SEHEMU YA 05
ILIPOISHIA
“leo nataka utoke tu niache mimi humu, ukibisha basi naenda kumwambia Malkia juu ya mambo yako.” alisema Amour akiwa hana anachojua chochote zaidi ya tukio la siku hiyo tu. Mwanamke yule kusikia hivyo ilibidi atoke tu na kumuacha Amour mule ndani.
TUENDELEE
Aligeuka na kumtazama Maya akiwa amelazwa pale kitandani na taratibu akamsogelea hadi pale na kukumbuka siku ile aliyowahi kufika hapa na akafanikiwa kumshika Maya nywele zake na gafla akajikuta amerejea chumbani kwake, lakini leo yupo dhahiri pale na kuamua kulikamilisha zoezi la siku ile, alisogeza mkono wake na kuanza kushika nywele za Maya zilizokuwa refu hali iliyomfanya Amour atabasamu na kusikia raha hasa pale aliitazama sura ya Maya ila vile vile alivyo Mrembo Aziza.
“Maya..wewe ni mrembo kweli, ila pole sana kwa hili lililo kupata” alisema Amour huku akiendelea na zoezi la kumshika Maya, Lutfiya alikuwa anachungulia kwa nje na kushudia Maya akishikwa vile.
“hee... Samir haogopi kumshika Maya, huyu anatafuta matatizo na Mfalme ngoja aonekane.” alisema huku akimtazama Amour akiendelea kumshika tu Maya.
Kwenye falme Amour anajulikana kama Samir na inaonekana ni mtu ambaye yupo kila siku na ni mfanyakazi wa nje akihakikisha kazi zote za nje kama kuwapa majani Farasi na kufanya usafi kwenye jengo la kifalme lote.
Hadi kufika mchana wa siku hiyo Malkia na mwenzake walianza kuwasili ndani ya ardhi ya mashariki ya Mbali ambapo ndipo anapopatikana mtu anayeitwa Dalfa, walizidi kuingia ndani zaidi ya mji huo na kukutana na idadi ya watu wengi maeneo ya Sokoni.
Taarifa za kuwasili kwa Malkia wa Eden zilimfikia Dalfa mwenyewe akiwa zake kwenye ibada maalumu ya kuabudu sehemu maalumu ndani ya jengo lile la falme yake. Alipopata taarifa ya kuwa Malkia wa Eden amekuja kumtembelea alishangaa sana maana Eden ni taifa kubwa mno na linasifika kwa kila kitu hasa utawala wake mkali.
Alielekea sehemu ya kukutana na wageni na kweli akapata kumuona Malkia Rayat akiwa sambamba na mlinzi wake wamekaribishwa sehemu tulivu, alifika pale na kutoa heshima kwa Malkia huyo kisha akakaa na kuanza kujadili mambo.
“Taifa lango dhalili limepata kutembelewa na kiongozi mtukufu wa Eden, ni bahati iliyoje hii” aliyasema hayo Dalfa akiwa mwingi wa tabasamu.
“ni heri kutembeleana kama hivi tukapata kujuana na kusaidiana kwa matatizo katika falne yetu.” alisema Malkia na kumfanya Dalfa atabasamu.
“huenda ikawa kweli juu ya maneno yako, nami ni miongoni mwa watu wanaosaidia sana viongozi wakubwa, kama kuna tatizo Eden basi tujuzane ili tufikie muafaka wa swala hilo.” aliyasema hayo Dalfa na kumpa nafasi ya kuongea Malkia.
