PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 32


 


SEHEMU YA 32 (MWISHO) 


ILIPOISHIA..... 


Kitendo cha kusogea tu eneo lile yalitokea majoka matatu marefu na yenye meno marefu huku yakirusha moto kutoka kwenye vinywa vyao. Hali ile ilimuogopesha Samir hadi kuruka kurudi nyuma. Walionekana kuwa na hasira sana na kila mmoja wapo alikuwa amesimama wima katika mti wake.


ENDELEA NAYO..... 


Alibaki kuwashangaa nyoka wale na kuona kuna mtihani kwake wa kusogea pale.


"Mbona sikupata habari juu ya nyoka hawa imekuwaje tena?" alijiuliza Samir akiwashangaa nyoka wale wakiwa wenye kutoa cheche za moto huku wakisimama wima. Alitazama kile kiboksi na kuona mahala anapotaka kufika ni kwenye mti ule wa katikati na hakukuwa na njia nyengine ya kufanya zaidi ya kwenda pale pale ili aweze kukamilisha zoezi lake la kuipata pete hiyo. Alisimama imara Samir na kushusha pumzi kwanza kuutoa uoga wote ulioanza kumtawala, alinyanyua kile kiboksi na kukifungua, kukaanza kuonekana miale ya mwanga ikichomoza kutoka kwenye kiboksi kile. Miale iliyofanya hata nyoka wale washtuke baada ya kuiona.Tararibu wakaanza kunyongea chini na kupoa kabisa. Hali ile ilimfanya hata Samir atambue ni utii wao na kuheshimu kile alichobeba. Tayari alisogea hadi pale kwenye ule mti na kuona wale nyoka wakimpisha wakakaa pamoja sehemu wakimuangalia Samir anachokifanya.


Bila kuchelewa akaanza kuutazama mti ule kwa makini kutafuta mahala ambapo ataweza kupitisha funguo ile ipate kuingia. Ilimchukua muda mrefu kutafuta hadi alipokuja kufanikiwa kupata alishukuru. Alichomeka ufunguo ule na muda huo huo yule nyoka wa katikati akaanza kutoweka ghafla akiwaacha wenzake wakiendelea kumshuhudia Samir.


Muda mfupi tu ule mti ukajigawa katikati na kuonekana mwanga mweupe ndani yake uliofanya kionekane kilichopo mule ndani. Samir hakuamini baada ya kuona kuna pete ambayo ilikuwa imewekwa katikati ya mti ule ikiwa inavutia. Alinyoosha mkono kuichukua pete ile huku akiwa mwenye kutabasamu. Wale nyoka walipata kushuhudia pete ile ikishikwa na Samir, hawakuwa na kazi tena ya kufanya taratibu wakaanza kutoweka huku Samir akiwa anaitazama pete ile kwa tabasamu kubwa.


Huku Eden ngoma bado ilikuwa nzito kwa Dalfa dhidi ya Faraj. Japo ni mdogo kiumri lakini uwezo wake alionao ulimfanya aheshimike na hata kumtoa jasho Dalfa muda wote. Akaona hapa atakosa kote kote ni bora apotee kumfuata Samir ambaye ndiye mwenye umuhimu naye.  Aliwatazama askari wa Mfalme Faruk waliokuwa tayar wameuawa pale chini, alichokifanya ni kuwaweka uwezo kama wake askari watano na muda huo huo wakanyanyuka na kusogea pale alipo Dalfa na kuwapa amri ya kumvamia Faraj nao wakafanya hivyo. Huku yeye alijitoa mwilini mwa Jamal na kumuacha akidondoka chini kwa uchovu maana ametumika pasi na kujua lolote. Haraka Dalfa akapotea eneo lile akifuata harufu tu kujua wapi alipoelekea Samir.


Huku Faraj aliachiwa kazi ya kupambana na askari wale wengi lakini muda huo huo askari wa Eden nao wakafika pale kuungana naye.


"Kuweni makini hawa wamepewa nguvu za kichawi!" alisema Faraj kuwaambia askari wale ambao walimuelewa na bila kusubiri wakanyanyua panga zao kuingia tena vitani kupambana na askari wale wa Faruk.


Upande wa pili katika falme ya Joha muda huo alikuwa ametulia na kijana wake Rahim wakiwa na baadhi ya makamanda wa majeshi yao.


