PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 7

 


SEHEMU YA 07


ILIPOISHIA


Sehemu iliyopita ya siku ya Jumamosi, kumbukumbu zinasema tulifikia Maya kazindukana na wakati huo huo Amour au kwa jina la Eden Samir akaamua kutoka mule ndani na kuwaacha waliokua wanakuja chumbani kumuangalia Maya baada ya kupata taarifa ameamka. 


SASA TUENDELEE... 


Ilikiwa ni jambo la kushangaza kwa Maya kuona kila mtu aliyefika pale akiwa anafuraha ya kumuona kana kwamba hakuweza kuwepo muda mrefu sana. Lutfiya alikuwa tu pembeni akiwatazama wenzake wakionesha kufurahi baada ya Maya kuweza kuamka. Hakupenda kabisa jambo hilo muda wote alionesha kukunja mdomo huku akijiuliza imekuwaje jambo hilo likawa ghafla hivyo aweze kuamka.


Huku kwa Maya alikuwa akisikiliza tu maongezi ya wafanyakazi baada ya kuuliza imekuwaje hadi aweze kuwa pale kitandani.

"Maya.. ni wiki ya pili sasa ulikuwa hapo kitandani, haikujulikana umezimia au umekufa maana kila mganga wa jadi unayefahamu kuwa ni hodari katika masuala hayo amefika kukutibia lakini hakuna tumaini lolote. Ikafika wakati watu tulikata tamaa na kusubiri tu matokeo yatakavyokuwa sisi tutayapokea. Maana wazazi wako wamehangaika sana kutafuta dawa walau uweze kurudisha uhai kama awali." alisema mfanyakazi mmoja akimweleza Maya. 


Alibaki kushangaa baada ya kupata kuambiwa kuwa ni zaidi ya siku kumi alikuwa amelala tu pale kitandani. Akili ilivurugika kabisa huku akitazama kitanda kile ambacho kiliweza kumbeba kwa siku zote hizo, alijaribu kuvuta kumbukumbu kuweza kujua kilitokea kitu gani hadi kupelekea kuwa hivyo lakini hakuweza kupata kumbukumbu zozote.


"Mama na baba yangu wapo?" aliuliza Maya huku akiwa ameshikilia shuka.


"Hivi tunavyoongea Mama yako alielekea Mashariki ya mbali kwenda kutafuta msaada wa kuweza kukusaidia, na tulivyosikia ni kwamba endapo watakapoipata dawa hiyo ya kukuponya wewe basi Eden inakuwa si mali ya Mfalme Siddik, kuna mtu anaitwa Dalfa na huyo ndie mtu ambaye alikuwa ana umwezo wa kukuponesha ugonjwa wako. Ulitupiwa uchawi wa kifo kabisa na ndio maana mama yako akaona bora aitoe Eden aimiliki Dalfa lakini wewe upone." alisema yule mfanyakazi.


"Uchawi? Inamaaa walitaka waniue? Ni nani huyo alifanya jambo hilo.?" aliuliza Maya akiwa anashauku ya kutaka kufahamu mhusika wa tukio hilo.


"Kuna mzee mmoja na tayari Mfalme ameweza kumpa adhabu yake, amenyongwa hadi kufa baada ya kujulikana anatumia uchawi uliokupumbaza siku zote hizo ukawa kama mfu. Hivi tunavyoongea naamini hata waganga wakija kukuona upo mzima watashangaa maana kila mmoja alikuja kutumia nguvu zake imeshindikana." alisema yule mfanyakazi na kauli hiyo ikamstaajabisha sana Maya baada ya kutambua kweli alikuwa nusu kufa.


Akawa anatafakari mwenyewe kama juhudi za kuokoa maisha yake kila mmoja alishindwa imekuwaje ameweza kuamka ghafla hivyo?

Mtu pekee aliyeweza kumuona pindi akiyafumbua macho yake ni Amour (Samir) na alipata kumuona akiwa anamfuta damu. Alikosa uhakika wa kuamini kama mtu aliyemuona anaweza kufahamu chochote kuhusu hali hiyo. Alishukuru tu kuona yupo salama kwa muda huo na taratibu wakamuandalia maji kisha wakamchukua kwenda kumsafisha mwili.


