SEHEMU YA 08
ILIPOISHIA
Samir alijisogeza karibu na vitabu vile akawa anakitazama kile kitabu huku akiona askari wakiwa wametapakaa sehemu ile kuhakikisha kila kitu pale kinateketea kwa moto.
ENDELEA NAYO......
Alitazama kwa makini sehemu ile kuona mafuta yakianza kumwagwa na askari kwenye vitu vingine huku wakizunguka. Pembeni aliona farasi amesimama pale huku akiwa amevishwa mangozi ya kuwekea baadhi ya mizigo kama maji nakadhalika. Aliona afanye kitu ili aweze kukitoa kitabu kile pale.
Alitazama huku na kule kuangalia hakuna anayemtazama kisha akaiangalia ile pete yake na kuanza kuongea maneno kadhaa huku akiwa amefumba macho yake. Sekunde kadhaa baada ya kufumbua macho alipotupa macho yale pele mbele hakuweza kuona kile kitabu kilichokuwa pale.
Vilimwagiwa mafuta vyote vilivyosalia pale na vitu vyengine kisha kikaletwa kiberiti na kuweza kuwasha vitu vyote pale. Watu walianza kusogea nyuma na wengine kuanza kuondoka zao baada ya kuona zoezi hilo linakwenda tamati. Wale waganga walikuwa wakimalizia kusoma mambo yao pale huku moto mkubwa ukiwaka eneo lile.
Zoezi hilo walibaki wale askari wakilimalizia na taratibu baadhi yao wakaanza kurejea kwenye falme wakiwa na wale wanganga. Samir alipeleka macho kwa yule farasi aliyekuwa karibu na kitabu kile na kuona mganga mmoja ndiye amepanda juu yake wakianza safari ya kurejea kwenye falme. Naye alipanda kwenye farasi wake kuondoka na wenzake.
Huku kwenye falme Maya alikuwa juu ya falme akiitazama Eden jinsi inavyoonekana kwa chini, alipata kuuona moto ule uliokuwa ukiwaka mbele kidogo na kutambua kuwa ni oda aliyotoa baba yake. Aliwaona watu wakirejea kutoka kule na mmoja wapo akiwa Samir.
Alibaki kumtazama tu na kumuona jinsi alivyo bize na kumtazama farasi mmoja aliyepandwa na mzee mmoja.
Hakumtilia maanani sana aligeuka na kushuka kule juu na kuelekea zake chumbani kwake, alifungua mlango na kuingia moja kwa moja akajitupa kitandani huku akiuacha wazi mlango.
Lutfiya alikuwa anamchunguza sana Maya kila nyenendo anazofanya, kuna jambo alihitaji kulifanya kwa Maya ikiwa kama moja ya kazi aliyopewa aifanye na Mfalme Faruk.
Alijisogeza hadi pale mlangoni mwa chumba cha Maya akiwa anazuga kufutafuta vumbi ukutani lakini macho yake yakiwa makini kuchungulia ndani.
Alipata kumuona Maya akiwa amejilaza kitandani hali iliyompelekea Lutfiya ageuke kutazama kama kuna mtu aliyekaribu anamuona. Alihakikisha usalama huo taratibu akaingiza mkono kwenye matiti yake na kutoa kikaratasi kilichofinyagwa, akaanza kukifungua huku akionesha kuwa na wasiwasi kuogopwa kukutwa pale. Alichota unga fulani uliokuwa ndani ya karatasi ile na kuanza kumtazama Maya aliyekuwa hana analojua akiwa amejipumzisha kitandani. Akaunyanyua mkono wake ulioshika unga ule na kuanza kunyunyizia pale mlangoni kusudi Maya atakapotoka aweze kuukanyaga. Ni wazi kwamba hakuwa mwema kwa binti wa Mfalme na yote haya anayafanya kwaajili ya Mfalme Faruk.
