekuwa pale. Alishikwa mkono kusogezwa pembeni kwanza huku akiwa ameshika chakula kile.


"Umefuata nini huku usiku huu?" aliuliza Generali akimshangaa Lutfiya. Alibaki kujin'gatan'gata maneno akijua tayari amekamatwa.


 "Huku hakuruhusiwi mtu yeyote kufika, ni hatari kwako ukikutwa huku muda huu." alisema Generali.


"Nisamehe Generali, ila sikuja kwa niya mbaya nilibeba hiki chakula kwaajili ya yule askari aliyekamatwa, bila shaka atakuwa mwenye njaa maana ni muda yupo humu bila kula." alisema Lutfiya akiongea kwa huruma. Generali alikitazama chakula kile na kuona ni kweli. Alichukua chakula kile na kumtazama Lutfiya alikuwa akitazama chini kama heshima.


"Kitafika usijali, usingeweza kumpatia chakula hiki maana askari walikatazwa asipewe chakula na mtu yoyote. Haya rudi haraka usije ukaja huku." alisema Generali na kumfanya Lutfiya ashukuru kwa kusaidiwa kazi hiyo. 


Alipopiga hatua kadhaa mbele akasimama, kwa huruma aliyooneshwa na Generali aliona naye ampashe habari yenye kuyalinda maisha yake. Aligeuka nyuma kumtazama Generali aliyebaki kushangaa kuona amesimama.


"Huenda usiku wa leo kukamwagika damu hapa Eden, kuwa makini na maisha yako Generali." alisema Lutfiya kwa mafumbo kisha akageuka na kuondoka haraka eneo lile.


Alibaki kushangaa kwa maneno aloambiwa na msichana huyo.

"Usiku wa leo kukamwagika damu? Eden hii au? Anamaana gani kusema maneno haya ya kutisha?" ni maswali ambayo Generali hakuweza kuyapatia jibu na kubaki kutazama njia aliyoondokea nayo Lutfiya. Alitazama chakula kile kwa muda huku fikra zake zikihama kwa kile alichoambiwa. Aliamua kuondoka na kusogea hadi kwenye ile selo na wale askari wakampa heshima kama mkubwa wao. 


Alifunguliwa mlango na kuingia ndani ambapo alimkuta Jamal akiwa dhoful hali kwa kipigo alichopata kilimfanya awe hoi huku damu nyingi zikimtoka mwilini mwake. Huruma ilimjia Generali huku akimsogelea kijana wake, alimtazama jinsi alivyochakazwa kwa kupigwa hadi kukosa nguvu ya kusimama vizuri. Alijitahidi kunyanyua sura yake na kupata kumuona Generali akiwa mbele yake.


"Ge ne ra liih... Nitoe hapa..wataniua hawa. Mfalme ataniua!" alitoa sauti ya upole na yenye huruma ndani yake Jamal akihitaji msaada wa kutoka pale alipo.


Generali hakuwa na namna ya kumsaidia muda ule. Alifungua kile chakula na kuanza kumlisha Jamal akiwa vilevile amesimama.


"Amekileta Lutfiya hiki chakula, na kuna maneno ameniambia ambayo sikuweza kuyaelewa hadi sasa.. Huenda usiku wa leo kukamwagika damu hapa Eden, kuwa makini na maisha yako Generali. Maneno haya yameniacha njia panda sijafahamu anamaanisha nini." alisema Generali huku akimlisha Jamal kile chakula. Aliposikia vile alianza kufurahi Jamal na hata kucheka baada ya kusikia hivyo. Akazidi kumshangaza Generali aliyekuwa anamtazama tu.


"Wanakuja... Wanakuja kuipindua Eden. Ni kweli damu zitamwagika, na endapo nikitoka katika mateso haya Mfalme atakuwa ni sadaka kwa usiku wa leo." alisema Jamal akionesha dhahiri kuwa na hasira na Mfalme Siddik. Hapo ndipo Generali akapata kutambua kumbe kauli ile ya Lutfiya ilikuwa na maana kubwa namna hiyo. Hapo ndipo akafahamu huenda swala hili limepangwa na watu wengi akiwemo msichana huyo Lutfiya aliyekuwa akiishi humo muda mrefu sana.


"Inamaana hata huyu msichana mnafahamiana naye?" aliuliza Generali na kumuona Jamal akitikisa kichwa kumaanisha ndilo jibu sahihi. 


"Nadhani mzee alikuwa na maana kubwa kuongea na wewe na kukueleza mengi kuhusu mimi, nadhani muda ndio huu, naomba uwe upande wangu kuhakikisha swala hili tunalikamilisha." alisema Jamal huku akimtazama Generali akiwa ameshika chakula kile. Alimuweka katika wakati mgumu wa kutafakari swala hilo kwa umakini zaidi.


Dalfa aliweza kuwasili Eden mapema sana baada ya kutumia nguvu za kichawi kumtoa kule mashariki na mbali.

Usiku huo bila kuchelewa alianza kusogea kwenye falme ili kutimiza azma yake. Muda huo kila raia alikuwa amepumzika ndani kwake mji mzima ulikuwa kimya huku vishindo vya askari vilisikika wakiwa wanatembea huku na kule kuhakikisha usalama. Alitembea bila kuhofia lolote Dalfa, alipishana na askari njiani bila kumsimamisha kuhoji. Ni wazi kwamba amedhamiria kufanya jambo hilo kwa uwezo wake unaomfanya aogopwe na kila mtu uwezo alionao ulimfanya asionekane na askari yeyote hadi alipoingia ndani ya falme husika. Moja kwa moja alielekea chumbani kwa Mfalme akijua kwa muda huu lazima atakuwa amejipumzisha.