Taarifa za kuweza kuinuka binti wa Mfalme zikaanza kutapakaa jiji zima hali iliyowafanya watu washangirie sana maana walikuwa wakifanya maombi kwa ajili yake.

Hadi kufika usiku vigingi vya moto viliwashwa jiji zima kufurahia kurejea kwa binti wa Mfalme, mji wa Eden ukawa unatoa  mwanga hata kwa baadhi ya mataifa mbalimbali walipata kuona mwanga ule na kuhisi huenda kuna kitu cha furaha kimetokea. Mfalme Siddik akiwa na Malkia Rayyat waliweza kuona pia mwaga ule na kuwafanya washangae huku majeshi ya askari wa Eden wakiwa nyuma yao.


Walitazamana baada ya kutambua miale ile ya moto ilikuwa ikitoka katika taifa lao la Eden na kufahamu kuwa huenda kuna jambo zuri limetokea. Hakuna kati yao wawili aliyeweza kuamini kile ambacho wanakihisi muda huo, wakabaki kutazama tu na kuanza kuongeza spidi farasi wao ili wafike haraka maana bado ni mbali sana.


Usiku ulipozidi watu wakaanza kuelekea zao kupumzika kila mtu mahala pake. Shuhuli ikawa kwa Amour ambaye hafahamu mahala pa yeye kwenda kupumzika. Alibaki kushangaa tu akiwa amesimama huku baadhi ya askari wakiwa wanatembea huku na kule ndani ya jengo hilo la kifalme kuweka ulinzi. 

Ilibidi ajitoe akili na kumfuata askari mmoja aliyekuwa amesimama.


"Wewe Samir vipi mbona hadi sasa upo macho?" aliuliza yule askari akiwa ameshikilia upanga wake huku akiwa kwenye vazi la kiaskari.


"Naomba msaada wako  ndugu yangu, mahala ninapolala nahisi kuna nyoka sijui maana naona vitu vinagongana tu sielewi na mimi ni muoga sana wa nyoka, nisaidie kuweza kumtoa nyoka huyo." alisema Amour akiweka sura ya huruma huku askari yule akitabasamu tu. Alimtia konzi la kichwa kisha akaanza kuongoza njia yule askari. Amour alibaki kushika kichwa chake kwa maumivu makali baada ya kupigwa konzi, taratibu naye akafuata kule ambapo anaelekea askari yule.


Walifika kwenye kibanda kimoja kilichopo karibu na zizi la farasi na askari yule akasogea hadi mlangoni na kuona umefungwa na kufuli, akamgeukia Amour.


"Naona matani yamezidi sasa, huyo nyoka umemsikiaje wakati hata mlango hujaufungua?" alisema yule askari na kumfanya Amour ashangae. Hakutegemea kama ni yeye ndio ataishi kweye kibanda hicho ambacho hakikuonesha kama kuna mtu anaishi humo. Kwa hasira yule askari akamsogelea Amour na kumpiga makonzi kadhaa kichwa huku yeye akijaribu kuyazuia kisha akaondoka zake yule askari.


Alibaki kumsindikiza tu kwa macho hadi alipotokomea.

"Haaah! ina maaa humu ndio kwangi?!... Hahahaha, hili balaa sasa." alisema Amour na kuanza kusogea hadi pale kwenye mlango.


Aliingiza mikono yake mfukoni na kuona funguo moja akawa anaitazama. Alishikwa na butwaa baada ya kuona funguo hiyo ambayo anaitumia kule kwao Magogoni kwenye chumba chake. Alishindwa kuelewa imekuwaje hadi kufika pale, aliingiza kweye kile kitasa na kufungua na kushuhudia mlango ukifunguka. Taratibu akaanza kuingia mule ndani na kuwasha taa ya kandili iliyokuwa pembeni, akapata kuona kitanda cha kamba kikiwa kimetandikwa vizuri na mito ya sufi, huku pembeni kukiwa na meza yenye vitabu vingi juu yake. Taratibu akaanza kusogea pale mezani na kuvuta kiti akakaa na kushika kitabu kimoja.


