SEHEMU YA 04
ILIPOISHIA.......
“Amour, karibu sana Eden..” alisema Nadhra na kumfanya Amour atabasamu baada kuanza kuzoea sasa hali ile.
“asante sana” alisema Amour.
ENDELEA NAYO.......
“leo ni siku kubwa sana kwako na naamini utaifurahia, sijui kama utalikumbuka jina langu.” Alisema Nadhra na kumtazama Amour ambaye alilisahau jina la mrembo huyo, lakini alipotambua uwepo wa pete ile akajikuta akiuliza moyoni na kutajiwa.
“unaitwa Nadhra” alisema Amour na kumfanya Nadhra atabasamu baada ya kujua sasa mhusika anaanza kuzoea zawadi aliyopewa.
“nimefurahi kwa wewe kulijua jina langu, karibu tena Eden.” alisema Nadhra na kumfanya Amour atazame kile chumba walichopo, kulikuwa na vitabu vingi sana vimepangwa kama Maktaba.
“na hapa ni wapi tulipo?” aliuliza Amour na kumfanya Nadhra anyanyuke na kuanza kutembea.
“ni chumba ambacho baba yangu alikuwa akitumia kusoma mambo ya kale na kupitia vitabu hivi na hata kuvifanyia kazi.” alisema Nadhra akishika shika vitabu, ilimbidi Amour naye asimame pale alipo na kuanza kutembea tembea kuangalia baadhi ya vitabu hivyo.
“baba yako alikuwa msomi na mpenzi wa kusoma vitabu eh?”
“bila shaka, alipenda sana kuiga mambo ya zamani maana anaamini hapo zamani watu wa Eden waliishi kwa amani na upendo tofauti na sasa”
“mh kwani sasa wanaishi vipi?”
“hakuna uhuru kama mwanzo, awali kulikuwa na watu waliokuwa na zawadi za asili uwezo na nguvu za ziada kuliko viumbe wengine, na walizitumia kusaidia watu na mambo mema na ni wachache sana waliotumia nguvu hizo kuwadhuru watu, lakini Eden ya sasa haiangalii huyu mbaya wala mzuri wao wakikujua kuwa una uwezo huo wakikukamata hukumu yako ni kama aliyopata baba yangu... walimnyonga mpaka kufa.” alisema Nadhra na kumfanya Amour ashtuke na kujiwa na huruma baada ya kufahamu kumbe baba yake na msichana huyo amefariki.
“pole sana Nadhra.. na unataka kuniambia hata wewe pia una nguvu hizo kama za baba yako?” aliuliza Amour na kumfanya Nadhra aitike kwa kutikisa kichwa kuwa anazo pia.
“na imekuwaje mimi niwe hapa Eden, nahusiana nini na mambo yenu haya?” aliuliza Amour na kumfanya Nadhra amsogelee na kuushika mkono ule uliokuwa na pete, akashika kile kidole na kuivua ile pete kiulaini kabisa hali iliyomfanya hata Amour ashangae maana ilikuwa kazi kweli kuitoa pete ile.
“hii ndio sababu, siku ambayo baba yangu anapewa hukumu ya kunyongwa ndipo siku ambayo pete hii ilipata kuwa kwenye kidole chako, niliagizwa na baba kuwa kama nahitaji kuwa naye kiroho basi niitupe pete hii kwenye kengele yeyote ile iwe ni kama njia moja wapo ya kumpata tena lakini katika kutafuta kwangu kengele nilikosa nilisikia sauti ya kengele ikipigwa kwa mbali hivyo nikaamua kuitupa pete hii juu angani nikiwa na imani ifike kwenye mlio niliousikia, na kwa bahati ni wewe ndiye uliyekuwa ukipiga kengele shuleni kwenu na ndio maana pete ile ikajivisha kwenye kidole chako. Hiyo ni bahati kwako na hata baba yangu amefurahi kwa kuweza kumfanya aishi tena japo si kama zamani.” alisema Nadhra na kumfanya Amour afahamu sasa ukweli wa pete ile.
“ina maana.. nilivyokuwa napiga kengele shuleni mlio ulifika hadi huku? Duuh ama kweli maajabu."
"huo ndio ukweli, na kwa kuwa umeweza kumfanya baba yangu awe anaishi kwa namna nyengine basi ameridhia yeye uwe badala yake.”
“badala yake? kivipi yaani, niwe mimi ndio baba yako?” alisema Amour na kumfanya Nadhra aachie tabasamu.
“sina maana hiyo, maana yangu ni kwamba zile nguvu zake zote wewe ndiye utakaye kuwa nazo kwa sasa na yeye amesharidhia hivyo.” alisema Nadhra na kumfanya Amour avute funda moja la mate kwanza maana ameshaambiwa fika kuwa wenye nguvu hizo wakikamatwa adhabu yao ni kunyongwa mpaka kufa.