“matatizo ni moja ya changamoto katika mataifa yetu, leo mimi ila kesho huenda ukawa wewe mwenye tatizo hivyo msaada kutoka moyoni unahitajika kama umeguswa na tatizo la mwenzako. Ni kweli Eden ina tatizo, na ni ndani ya falme ikinigusa mimi hasa. Ni binti wa Mfalme amepatwa na balaa, huenda nikasema ni kama amekufa hivi maana ni siku ya nane sasa inaenda kuitafuta wiki ya pili Maya amelala tu haamki, inasadikika kuna mzee mmoja aliweza kumtupia uchawi ambao ndio chanzo cha yote haya na alipobanwa ili aweze kutoa kitu alichoweka kwa Maya alikataa katakata na kuona bora afe, na kweli falme ikamnyonga... tumejaribu kila mtaalamu aweze kutoa msaada wake lakini wapi hadi tumetoa ofa kwa wananchi kwa mganga yeyote atakayeweza kufanya kazi hiyo atapata zawadi, wamejitokeza wengi mwisho hakuna kilichofanikiwa. Ni mtu mmoja tu aliyenipa ushauri kuwa huenda Dalfa akafanikisha hili na Maya akapata kuwa salama kama awali hivyo nikaona hakuna haja ya kuendelea kukaa nikafunga safari ya kuja huku lengo ni kuonana na wewe uweze kunisaidia kwa hilo” alisema Malkia kwa unyonge sana.
Dalfa alimtazama kisha akatabasamu kisha akasimama na kuanza kutembea tembea kwa kujiamini.
“kwa Dalfa swala hilo ni dogo sana na jinsi ulivyoongea nimeelewa kitu, uchawi wa kumfanya mtu awe kama amekufa ni mbaya sana na huenda muda wowote mtu huyo akafa kweli, uchawi huo alikuwa nao Malkia wa zamani Sabiha, na ni mimi ndiye mtu pekee niliyeweza kupambana naye kipindi hicho na kufanikiwa kumdhibiti na kuchukua nguvu zake, alikuwa na nguvu za ajabu sana ambazo hadi sasa nazitumia mimi, kuna mzee alikuja kuiba ujuzi wa nguvu hizo na akakimbia na baadhi ya vitu ambavyo nilivihitaji japo sikuweza kumuona, na huenda ndiye huyo mtu aliyemfanya binti yenu hadi leo awe mfu aliye hai, mmenisaidia kumuua mtu huyo sasa naimani hakuna mwenye nguvu hizo tena ni mimi pekee ndiye niliye nazo..” alisema Dalfa na kuanza kucheka sana baada ya kusikia hivyo kisha akamgeukia Malkia.
Aikuja mpambe wake Dalfa na kuleta karatasi zilizoonyesha ramani na mataifa mbalimbali kisha akampa Malkia aangalie
“tazama mwenyewe, taifa la Googolee, Nakya, Sabhaa, Niang na mengine madogo madogo, viongozi wake walikuja kwangu kutaka msaada na mikataba yao hiyo tuliandikishana kama kupeana ahadi, nawasaidia na wao wananiachia ardhi yao, ndio maana Dalfa anaitwa MFALME WA MASHARIKI mataifa hayo yote yapo chini yangu.
Nakuhakikishia Maya atapona kabisa maana damu yako haiwezi kupotea angali wewe unaona, wewe ndio mama una uchungu na mtoto wako unajua umepata tabu gani hadi Maya kufikia umri huu hivyo unatakiwa kusimama kama mama kuhakikisha mwanao anatoka kwenye umauti huo wa mateso, kama upo tayari Eden iwe chini yangu tuandikishiane hapa, sihitaji mali, sihitaji dhahabu, almasi wala silaha bali ardhi yako, ardhi ya Eden ndio kitu kinachotakiwa hapa, kama upo tayari tunaanza safari sasa hivi kurejea Eden, na kama hutolikubali hili basi subiri tu matokeo siku Saba kuanzia leo kama zikipita Maya ataitwa marehemu.” alisema Dalfa na kumfanya Malkia azidi kuchanganyikiwa baada ya kuambiwa hivyo, alitegemea ampe mali zote za thamani ili mwanaye apone lakini Dalfa alisimama kwenye msimamo wake akiitaka Eden tu.