Alipolikamilisha zoezi hilo akaanza kunuia maneno fulani pale huku akitazama pale chinii alipomwaga unga ule na mwengine kuuelekezea kwa Maya, alishangaa anasukumwa na kitu nyuma yake hali iliyomfanya haraka afiche kile kikaratasi chenye unga ule kisije kuonekana, alipogeuka kutazama alishangaa kumuona Samir akiwa amebeba tenga kubwa la nguo.
"Eh samahani kwa kukusukuma Lutfiya sikujua kama upo mbele." alisema Samir akionesha hakuwa anafahamu kinachoendelea.
"Ah wewe umefuata nini huku?." aliongea Lutfiya kwa sauti ya chini huku akionesha kuwa na hasira.
"Nimetumwa nilete nguo za Maya zimetoka kufuliwa. Ndio nampelekea, samahani kidogo nipishe" alisema Samir na kumfanya Lutfiya ashtuke kusikia hivyo, ilibidi amzuie Samir akijua kupita kwake mlangoni kutaharibu mipango yake.
"Hebu subiri kwanza, unataka kuingia nani kakuruhusu? Maya anaoga na hata mimi kaniambia nisubiri hapa nje akimaliza ndio niingie."
"Ah sasa inakuwaje.?"
"Wewe uache tu huo mzigo hapa nikiingia nitampelekea." aliema Lutfiya huku akimtazama Samir aliyeonekana kutojua lolote.
"Ah usijali Lutfiya wacha nimsubiri tu hapa hapa akimaliza nitaingia tu, nataka nikamjulie hali pia maana tangu jana sikuweza kumuona." alisema Samir na kutua lile tenga chini naye akakaa.
Hali ile ikamfanya Lutfiya amtazame Samir kwa jicho la hasira kwa kuona anamharibia mipango yake. Samir aligeuka na kuutazama mlango ukiwa wazi haukufungwa.
"Una maana Maya anaoga huku mlango ukiwa wazi kweli?" aliuliza Samir huku akimtazama Lutfiya.
"Ndio maana amenimbia nisubiri hapa mlangoni pasitokee mtu kutaka kuingia ndani." alisema Lutfiya na Samir akanyanyuka zake na kuusogelea ule mlango hali iliyofanya Lutfiya ashangae.
Aliposogea pale akaanza kutazama chini na kuweza kuuona ule unga ukionesha kumwagwa pale, hakutaka kuonesha kama ameona lolote aligeuka na kwenda kwenye tenga lake na kulinyanyua na kurudi pale mlangoni.
"Wewe Samir unataka kufanya nini?" alishangaa Lutfiya akiwa amemkodolea macho Samir, Nae hakutaka kumjibu lolotea aliusukuma ule mlango na kumfanya Lutfiya amzuie kwa kumshika mkono.
"Hebu rudi wewe..!" alionekana kupagawa Lutfiya lakini maneno yake hayakuweza kumzuia Samir kuingia mule ndani huku akiiruka ile dawa ambayo Lutfiya aliiweka pele mlangoni kwa ajili ya Maya.
Samir aliingia na kumfanya Maya anyanyuke pale kitandani na kuweza kumuona Samir akiwa amebeba lile tenga.
"Eh pole sana jamani, sasa kwanini wamekupa wewe huu mzigo uulete wakati sio kazi yako?" aliongea Maya huku akimzama Samir aliyekuwa anatua lile tenga.
"Naona wote wanafanya kazi ndio maana nikaona nikuletee nguo zako Maya." alisema Samir.
"Haya asante sana Samir." akisema Maya huku akiwa mwenye tabasamu.
"Umeshamaliza kuoga mara hii?" aliuliza Samir na swali hilo likamfanya Lutfiya pale mlangoni ashike mdomo kusikia vile.
"Mh mbona nilioga mapema sana, nipo tu nimepumzika hapa." alisema Maya.
Samir kusikia vile akageuka kutazama mlangoni alipotokea.
"Lutfiya ingia kumbe tayari alishamaliza kuoga." alisema Samir kwa sauti hadi Maya akashangaa.
Maneno yale yalimfanya Lutfiya pale mlangoni ashike kichwa kuona Samir anazidi kumharibia.