Ghafla akatokea yule msichana Nadhra akiwa mwenye tabasamu huku amesimama pembeni ya Amour.


"Umenishtua! sikutegemea kama utatokea muda huu." alisema Amour akiwa anamtazama Nadhra, alisogeza kiti naye akakaa huku akishika kitabu kimoja.


"Nimekuja tu mara moja kukusalimia, naona umeanza kuzoea mazingira ya hapa Eden. Hivyo ndivyo alikuwa akiishi Samir wa awali, kila mtu alikuwa akimdharau kwakuwa ni dhaifu, ila tambua kwamba hapo ulipo unauwezo wakufanya chochote kile ambacho nguvu za kawaida haziwezi kufanya. Na kuhusu kuamka kwa Maya yoyote atakaye kuhisi au kukuuliza usiseme lolote fanya kama haufahamu kitu, Nadhani kuna watu wameshamuhisi Samir wa mwanzo." alisema Nadhra na kumfanya Amour ashangae.


"Wamemuhisu kwa lipi? amefanya jambo gani kwani.?"


"Alilaghaiwa na baadhi ya watu wa taifa fulani awe anatoa siri za ndani ya Falme. Akawa mara kwa mara anatoka na kukutana nao kwa siri kuwapa baadhi ya taarifa za siri kutoka ndani ya falme. Nadhani kuna watumishi wa Mfalme wamelijua swala hilo na wakaanza kumfuatilia tangu siku hiyo. Na nikwambie tu jambo geni kwako, Samir  mwenyewe ameuliwa na wale watu aliokuwa anawapelekea taarifa kutoka ndani ya falme na wamemzika kabisa. Hivyo hakuna yeyote huku Eden anayefahamu kama Samir ameuawa hivyo sura, nguo na muonekano wako hivyo ulivyo ndio Samir alikuwa hivyo hivyo... Wacha niondoke nitaonana na wewe siku nyengine." alisema Nadhra na kumfanya Amour atambue kwamba kumbe analitumia jina la mtu ambaye ameshafariki.


Muda huo huo Nadhra akatoweka huku akimuacha Amour akiwa ameelewa baadhi ya mambo. Alikiweka kile kitabu alichoshika na kusogea kwenye kile kitanda kujilaza na kuanza kuutafuta usingizi huku mji mzima ukiwa wenye furaha kwa tukio kubwa lililotokea.


Asubuhi kulipambazuka na kila mmoja akawa  anafanya kazi zake ambazo amepangiwa kufanya. Hata kwa Amour baada ya kusafisha maeneo kadhaa ya falme akawa anasafisha mabanda ya farasi.


Kule ndani Maya alikuwa amepambwa vizuri na kuandaliwa chakula. Akasogea mezani pale kisha Lutfia akafika kumnawisha binti huyo wa kifalme. Alikuwa akimtazama kwa jicho la chuki sana bila Maya kufahamu kama anatazamwa vile. Baada ya kumaliza kufanya zoezi hilo alitoka zale nje na moja kwa moja akaelekea nyuma ya jengo la kifalme.


Alitazama huku na kule kisha akaingiza mkono wake kwenye titi lake la kushoto na kutoa karatasi iliyofungwa kama barua. Alinyoosha mkono mbele kama anapokea kitu kutoka mbinguni na dakika kadhaa akatokea njiwa na kutua kwenye mkono wake. Haraka aliifunga ile karatasi kwa kamba kwenye mguu wa njiwa yule na baada ya kulikamilisha hilo  akaruhusu aondoke ndege huyo akapeperusha mabawa yake kuelekea sehemu, naye Lutfia akageuza na kurudi zake ndani ya Falme.


Siku hiyo majeshi ya mfalme ndio yalikuwa yanawasili Eden huku Malkia pamoja na Mfalme Siddik wakiwa mbele wanaongoza njia. Walipokelewa kwa heshima njia nzima baada ya kuingia Eden, kila mtu alishuka chini kutoa heshima kwa viongozi hao waliokuwa juu ya farasi wao wakielekea kwenye falme. Hata walipokaribia kwenye jengo la kifalme baadhi ya askari waliokuwa eneo hilo waliinama na kupiga goti moja chini kutoa heshima hiyo kwa viongozi hao.