Alimtazama mfanyakazi wake ambaye naye alikuwa njia panda akisubiri tu uamuzi wowote atakao uchukua Malkia juu ya swala hilo, alipoangalia mikataba ile ya viongozi mbalimbali ambao wameacha mataifa yao kwaajili ya kusaidiwa na Dalfa akaona kweli taifa si lolote mbele ya utu wa binadamu. Hasa yeye binti yake wa kipekee ndiye mwenye tatizo hilo. Nafsi na moyo wake ukaridhia afanye makubaliano hayo ili leo hiyo hiyo aondoke na Dalfa kwenda kumtibu binti yake.
Siku hiyo kule Eden Amour alikuwa hado ndani mule kwa Maya, baada ya kujiridhisha na kuhakikisha usalama wa Maya alitoka zake nje na kuzunguka jengo la kifalme kwa umakini.
Hakika lilivutia sana huku wafanyakazi wengi wakitembea huku na kule kila mtu akiwa bize. Alivutiwa na mandhari ya jengo hilo na punde tu akajikuta amerejea maeneo ya shuleni kwao, alitabasamu tu baada ya hali hiyo kuanza kuizoea. Alirudi zake darasani kuendelea na vipindi.
Baada ya muda wa kipindi kuisha Amour alielekea kugonga kengele kuashiria vipindi vyengine kuendelea lakini alipomaliza zoezi hilo akitaka kupiga hatua kurejea darasani alipata kuona kidole chake alichovaa pete kinambana, na alipotazama alipata kuona picha ya Malkia akiwa anatazama kwenye meza moja kukiwa na makaratasi huku akiwa anaonekana mwanaume amesimama.kumtazama.
“hii nini tena...eti..” alisema Amour akiiuliza pete ile.
“Ni Mashariki ya mbali, ndani ya jumba la Mfalme wa mashariki anaitwa Dalfa, Malkia ameenda huko kutaka msaada wa kumponesha binti yake Maya, na hiyo ni mikataba ambayo Malkia amepewa kuweka saini yake ili Maya apone, na endapo akipona basi Eden inakuwa mikononi mwa Dalfa ambaye ana mpango wake muhimu anataka kuufanya.” ilisema ile pete na kumfanya Amour akiwa amesimama pale ashangae, alistaajabu kusikia vile.
“ina maana Mfalme hata nae amekubaliana na swala hii?”
“hapana hajakubaliana nalo abadani, yupo njiani anawahi kama ataweza kumzuia Malkia kusaini, naamini hataweza kumuwahi yupo mbali sana.”
“mh sasa itakuwaje ina maana Eden inakwenda kupotea kirahisi hivi?kwani mimi siwezi kumfanya Maya apone?”
“Ni rahisi wewe kumponesha Maya, ila kama utafanya hivyo juwa kwamba maisha yako yote yatakuwa Eden.”
“mmh na kama nikiwa huko vipi kuhusu shule huku? Na vipi nyumbani si watanitafuta!”
“Amour wa huku atabaki na kuendelea kuishi na ataonekana kama Amour ila wewe ukienda kule hautakuwa tena Amour, utaitwa Samir.” ilisema ile pete na kumfanya Amour pale alipo akumbuke jina la Samir alivyokuwa akiitwa na yule mfanyakazi Lutfia.
Alibaki kutafakari achukue umuzi gani kati ya hiyo aloambiwa maana kinachokwenda kutokea ni kukubaliwa tu Malkia aweze kusaini ile mikataba.
"Kama mimi nina uwezo wakumponesha Maya kuna haja gani ya Malkia kuendelea kumsujudia Dalfa? Hapana .." alisema Amour moyoni huku akiitazama ile pete, alichokifanya ni kuomba pete ile iweze kumtoa pale alipo haraka awahi kule Mashariki ya mbali.
Punde tu akapotea eneo lile la shule na hakuna hata mmoja ambaye aliyeweza kuona tukio hilo.
