SEHEMU YA 31
ILIPOISHIA.....
Alikosa nguvu ya kuendelea kusimama Lutfiya akaenda chini kama mzigo huku damu nyingi zikimtoka. Maya alibaki kumtazama tu na kidogo moyo wake ukapata kutulia baada ya kulifanikisha zoezi hilo kwa mikono yake huku akishuhudia Lutfiya akikata kauli pale pale.
ENDELEA NAYO......
Huku chini mapambano yalizidi kushika kasi. Safari hii hakuna askari wa Eden aliyemheshimu Generali baada ya kujua kuwa alikuwa akishirikiana na upande wa pili ambao ni adui kwao. Kwa upande wake yeye hakuona haja ya kuhofia lolote ilibidi ashirikiane na Mfalme Faruk kulikamilisha zoezi wanalotaka lifanikiwe.
Huku Samir alikuwa ni zaidi ya katili, aliweza kupunguza askari wa Mfalme Faruk kwa kasi zaidi na kwa muda mfupi sana huku akizidi kusogea mbele zaidi. Na mwishowe akapata kukutana na mtu na baba yake wakiwa mbele wanamtazama Samir aliyeonekana kubadilika kabisa hata macho yake kuwa makali. Mfalme Faruk aligeuka kumtazama mwanaye Jamal ambaye hakutaka hata kusubiri alisogea na upanga wale bila kuhofia jambo.
"Sitojali unauwezo kiasi gani nitahakikisha nakumaliza, huwezi kutuvurugia mipango yetu angali tushayakamilisha na kuwa na furaha" alisema Jamal akiwa amekamata panga lake sawiya.
"Kwani kitu gani kimewafanya hadi muitamani Eden angali mnataifa lenu kubwa tu.! Kwanini mnakuwa na mioyo ya tamaa, tazama umemuua Mfalme ndani ya Eden, unamuua kiongozi wa taifa nini unategemea kwa wananchi wake." Alisema Samir akiwa anahasira moyoni.
"Ni pete... Ndicho kitu kikubwa tunachokihitaji sisi na ndio maana tunaitaka Eden kwa hali na maili. Pete ya Mfalme wa Eden wa enzi na enzi ndio tunaitaka sisi, tukiwa ndani ya taifa hili tunauwezo wa kuitafuta kujua wapi ilipo. Usifikirie kutajwa kuwa wewe ndio Mfalme ukadhani utakuwa hivyo kweli,. Huwezi kuiongoza Eden angali unatumia uchawi. Uchawi katika taifa hili ni kosa kubwa sana nadhani wafahamu hivyo. Halafu wewe.. Si ulifukuzwa na mkapewa adhabu ya kutorejea tena Eden. Imekuwaje umerudi tena.!" aliongea Jamak kwa kupaniki, hakika hakufurahishwa na uamuzi wa Mfalme Siddik kumchagua Samir kuwa ndiye Mfalme wa Eden bila kujali kama alikuwa mwenye adhabu. Hali hiyo ndiyo ikamfanya Jamal kummaliza Mfalme kwa upanga wake kwa hasira baada ya kutangazwa vile.
"Huwezi kubishana na Mfalme Siddik kwa maamuzi yake, huenda ameona ninamsaada kwa watu wake ndio maana amenikubali na kunichagua. Na hapa unaponiona naiongoza Eden kama Mfalme hivyo usifikirie unaongea na Samir yule wa zamani." maneno hayo yalizidi kumuumiza Jamal, hakutaka kusikia mtu mwengine yeyote anaikamata nafasi hiyo. Alinyanyua upanga wake kwa hadira na kumfuata Samir aliyebaki kumtazama Jamal akiwa kwa hasira zote, hata alipofika wakaanza kuoneshana kila mtu uwezo wake wa kupambana.
Maneno yale yote yaliyoongelewa pale yalimfanya Dalfa ashtuke baada ya kusikia kumbe Samir tayari ameshatangazwa kuwa ndiye Mfalme mpya wa Eden. Akaona njia pekee ya kumdhibiti kijana huyo ni ile ambayo Jamal anapambana naye. Haraka na kwa uwezo wa ajabu akapotea pale na kujibadili kuwa kivuli kikimfuata Jamal akiwa anazidi kujitetea pale kwa Samir. Hakutaka kuendelea kupoteza nguvu zake Samir aliamua kuachia pigo ambalo lingeweza kumuangamiza kabisa Jamal aliyekuwa akitumia upanga wake bila mafanikio. Aliachia shambulizi la aina yake na muda huo huo kivuli hile cha Dalfa kikaingia mwilini mwa Jamal na haraka akakinga mkono wake na nguvu zile za kichawi alizotumia Samir zikadunda pale.
Alishangaa Samir kuona vile maana hakutegemea kama binadamu wa kawaida angeweza kuzuia shambulizi hilo.