"Nahisi hadi kufikia kesho yule mpumbavu aliyemchukua Maya wakaondoka atakuwa amedhibitiwa na Mfalme Siddik. Maana hawezi kumdhuru Mfalme akijua ni baba wa Maya, hivyo nafasi hii ndio sisi tunaitumia kukamilisha zoezi letu.. Baba .. mimi naamini kesho tunakwenda kufanya mapinduzi makubwa sana Eden na tutaichukua tu kuwa mikononi mwetu. Tukifanikiwa tu basi swala la kuitafuta pete ile lazima tutaipata tu na hakutakuwa na mtu yeyote wa kututisha." alisema Rahim akionesha kuwa na uchu wa kuimiliki Eden. 


Baba yake Mfalme Joha alibaki kumtazama tu na kushusha pumzi.

"Rahim mwanangu, mimi nadhani tusilazimishe kitu ambacho hakiwezekani. Yule kijana tumeshafahamu kuwa anatumia uwezo wa nguvu za kichawi kamwe hatuwezi kupambana naye. Mfano mzuri ni pale tulipopeleka askari wa kwanza wakauliwa wote, tupate funzo kupitia hili kwamba hata kungekuwa elfu hatuwezi kushindana kwa nguvu hizo. Isitoshe anasaidiana na mwenzake hivyo inakuwa ni hatari katika maisha yetu angali hapa tunaishi kwa amani. Kama shida yako ni binti wa Mfalme kumuoa na amekiri kwamba hakuhitaji basi tusilazimishe kitu ambacho hakina faida katika familia yetu. Nakuhitaji sana mwanangu uje kuiongoza falme hii, achana na mambo hayo tena angalia ufalme wako ambao siku chache unakuja kuuongoza. Askari hawa ni muhimu sana katika kutulinda katika siku za baadae hatupaswi kuwapoteza kwa jambo ambalo haliwezaniki. Nakutegemea wewe na wewe ndiye uliyebaki baada ya mama yako kufariki hivyo sitapenda nikupoteze na wewe." alisema Mfalme Joha akimsihi mwanaye aachane na habari za kurudi tena Eden kuanzisha vita.


Alinyanyuka pale alipokaa na kuelekea zake chumbani kwake akimuacha Rahim na baadhi ya askari pale wakiwa wamekaa. Alinyanyuka kwa hasira baada ya kuona baba yake amebadili maamuzi waliyokubaliana.


"Hapana siwezi kuliacha swala liende tu kirahisi angali tumepoteza wenzetu kwa swala hili. Hakuna kumsikiliza baba yangu ni mimi ndiye ninayetoa amri ya kwenda Eden kesho alfajiri... sawa..!" alifoka Rahim na kutoa amri hiyo. Askari walitazamana tu na kutii kile alichosema.


Huku kwa Samir alianza kutoka nje ya msitu ule huku akiwa ameshika pete ile ya Mfalme wa kwanza wa Eden. Safari hii pindi alikuwa anapita kwenye njia ndani ya msitu ule hakukuwa na mnyama wala ndege aliyeweza kupaza sauti yake ikapata kusikika. Wote walikuwa kimya wakijua anayepita eneo hilo ni mtu mkubwa sana hivyo inawalazimu kumpa heshima yake. Hakika hata yeye binafsi alipata kuona raha yake na kuona kweli pete ile ina heshima kubwa mpaka kwa wanyama wa msitu ule ambao unaogopwa.

Alipotoka nje ya msitu ule alipata kukumbana na sura ya Dalfa akiwa amesimama mbele huku akiwa ameshika fimbo yake ndefu yenye maandishi ya kichawi.


"Hongera sana kwa kuingia ndani ya msitu huu na kutoka ukiwa hai. Ni wazi kwamba kile ulichokifuata umekipata ndio maana umetoka muda huu. Nimefurahi kukuona ukiendelea kuishi ukiwa na afya tele hivyo sitapenda nikudhuru mwili wako kijana wangu. Nipatie hicho ulichokipata huko ulipotoka." alisema Dalfa akiwa anamtazama Samir aliyebaki kusimama tu. Dalfa alimtazama Samir mkononi na kuona kile kiboksi akiwa amekishika. Kwa haraka isiyo ya kawaida alifika pale na kumpora kiboksi kile hali iliyomfanya hata Samir ashangae na kubakia kucheka tu, Dalfa alikifungua kiboksi kile na kufanikiwa kuiona pete ikiwa mule na funguo.