Na muda huo Mfalme alikuwa kitandani usingizi hauji abadani kila akifikiri matukio yanayomkabili. Hadi sasa anaishi mbali na familia yake jambo ambalo hakuwahi kufikiria kama lingeweza kutokea. Ilikuwa ni familia ya furaha pindi waishipo pamoja, lakini furaha imepotea baada ya binti yake kugundulika kuwa na mahusiano na mlinzi wake. Alijikuta akisikitika tu kwa kile kilichotokea maana ni aibu na pia adhabu ile ilimgusa moyoni kama mzazi. Hakuwa na la kufanya kwa binti yake kama msaada wa kuikwepa adhabu hiyo jambo ambalo alihisi ndio sababu ya Malkia kuchukia na hata kutotamani aendelee kuishi tena Eden hasa baada ya kutambua binti yao yumzima. 


Akiwa kwenye kutafakari hayo alipata kuona taa inaanza kufifia mwanga na mwishowe kuzima yenyewe. Alishangaa kuona hali hiyo ambayo haikuwahi kutokea hapo awali. Ghafla ile taa ikawaka tena mwanga mkali na kufifia tena ghafla, ikawa ni kama mchezo hali ambayo ilimtia hofu Mfalme na kuinuka pale kitandani kusogea karibu na taa. Alipotaka kuishikaa ghafla ikazima na kufanya giza lichukue nafasi yake mule chumbani. Upepo ukaanza kuvuma nje na hali ya hewa ghafla ikabadilika na matone ya mvua yakaanza kudondoka taratibu na hatimaye ikanyesha mvua kubwa kabisa. 


Muda huo Mfalme Faruk ndio alikuwa anaingia ndani ya Eden huku akifuatwa na majeshi yake yaliyokuwa moto kupambana siku hiyo ili wamkomboe mtoto wa Mfalme wao.


Huku Mfalme hali ile ilimfanya apatwe na hofu kuona hali ya hewa kubadilika ghafla, radi za kumurika mwanga zilirindima na kufanya Mfalme apate akili ya kwenda kufunga madirisha. Alipofunga dirisha na kugeuka nyuma alipata kushtuka baada ya kuona kuna mtu amepita mbele yake na kupotea. Alitoa macho kutazama vizuri huku akiangalia huku na kule bila kuona kitu. Ilimbidi apapase hadi kufika kwenye droo ya kabati na kuchukua tochi, akawasha na mwanga ukaweza kumurika chumba kile huku akimurika huku na kule kuangalia kama kuna anayemfanyia vitisho hivyo. Punde tu mwanga wa taa ukarejea na kurudi kama awali hali iliyompa imani ya usalama Mfalme na kumtoa hofu. Aligeuka kurudisha tochi ile ambayo ilimsaidia kwa muda mchache sana. Alipotaka kurudi zake kitandani kupumzika alishangaa kumuona mtu mbele yake akiwa amesimama, ilimbidi amtazame kwa makini kumuangalia, alishtuka baada ya kumfahamu mtu yule aliyeko mbele yake.


"Unashangaa kunikuta muda huu nipo hapa ndani kwako?"


"Dalfa! Nimi kimekuleta Eden, na umefuata nini hapa ndani kwangu?" aliuliza Mfalme baada ya kumtambua Dalfa ndiye aliyeko mbele yake.


"Shida yangu ni kumpata Samir kwa sasa, ila nitataka kitu chengine hapo baadae. " alisema Dalfa huku mvua kubwa nje ikinyesha.


"Samir hayupo Eden, na sidhani kama ataweza kurejea tema katika ardhi hii. Sasa sijui utampataje." alisema Mfalme akimtazama Dalfa.


"Ni rahisi kumpata, na ipo siku atakuja tu akiwa na binti yako." alisema Dalfa na kuanza kubadilika macho kuwa ya kutisha. 


Mfalme kuona vile akajua ni uchawi anaotumia Dalfa. Akataka amuwahi  akihofu kudhurika, alikimbilia upanga wake na kuushika vyema akageuka kupambana na Dalfa, ajabu hakuweza kumuona tena mule ndani hali iliyomfanya ageuke kila pande kutazama bila kumuona. Dalfa alitokea nyuma ya Mfalme na kuanza kupandisha uchawi wake mikononi akidhamiria kumuwekea Mfalme Siddik ambaye alipogeuka tu alishuhudia akikabwa shingo yake kwa mkono. Alitaka kunyanyua upanga wake lakini haukuweza kunyanyuka, ni wazi kwamba Dalfa amezuia hilo. Taratibu uchawi ule ukaanza kushuka na kuingia mwilini mwa Mfalme.


NINI KITAJIRI HAPO EDEN? DALFA NDANI YA CHUMBA CHA MFALME SIDDIK AKIMTIA UCHAWI WA KUMDHURU NA HUKU MFALME FARUK YUPO NJIANI KUJA KUFANYA MAPINDUZI.. PATAMU HAPO

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA (29)

Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group