Alirudi nyuma Jamal huku akijitazama mwili wake akijihisi ni wa tofauti. Alijiona ni mwenye hali ya hasira dhidi ya Samir, haraka isiyo ya kawaida akamsogelea Samir na kupambana naye, safari hii hata Samir alishangaa kuona Jamal amekuwa na uwezo wa kupambana naye. Alipata kutambua kuwa Jamal yule wa awali sio wa sasa pindi alipojaribu kumkita panga la kifua na papo hapo Jamal akapotea na kutokea upande wa pili wa Samir. Hali ile hata Mfalme Faruk alishangaa maana ni uchawi ndio unatumika kufanya jambo hilo. Huku askari wa Eden walizidi kupambana na askari pinzani kwa kila jitihada zao. Wakimfikiria Mfalme wao jinsi alivyouawa kinyama hawakuwa na huruma nao tena. Askari kadhaa wakamzingira Generali akiwa ameshikilia upanga wake, aliwatazama askari wake na kuona ni vijana wake aliokuwa anawafundisha mapambano lakini leo imekuwa tofauti baada ya yeye kuwa upande wa pili. Askari wale bila kuuliza wakaanza kum shambulia Generali bila kumtazama usoni.
Walipambana kwa pamoja hawakutaka kukubali kushindwa mbele ya mwalimu wao huyo. Generali alikuwa akiwadhibiti askari hao kwakuwa ameshajua uwezo wao hivyo hakuwa anatumia akili nyingi. Askari wale walipoona wanazidi kupunguzwa ilibidi waongezeke tena wengine zaidi ya hao. Hali ile ilimfanya hata Generali ashushe pumzi akihema kwa kwa kuchoka. Hawakutaka kumpa nafasi ya kupumzika walizidi kumuandama.
Huku kwa Mfalme Faruk alikuwa akiendelea kupambana na askari wengine. Hakika siku hiyo ilikuwa ni ya aina yake huku wananchi wakichungulia madirishani usiku ule wa mbaramwezi.
Jamal alikuwa akiwashangaza watu wengi kwa kuonekana akipambana na Samir ambaye alifahamika kutumia nguvu za kichawi. Hata Maya baada ya kutoka mule ndani aliweza kuona Samir akiendelea kumdibiti Jamal aliyeonekana kuwa na uwezo mkubwa. Hali ile ikamfanya Samir atambue hapambani na Jamal yule aliyemzoea, ilimbidi atumie nguvu na akili za ziada kuhakikisha anamdhibiti mpinzani wake.
Huku kwa Generali mambo yalianza kuwa magumu, askari wa Eden walimuandama mkubwa wao huo aliyeisaliti Taifa lake na kuwa upande wa adui zao. Walimshambulia General huyo ambaye alijitahidi kuwazuia lakini mwishowe nguvu zilimuisha na kuanza kuruhusu kujeruhiwa katika baadhi ya sehemu za mwili wake kwa mapanga. Alirudi nyuma na kushuhudia damu zikichuruzika mgongoni na sehemu za mikono yake.
Alikamata panga lake vyema na kumeza mate huku akiwatazama askari wale waliokuwa hawana masihara juu taifa lao. Umakini wao na umoja ulijidhihirisha pale ambapo Generali akipotaka kuendelea kupambana nao na wakafanikiwa kumkata misuli ya mguu na papo hapo akaenda chini akipiga magoti. Hakuweza tena kusimama muda ule na taratibu akasogea askari mmoja aliyekuwa akiwaongoza wenzake, akawa anatazamana na Generali aliyekuwa ametapakaa damu mwilini.
Hakutaka kuongea naye tena maana ingemfanya amuonee huruma, alinyanyua upanga wake juu na kuupitisha kwa nguvu shingoni kwa Generali aliyekwenda chini kama mzigo huku damu nyingi zikitapakaa pale chini na ndio ukawa usiku wa mwisho wa maisha yake.
Askari wale walitazamana kila mtu akiwa anahema kwa kazi nzito hadi kuweza kummaliza aliyekuwa Kiongozi wao.
Huku kwa Samir alizidi kupambana na Jamal ambaye alionekana kuwa shapu kuliko vile alivyozoeleka. Samir baada ya kutambua kuwa anayepambana naye si mtu wa kawaida akaamua kuzidisha ujuzi na kuzitoa nguvu zake za ziada alizonazo. Hali ile ikamfanya hata Dalfa aliyekuwa ndani ya Jamal ashtuke. Uwezo ule wa Samir ulimfanya Dalfa atambue kuwa kuna nguvu za ziada anazo kijana huyo hivyo lazima ahakikishe usiku huo anamtia kila kitu alichonacho Samir ili apate kuwa yeye pekee mwenye uwezo wa kila kitu.
