PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 6


 SEHEMU YA 06


ILIPOISHIA


"Narudi Eden, ole wako nimkute mwanangu hali yake ipo vilevile hakika kichwa chako kitakuwa halali kwangu." alisema Malkia Rayyat akionesha kukasirika sana, aliruhusu farasi wake na kuanza kukimbia spidi kurejea Eden.


TUENDELEE


Faisar ilibidi amsogelee Samir akimtazama kwa makini, alisogea mpaka kwenye kinywa chake akimnusa huenda labda alikuwa amekunywa pombe na ndio maana amekuwa na ujasiri sana siku hiyo.

"Mbona una ninusa hivyo wewe?"


"Hebu niambie ukweli Samir, leo imekuwaje mpaka  umechangamka kiasi hicho? Na nani kakwambia kuwa sisi tupo huku?" aliuliza Faisar akiwa anamtazama Samir usoni.


"Ni yule mganga ndiye aliyetoa taarifa hizo na hadi sasa tunaongea Mfalme na jeshi lake wanakuja huku wakijua fika kuwa Malkia amekuja kwa Dalfa akubaliane naye kuitoa Eden ili Maya apone." alisema Samir na kumfanya Faisar ashtuke baada ya kujua kumbe Mfalme ameshajua.


"Sasa Maya ameponaje na wakati tulimuacha akiwa kwenye hali mbaya?"


"Ndio hivyo sasa wewe tambua kuwa Maya amepona." alisema Samir kwa ufupi hahitaji kuulizwa maswali mengi.

Faisar alipanda kwenye farasi wake  na kuanza kuondoka.


"Sasa mbona unaniacha  nipandishe na mimi." alisema Samir.


"Wewe ulikuja vipi huku?" aliongea Faisar akiwa amesimamisha farasi na kumtazama  Samir.


"Ah samahani basi endelea na safari yako muwahi Malkia haraka." alisema Samir na kumfanya Faisar asikitike huku akitabasamu. 


Hivyo ndivyo wanavyomtambua Samir kuwa kidogo ana ugonjwa wa kusahau na mtu dhaifu sana ndio maana akapewa kazi kwenye falme ya kufanya usafi ndani ya falme ikiwa pamoja na kulisha farasi majani.


Alisogea pembeni na kuitazama pete ile na kuomba apate usafiri wa farasii na punde tu akatokea farasi mweusi mbele yake hali iliyomfanya atabasamu. Alipanda farasi huyo safari ikaanza kurejea Eden baada ya kumzuia Malkia asiandike chochote kwenye mkataba ule.


Huku kwa Dalfa hakuwa na wasiwasi juu ya Maya na kuona ugonjwa alionao binti huyo hakuna wakuweza kumponesha zaidi yake maana nguvu zile anazozitumia yeye tu na hakuna mwengine, hivyo alijiamini kuona lazima watarudi tena kutaka msaada.


Njiani Malkia akiwa sabamba na Faisar walipata kuona majeshi mbele yanakuja. Waliwatazama vizuri walipata kutambua kuwa ni majeshi ya Eden yakiongozwa na Mfalme Siddik aliyekuwa mbele. Alishtuka lakini hakukuwa na jinsi ilimbidi ajikaze na kukubaliana na lawama zote zitakazomshukia kutoka kwa mumewe. 


Mfalme alisogea hadi pale alipo Malkia na kubaki kumtazama kwa hasira huku majeshi yake yakiwa nyuma.

"Umeshaigawa Eden yangu kwa Dalfa?" ni swali lililomfanya Malkia Rayyat atazame tu chini.


Faisar alimtazama Malkia wake aliyekuwa hana la kusema ikabidi amtetee.

"Mfalme wangu, Hat..."


"Naomba unyamaze wewe nikiwa naongea na mke wangu. Tena wewe ndio sababu unawezaje kumruhusu Malkia akatoka nje ya Eden bila kuniambia lolote. Mmeshaigawa Eden yangu ndio mnarudi sasa mnaenda kukaa wapi sasa,!?" alifoka kwa ukali sana Mfalme.