"Kafanyaje Lutfia mbona unamuita?" aliuliza Maya akiwa haelewi kinachoendelea.
"Nilimkuta hapo mlangoni nikiwa nataka kuingia akanizuia na kusema ulikuwa unaoga ndio maaa nikashangaa kukukuta umepumzika." aliongea Samir na kumfanya Maya ashangae, Lutfiya hakuwa na jinsi aliamua kuingia mule ndani na kuiruka ile dawa aloiweka mwenyewe na kufanya iharibike kile kitu alicho dhamiria kukifanya kwa Maya. Taratibu alisogea hadi pale waliposimama.
"Kwani uliingia humu Lutfiya nikakwambia naoga?" aliuliza Maya akiwa anamtazama Lutfiya aliyekuwa anatazama tu chini kwa aibu.
"Nisamehe binti wa Mfalme, sikutaka mtu akusumbue ukiwa umepumzika maana umetoka kwenye misukosuko hivyo isingependeza ukasumbuliwa." alijitetea Lutfiya.
"Hapana wala usijali kuhusu hilo, mimi nipo sawa kwasasa na huyu alikuwa analeta hizi nguo tu hakuwa na shida." aliongea Maya.
"Sawa nimekuelewa binti wa Mfalme."
"Haya mnaweza kwenda wote mniache sasa." alisema Maya na kuwafanya Samir na Lutfiya wageuge kuondoka zao. Hata waipotoka nje Samir aliongoza njia yake moja kwa moja kueleea kwake huku Lutfiya akimtazama kwa hasira sana kuona amemharibia mipango yake kwa mara pili, aligeuka na kuongoza njia yake.
Samir moja kwa moja alirudi kwenye kibanda chake na kujilaza kweye kitanda huku akishusha pumzi kwa uchovu. Aligeuza kichwa na kutazama kile kitabu akiwa amekiweka pembeni ya kitanda, taratibu alinyoosha mkono na kukichukua akawa amekishika huku akikitazama. Alikumbuka muda ule alipopeleka farasi zizini wakiwa wametoka kule mtaani kuchoma vitu vya ile nyumba ya akina Nadhra na ndio muda hata wale waganga nao wakiweza kuwaingiza farasi wao kwenye zizi hilo. Na walipoondoka ndipo nafasi hiyo aliitumia kusogea kwa yule farasi ambaye muda ule alikuwa karibu na vile vitabu kabla ya vile vitabu kuchomwa moto.
Aliweza kumshika farasi yule kwenye ile ngozi aliyovalishwa ikiwa kama ni kifaa cha kuwekea maji na vitu vyengine. Aliongea maneno kadhaa na kufanya pete ile iliyopo kidoleni kuwaka na kuweza kuona kitabu kile kwenye lile ngozi. Alikichukua na haraka akatoka mule zizini na kwenda kukihifadhi kwake, akiwa ndani alishangaa kuona pete ile ikiwa inambana sana na alipotazama aliona tukio ambalo lilikuwa likiendelea muda ule.
Alimuona Lutfiya akiwa mlangoni kwenye chumba cha Maya, hali ile ikamfanya Samir atambue kuwa kuna jambo baya Lutfiya anataka kulifanya kwa Maya, haraka alichoropoka mule ndani kama upepo na kuelekea huko kujaribu kumuwahi Lutfiya.
Yote hayo alikuwa akiyakumbuka akiwa amekishika kitabu hicho pale kitandani. Alianza kuwa na wasiwasi kuhusu Lutfiya maana ni tukio la pili sasa anapata kumuona akitaka kumfanyia Maya. Nafsi yake ilimsuta kuendelea kumnyamazia Lutfiya kwa matendo yake yale muda huo huo akanyanyuka na kuelekea moja kwa moja kumfuata Lutfia.
Huku upande wa pili Mfalme Faruk baada ya kukaa na kutafakari kwa kina kuhusu kazi aliyompatia Lutfiya kule Eden kuweza kufeli, alitafuta njia nyengine ya kulikamilisha swala hilo. Muda huo huo Jamal aliingia na kumkuta baba yake akiwa ametulia kwenye kiti chake cha kifalme akitafakari.