“naomba niulize swala moja tu...lengo hasa ni nini la mimi kutaka nirithi nguvu za baba yako, kuna kitu gani kinaendelea hapa kati ambacho mimi sikijui?”
“iko hivi, kama nilivyo kueleza awali baba yangu ni mtu anayependa kusoma vitabu vya kale, alipokuwa akiisoma Eden ya zamani iliyokuwa ikiongozwa na Wafalme kama Yassir, Saleh na malkia Samira uongozi wao ulikuwa wa upendo muda wote baina ya raia na ufalme, vilevile nguvu hizi zilikuwa kwa watu wengi ambao walikuwa huru kwa kujilinda wao wenyewe na kusaidia wengine hasa katika matatizo ya kifalme, tofauti na sasa wanataka kuua kabisa mambo hayo na Mfalme awe ni mtu wa kuogopwa na watu wake siku zote jambo ambalo halikuwepo hapo awali ndani ya Eden. Eden imegeuzwa sio Eden ile ya uhuru wa watu na ndio maana baba yangu akatumia njia ya kumuadhibu Mfalme kwa kumsababishia binti yake asipate kuamka kitandani kwa muda wa masiku mengi ili akubali na kuwaachia watu wenye nguvu za asili waendelee kuishi kama wengine na si kuwanyonga kama anavyofanya, hivyo basi wewe ndio utakuwa mtu pekee wa kuhakikisha swala hili linakaa sawa utumie akili na nguvu utakazopewa kumshawishi Mfalme Siddik akakuelewa” alisema Nadhra kwa kina zaidi kumuelewesha Amour ambaye aliyasikia yote na kujua sababu ya yote haya.
Alimkumbuka yule binti wa kifalme aliyemuona kweli akiwa kitandani tu kumbe aliyefanya haya ni baba yake Nadhra na lengo ni kumfanya Mfalme Siddik akubaliane na matakwa yao, akaona kweli kuna haja ya kufanya jambo ili haya mambo yawe sawa watu wapate kuwa na amani na Eden yao. Alitafakari kwa kina na kuona wacha ajitoe kimasomaso kama nguvu atakuwa nazo basi hakuna haja ya kuogopa.
“sawa... nitakuwa na wewe katika swala hili Nadhra.” alisema Amour kwa ujasiri na kumfanya Nadhra afurahi akamsogelea na kumkumbatia kwa kuona ameeleweka.
Basi taratibu za kupatiwa nguvu za mzee yule zikafanyika ndani ya chumba kile ambapo Amour ilimbidi alazwe kwenye meza ndefu kisha Nadhra akaanza kufanya maombi yake kwa kutumia nguvu za ajabu, roho ya mzee wake ilifika nayo ikaanza kutoa sasa nguvu zake zote na kumkabidhi rasmi kijana huyo ambaye alikuwa akitokwa na jasho jingi sana mwilini na hata baada ya muda alipoteza fahamu baada ya zoezi lile kukamilika.
Upande wa pili ilikuwa ni msako kila mahala ndani ya Eden baada ya kufahamika Malkia pamoja na mfanyakazi wake mmoja kutojulikana walipotokomea, askari wa kifalme walienda mpaka mipakani kwa Eden kuwatafuta wakizunguka na farasi zao huku na kule bila mafanikio jambo lililomfanya Mfalme azidi kuchanganyikiwa maana mwanaye mgonjwa na mkewe pia ndio hivyo akihisi amepotea. Hakuwa nyuma na yeye alihakikisha anashiriki zoezi hilo kikamilifu kuhakikisha Malkia anapatikana. Yule mzee aliyempa ramani Malkia ya kufika kwa Dalfa alikuwa tu kimya muda wote akificha ile siri japo moyo wake unamuuma sana kuona Eden inakwenda kuuzwa na Malkia, hadi askari na Mfalme walipoanza kukata tamaa jioni kabisa ikiingia ndipo mzee yule uzalendo wa kuficha siri ile ukamshinda ilimbidi amueleze ukweli wote Mfalme Siddik ambaye baada ya kuambiwa hivyo alistaajabu.
“ATI NINII?..”
“Ndio hivyo Mfalme wangu, Malkia aliniziba mdomo nisiongee kuhusu swala hilo lakini kwa akili yangu naona Eden inakwenda kuwa mikononi mwa Dalfa jambo ambalo sidhani kama utaliafiki na ndio maana nimeona bora nikueleze tu ukweli.” alisema Mzee yule na kumfanya Mfalme akasirike sana kusikia hivyo.