"Siku zote nimekuwa nikitaka jambo hili litimie, naamini nakwenda kuwa yule niliyetaka niwe. Kwa kuipata pete hii sidhani kama hata hizo nguvu ulizonazo zitaendelea kuwa katika mwili wako. Nashkuru kwa kunitolea pete hii maana nisingeweza nafahamika mimi ni nani.!" alisema Dalfa na kutoa ile pete na kuanza kuiweka kwenye kidole chake huku akiwa mwenye kutabasamu. Akimtazama Samir ambaye hakuonesha dalili zozote za kumzuia kuichukua pete ile hali iliyomfanya hata Dalfa mwenyewe ashangae.


Taratibu Samir alisogea karibu na Dalfa akiwa hana wasi hata chembe.

"Siku zote ubaya hulipwa kwa ubaya, matendo ambayo umewafanyia watu kuwadhulumu vitu vyao leo ndio unafika kikomo. Ulijifanya unajua kila kitu basi kuna wanaojua kidogo lakini chenye faida sana. Sina sifa za kuupata ufalme kwa faida yangu mimi laa, nipo kwa ajili ya kuwasaidia watu wengine pia ili tuwe kitu kimoja.... Pete ya Mfalme wa Eden hii hapa ninayo kwenye kidole changu mimi." alisema Samir akionesha kiganja chake kuonesha pete aliyovaa ikiwa kidoleni.


Hali ile ikamfanya Dalfa ashangae na kugeuka kuitazama pete aliyovaa yeye muda huo. Alishangaa kuona pete ile ikianza kujibana na kufanya kukiminya kidole chake. Taratibu akaanza kuona moshi ukianza kutoka chini ya unyayo wake na kuanza kupanda juu taratibu. Alishangaa sana tukio hilo na kujikuta miguuni akijiona mwepesi sana huku moshi ule ukizidi kupanda kwenye magoti.


"Umenifanya nini wewe mpumbavu!!!" alijikuta akipandwa na jazba baada ya hali ile kushuhudia ikimtokea.


"Hizo nguvu zilizopo kwenye mwili wako sio zako. Hivyo hapo ndio zinakuaga kwa mara ya mwisho zirudi kwa mwenyewe. Usishangae Dalfa haya ndio malipo yako kwa yale uliyofanya." alisema Samir akiwa anamaanisha kweli. Kauli hiyo ikamfanya Dalfa ashangae na kuona ni dhahir nguvu alizonazo zinazidi kunyonywa tu kwa pete ile. Alijaribu kuzia lakini haikuwa rahisi hadi kuangusha fimbo ile alioishika. Alijaribu kupotea arudi katika ardhi yake lakini ajabu alishangaa kujiona amerudi Eden tena pale ambapo alipotoka akishuhudia wale askari aliowaweka nguvu wakianza kuwa wachovu ghafla. Hali hiyo ikawafanya askari wa Eden watumie nafasi hiyo kuwakata kwa mapanga hadi kuwamaliza wote, Jamal alikuwa tayari katumiwa sana na Dalfa hivyo hakuwa na nguvu za kuendelea kupambana hali iliyomfanya ashambuliwe na kuuliwa kiurahisi sana na askari wa Eden. 


Dalfa alibaki kutazama tu asielewe afanye nini huku moshi ule ukizidi kupanda na kufika tumboni. Muda huo huo Samir alitokea naye akiwa amekamata fimbo ile ya Dalfa aliyoiangusha kule. Askari wote wakawa wanatazama kinachoendelea pale huku Maya akisogea taratibu hadi akiposimama Faraj wakiwa wanamtazama Dalfa.


"Huyu mnayemuona hapa ndiye Dalfa.. mtu ambage ameleta tafarani nyingi sana ndani ya Eden. Huyu ndiye aliyemuwekea uchawi Maya akawa kitandani kwa majuma kadhaa kama amekufa, lengo akijua Mfalme na Malkia watamtafuta ili aweze kumsaidia Maya naye aichukue Eden. Huyu ndiye aliyemuua Mfalme Siddik hadi sasa mwili wake upo ndani. Hii yote ni tamaa ya kuitaka Eden. Sidhani kama mtu huyu anastahiki kuendelea kuishi kwa hiki alichokifanya." alisema Samir na taratibu wananchi wakaanza kufungua milango ya nyumba zao kutoka nje kwenda kushuhudia kinachoendelea baada ya kujua mambo yamekuwa shwari. Walifika eneo lile na kumshuhudia Dalfa mwenyewe. Kwa wale waliokuwa wakimfahamu walishangaa kuona leo amekamatika kirahisi. Hasira alizonazo Dalfa alitamani kufanga jambo lakini haikuwa rahisi. Pete aliyoivaa mwenyewe haikuwa ya kawaida, ilizidi kunyonya nguvu zake zote na muda huo huo ule moshi na pete ile vikapotea na kumuacha Dalfa akiwa amesimama pale. Faraj na Samir walitazamana na kufahamu kwasasa Dalfa hana kitu chochote mwilini mwake hata yeye mwenyewe alishangaa kuona amekuwa tofauti na alivyo mwanzo. 


