SEHEMU YA 29
ILIPOISHIA.....
Dalfa alitokea nyuma ya Mfalme na kuanza kupandisha uchawi wake mikononi akidhamiria kumuwekea Mfalme Siddik ambaye alipogeuka tu alishuhudia akikabwa shingo yake kwa mkono. Alitaka kunyanyua upanga wake lakini haukuweza kunyanyuka, ni wazi kwamba Dalfa amezuia hilo. Taratibu uchawi ule ukaanza kushuka na kuingia mwilini mwa Mfalme.
ENDELEA NAYO......
Baada ya muda aliachiwa na hapo Dalfa akajua tayari lengo lake limetimia. Mfalme akawa anafurukuta pale alipoachwa, alienda chini kwa kupiga magoti huku akihisi vitu vizito vinazama kwenye koo lake na kumfanya ashike shingo yake kujaribu kuzuia vile vitu anavohisi kuzama ndani lakini haikuwa rahisi. Hali ile ilimfanya hata ashindwe kupumua vizuri na ghafla akadondoka chini kwa kukosa pumzi ya kutosha. Dalfa alitabasamu baada ya kufanikisha azma yake. Alijua kwa kufanya hivyo lazima familia ya Mfalme itafika kujua hali yake na Samir hatamuacha Maya peke yake lazima ataongozana naye. Aliweka mipango yake sawa mule ndani ya chumba kile akikijaza uchawi ili hata akiondoka apate kujua kinachoendelea siku zote. Alipokamilisha zoezi lake ghafla tu akapotea kurudi Mashariki na mbali.
Mfalme Faruk alitoa amri kwa askari wake waanze mashambulizi ya kupambana na askari yeyote anayewazuia wao kuingia ndani ya falme kuweza kujua kuna vita nje inaendelea. Majeshi ya Eden yakaanza kutoka ndani ya falme sasa kwenda nje kuwapa msaada wenzao, hakika ilikuwa ni vita ya aina yake usiku ule huku mvua ikizidi kushika kasi.
Wafanyakazi ndani ya falme wakawa wanarandaranda huku na kule kila mmoja akijaribu kuyaokoa maisha yake.
Lutfiya baada ya kufahamu hali imeshabadilika alianza kufanya mipango ya kurejea tena kule selo alikofungwa Jamal.
Moja kwa moja Generali alitoka na askari watano na kwenda kumuwekea ulinzi Mfalme. Hata alipofika alibisha hodi lakini hakuweza kujibiwa. Ilimbidi aufungue mlango na kuingia hadi ndani ambapo alimkuta Mfalme akiwa kitandani amelala. Alisogea hadi pale na kuanza kumuamsha huku akimweleza hali iliyopo huko nje. Ajabu kila anavyozidi kuongea haoni dalili za Mfalme kuweza kuamka, akahisi huenda amepatwa na tatizo haraka akamgeuza Mfalme na kushangaa kuona ni wa baridi mwili mzima. Alipeleka sikio lake kifuani kusikiliza mapigo ya moyo lakini jibu alilolipata lilimfanya ashtuke bila kuamini. Aligeuka kuwatazama askari wake ambao nao walikuwa wakimtazama na kupata kujua huenda Mfalme amepatwa na tatizo. Generali alibaki kujiuliza na imekuwaje hadi Mfalme kuuawa angali watu waliowavamia hawajaingia ndani ya Falme. Aliyakumbuka maneno ya Lutfiya muda ule na kuhisi huenda ndiye mtu pekee aliyefanya mauaji hayo, ni wazi kwamba Mfalme amefariki kwa kile anachokiona mbele yake. Alipandwa na hasira sana maana hakutegemea kama atampoteza kiongozi wake kwa namna hiyo. Ilimbidi atoke kwa hasira na kutokuwa na huruma tena juu ya kile alichoombiwa na Jamal alitoka akiwa mwenye jazba huku askari wale wakimfuata. Hata alipofika nje aliutoa upanga wake na kuanza kukimbia kwenda kuunganana na askari wake kupambana na askari wa Mfalme Faruk.