Muda huo huo Faraj akapata kuwatokea eneo hilo. Alipata kujua kinachoendelea ndani ya Eden na kujua Samir atakuwa yupo matatizoni. Hata alipotazama mbele yake alimuona Samir akizidi kupambana na Jamal ambaye alionekana kuwa makini sana. Hakutaka kuchelewa haraka akasogea mahala pale na kumfanya hata Samir ashangae. Jamal alirudi nyuma akiwa amekamata upanga wake.
"Elewa kwamba unapambana na watu wawili hapa." alisema Faraj huku akimuangalia Jamal akiwa anahema akiwatazama.
"Nililijua hilo mapema ndio maana nimekuwa makini." alisema Samir.
"Huyu nitapambana naye wewe nenda kule msituni kaitafute ile pete, nadhani ndio yenye umuhimu sana." alisema Faraj akimweleza Samir ambaye akapata kuyaelewa maneno yale. Alihofia kuondoka pale huenda akamwachia mtihani mkubwa Faraj. Faraj akampa imani ya kuwa asihofie lolote hali iliyomfanya Samir kuridhia.
Dalfa akiwa ndani ya mwili wa Jamal alibaki kutazama tu asijue kinachoongelewa pale. Aliona Mtoto yule akipiga hatua kadhaa kusogea mbele huku Samir akiwa nyuma, taratibu aligeuka na kuondoka zake kuanza safari ya kuelekea kwenye ule msitu usiku ule.
Dalfa kuona vile akataka amfuate kujua wapi anapoelekea Samir lakini alishangaa kuona mahala pale waliposimama kukiwaka moto pembeni uliozunguka duara, hata yeye alishangaa ikambidi ageuke kumtazama Faraj aliyekuwa amesimama tu akimuangalia.
"Nishakufahamu kuwa wewe ni Dalfa, na lengo lako hasa ni kuichukua ardhi hii iwe mikononi mwako." alisema Faraj akiwa anamtazama Dalfa aliyekuwa kwenye mwili wa Jamal.
"Wewe ni nani?" aliuliza Dalfa akiwa mwenye kushangaa. Faraj alisogea tena hatua kadhaa mbele akiwa mwenye hasira sana.
"Mimi ndiye niliyestahiki kuwa na nguvu hizo ulizonazo, ila kwa ujanja na tamaa zako ukaiba kutoka kwa baba yangu na kuamua kwenda mbali kuunganisha taifa lako. Unatumia vibaya uwezo ulonao na kuamua kuwanyonya
watu na mali zao, kwani huwezi kumsaidia mtu hadi umyang'anye mali yake. Baba hakuwa hivyo hata kidogo, na nilipata kuambiwa ni wewe ndiye ulimuwekea uchawi Maya ili uje kuichukua Eden pindi watakapokuja kuomba msaada kutoka kwako. Baba yangu alipokea adhabu ya kunyongwa bila kosa lakini alijua nini anafanya, ila kwahilo tu utalipa na sitaweza kukusamehe." alisema Faraj akionekana kuwa hasira.
Dalfa alimtazama na kubaki kucheka mwenyewe. Kauli za mtoto huyo zilimfanya hata yeye ashangae na kuona ni vitisho vinavyoongelewa pale..
"Hadi sasa najikuta mwenye tabasamu, nakaribia kuitawala Eden na nimepata kufahamu kumbe kulikuwa na wengine waliokuwa wanaitaka ardhi hii. Tafadhali mtoto wangu usitafute matatizo yasiyo na lazima." alisema Dalfa na kutaka kupotea eneo lile lakini Faraj kwa uwezo wake akamzuia jambo ambalo hata Dalfa hakutegemea kabisa. Hapo ndipo akafahamu kumbe anayeongea naye anauwezo mkubwa sana kama alionao Samir. Ilimbidi ageuke kumtazama vizuri Faraj pale aliposimama akionesha kujiamini. Dalfa akaona kuna haja ya kupambana na kijana huyo azichukue nguvu hizo kabda ya kumaliza kwa Samir. Aliandaa shambulizi lake imara lakini aliona akirushwa kwa nguvu na upepo mkali hadi kudondokea kwenye moto.
Kitendo kile kilimkasirisha Dalfa na kunyanyuka haraka huku akitumia uwezo wake kuuzima moto ule uliokuwa ukitanda kwenye nguo zake. Naye akaanza kujibu mashambulizi na ikawa ni vita ya kutumia uchawi. Huku askari wa Eden walikuwa wakiwamalizia baadhi ya watu wa Mfalme Faruk ambaye muda huo alikuwa amewekwa kati na askari kadhaa wakiwa wamemzingira. Alibaki akihema sana kutokana na kupambana kwa muda mrefu. Aliitazama idadi ile ya askari na kuangalia pembeni kuwaona jinsi askari wake wanavyozidi kumalizwa. Alimuangalia mwanaye Jamal na kuona jinsi anavyopambana na mtoto Faraj wakioneshana uwezo walionao. Alitazama upanga wake ulio mkononi mwake na kuukamata sawasawa.