Hakutaka hata kuchelewa aliandaa jeshi la watu elfu moja naye akiwemo na kuanza safari ya ghafla kuelekea huko Mashariki ya Mbali kuwahi kama wataweza kulizuia jambo hilo ambalo Malkia aliwahi kwenda huko mapema.
Alifika mbali sana na mfanyakazi wake na walikwenda mbele walipata kuona kijiji kimoja ikabidi wasogee hapo na kutafuta mahala pa kupumzika kwanza maana usiku ulishaingia.
Walifika kwenye nyumba moja ambayo ilikuwa karibu na njia ya kuelekea na safari yao ikabidi wafike hapo kuomba hifadhi, walimkuta Mzee mmoja ambaye baada ya kuwaona akafahamu ni watu wanaotoka Eden.
Mpambe wa Malkia aliyeitwa Faisar ndiye alikuwa akiongea na mzee yule na kumueleza kuwa aliye naye ni Malkia wa Eden, mzee yule kusikia vile ilibidi atoe heshima kwa Malkia Rayat na kuweza kuwakaribisha ndani, Aliwaandalia chai ya moto usiku ule na Malkia pamoja na Faisar wakapokea na kuanza kunywa huku maongezi ya hapa na pale kwa mzee yule yakiendelea.
“Eden inakumbukwa hapa kijijini kutokana na matukio ya nyuma yaliyowahi kutokea, kuna mwanamama mmoja alikimbia kutoka Eden na kuja kujihifadhi hapa akiwa na watoto wawili na ilisadikika mtoto mmoja alipewa na Mfalme wa kipindi hicho akimbie naye maana walizaliwa mapacha na mmoja ilibidi auawe kama ilivyo mila za Eden kipindi hicho, sasa waasi kusikia hivyo ilibidi wamtafute mama huyo na kufanikiwa kutambua kuwa alikuwa kijiji hichi, walichokifanya ni kuchoma moto nyumba zetu ikawa ni vita sasa na kwa bahati Mfalme aliwasili na kuanza kuwadhibiti akishirikiana na wanakijiji hadi wale waasi wakatoweka lakini waliacha majonzi kwenye kijiji waliua watu wengi na kuharibu mali zetu kipindi hicho ningali kijana.” alisema Mzee yule akisikilizwa kwa makini.
“nilipata kusimuliwa hayo matukio aisee kumbe ni kijiji chenu ndio kimekumbwa na balaa hilo, poleni sana.” alisema Malkia akiwa ameshika kikombe.
“tushapoa na ndio hivi tunaendelea na maisha mapya hayo yalipita muda sana.” alisema Mzee yule na maongezi yakaendelea.
“haya mlikuwa mnaelekea safari ya wapi?” aliuliza Mzee yule na kumfanya Malkia amtazame Faisar.
“tunaenda mbali kidogo na mji kuna mtu tunaenda kuonana naye ndio maana tukaona wacha tutafute hifadhi kwanza ili hapo kesho mapema tuweze kuendelea na safari.” alisema Faisar.
“ahaa basi sawa mtapumzika hapa usiku huu na hapo kesho mtaweza kuendelea na safari yenu” alisema mzee yule na kuwafanya Malkia na mfanyakazi wake wamshukuru kwa ukarimu wake, waliandaliwa sehemu ya kulala na mzee yule ambaye alionekana kuishi mwenyewe tu.
Asubuhi kulipo pambazuka baada ya kutoa shukran kwa Mzee yule Malkia alitoa kidani cha dhahabu na kumkabidhi mzee yule kama shukrani kwake na safari ikaanza tena kuelekea huko.
Huku nyuma Mfalme alikuwa na askari wake aliotoka nao kwenye falme kuelekea nao huko huko Mashariki ya Mbali kuwahi kumzuia Malkia asije kufanya lolote na Dalfa.
Upande wa pili kwa Amour asubuhi ya siku hiyo akiwa zake darasani akiendelea na masomo yake alipata kuona kuna mwanga wa kung'aa ukitokea kwenye pete yake hali iliyomfanya ashtuke na kuamua kuiziba pete ile kwa mkono wa pili. Ilimbidi aushushe mkono huko chini ya dawati na kutazama pete ile ikimuonesha binti wa kifalme Maya akiwa bado amelala pale kitandani huku pembeni akionekana mfanyakazi mmoja aliyekuwa akimhudumia lakini akionekana kuwa na wasiwasi huku akichungulia huku na huku ili asionekane.
Alitoa kichupa kidogo ambacho kilikuwa na unga fulani kisha akaukoroga kwenye maji yaliyopo kwenye bakuli huku akiwa mwenye wasiwasi. Amour akahisi huenda mtu yule akawa si mwema kwa Maya.
“wewe unataka kufanya nini hapo?” alisema Amour kwa sauti na kufanya darasa zima wageuke kumtazama.