Hapo ndipo Samir akatoa amri auawe kwa kunyongwa lakini Maya akazuia. Watu wote walimtazama Maya kuona amezuia Dalfa asiuliwe. Hata yeye Dalfa aligeuka kumtazama Maya kuona huruma ile aliyonayo, akapiga magoti akizidi kuweka kuruma ili apate kusamehewa. 


Maya alichukua upanga wa Faraj na kumsogelea Dalfa akiwa pale amepiga magoti.

Hali ile ikamfanya Dalfa aangue kilio kuona anakwenda kuadhibiwa kifo. Hata alioposimama karibu yake Maya alibaki kumtazama Dalfa aliyekuwa na sura ya huruma.


"Nakuomba sana Maya.. sitaweza kufanya lolote kuanzia sasa.. nisamehe Maya nakuomba." alisema Dalfa kwa huruma ya hali ya juu. Huruma ambayo haikuweza kumbadilisha Maya kile alichokusudia. Mtu aliyemfanya awe kitandani muda mrefu leo hii anamuomba msamaha, mtu aliyemuua Mfalme ambaye ni baba yake leo hii anahitaji kusamehewa. Hakuweza kusikiliza kauli yeyote kutoka kwa Dalfa na bila huruma aliupitisha upanga wake kwenye shingo ya Dalfa na kutenganisha kichwa na kiwiliwili pamoja na kuacha damu zikiruka na kuchafua nguo za watu wa pembeni, papo hapo Dalfa akaenda chini na ndio ukawa mwisho wake.


Watu waliangua shangwe baada ya kuona Eden imerudi katika mikono salama tena. Askari pamoja na wananchi wote wakaenda chini na kuweka vichwa vyao chini kumpa heshima Samir kama Mfalme wao mpya. Hata Faraj pamoja na Maya wakafanya hivyo na kumfanya Samir aangushe chozi la furaha kuona amekamilisha kazi aliyoipanga kuifanya. Hakika usiku huyo ulikuwa ni wa furaha kwa kila mtu japo askari wengi wamepoteza maisha kwa vita hiyo ya usiku.


Iliwabidi wananchi wakisaidiana na askari kuanza kukusanya maiti za askari wao na kuwahifadhi mahala huku maiti za adui zao wakiwachukua na kwenda kuwatupa mbali maporini.


Iliwabidi Samir na Maya waingie ndani sasa kuutazama mwili wa Mfalme Siddik, ni wazi kuwa amefariki na kuwaachia majonzi watu wake. Maya alilia sana kumpoteza baba yake lakini haikuwa na jinsi jambo hilo limefanyika. Ilimlazimu Faraj arudi kule kwenye kijiji chake cha Gu Ram kwenda kumpa taarifa Malkia Rayyat ambaye alishtuka kusikia hivyo. Huzuni na majonzi yalimuandama baada ya kutambua mumewe ameuawa. Bila kusubiri wakaanza safari ya kurejea Eden kwaajili ya mazishi ya mumewe.


Eden nzima taarifa hizo zilisambaa na kila mtu alilia kwa jinsi alivyokuwa akiongoza taifa hilo Mfalme wao. Basi taratibu za mazishi zikaanza kufanyika usiku ule  ili panapokucha Mfalme aweze kupelekwa kuzikwa. 

Na alfajiri ya siku hiyo Rahim aliongozana na vikosi vya askari wengi kuelekea Eden lengo ni kutaka kuipindua falme hiyo bila kujua kilichotokea.


Hadi kulipopambazuka kila mtu alikuwa tayari kwa ajili ya kuuaga mwili wa Mfalme Siddik. Kwenye barabara kuu walisimana watu pande mbili kuusubiri mwili wa Mfalme upite ili waweze kuuaga. Baada ya muda askari wa Eden waliutoa mwili wa Mfalme ukiwa kwenye jeneza na kuanza kulibeba kuelekea kunako makaburi ya wafalme wote waliopita. Mji mzima ulikuwa ni kilio kwa wananchi huku jeneza likipita kuelekea makaburini. Majeshi yote ya askari walikuwa nyuma wakiusindikiza mwili huo. Hakuna aliyebaki ndani kila mtu alielekea makaburini kushuhudia safari ya mwisho ya Mfalme Siddik.