Huku ndani Lutfiya alifika karibu na selo ile na kumuona amesimama askari mmoja tu pale mlangoni akilinda. Alijitwisha ujasiri wa kummudu askari yule na bila kuhofia lolote alijitokeza na kusogea hadi pale aliposimama askari yule. Alimshangaa kumuona msichana huyo akimfuata.
"Unataka nini huku muda huu?" alisema yule askari aliyejazia kwa mwilini wake wa mazoezi. Alishuhudia msichana huyo akimsogelea huku akiwa mwenye kujiregeza kimwili. Alimshika askari yule na kuanza kumpapasa, kwa ujio ule ukamfanya yule askari akili zihame kutoka kwenye kazi yake na kumtamani Lutfiya.
Alishindwa kuvumilia alijikuta akimvuta msichana huyo aliyetoa mguno wa mahaba akizidi kumpagawisha yule askari akajisahau. Jamal alipata kusikia kelele hizo na kujua kuna kinachoendelea hapo nje.
Yule askari alianza kushusha mabusu kedekede kwa Lutfiya aliyekuwa anamvizia askari huyo akae sawa. Alimuacha auchezee mwili wake na mwishowe akamkumbatia kwa mahaba na hapo akatoa kisu kidogo alichokiweka kiunoni na bila huruma akamkita nacho shingoni askari yule aliyepiga ukelele wa maumivu huku akiishika shingo yake na kwenda chini damu zikitiririka. Lutfiya alimtazama tu bila huruma anainama na kuchukua funguo iliyo kiunoni kwa askari yule na kufungua mlango ule wa selo.
Haraka alisogea kwa Jamal ambaye alitabasamu kumuona ni Lutfiya ndiye aliyemsaidia. Alifunguliwa kamba za mikononi na kuwa huru. Alimkumbatia Lutfiya kwa kuweza kumuokoa katika selo ile.
"Wamekuja, Eden yote askari wetu wametanda kupambana na askari wa Eden." alisema Lutfiya akiwa anampatia upanga Jamal.
"Sawa, ngoja nimtafute kwanza Mfalme kwasasa, ila kuwa makini Lutfiya." alisema Jamal akimwambia msichana huyo jasiri, alimuitikia na Jamal akatoka mule ndani haraka kuelekea kwa Mfalme ana hasira naye.
Ilikuwa ni vita ya aina yake huku majeshi ya Mfalme Faruk yakiwa na hasira dhidi ya adui zao. Hawakuwa tayari kupoteza nafasi hiyo kubwa siku hiyo. Walipambana kwa juhudi zote kuhakikisha wanawadondosha askari wote wa Eden. Nao hawakuwa nyuma kuwazuia watu hao na kutokubali Eden ipate matatizo. Ilikuwa ni siku ya kumwaga damu kulinda jina la Eden.
Generali alitoka ndani ya falme kuungana na vijana wake kuwamaliza wale wavamizi. Alionesha kuwa na hasira sana hakutaka kuwa na huruma pindi anapoushusha upanga wake kwenye mwili wa mtu. Hali ile ikamfanya Mfalme Faruk ashangae maana walishakaa kuongea naye hivyo kitendo anachokifanya Generali ni sawa na kuwageuka. Haraka naye akashuka kwenye farasi na kukamata upanga kuingia vitani. Alikuwa ni mpambanaji mzuri wa kutumia upanga hali iliyofanya kwa muda wa dakika kadhaa kuangusha askari wa Eden tisa huku akizidi kusogea mbele kumfuata Generali.
Jamal alipofika nje ya chumba cha Mfalme akaupiga teke kwa nguvu mlango ukapata kufunguka. Lutfiya alipofika pale alipata kuona Jamal akiingia mule ndani, haraka naye akafuata kupata kushuhudia kinachoendelea. Alisogea mpaka pale alipolala Mfalme na kuanza kumuamsha kwa nguvu apate kumhoji maneno kadhaa kabla hajafanya kile alichokusudia. Kitendo cha kumgeuza Mfalme kilimfanya hata yeye awe na mashaka baada ya kuona mwili ukiwa regevu. Lutfiya alipofika pale alimuona Jamal akiwa anamuamsha Mfalme bila tumaini.