Aliponyanyua kichwa akashangaa kuona anatazamwa na ghafla wanafunzi wakaanza kuangua kicheko huku Mwalimu wa Hesabu aliyekuwa ubaoni ilibidi amshangae Amour.
“wewe una kichaa? Unaongea na nani?” aliuliza Mwalimu yule na kumfanya Amour akose jibu la kusema, hakutaka tena kukaa alinyanyuka na kusogea mbele kwa mwalimu.
“nahisi sipo sawa naomba niende nje mwalimu” alisema Amour na bila kujibiwa akafungua mlango na kutoka nje akikimbia hadi uwani. Aliitazama ile pete na kuona bado yule mfanyakazi anakoroga ule unga kwenye maji.
Alitamani kupotea tu ghafla atokee kule lakini alishindwa afanyeje, akajikuta akikasirika na kukunja ngumi kwa mkono ule aliovaa ile pete kuona huenda kuna kitu anafanyiwa Maya, na kitendo cha kukunja ngumi tu akapotea ghafla na kutokea pale pale chumbani ambapo Maya alikuwa amelala. Na kweli alimuona mwanamke yule akiwa anaingiza kitambaa kwenye yale maji aliyochanganya na unga ule na kutaka kumkanda kanda Maya.
“wewe unataka kufanya nini?” alisema Amour na kumshtua yule mwanamke akatupa kile kitambaa na kurudi nyuma, alipomtazama Amour akajikuta akijenga tabasamu.
“ah hehe.. Samir umefikaje hapa...ah nilikuwa namfutafuta Maya jasho.” alisema yule mwanamke akionekana kutokuwa na amani.
“nini..? umeniitaje....Samir?” aliuliza Amour baada ya kusikia akiitwa jina tofauti na lake.
“hee sasa unataka nikuite nani?” alisema mwanamke yule na kumfanya Amour ajishangae kwanza. Ajabu alipojiangalia akajiona yupo kwenye mavazi tofauti na nguo zake za shule, alikuwa kwenye mavazi ya kizamani nguo zilizoishaisha hadhi yake zikiwa zimechakaa, hakika alistaajabu sana kujiona vile na alipoangalia kidoleni kwake pete ile kama kawaida ipo.
Alihisi huenda ndio ilivyopangwa iwe hivyo na kuendelea kumtazama yule mwanamke.
“sasa mbona umeshtuka sana hadi ukatupa kitambaa, kuna kitu kinachoendelea hapa?”
“mh wala hakuna kitu, umenishtua tu” alisema mwanamke yule.
“sawa, ila naomba nimfute mimi jasho leo Maya wewe kafanye kazi nyengine.”
“hapana wewe kazi zako ni nje na si huku ndani hivyo huwezi kufanya hivi hata Mfalme au Malkia akikuona huku utapata tabu, nenda zako tu.” alisema Mwanamama yule aliyefahamika kwa jina la Lutfiya na kuokota kile kitambaa.
Amour akaona ni ujinga kumruhusu huyu mtu aendelee na jambo lile, alimsogelea na kumpokonya kile kitambaa kisha akachukua yale maji yaliyo changanywa kwa unga ule na kuyamwaga. Lutfiya alishangaa huku akiyatazama maji yale.
“haa yaani unamwaga maji yaliyoandaliwa kwaajili ya Maya?“
alisema yule Lutfiya na kumfanya Amour amtazame kisha akamsogelea zaidi mpaka.
“ndio nimemwaga, ulitakaje sasa, ninaweza nikayapiga deki haya nikupake mwilini mwako ili nione ulitaka kumfanya nini Maya” alisema Amour akimtia mkwala yule mwanamke ambaye kusikia vile akahisi huenda jambo lake alilotaka kulifanya limejulikana.
“basi Samir tuyaache hayo, naomba na leo nitunzie siri hii kama umeona chochote, nakuomba sana na nitakulipa kama vile tulivyolipana.” alisema Lutfiya na kumfanya Amour ashangae.
Maneno yake yalimfanya ahisi hapa kati kuna kitu kinaendelea na huyu mama si mwema kwa Maya.
“nakuomba utoke nje tu kwanza.” alisema Amour na kumfanya hata yule mama ashangae.
“mimi nitoke nje tena Samir?..siwezi kutoka tena wewe mfanyakazi wa nje ndio utoke umesahau sheria za Falme?.. siwezi kufanya tena jambo hili."
“leo nataka utoke tu niache mimi humu, ukibisha basi naenda kumwambia Malkia juu ya mambo yako.” alisema Amour akiwa hana anachojua chochote zaidi ya tukio la siku hiyo tu. Mwanamke yule kusikia hivyo ilibidi atoke tu na kumuacha Amour mule ndani.
ITAENDELEA
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA TANO (5)