Amour alipata kuona hilo naye akaiga kama walivyofanya wenzake kwa kutoa heshima huku mfalme akishuka kwenye farasi na taratibu akasogea kwa mkewe na kumsaidia kumshusha. Wakaanza kuongoza njia kuelekea ndani wakiwa wameshikana mikono huku Malkia akiwa na hamu kubwa sana kujua kuhusu mwanaye. Amour alibaki kuwatazama huku akitabasamu na muda huo huo akashangaa anasukumwa na askari mmoja pembeni yake.


"We boya umesimama tu hapa hebu peleka farasi zizini unashangaa tu hapa.!" alisema yule askari na kumfanya Amour akumbuke kazi yake hiyo, haraka akasogea kwa farasi wale na kushika kamba kuwapeleka kwenye zizi.


Huku ndani walipoingia moja kwa moja walielekea chumbani kwa binti yao huku wakiona wafanyakazi wa ndani humo wakiwapa heshima yao, hata walipofika baada ya kuufungua mlango ule walistaajabu kumuona Maya akiwa amepambwa vyema akiwa ni mwingi tabasamu usoni. Hali ile ikamfanya mama yake ashindwe kujizuia akasogea hadi pale na kumkumbatia mwanaye huyo.


"Oh mwanangu siamini kama upo mzima leo, nimekuwa na mashaka juu ya maisha yako Maya hadi kuamua kwenda mbali sana." alisema Malkia Rayat akiwa amemkumbatia mwanaye, alijikuta hata anatoa chozi kwa furaha baada ya kufahamu kuwa Maya ni mzima.


"Nimeambiwa yote mama, na nimeona jinsi gani umekuwa mwema kwangu muda wote umekuwa ukinihangaikia mimi niweze kurudisha fahamu, nipo salama mama yangu na nafuraha kukuona tena." alisema Maya akiwa mwenye kutabasamu huku akiwa amekumbatiana mama yake.


Mfalme alikuwa anawatazama mtu na mwanaye huku akiwa mwenye furaha, alisogea pale naye akamshika mwanaye kumpa pole kwa kile kilichotokea. Ikawa ni furaha kwao kuona binti yao yupo salama tofauti na walivyomuacha.


Baada ya muda mfalme alitoka na kumuacha Malkia mule ndani na kuelekea chumbani kwake kujipumzisha. Alianza kuwaza mambo tofauti na kujihisi alikosea kitendo cha yeye kukataa Eden isiweze kuchukuliwa na Dalfa ili binti yao aweze kupona. Alihisi ataonekana wa tofauti hasa kwa Maya endapo atakapoambiwa kuwa baba yake hakutaka kuiachia Eden yake, hivyo alikuwa radhi Maya afe kuliko kuiruhusu Eden iwe mikononi mwa Dalfa.


Muda huo huo mlango ukagongwa na askari wawili walionekana kuingia na kusogea karibu na Mfalme.


"Ehee mmefanikiwa.?" aliuliza Mfalme akiwa anawatazama askari wake.


"Hadi sasa hatukuweza kumpata wala kujua alipo. Ila wengi wanasema amekuwa akionekana mitaani mara kwa mara." alisema askari mmoja akimueleza Mfalme.


"Mmefika walipokuwa wanaishi?"


"Ndio Mfalme tumefika na hatukuweza kumuona. Na tumepata kuona vitabu vingi sana mule ndani huku vengine vikiwa havijulikani ni lugha gani iliyotumika kuandikwa mule." alisema askari wa pili wakiwa wamesimama imara kumueleza Mfalme Siddik.