"Amka usinizuge hapa!" alifoka Jamal akihisi Mfalme anaigiza kuwa vile. Haraka Lutfiya akasogea pale na kupeleka sikio lake kifuani mwa Mfalme. Kulikuwa kumetulia hakukusikika mapigo ya moyo akifanya kazi, ni wazi kwamba Mfalme amefariki. Aligeuka kumtazama Jamal alikuwa anashangaa.
"Nini! Nini kimetokea?" aliuliza Jamal akiwa kama kachanganyikiwa.
"Inaonekana amekata roho muda tu."
"Ati nini! Amekufa.? Ah hapana hebu muamshe nami nimuadhibu kwa vile alivyonifanya. Muamshe..!" alifoka Jamal lakini hakukuwa na ujanja. Lutfiya alinyanyuka na kusimama pembeni akimuacha Jamal ahakikishe mwenyewe.
Taratibu alisogea hadi pale na kumtazama Mfalme vile alivyo, alishka upande wa moyo wake akapaka kutambua kuwa kweli umesimama. Hasira zote alizokuwa nazo zilipotea zote na kujiwa na moyo wa ubinadamu.
"Imekuwaje mbona sielewi?" aliuliza Jamal akimtazama Lutfiya. Hakukuwa na jibu lengine tofauti na kile wanachokiona mbele yao. Ilimbidi arudi nyuma Jamal huku akijiuliza maswali maana hakuna jeraha lolote mwilini mwa Mfalme.
"Tuachane na hili swala twende tukatoe msaada kwa wenzetu huko nje." alisema Lutfiya na kuanza kutoka mule ndani. Jamal hakuwa na jinsi aligeuka naye kutoka nje.
Generali alizidi kuwapunguza askari wa Mfalme Faruk ambaye naye hakuwa nyuma kuwadondosha watu wa Eden huku akiwa anazidi kumsogelea Generali ambae hakuwa anafahamu kama anafuatwa. Hata alipomkaribia walipata kutazamana huku kila mmoja akiwa anahema sana. Walirushiana mashambulizi kadhaa kisha wakasogeleana kila mmoja akionesha kukwazika.
"Mbona unaenda kinyume na tulivyopanga Generali? Inamaana umenisaliti?" aliongea Mfalme huku panga lake likiwa limezuiwa lisipenye mwa Generali.
"Hatukupanga kufanya mauaji kwa Mfalme, tulitaka tumtoe madarakani lakini si kumuua. Mnamtumia Lutfiya ameweza kumdhuru Mfalme na kumuua, sitaweza kukubaliana na swala hilo hata kidogo." alisema Generali akiwa mwenye hasira sana.
"Nini...? Inamaana Mfalme ameuawa?" alipatwa na mshangao baada ya kusikia taarifa hizo.
"Unauhakika Lutfiya kama ndiye aliyefanya jambo hilo?"
"Nani mwengine wa kumhisi aliyekuwa na tafauti na Mfalme, alifahamu kama mnakuja ndio maana amerahisisha kazi hiyo. Alijuwa fika kwamba kuna vita itatokea." alisema Generali huku askari wao wakizidi kuchinjana bila huruma.
"Hawezi kufanya jambo zito hilo mwenyewe hana ujasiri huo. Na isitoshe kama Mfalme amekufa hakuna haja ya kumlaumu mtu lengo letu ndio litatimia kwa wepesi, kikubwa wewe ni kuungana nasi tuwe kitu kimoja, utakuwa hata waziri pindi Eden ikiwa mikononi mwetu." alisema Mfalme Faruk akimtamanisha Generali ambaye maneno hayo akayatafakari mara mbili mbili.
Jamal alipotoka mule ndani na bila kuangalia sura ya mtu. Alitumia uwezo wa kutumia upanga kuwapunguza askari wengi wa Eden. Hakika kulionesha kila dalili za Eden kushindwa angali wapo katika ardhi yao, hali iliyofanya Generali atazame majeshi yanavyozidi kupungua kila dakika. Mfalme Faruk akazidi kumshawishi awe upande wao akijua Generali ndiye mwenye kauli ya kuamrisha askari wake nini wafanye.