"Ni muda sasa umepita tangu umpe kazi yule mwanamke na sioni chochote kinachoendelea, kama imeshindikana hivyo tutafute njia nyengine ya kufanya." aliongea Jamal huku akimtazama baba yake.
"Jamal.. hili swala sio la mara moja kama unavyofikiri, elewa kwamba ile ni falme kama ilivyo hii. Tazama askari waliopo nje na ndani wakiweka ulinzi na ndio hivyo hivyo ilivyo mule ndani ya falme ya Eden. Huyu msichana anafanya kila jitihada kuweza kufanya kazi tunazompa na sio kama hafanyi, anafanya lakini kunakuwa na vizuwizi vya hapa na pale. Hivyo hupaswi kukata tamaa mapema hivyo na tambua hili swala ni kwa ajili yako hivyo ukijifanya kuwa na haraka unaweza kukosa tunacho kihitaji." alisema Mfalme Faruk akimtazama mwanaye.
"Sawa nimekuelewa, lakini tunavyokwenda taratibu tunafanya swala hili liwe gumu zaidi, hii ndio nafasi ya kuhakikisha Maya tunamteka kiakili kusudi aonekane alitoka kuugua. Sasa tukichukua muda watu wote wakamuona amerudi hali yake ya kawaida tukija kufanya jambo letu lazima litachunguzwa ijulikane chanzo." alisema Jamal na kumfanya baba yake atazame pembeni kulitafakari swala hilo.
Aliona anachoongea mwanaye ni swala la msingi sana.
"Sawa umeongea jambo la msingi sana kuujali muda, nitatuma ujumbe kwa Lutfiya aweze kujitahidi kwenye hilo." alisema Mfalme akimtia moyo mwanaye.
Huku kwa Samir aliweza kumuona Lutfiya akiwa zake kwenye koridoo moja wapitayo watu akifanya usafi.
Alimsogelea hadi pale jambo lililomfanya hata mwanamke huyo ashangae kuona anafuatwa.
"Samir una shida gani muda huu wa kazi?" aliuliza Lutfiya akiwa ameshika kitambaa akisafisha kuta za mahala pale na baada ya kumuona Samir ikabidi asitishe zoezi hilo.
"Shida yangu ni wewe." aliongea kwa kujiamini huku akimtazama Lutfiya.
"Unataka nini kutoka kwangu? huu muda sio wa kuanza kuongea lakini.!"
"Sikuja kuongea ila itakuwa ni kitendo cha mara moja tu endapo ukiniambia unataka kumfanyia Maya kitu gani?." aliuliza Samir huku akiwa anamtazama Lutfiya kwa umakini zaidi.
"Samir.. mbona sikuelewi unamaanisha nini?" aliongea Lutfiya akijifanya hajaelewa chochote.
"Kipi hujaelewa hapo? inamaana unavyofanya kwa Maya hujui, mara ya ngapi sasa nakukuta ukiwa katika matukio ya ajabu, mwanzo ulitaka kumpaka nini sijui Maya nilipotokea ukaanza kujikosha, leo tena umeweka sijui madawa gani mlangoni kwake, ulikuwa na lengo gani naye? ulitaka awe chizi au umuue?" alisema Samir akiwa amemkazia jicho Lutfiya.
"Haa jamani Samir sikuwa na maana hiyo, naomba tu tuyamalize hayo nisamehe kwa kilichotokea."
"Kwanini hukutaka niingie ndani ukanidanganya Maya anaoga?. Nataka nijue tu unampango gani na Maya au nikamwanbie mwenyewe?"
"Ah hapana nakuomba sana usiende kuongea lolote kwa Maya kuhusu mimi nakuomba sana Samir." alibembeleza Lutfiya baada ya kuona swala hilo linaweza kuwa kubwa.