"Huyu binti atafutwe pale alipo, nahisi hatakuwa kimya kwa kile tulichofanya kwa baba yake hivyo yatupasa kumuwahi mapema kumkamata. Na nyumba hiyo mtoe kila kitu ndani muvichome moto nje maana huwezi juwa kama kuna uchawi ambao bado upo umewekwa humo ndani, mkawape taarifa wale waganga muongozane nao kulifanikisha hilo swala huenda likaenda kimila." alisema Mfalme Siddik na kuwafanya askari wake wamuelewe kila anachosema. Walitii amri hiyo na kugeuka kuondoka zao kuifanya hiyo kazi. Muda huohuo Malkia Rayat akaingia na kumkuta kumewe akiwa amekaa.


"Kuna jambo linaendelea.?" aliuliza Malkia akiwa anamtazama Mfalme.


"Yule mzee mchawi tuliomuua ana binti yake aliyekuwa akiishi naye. Napata mashaka juu yake pia huenda alikua anashirikiana na baba yake. Huenda pia akawa anajipanga kufanya kitu ndani ya falme hii kama kulipa kwa kile alichofanyiwa baba yake. Hivyo nisingependa yote yatokee hayo ndio maana nimewapa kazi askari ya kumtafuta huyo binti na kuchoma moto vitu vyote vilivyomo kwenye nyumba yao, wachawi huwa na mambo ya kuacha urithi hivyo sitaki tena yajirudie kwa mwanangu yale yaliyotokea." alisema Mfalme akionesha msimamo wake, Malkia aliafikiana naye jambo hilo.


Ilibidi waongozane na wale waganga kuelekea kwenye nyumba inayosadika baba yule mchawi alikuwa akiishi humo na binti yake. Msafari huo wa ghafla ulimfanya hata Amour (Samir) ashangae na kushikwa na sintofahamu. Alishangaa pete yake aliyovaa inambana na kumfanya anyanyue mkono wake kuitazama.


"Samir nakuomba sana uende na hao watu wanataka kuingia nyumbani kwetu wafanye uharibifu. Kuna kitabu chekundu kimefungwa kwenye kitambaa nakuomba sana ukichukue wasikiharibu. Ni muhimu sana kwangu naomba msaada wako." ilisikika sauti ya Nadhra na kumfanya Samir atambue kwamba msafari ule kumbe unaelekea nyumbani kwa akina Nadhra.


Haraka naye akachukua farasi na kuanza kuwafuata wale askari wakiwa na baadhi ya waganga wao.


Upande kwa pili kwenye Taifa moja jirani na Eden lilikuwa na maadhimisho ya kuwakumbuka baadhi ya viongozi wao siku hiyo. Mfalme wa taifa hilo Faruk alikuwa akiwaongoza wananchi wake katika sikukuu hiyo ya kuwakumbuka viongozi waliotawala nchini humo.

Pembeni aliongozana na kijana wake wakiume Bilal akiwa amechorwa masizi mekundu kwenye paji la uso kama mila zao katika maombi hayo. Mila na desturi zao zilifuatwa huku  baadhi yao wakiandaa vyakula mbalimbali. Kwao ilikuwa sherehe ndani ya Taifa hilo na siku hiyo ilikuwa kubwa kwao hasa kwa Bilal ambaye alikuwa akisubiri jambo fulani kwa hamu sana. Baada ya mila kadhaa na kufanya matambiko na wazee wa zamani Mfalme huyo alinyanyuka na kijana wake na kuanza safari ya kuelekea kwenye falme yao kupumzika. Walipanda farasi wao huku nyuma askari kadhaa wakiwasindikiza kuwalinda. Waliwapita wananchi waliokuwa wakitoa heshima mtu na mwanaye huyo hadi walipotoka kwenye sehemu hiyo ya sherehe wakiwaacha waendelee kula kwa pamoja.


"Ulishawasiliana na Lutfia kule Eden?" aliuliza Bilal akiwa juu ya farasi huku akimtazama baba yake.


"Ni muda niliwatuma watu wakapate habari kuhusu lile swala lakini hadi sasa sikupata jibu kamili." alisema Mfalme Faruk akiwa anapelekwa na farasi wake taratibu kuelekea kwenye falme.


"Hili swala lisichukue muda hivyo baba tunaweza kufeli mpango wetu."