Wakati yanaendelea yote hayo Faraj pamoja na Samir walikuwa wameshapata ishara kwamba Eden ipo kwenye matatizo.
"Lakini ni haramu kwangu kuikanyaga Eden, tayari tumeshafukuzwa hatuna mamlaka ya kurudi tena." aliongea Samir akiwa anamtazama Faraj wakiwa kwenye jabari wamekaa.
"Siku zote mitihani lazima iwepo katika maisha, tambua kwamba ilikuwa ni changamoto tu ambazo hata huko mbeleni utakumbana nazo. Siku ile nilikueleza kuhusiana na yale niliyoota kwamba kuna pete unavalishwa, amini kwamba wewe ndiyo Mfalme mpya wa Eden na hakuna mwengine wa kuweza kuisaidia isipokuwa wewe mwenyewe.
Wanagombea Eden wakijua kuna Pete ambayo ni muhimu sana pindi ikipatikana, na kamwe hawataweza kuipata maana hawafahamu ilipo." alisema Faraj na maneno yake yakaanza kumfumbua akili Samir.
"Inamaana hakuna anayejua ilipo pete hiyo?"
"Kwasasa hakuna anayefahamu ilipo, niliwahi kufuatilia swala hilo na kusoma vitabu vingi vya kale nikapata kutambua mengi, na nilipokaribia kujua ilipo pete hiyo nilisita, maana ningefahamu ndio ningekuwa kiongozi ila nilishaapa kwamba sitakuja kuiongoza Eden. Taifa lililoua wazazi wangu nisingeweza kuwa kiongozi wao maana ningehisi nawakosea wazazi wangu." alisema Faraj huku Samir akipata kujua kumbe Faraj alikataa mwenyewe. Alitoa kiboksi kidogo Faraj kisha akampatia Samir.
"Ndani yake kuna funguo, funguo ya kuufungua mti wa ufalme. Mti uliopo ndani ya msitu ule mliotakiwa kuingia mule. Mimi naamini utafanikiwa kuipata pete hiyo endapo utakapoufungua huo mti." alisema Faraj huku akimkabidhi Samir kiboksi kile.
"Ni ule msitu tuliopaswa kutupwa! Mh, na nitaujuaje huo mti kama ndio maana ule ni msitu!"
"Muda wote unaotembea hakikisha hicho kipo mkononi mwako, ndicho kitakuelekeza hadi sehemu husika. Cha msingi ni kuwa makini tu." alisema Faraj akimueleza Samir.
Maneno yale yalimjaa akilini na kuona ana kazi kubwa ya kufanikisha zoezi hilo.
"Ila usimweleze mtu yeyote swala hili hata Maya pia, kamilisha kila kitu wewe mwenyewe na hapo ndipo watakapojua." alisema Faraj.
Samir alipata kuelewa na kushika yote aliyoelezwa. Ilimbidi anyanyuke huku akitazama mazingira ya pale walipo ndani ya Gu Ram.
"Wacha nielekee Eden, nikafanye kile ninachokiona ni sahihi na chenye kuleta amani kwa watu." alisema Samir na Faraj akasimama pia huku akimtazama.
"Naamini utafanikiwa, ipo siku utakuja kuwa mkubwa sana katika kutawala." alisema Faraj akimpa mori ya kufanikiwa Samir. Alimpa mkono kama kumuaga na baada ya zoezi hilo akakamata upanga wake Samir na muda huohuo Maya alipata kutokea na kuwaona wawili hao wakiwa wamesimama pale lakini alichelewa. Samir alipotea ghafla akimwacha Faraj pale akiwa mwenye kutabasamu.
"Faraj?" aliita Maya na Faraj akageuka kumtazama. Alisogea Maya hadi pale alipo Faraj na kusimama pale alipotoka Samir.