"Hatukufanya lolote baada ya kuambiwa Maya ame.."


"Nyamaz...! Nini? Hebu malizia ulichokuwa unakisema." alisema Mfalme baada ya kumsikia Faisar akiwa anataka kuongea kitu.


"Baada ya kuambiwa kuwa Maya amepona ndio Malkia akaacha kufanya lolote na ndio maana tunarudi kuona kama ni kweli Maya amepona." alisema Faisar na muda huohuo Samir ndio alikuwa anafika sehemu ile na kuwakuta wakiwa wamesimama pale wakiongea.


Alitazama yale majeshi jinsi walivyo wengi akabaki kuengaenga tu maana mambo hayo amekuwa akiyaona kwenye runinga tu.

"Maya amepona?  Taarifa hizo amewapa nani?" aliuliza Mfalme akistaajabu kuambiwa vile. 


Faisar alimgeukia Samir kumtazama na kumfanya Mfalme ageuke naye kumtazama Samir.


"Samir ndio katuambia" alisema Faisar na maneno yale yalimfanya Mfalme acheke sana huku akimtazama Faisar. Alishuka kwenye farasi na kuanza kusogea taratibu pale aliposimama farasi wa Samir. Alimshika farasi yule huku akiwa mwenye kutabasamu. 


Samir alikuwa anamtazama tu Mfalme jinsi alivyokuwa akifurahi, furaha ya kuona hawakuweza kufanya kitu chochote kwa Dalfa. Na yote ni kwasababu ya Samir ambaye ndiye aliyewahi kumzuia Malkia Rayyat.


Alirudi kwenye farasi wake na kumpanda kisha akageuka alipotoka akiwatazama majeshi yake aliyoongozana nayo.

"Tunarudi Eden muda huu hakuna kibaya kilichotokea. Eden bado ni ya Siddik." aliongea Mfalme huyo na kuwafanya wau wote washangirie kuona hakuna kilichoharibika.


Malkia Rayyat alibaki kutazama tu na kuona majeshi hayo yanaanza kugeuza. Alimtazama Samir ambaye naye baada ya kuona anatazamwa akawa anaangalia kwa kuibia. Safari ikaanza wote wakirejea Eden huku Malkia akiwa anamuwazia tu mwanaye kwa kile alichosikia kutoka kwa Samir.


Alikuwa na hamu ya kujua kama ni kweli au laa, na kama sivyo basi kile alichoahidi kukifanya kwa Samir lazima akitekeleze.


Huku kwa Dalfa hakuwa na wasiwasi kabisa juu ya kuimiliki Eden. Baada ya kuwasili Malkia kwake na kumueleza hali halisi moyoni alianza kujiwekea tumaini la kuimiliki Eden. Muda mchache mbele alifika mkewe ambaye ni Malkia wa Taifa hilo la Mashariki. Alisogea hadi pale alipo mumewe naye akakaa kwenye kiti chake huku akimtazama Dalfa akiwa mwenye furaha.


"Nategemea kuimiliki Eden majuma kadhaa yajayo." alisema Dalfa na kumfanya mkewe Malkia Saadie ashangae.


"Unataka kuniambia alifika hapa Mfalme wa Eden leo ?"


"Alifikia mkewe na ndio aliyetaka msaada juu ya yule binti yao."


"Sasa imekuwaje, ameshakubaliana nawe?" aliuliza Malkia Saadie.


"Alionekana wazi kukubali hadi kushika wino ili apate kuandika makubaliano yetu, gafla tu akatokea Mtumishi wake kuja kumpasha habari Malkia kuwa binti yule amepata nafuu na kuamka."


"Ati nini? inamaana ndio basi tena?" aliongea Malkia Saadie akionesha kushtushwa na habari ile.


"Haiwezi hata siku moja kutokea hivyo. Naamini uchawi ambao anao binti yule ni Dalfa pekee ndiye anaweza kuutoa kwenye  mwili ule na Eden inakuja kuwa yangu, hilo ondoa shaka Malkia wangu." alisema Dalfa akimtuliza mkewe ambaye maneno yale yalimpa tumaini la kuweza kuwa ndani ya Eden kama Malkia.