"Nahitaji kujua tu ukweli yote hayo unayomfanyia Maya ni kwasababu zipi?" alisema Samir na hali ile ikamfanya Lutfiya awe mpole. Baada ya kubanwa sana aliona aeleze tu ukweli huenda asipofanya hivyo anaweza kukamatwa siku.
"Wewe Samir unafanya nini hapo muda huu.!" ilisikika sauti ya Malkia na kumfanya Samir ashtuke baada ya kujua ni Malkia, alimpa heshima yake pale huku Lutfiya akiona ndio nafasi ya yeye kuepukana na Samir. Haraka aligeuka na kuendelea na kazi yake.
"Muache mwenzako afanye kazi Samir usimsumbue, hebu nenda nje kaendelee na kazi zako huko." alisema Malkia na kumfanya Samir ageuke na kuondoka zake eneo lile akiwa ameshindwa kujua sababu za Lutfiya kuweza kufanya mambo yote hayo.
Malkia alimtazama hadi alipotokomea Samir kisha akamsogelea Lutfiya.
"Kuna jambo nahitaji kulifahamu Lutfia." alisema Malkia na kumfanya Lutfiya ageuke kumtazama Malkia Rayat kumsikiliza.
"Jambo gani Malkia wangu?"
"Ni kuhusu Maya mwanangu."
"Maya? kafanya kitu gani Maya?"
"Hapana, ni kuhusu tukio ambao lilitufanya tukeshe na kuhangaika kila sehemu kwa ajili ya tatizo lake. Waganga wamefanya kila njia kumponesha lakini ilishindikana. Nataka nijue aliamka mwenyewe au kuna sababu ambazo zimepelekea yeye kuweza kurudisha uhai tena?" aliuliza Malkia na swali lake hilo likamuweka njia panda Lutfiya.
"Malkia, nini una maanisha lakini. Mimi nadhani hayo maswala tungeyasahau kabisa maana yatakutia mawazo yasiyo na msingi, na jambo la kushukuru Maya yupo salama sasa tupo naye tena na hili ndilo tulikuwa tukilisubiri muda wote hata ukaamua kwenda Mashariki ya mbali ili Maya aweze kuamka." alisema Lutfiya akimueleza Malkia Rayat.
"Sio kwamba nimechukia kurudi kwa mwanangu laa, nina furaha sana kumuona tena akiwa mwenye tabasamu muda wote. Ila akili inafikiria mbali sana, nahisi uchawi bado unaendelea kwa mwanangu. Na huenda mtu aliyemfanya hivi mwanangu si yule mzee peke yake huenda kuna watu wengine wanazidi kumuandama mwanangu. Sina uhakika wa asilimia zote kama Maya amepona kabisa, nina wasiwasi juu ya mwanangu huenda wakawa wamempa uhuru kwa muda." aliongea Malkia Rayat akionesha kuwa na mashaka juu ya binti yake.
"Mh swala hilo sikuwa nalifikiria kabisa Malkia wangu, ila uliponiambia tu hata mimi nimejawa na hofu moyoni. Maya inabidi aangaliwe sana asiwe mwenye kuachwa tu huru muda mrefu." aliongea Lutfiya.
"Nina mpango wa kumtafutia mtu wa kuweza kumlinda, safari zake za kwenda kuzunguka baadhi ya miji akiwa na wenzake wa kawaida sitaki tena niisikie nahofia lisije kutokea kama la kipindi kile huko njiani wanavamiwa yakaanza matatizo yale yale."
"Cha msingi ni hicho apewe ulinzi wa kutosha." alisema Lutfiya akichangia mada hiyo na kumpa ushauri Malkia.
Moyoni alipata tumaini jipya la kuona kuna nafasi kumbe ya kuendelea kujaribu tena jambo kwa Maya, kama Malkia hadi sasa ana wasiwasi kuwa mwanaye huenda hajapona basi hata akimfanyia kitu alichoagizwa kufanya na Mfalme Faruk kwa Maya hatajulikana kama ni yeye bali itadhaniwa ni ugonjwa ule ule unamsumbua. Malkia aligeuka na kuondoka zake baada ya kupata ushauri kwa mfanyakazi wake huyo bila kujua si mwema upande mengine.