Baada ya nusu saa Rahim aliweza kuwasili na majeshi yake ndani ya Eden. Ajabu wakipofika hawakuona mtu yeyote ambaye anakatiza mitaa zaidi ya kuku na mbwa wa mitaani. Hali ile ikawafanya wapate mashaka. Ilibidi wazidi kusogea mbele hadi walipofika kwenye falme nje na kukuta lango limefungwa.


"Wameenda wapi hawa watu?" aliuliza Rahim huku akiangalia huku na kule na askari wake. Wakiwa katika sintofahamu hiyo waliona ndege wengi wakiruka juu angani wakitokea sehemu moja kuelekea pengine. Ishara ile iliwajulisha huenda kuna watu wanakuja. Wakasimama sawiya na kukamata mapanga yao kujiandaa kwa lolote. Hammadi.... walichokiona mbele yao askari hao wa Rahim wote wakaweka silaha zao chini taratibu kuashiria wamesalimu amri.  Idadi kubwa ya wananchi pamoja na askari wa Eden iliwaogopesha sana na kujua kamwe hawataweza kuwamaliza watu wote pale. Rahim aliwashangaa askari wake kuona wamechukua uamuzi ule wa haraka kabla hata hawajapambana.


Hata baada ya kuwasili Samir pale mbele yao ilimfanya Rahim ashangae kuona mtu huyo amevaa mavazi ya kifalme. Walibaki wakitazamana kwa muda, bila kutegemea Rahim alitupa upanga wake chini na kuinama kumpa heshima Samir akikubali kuwa ni Mfalme. Hata askari wake waliungana naye wakamfuata kumpa heshima ile Samir. Jambo lao walilokuja kulitimiza liliishia hewani baada ya kuona pamoja na kuwa na nguvu za kichawi Samir lakini watu wameridhia kuongozwa naye hivyo hawakuweza kuwabadilisha mawazo yao.

Hawakuwa na uwezo wa kufanya lolote hata Samir alijua fika kuwa walikuja kwa shari, hakutaka kuwadhuru aliwaamuru waondoke haraka sana na Rahim akafanya hivyo pamoja na askari wake kurudi katika falme yao.


Baada ya siku kadhaa Malkia Rayyat alimkabidhi rasmi Samir falme ile aiongoze naye akabakia kuwa mama wa Maya. Jambo hilo Samir alilikuza na kuamua kuandaa harusi kabisa na kuweza kumuoa Maya na kumkabidhi rasmi kuwa Malkia na Malkia Rayyat sasa akatoka kwenye cheo cha umalkia na kubakia kuwa mama wa Malkia. Maya aliichukua pete ile ya Samir ambayo aliichukua kule msituni na kuweza kumvalisha mumewe huyo na kufanya tukio lile la Faraj alilolitabiri litimie.


Baada ya siku kadhaa kupita Maya alihitaji kuelekea kule nyumbani kwao Samir (Tanzania). Ilimbidi mwanaume amfuate Faraj kumueleza jambo hilo. Alibaki kutabasamu tu huku akimtazama Samir.


"Sio rahisi tena kurudi kule ulipotoka Samir. Madam umeshaivaa pete hiyo basi maisha yako yatakuwa ni huku huku Eden na sio kurudi kule tena. Kule kuna mtu kama wewe na ataendelea kuwepo siku zote ni sawa na wewe jinsi ulivyochukua uhalisia wa Samir. Kwahivyo kuanzia sasa sahau jina lako la Amour na uelewe kwa sasa wewe ni Mfalme Samir." alisema Faraj akiwa kwenye kijiji chake cha Gu Ram na kumfanya Samir apate kutambua kuwa hawezi tena kurejea Unguja na maisha yake yote ni Eden.


Alikubaliana na hali hiyo wakaendelea kuongea mambo mengi sana huku akimpa nafasi Faraj ya kuhama na watu wake kuja kuishi Eden akiwaahidi kuwapa sehemu za kuishi.

Faraj alishukuru kupewa nafasi hiyo lakini hakuwa tayari kuishi Eden, alitamani kuendelea kuishi Gu Ram miaka mingi zaidi ili aweke historia. 


Samir alimuelewa na baada ya muda aliagana na rafiki yake huyo kurudi zake Eden akiwa kama Mfalme.


                 MWISHO


Asanteni kwa kuwa pamoja mwanzo wa simulizi hii mpaka mwisho wake, ukiwa na maoni ushauri na mawazo basi karibu sana. Tukutane kwenye simulizi nyengine. 🥰🥰🥰🥰

Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group