"Ameelekea wapi Samir mbona ghafla hivyo?" aliuliza Maya akimtazama Faraj.
"Kuna mahala ameenda ila hatachelewa kurudi." alisema Faraj akificha ukweli. Maya alikubali maelezo yale na kurudi nyuma akitazama pale aliposimama Samir, akapeleka mkono wake wa kulia kama kumpa baraka huko aendako. Lakini kitendo cha kushika tu pale chini naye akapotea, hali ile ilimshtua Faraj asijue imekuwaje.
Haraka akaanza kukimbia kurudi kwake kuangalia kwenye vitabu vya kale maana jambo lile ni ishara ya kitu fulani.
Huku Eden mambo yalizidi kwa upande wa askari wa Eden. Kwa maneno yale aliyoahidiwa Generali moyo wake ulitekwa na matamanio ya madaraka kama alivyoahidiwa na Mfalme Faruk. Na taratibu akaanza kuwajaza sumu ya maneno baadhi ya askari wake kwamba warudi nyuma na kukubali kushindwa. Kauli hiyo ilishangaza wengi ambao wanauchungu na taifa lao. Lakini Generali alisimama kwenye neno lake akiwaamuru askari wake wakubali kushindwa angali bado wana nguvu za kupambana.
Taarifa hiyo ikaanza kusambaa kwa askari wote kuwa wakubali kuwa wameshindwa. Hii inamaana kwamba majeshi yao hayana uwezo wa kupambana na majeshi ya Mfalme Faruk. Kwakuwa Generali ndiye aliyesema iliwalazimu kufuata amri huku wakijua kushindwa kwao ndio kunawapa nguvu wapinzani wao kuitawala Eden rasmi. Kauli ile iliwafanya wakina Jamal na askari wao wafurahi sana na kuona kile walichokidhamiria kinakwenda kuwa. Lutfiya alishangiria sana kuona taifa lake linakwenda kushika madaraka.
Wakati hayo yakiendelea nje huku ndani ya chumba cha Mfalme alipata kutokea Samir moja kwa moja. Alipotazama pale kitandani alishtuka kumuona Mfalme akiwa vile, taratibu akamsogelea na kuanza kumuita. Ghafla Maya naye akapata kutokea pale pale akiwa ameweka mkono chini.
Alipotazama chumba kile kwa makini alishtuka kufahamu ni chumba cha babake. Alimuona Samir akiwa pale anamtikisa Mfalme akionesha kulala. Naye akasogea hadi pale na kumfanya hata Samir ashangae maana aliondoka kule kwa siri na aliyemuona ni Faraj.
"Samir baba yangu kafa nywa nini?" aliuliza Maya na kuanza kumuita baba yake. Aliita na kuita bila kuona Mfalme kuinuka, hapo ndipo kilio kikaanza kwa binti huyo wa Mfalme huku Samir akiwa anamtazama Mfalme aliyeonekana kweli amefariki.
Huku mashariki ya mbali Dalfa alibaki kutabasamu baada ya ule uchawi aliouacha mule ndani ya chumba cha mfalme umemjulisha kwamba Samir amefika.
"Sikuachi safari hii, nachukua kila kilicho kwenye mwili wako na ndio muda muafaka wa kuimiliki Eden." alisema Dalfa akiwa kwenye chumba chake cha kufanyia ibada. Alichukua mkuki wake mrefu wenye maandishi ya kichawi na bila kuchelewa akapotea kuelekea Eden.
Hadi muda huo Eden ilikuwa tayari imeshikwa na Mfalme Faruk baada ya askari wote wa Eden kukubali kile walichoagizwa kufanya na Generali mkuu. Askari wa Faruk walipiga kelele za furaha baada ya kufanikiwa kuwanyamazisha majeshi ya Eden. Mfalme alimtazama Generali kwa tabadamu na kumsifu kwa kile alichokifanya.