Njiani Samir alikuwa akitafakari kama kweli alichokisema kinaweza kutokea kweli au laa. Alijipa imani ya kuwa lazima Maya atakuwa salama kutokana na vile alivyoambiwa na ile pete. Alichokifanya ni kutaka kutangulia yeye kabla ya msafara huo haujafika kwenye falme ili akapate kujua kuhusu Maya. Alisogea mpaka mbele alipo Mfalme.


"Mfalme, nahitaji niwahi Eden ili nisafishe falme iwe safi maana hakuna mtu wa kufanya kazi hiyo kule." alisema Samir akiwa juu ya farasi, Mfalme alimtazama huku akiwa mwenye kutabasamu. 


Usijali nitajaribu kukutetea maana umefanya Eden iwe mikononi mwangu tena., wahi haraka kabla hatujafika" alisema Mfalme Siddik na kumfanya Samir atii alivyoambiwa.


Alimruhusu farasi wake aongeze spidi huku akimshikilia kwa nguvu asije kudondoka. Mpambe wa karibu na Mfalme alijisogeza kwa Mfalme akiwa anamtazama Samir akiwa anatokomea.

"Huyu Mfalme nina wasiwasi naye sana tangu kipindi kile cha kuwapoteza askari wetu akiwa ameongozana nao lakini mwishowe akarejea peke yake angali hawezi kupambana. Sasa leo hii huku amefikaje na amefuata nini huku?" alihoji yule mpambe aliyefahamika kwa jina la Fakiy.


"Awali nilishtuka kumuona huku Samir lakini nilipopata kutambua kuwa yeye ndiye aliyemzuia Malkia asiweze kuandika lolote kwenye ile mikataba basi sina shaka naye kabisa. Samir hana lolote analojua akili zake mwenyewe unazijua hivyo ukimtilia shaka naona ni sawa na bure Fakiy. Wacha akasafishe mabanda ya farasi usimfikirie hivyo." alisema Mfalme akiwa hana shaka na Samir.


Fakiy akabaki kuvuta pumzi na kuishusha baada ya kuona Mfalme anamuamini Samir, safari iliendelea ya kurejea Eden. Kuna mambo Samir wa awali aliweza kuyafanya na kuwapa mashaka kuwa huenda akawa anashirikiana na baadhi ya mataifa mengine na ndio maana hata Fakiy amekuwa na mashaka naye hadi leo.


Samir alipofika mbele akaona atulie sehemu na kumuweka farasi pembeni kisha akaitazama ile pete akihitaji kuona hali ya Maya kule ndani. Muda mfupi tu alipata kuletewa kuona Maya akiwa bado yupo kitandani akiwa na wafanyakazi ambao walikuwa wakihudumia kumkanda kwa maji ya moto.


Alipatwa na hofu ya kutokujiamini kama ataweza kweli kumsaidia Maya kuweza kuamka pale kitandani, alijipa moyo na kuona lazima atalifanikisha swala hilo, aligeuka kuweza kupanda farasi wake ajabu hakuweza kumuona yule farasi pale alipomuacha. Alitazama huku na kule bila kutambua alipokimbilia. Aliitazama pete ile na kuona ndio msaada kwake wacha aituie. Ilimbidi aitazama ile pete na kuomba aweze kufika Eden muda huo, alifumba macho yake na sekunde kadhaa alipofumbua alijikuta yupo kwenye zizi la farasi. Alistaajabu huku akitazama huku na kule bila kuona mtu yeyote aliyeweza kuwa karibu na mahala hapo. 


Haraka alitoka mule ndani yaa zizi na kuanza safari ya kuelekea ndani ya Falme. Alipowasili tu baadhi ya wafanyakazi walimshangaa.


"Wewe ulikuwa wapi muda wote unatafutwa, tazama maeneo yalivyo machafu hivyo, unajisahau sana Samir ndio maana unadharaulika na kila mtu humu ndani utakuwa lini wewe?" alisema mfanyakazi mmoja akiwa amebeba tenga la matunda na kuamua kuelekea zake ndani akimuacha pale Samir akiwa amesimama.