"Usijali naamini kila kitu kitakwenda sawa, namuamini Lutfia kwa muda mrefu sana hawezi kutuangusha." alisema Mfalme akiwa mwenye tabasamu.


Muda mfupi tu waliona njiwa mweupe akiwa angani na taratibu akaanza kushuka usawa ule. Mfalme alinyoosha mkono na kumfya njiwa yule atue pale mkononi mwake. Alimpekuwa na kuona amefungwa kikaratasi mguuni ikambidi amfungue na kuchukua kuifungua palepale. Aliisoma kwa umakini mkubwa huku Bilal akiwa anamtazama tu baba yake usoni akionesha kuwa makini kusoma maelezo yaliyo kwenye karatasi lile.


Baada ya muda aliweza kumaliza kusoma, alivuta pumzi na kuishusha kwa nguvu huku akimtazama kijana wake.


"Vipi kuna kitu gani kipya?" aliuliza Bilal akiwa anamtazama baba yake.


"Maya ameamka, na lile zoezi nililompa Lutfia limefeli pia, kuna mtu mule aliweza kumuona akifanya lile jambo la kumuwekea ile dawa Maya hivyo ikambidi aache." alisema Mfalme na kumfanya mwanaye akasirike sana kusikia vile. Wote wakawa hawana raha kabisa baada ya kupokea taarifa hizo maana hawakutegemea kama wanaweza kufeli mpango wao huo. Walibaki kimya kila mtu huku taratibu wakielekea zao kwenye falme.


Huku nyuma baada ya kuwasili kwenye nyumba ile askari wote wakaanza kuingia mule ndani na kuanza kutoka kila kitu kilichokuwa mule. Raia wa kawaida walishangaa jambo hilo na taratibu wakaanza kujaa sehemu ile wakishuhudia askari wale wakifanya kazi hiyo ya kurusha vitu nje kuhakikisha kila kitu mule ndani kimetolewa. Samir alijichanganya na wananchi wakawa wanatazama kinachoendelea huku macho na akili yake yote kikiwa kwenye kitabu alichoambiwa. Alisimama Mganga mmoja na kuwageukia wananchi huku akia ameshika pembe ndefu ya Tembo.


"Nyumba hii alikuwa akiishi mtu ambaye aliyeweza kumuweka uchawi binti wa kifalme na kila mtu analijua hilo, hivyo leo tunachoma moto kila kitu kilichopo huku na ni baada ya binti wa kifalme kuweza kurudi katika hali yake ya awali na sasa nimzima. Kila mtu atashuhudia kinachokwenda kutokea hapa tunachoma uchawi wote ambao uliweza kubaki humu ndani huenda ungeweza kuwadhuru hata raia wa kawaida na hata kwa falme pia. Na Mfalme ametoa zawadi nono kwa mtu yeyote ambaye ataweza kumuona binti wa mzee yule mchawi popote pale basi atoe taarifa haraka kwa askari wa kifalme haraka sana." alisema yule mzee  na kuwafanya watu wote watambue lengo hasa la askari wale kutoa vitu ndani. Walimalizia kwa kuvitoa vitabu vyote na kuvitupa sehemu moja, Samir alipata kuona kitabu kile ambacho aliambiwa ahakikishe kisichomwe moto wala kuharibika. 


Alishuhudia kuona mafuta yanaletwa na askari kadhaa kwa ajili ya kunyunyiza kila kitu vipate kuchomwa moto, wale waganga wakaanza kazi yao ya kufanya maombi pale ili waweze kuvunja nguvu zote za kichawi eneo lile.


Samir alijisogeza karibu na vitabu vile akawa anakitazama kile kitabu huku akiona askari wakiwa wametapakaa sehemu ile kuhakikisha kila kitu pale kinateketea kwa moto.


JE! ATAKICHUKUAJE KITABU HICHO? NA UPANDE WA PILI KWA MFALME FARUK, WAKIWA WANASHIRIKANA NA LITFIA, WANA SIRI GANI JUU YA MAYA? USIKOSE SEHEMU YA 08 KUPATA MAJIBU YA MASUALA HAYO

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA NANE (8)



Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group