Huku upande wa pili Mfalme alikuwa anazidi kuja na vikosi vyake huku akiwa juu ya farasi, kuna fikra zinamtuma huenda mkewe akawa tayari kashaigawa Eden kwa Dalfa. Akifikiria hivyo moyo unamwenda mbio anachapa farasi ili aweze kuongeza kasi zaidi huku jeshi likimfuata.
Malkia alitazama mikataba ile na taratibu akaanza kuonesha ishara ya kukubaliana naye. Alikamata unyoya wa ndege ambao unatumiwa kama kuchovya kwenye wino ili ipate kuandika kwenye karatasi. Alitazama ule mkataba na taratibu akaanza kuchovya kwenye wino apate kuweka saini yake.
Dalfa alikuwa akitazama tu akijawa na shauku ya kuipata Eden kupitia jambo hilo huku kikosi cha majeshi ya Mfalme Siddik pamoja naye wakiwa wanawasili ndani ya jiji la Mashariki ya mbali na bila kupoteza muda wakaelekea kwenye makao makuu anayokaa Dalfa.
Malkia aliona bora liwe hivyo wawe maskini lakini binti yake apate kuwa mzima. Alishusha pumzi kwa nguvu na kuanza kupeleka mkono kwenye karatasi na ghafla mlango ukapata kufunguliwa kana kwaba ameingia mtu. Wote walisitisha zoezi hilo na kuangalia mlangoni. Malkia alistaajabu kumuona mmoja wa wafanyakazi wake wa ikulu ameweza kufika hapo.
"Wewe ni nani unaingia humu bila kutoa heshima, umetokea wapi?" aliuliza Dalfa akionesha kukasirika huku akimtazama yule mtu.
Malkia alipomuona mtu huyo.
"Samir...! Umefuata nini huku wewe?" alistaajabu Malkia baada ya kumuona mtumishi wake akiwa hapo muda huo.
Taratibu Samir alisogea akaanza kusogea pale walipo huku akimtazama Dalfa kwa jicho la aina yake. Alishapata historia ya mtu huyo jinsi anavyojimilikisha ardhi za watu pindi awasaidiapo. Alisogea karibu na Dalfa kabisa waabaki wanatazamana wawili hao huku Malkia akishangaa kumuona mtumishi wake huyo dhaifu leo amekuwa mwenye kujiamini kiasi hicho. Hata mlinzi wa Malkia Faisar alibaki kushangaa jambo hilo kumuona Samir amekuwa jasiri sana.
"Dalfa.. kiongozi mwenye wadhifa mkubwa, kiongozi mwenye nguvu kubwa na tajiri wa ardhi zitokazo kwenye mikono ya koo na falme mbalimbali. Unajisikiaje kukumbatia falme za watu hivyo na kumiliki vilivyomo ndani yake kuwa vyako?. Hivi Dalfa, hauna ubinadamu wewe wa kumsaidia mtu matatizo yake hadi na wewe ufaidike kwa kumshusha mtu wadhifa wake na kumpokonya ardhi yake anayowaongoza watu! huna ubinadamu kwanini?" aliongea Samir (Amour) akiwa mwenye kujiamini bila kujali mtu huyo ana uwezo mkubwa kiasi gani.
Maneno yake yalimtia hasira Dalfa akawa anamtazama kwa ukali Samir aliyekuwa hana hata woga wa kuongea. Hata Malkia alibali kushangaa huku akiwa ameshikilia unyoya ule.
"Samir... unaongea upumbavu gani wewe mbona sikuelewi, Na umejuwaje kama tupo huku? Nani kakuleta hapa.?" aliongea kwa ukali Malkia na kumfanya Samir ageuke kumtazama Malkia Rayyat.
"Ninachokiongea Malkia wangu ni cha maana kubwa sana, huyu mtu anachokifanya sio ubinadamu hawezi kumsaidia mtu bure bila kujinufaisha na yeye." aliongea Samir akiwa mwenye kujiamini.