"Ina maana huyu Samir alikuwa anadharaulika sana humu ndani? Maana kila mtu Samir Samir, nami natakiwa niende na tabia hiyo hiyo ya Samir nisije kujulikana hapa ikawa balaa." alisema Amour baada ya kujua mwenye jina la Samir alikuwa akidharauliwa sana ndani ya falme. Ilimbidi naye aishi maisha hayo hayo ya kudharauliwa asije kuonekana tofauti, alipokumbuka swala la Maya haraka akaelekea ndani kujua atamsaidiaje.


Alifika ndani na kuona wafanyakazi wakiendelea kuzunguka huku na kule kumhangaikia Maya. Hakuwa anaruhusiwa kuingia ndani mara kwa mara lakini alijitahidi asipate kuonekana na macho ya watu wengi hadi alipofika kwenye mlango wa chumba ambacho binti huyo wa kifalme amehifadhiwa. Alipochungulia aliona baadhi ya wafanyakazi wakiwa wanamhudumia Maya mule chumbani.


Aliitazama pete ile nakuongea maneno kadhaa punde tu wale wafanyakazi wakaanza kutoka mmoja mmoja mule ndani. Alijibanza mahala hadi walipotoka wote naye taratibu akaingia mule ndani na kusogea hadi pale kitandani. Alimtazama Maya akiwa bado amelala pale huku sura yake ikimfanya Samir amkumbuke Aziza msichana anayesoma naye shule moja. 


Alimeza funda moja la mate na kuupeleka mkono wake kichwani kwa Maya, alishangaa kuna maneno yanatokea mbele yake.

"Yatamke maneno hayo huku ukiuweka mkono kifuani kwake." ilisikika sauti kutoka kwenye ile pete na kumfanya Samir afuate kile anachoambiwa.


Aliupeleka mkono wake kifuani kwa Maya na kuyatazama yale maneno yaliyokuwa mageni kwake akajitahidi kuyasema.

" vamos partir dentro de uma hora....vamos partir dentro de uma horaa.....vamos partir dentro de uma horaaa" aliona moshi mweusi ukitoka puani na kwenye masikio ya Maya, akabaki kushangaa tukio hilo ambalo hakutaraji kuona hivyo. 


Ghafla Maya akatema donge la damu na papo hapo akapata kufumbua macho huku damu zikimtoka mdomoni huku akiwa anahema kama mtu aliyekimbizwa. Samir kuona vile alishtuka sana, haraka akachukua kitambaa na maji ya moto kidogo yaliyo pembeni akaanza kumfuta damu ile.


"Maya.. umeamka!" alisema Samir akimtazama Maya aliyekuwa anahitaji kuinuka kuweza kukaa. Samir alimsaidia kumnyanyua huku akiweka mto ukutani Maya akapata kuegemea.


Akawa anatazama mule ndani kulivyo na kuona kuna madawa kibao yaliyokuwa pembeni, alimtazama Samir akiwa anamfuta futa damu na hapo ndipo akapata kujiona jinsi alivyo akiwa amefunikwa mashuka mazito.

"Samir.. nini kimetokea kwani mbona nipo kitandani? Na imekuwaje natokwa na damu hivi?" alisema Maya akiwa anajitazama jinsi alivyo.


Amour (Samir) hakujua amjibu nini muda huo lakini punde tu alishangaa kuona wafanyakazi wa mule ndani wakiingia na kushikwa na butwaa hawaamini kile ambacho wanakiona. 

Walianza kupiga mayowe ya furaha na kuwafanya watu wasikie huku  wakisogea hadi pale na kuanza kumkumbatia Maya ambaye muda wote alikuwa hata haelewi nini kimetokea. Nafasi hiyo ndio aliitumia Samir kutoka mule ndani baada ya kujua jambo alilopaswa kulifanya limefanikiwa. Alipata furaha kuona vile huku akitoka nje na kupishana na watu wakikimbia kuelekea kumuona Maya baada ya kupata taarifa kuwa ameamka.


ITAENDELEA.......

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA SABA (7)

Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group