Wazo la kumuwekea ulinzi Maya hakubaki nalo mwenyewe akimjulisha na Mfalme Siddik swala hilo. Wakawa wanajadili namna ya kuwapata watu mahodari wa kumlinda binti yao. Njia pekee ya kulifanikisha hilo ni kutoa matangazo kwa raia ambaye mwenye nguvu na shababi wa kweli wakiandaliwa mapambano baina yao ili apatikane mshindi aweze kuwa mtu wa kumlinda Maya muda na wakati wowote. Vipeperushi vilisambaa Eden na nje ya Eden kote kuhusu mashindano hayo ya kumtafuta shababi.
Upande wa muhusika mwenyewe Maya hakupendezwa na hatua ambayo wazazi wake wameichukua. Hakupenda swala la kulindwa kila wakati maana alianza kuyazoea maisha ya kuwa na uhuru muda wote.
"Hii ni kwaajili ya kukulinda mwanangu na si vingine." alisema Mfalme akiwa chumbani kwa binti yake baada ya kumpelekeea taarifa hizo.
"Sijapenda mlivyofanya baba, muda wote nitakuwa nasimamiwa tu na mtu sitapata uhuru wa kufanya mambo yangu." aliongea Maya akiwa amenuna.
"Uhuru unaotaka wewe ndio umepelekea wewe kupata matatizo hayo, umeenda na wenzako mmevamiwa na watu huko mmerudi wachache wengine wameuliwa huko, hata siku moja haijapita na wewe ukaanza kuugua na kukupelekea ukapoteza fahamu wiki mbili nzima umetutia wasiwasi, mimi kama baba ndio nimeamua hivyo kwaajili ya usalama wako." alisema Mfalme Siddik na kugeuka kuondoka zake akiwa tayari amefikisha ujumbe huo kwa mwanaye. Maya alikasirika sana lakini na kujituoa kitandani akichukia uamuzi ule wa wazazi wake, hakupenda maisha ya kulindwa.
Taarifa za mapambano hayo zilimfikia Dalfa kule Mashariki ya mbali na kumfanya akasirike baada ya kutambua kumbe ni kweli Maya ameweza kuamka. Hadi wanamtafutia ulinzi basi ni wazi kwamba binti huyo yupo salama kiafya.
"Hili swala limewezekana vipi? Ni nani ameweza kumtoa uchawi ule bila kutumia nguvu zangu,?aaaaaah." alikasirika sana Dalfa baada ya kujua ameikosa Falme ya Eden, alijua kwa vyovyote lazima Malkia Rayat angerudi tena kwa ajili ya mwanaye hivyo lazima wangekubaliana tu kuiacha Eden iwe mikononi mwa Dalfa ambaye ndio alikuwa akitarajia hilo siku zote kuimiliki Eden taifa maarufu. Haraka akatoka zake na kwenda kwenye chumba chake cha kufanyia maombi yake huko. Hata alipofika aliufunga mlango na kuanza kubadilika sura kuwa ya kutisha sana. Alisogea kwenye karai moja likiwa kwenye moto huku likiwa na mafuta ndani yake. Alinyoosha mkono huku akiongea maneno fulani kwa lugha ya kichawi na kufanya mafuta yale yatulie kama maji angali moto unawaka sana. Alizidi kuomba huku akiwa amefumba macho yake mkono wake ukiwa umeelekea kwenye mafuta yale na dakika kadhaa alipofumbua macho yalikuwa yanangara kama macho ya paka na kwenye yale mafuta kukawa kunaonesha tukio lililopita pindi Maya alipokuwa kitandani amelala akiwa hajitambui, lengo ni kujua kitu gani kilitokea hadi kuweza kumfanya Maya akaamka.
JE! SAMIR ATAJULIKANA KUWA NI YEYE NDIYE ALIYEMSAIDIA MAYA? IKIWA NDIO ATAPEWA ADHABU GANI?
USIKOSE SEHEMU IJAYO
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA TISA (9)