Furaha aliyokuwa nayo Lutfiya haikuwa ya kawaida maana alifanya mengi sana kuihakikishia taifa lake linaikamata na kuitawala Eden kama walivyopanga. Ikawa ni sherehe ya kushangiria ushindi huo wakizunguka kila mtaa usiku ule huku wananchi wakiwa zao ndani wakichugfulia yanayoendelea nje. Kwa kuona shangwe zile zikizidi kila dakika wakaamini Ufalme wa Siddik umepinduliwa na sasa tawala mpya unaingia madarakani.
Baada ya muda ilibidi Generali awaeleze askari wake wote hali halisi ya Mfalme wao. Wote walipiga magoti chini kwa huzuni baada ya kusikia Mfalme Siddik ameuawa.
Baadhi yao walipatwa na hasira sana na kujua huenda hawa waliowavamia ndio waliofanya mauaji hayo lakini hawakuwa na jinsi wanafuata amri kutoka kwa Generali wao.
Huku ndani ya falme ilikuwa ni huzuni kwa Maya akimtazama baba yake pale kitandani akiwa tayari amekata kauli. Hali ile ilimfanya Samir akumbuke tukio la nyuma kabisa pindi Maya alipokuwa kitandani akiugua. Alihisi na hili pia laweza kuwa kama lile la awali. Alimshika mabega Maya na kumtaka akae kwanza pembeni kisha akasimama karibu na mwili wa Mfalme.
Alimtazama kwa dakika kadhaa huku Maya akiwa anajifuta machozi akionesha kuwa na uchungu.
Samir alishika masikio ya Mfalme na kuyaziba kwa vidole huku akinena maneno fulani na kuanza kubadilika taratibu macho yake yakin'gaa sana. Ilimchukuwa dakika kadhaa na hata alipotoa vidole vile moshi mweusi ulianza kutoka masikioni mwa Mfalme na hata puani. Hali hiyo ilimstaajabisha sana Maya na kujikuta akisimama taratibu huku akimtazama baba yake akitokwa na moshi ule mweusi sana ambao ulionekana kuna nafsi za viumbe wakiwa wanafurukuta kuonesha hawakutaka kutolewa ndani ya mwili ya mwili wa Mfalme Siddik. Hata baada ya kuzidi kuomba sana Samir aliutoa ule uchawi ndani ya mwili huo alipata kuona Mfalme akitapika damu iliyomshtua Maya.
Samir alichukua kitambaa na kuanza kumfuta Mfalme na hapo ndipo Maya akakumbuka siku ile ambayo alikuwa kitandani akiugua, na siku alipoamka alipata kumuona Samir akimfuta damu kama hivyo anavyofanya sasa. Akapata tumaini jipya huenda baba yake naye akawa mzima. Haraka akasogea pale na kumtazama baba yake, ilikuwa ni bahati kuonekana Mfalme akianza kupumua kwa mara nyengine.
"Amewekwa uchawi ndio maana, ni kama ilivyokuwa kwako awali." alisema Samir akiwa anamtazama Mfalme pale kitandani.
"Ni nani sasa aliyefanya haya?" aliuliza Maya huku akionekana kuwa na hofu.
"Huyu lazima atakuwa Dalfa, ndiye mwenye uwezo wa kufanya haya na nadhani hili amelifanya kusudi baada ya kufeli kwako." alisema Samir na Maya aliposikia jina la Dalfa alizidi kuogopa. Hakuna asiyemfahamu Dalfa kwa jinsi alivyo na uwezo wa kutumia nguvu za kichawi na muda huo huo Dalfa ndio alikuwa anawasili ndani ya Eden.
ITAENDELEA.......
NGOMA IVUMAYO SANA MWISHO HUPASUKA, NAONA TUNAKARIBIA KUFIKA MWISHO WA SIMULIZI YETU. KITIMTIM NDANI YA EDEN, MFALME FARUK AMESHAJIPA USHINDI NA DALFA AMESHAINGIA KUJA KUMMALIZA SAMIR, VIPI MASHABIKI WA SAMIR MUTAWEZA KUVUMILIA YATAKAYOMKUTA MTU WENU? 🙆🏻♂️ Kwavile kesho ni mapumziko basi tukutane siku ya Jumatatu tujue kilichojiri
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA THELATHINI (30)