Alionekana wa tofauti sana maana maneno anayoongea kwao ni kama mageni. Anaona vile anavyoishi yeye akiwa Tanzania basi ndio kama wanavyoishi huko Eden na ndio sababu kuongea yote hayo akiona hakuna ubinadamu wa kusaidiana hadi walipane kwa namna hiyo.
"Naomba uniache nimalize swala hili hali ya Maya nadhani unaifahamu." aliongea Malkia huku akisogea kwenye ule mkataba aweze kuandika kukubaliana na Dalfa.
Samir alisogea hadi pale na kuichukua ile karatasi akaikunja ya kugeuka kumpatia Dalfa mwenyewe aliyebaki kumshangaa kijana huyo.
Alimtazama Malkia huku akiwa mwenye kujiamini Samir.
"Maya yupo salama ameamka." aliongea Samir na maneno yale yaliwashtua wote mule ndani.
"We Samir.. unachokiongea una uhakika nacho au?" aliongea Faisar akiwa pembeni mwa Malkia.
"Umesemaje..Maya ameamka?" alistaajabu Malkia akiwa anamtazama Samir hadi kudondosha ule unyoya.
Dalfa habari zile zilimshtua na kutoamini kile asemacho yule mtumishi wa Malkia huku akimtazama kwa makini.
"Ninachokisema ni cha kweli kabisa Malkia na ndio maana nimefika hapa kukupatia taarifa hii, Maya amepona hivyo tunaweza kurudi tu Eden." alisema Samir na kumfanya Dalfa aangue kicheko pale wakageuka kumtazama akionekana kufurahi.
"Hivi ugonjwa uliopo kwa Maya mnaujua au mnausikia!. Waganga wenu wangapi wametaka kumtibia wakashindwa na mwishowe wanawaambia muende kwa nani!. Hahahahaha....Dalfa ndiye mtu pekee anayeweza kumfanya Maya akaweza kuamka. Ila kama hamtoamini hakuna shida rudini Eden mkaendelee kumuuguza mgonjwa wenu ila mtarudi tena hapa hahahahaha." alicheka sana Dalfa na kusogea kwenye kiti chake kukaa.
"Nendeniii mnachelewa." alisema Dalfa akiwa mwenye kutabasamu hali iliyomfanya Malkia awe njia panda.
Samir hakutaka kusubiri tena alimsogelea Malkia na kumkamata mkono hali iliyowashangaza watu wote mule ndani. Akaanza kuongoza njia akiwa na Malkia wakitoka nje, Faisar mwenyewe alibaki kushika mdomo kuona mtumishi wakiume amemshika Malkia mkono wake jambo ambalo haliruhusiwi kwa mtu yeyote kumshika Malkia zaidi ya Mfalme Siddik.
Alibaki kumtazama tu usoni huku akiwa anapelekwa tu na Samir wakitoka hadi sehemu walipo wahifadhi farasi zao.
"Hebu niache wewe, nani kakupa ruhusa ya kunishika kiasi hiki! Hivi leo umeingiwa na ujasiri gani wa kufanya vitu hivi kwa kujiamini." aliongea Malkia akiwa amekasirika kwa kushikwa vile.
Hakuwa anajua Samir kama lile ni kosa kubwa sana alilofanya ikabidi azoee sasa sheria za huko taratibu. Alijirudi na kuwa mpole huku akiomba samahani kwa kile alichokifanya. Malkia alipanda kwenye farasi akiwa amenuna sana.
"Narudi Eden, ole wako nimkute mwanangu hali yake ipo vilevile hakika kichwa chako kitakuwa halali kwangu." alisema Malkia Rayyat akionesha kukasirika sana, aliruhusu farasi wake na kuanza kukimbia spidi kurejea Eden.
ITAENDELEA.
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA SITA (6)
Je! Vipi Amour, atasalimikaje na hili suala wakati yeye ndio yupo huko huko?