Alinyanyua upanga wake na kuendelea kupambana na askari wale. Wingi wao ulimfanya hata Mfalme ashindwe kuwamudu, walimbana na kufanikiwa kumdhibiti akaenda chini baada ya kupata majeraha kadhaa. Damu zilimchuruzika kutoka mwilini na kubaki kuzitazama tu. Alivuta nguvu zake na kujaribu kuinuka lakini haikuwa rahisi, walipita askari wawili haraka na kumkata tumboni pamoja na shingoni na papo hapo akaangusha upanga wake kwa kukosa nguvu, akaenda chini kama mzigo na ndio ukawa mwisho wa Mfalme Faruk.
Maya pamoja na wafanyakazi wa mfalme wakaanza kuwasaidia baadhi ya askari waliopata majeraha kwenye vita hivyo na kuwaweka mahala pamoja.
Huku upande wa pili Dalfa alizidi kushindana na Faraj muda wote, hata yeye aliona ni dharau kubwa kwa mtu kama yeye kushindwa na mtu wa rika lile. Aliona atumie njia mbadala ya kumkabili Faraj maana amekuwa ni hatari.
Alichokifanya ni kujigawa mara mbili huku akitumia nafsi ya Jamal pia wakaanza kupambana na Faraj pale. Awali ilikuwa ni ngumu kwa Faraj kuweza kuwamudu watu hao wawili. Alijikuta akishambuliwa kwa haraka sana hali iliyomfanya arudi kwanza nyuma kujipanga. Haikuwa kazi rahisi usiku huo hasa kwa Faraj ambaye alifahamu kuwa anapambana na nafsi zaidi ya moja pale. Hivyo ikamlazimu kuwa makini sana dhidi ya mhusika mkuu wa yote hayo Dalfa ambaye akili yake ilikuwa kwa Samir na kutofahamu alipoelekea. Ilimlazimu kuzidisha kasi ya mashambukizi kwa Faraj kusudi amfuate alipoelekea Samir.
Hilo alilifahamu Faraj na kuzidi kumbana Dalfa asiweze kutoka mule katikati ya moto.
Huku kwa Samir alikuwa ameweza kuukaribia msitu ule, aliutazama jinsi ulivyokuwa mkubwa na wenye kutisha usiku ule. Sauti za wanyama wakali zilisikika na kuleta hofu hasa kwa binadamu apitaye karibu na msitu huo. Ila kwa Samir ilikuwa ni lazima kuingia ndani ya msitu kuitafuta pete ile inayosadikika ni ya Mfalme wa zama hizo. Hata alipofika kwenye njia ya kuingilia ndani alibaki kutazama tu huku akishusha pumzi kutoa hofu iliyoanza kutanda moyoni. Taratibu akaanza kupiga hatua kuingia ndani ya msitu ule huku milio ya wanyama wakali ikisikika usiku ule.
Kwa uwezo alionao Samir alipoingia ndani ya msitu ule alinyoosha mkono wake mbele ukapata kuangaza mwanga kutoka kiganjani kwake na kuruhusu kutanda mbele yake. Kitendo kile kiliwafanya hata baadhi ya wanyama wakali waliokuwa kando yake watambue kuwa kiumbe huyo si wa kawaida. Alitoa kile kiboksi alichokabidhiwa na kukifungua akikielekezea mbele yake huku akitazama. Alianza kuelekezwa mahala pa kuelekea ambako ndipo anapaswa afike. Simba na wanyama wakali wengi walikuwa wakimtazama tu huku sauti zao kali zikisikika lakini hawakuwa na nguvu hata ya kumsogelea Samir pindi anapotembea. Haikuwa safari fupi kama alivyodhani alizidi kutembea zaidi kuingia ndani huku akiwa anatazama huku na kule akioishana na wanyama wengi ambao walikuwa wakimtazama tu. Hadi alipofika sehemu moja ambapo alipata kuona mwongozo alioushika ukionesha eneo hilo. Alitazama sehemu ile na kuona kuna miti mitatu mirefu sana na ikambidi asogee karibu. Kitendo cha kusogea tu eneo lile yalitokea majoka matatu marefu na yenye meno marefu huku yakirusha moto kutoka kwenye vinywa vyao. Hali ile ilimuogopesha Samir hadi kuruka kurudi nyuma. Walionekana kuwa na hasira sana na kila mmoja wapo alikuwa amesimama wima katika mti wake...
NINI KITAJIRI HAPO...?
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA THELATHINI NA MBILI (32)
