SEHEMU YA 03
ILIPOISHIA.......
Wakaamua waache kwanza mada hizo watafute chai maana baadae wana kikao na walimu wao.
ENDELEA NAYO......
Upande wa Eden katika jumba la kifalme wahudumu walikuwa wakitumwa tu huku na kule na waganga wa jadi pamoja na wataalamu wa mambo ya kichawi kuhakikisha wanamsaidia binti wa kifalme ambaye inasadikika yupo kitandani takribani wiki nzima. Kila mganga anayeletwa pale anafanya mambo yake na kutoa dawa za kutumia lakini inashindikana. Uchawi ambao ulioachwa na baba wa binti Nadhra ni mkubwa sana kiasi kwamba hakukuwa na mtaalamu wa kuweza kuutoa uchawi huo. Mwisho wa siku mganga wa mwisho aliposhindwa kumtibu binti huyo alimfuata Mfalme Siddik na kumpa heshima yake kisha akakaa kumueleza.
“hapa utaita kila mganga aje kumsaidia binti yako lakini ninachokwambia ndio ninachokiona kwenye utaalamu wangu, uchawi ulio tupwa kwenye mwili wa mwanao ni uchawi wa miaka mingi iliyopita. Uchawi huu ulitumiwa na binti wa kifalme wa zamani aliyeitwa Sabiha, yeye alikuwa na pacha wake ambaye ndiye alikuwa Malkia wa enzi hizo akiwa na mumewe aliyeitwa Saleh, hivyo huyo Sabiha baada ya kufariki ndugu yake yeye ndio akawa Malkia wa Eden akawa anaiongoza vyema miaka yote. Sasa naye baada ya kufariki kwenye vita moja huko Mashariki ya mbali kuna mtu alifahamika kwa jina la Dalfa aliweza kuchukua nguvu zake na kujimilikisha yeye na ni Mfalme wa nchi ya huko Mashariki. Sasa uchawi aliotupiwa Binti yako ni ule wa Malkia Sabiha uliochukuliwa na Dalfa hivyo kama kupona huyu basi ni lazima apatikane mtu ndani ya falme yenu mwenye nguvu kama hizi ili aweze kuutoa uchawi huu, au laa apatikane huyu Dalfa muweze kumshawishi aje kumtibia binti yenu jambo ambalo sidhani kama litakuwa jepesi maana ana sheria kali sana." alisema Mzee yule mganga akimueleza Mfalme Siddik akiwa pembeni na Mkewe Malkia Rayat.
“Kama unapajua hata kesho twende huko Mashariki ya mbali tukaongee naye huyo Dalfa amponeshe mwanangu, anateseka sana” alisema Malkia Rayat akionesha kuumizwa na tatizo lililomkuta binti yake.
“Malkia wangu... tatizo sio kuonana na Dalfa tatizo ni matakwa anayohitaji yatimizwe, historia yake huyu mtu amechukua falme za watu wa nne na sasa anazimiliki yeye na ni kutokana na makubaliano tu kama haya baadhi ya wafalme ambao wanataka msaada kutoka kwake, yeye anawapa sharti la kuzichukua falme zako au eneo la utawala wa Mfalme huyo na wanakubali kusudi matatizo yao yaishe na ndio maana akapewa jina la MFALME WA MASHARIKI YA MBALI. Sasa nahofia tukaipoteza pia Eden ikawa mikononi mwa Dalfa." alisema yule na jambo hilo kwa Mfalme hakutaka kulisikia kabisa, anaipenda Eden kupita maelezo hawezi kuiacha ikachukuliwa kirahisi.
Wakati yeye akiifikiria Eden yake mkewe Malkia Rayat alikuwa akimfikiria binti yake kuhusu ile hali aliyonayo. Ni kama amekufa japo mapigo ya moyo yakisikika tu yakifanya kazi mara moja moja sana jambo lililomfanya Malkia huyo ahofie kumpoteza kabisa binti yake.
Basi mzee yule alipo waeleza yote hayo akanyanyuka na kuondoka zake akiwaacha wenyewe waamue moja kati ya hayo aliyowaeleza.
“Siddik nisikilize kwa makini, Maya ndiye mtoto wetu pekee tuliojaaliwa kuzaa na hatuna mtoto mwengine zaidi yake, yeye anatuangalia sisi tumsaidie katika maisha yake ili aje kuwa na matendo kama yetu, mimi naamini tunaweza kumtafuta huyo Dalfa na tukakaa naye tukaongea akachagua kitu hata chengine ili tu amsaidie mwenetu, nakuomba sana uwe jasiri kwa hili katika kuokoa maisha ya Maya." alisema Malkia Rayat.
“Huyu mtu yeye anataka kumilikishwa Falme, anakusaidia kisha wewe Mfalme au Malkia unakuwa raia tu wa kawaida yeye ndio anakuwa Mfalme, hadi kuitwa Mfalme wa Mashariki ya mbali juwa kuwa anajulikana, hawezi kukusikiliza kama hutatoa nchi yako jambo ambalo katu sitalifanya hata kama nimelala usingizi, Eden itabaki kuwa Eden." alisema Mfalme Siddik kwa kusisitiza.
“Una maana gani sasa moyoni mwako kama baba wa Maya? Una maana bora afe mwanao ili wewe uendelee kuongoza watu? Si ndio una maana hiyo?nijibu.." alisema Malkia Rayat kwa ukali na kumfanya hata mumewe akose jibu la kusema, alinyanyuka Malkia na kuondoka zake kwenda chumbani kwa binti yake huyo aliyeko kitandani tu wahudumu wakimfuta futa na kumuangalia muda wote.
Alitokwa na machozi mama mtu baada ya kuzidi kuumia kuona hali ya mwanaye pale kitandani, alisogea mpaka pale na kukaa kisha wale wahudumu wakaamka na kumpa heshima kisha wakatoka zao nje kumuacha mama akimuangalia mwanaye kwa huzuni.
“Maya mwanangu, mimi mama yako nakuombea tu lazima utapona ni lazima, huwezi kuniacha mimi au baba yako tukiwa hai wakati wewe bado kijana unapaswa kuongoza hii Eden kama Malkia kama mimi mama yako, amka mwanangu...amkaaa!" alisema Mama mtu huku akiushika mkono wa mwanaye na kuuweka shavuni kwake.
Muda huo Mfalme alikuwa akichungulia tu na kuona jinsi mkewe anavyomlilia mwanaye, hata yeye kama baba aliumia sana kuona binti yake yupo kama maiti tu pale kitandani, aliyazuia machozi yasimbubujike na kugeuka akaondoka zake pale.
Alijifungia chumbani kwake akitafakari sana swala linaloendelea, kichwa chake kilijigawa mara mbili kiakili kuwa aende kwa Dalfa amueleze matatizo ya mwanaye na atakapotaka kuichukia Falme ya Eden akubali kisha mwanaye apone naye Mfalme awe raia wa kawaida kama wananchi wake au aendelee na Ufalme wake kama kawaida lakini akijua mwanaye si wakupona tena lazima atakufa!. Ni maswali ambayo alikaa akiyatafakari mwenyewe zaidi ya lisaa lizima bila kupata majibu.
Dakika chache aliingia Malkia Rayat akionesha kupooza huku sura ya majonzi ikimtawala, alisogea hadi kwa mumewe ambaye naye alisimama na kumkumbatia mkewe wakabaki wamekumbatiana wawili hao.
“Mfalme... naomba umsaidie mwanangu...nakuomba sana..” alisema Malkia Rayat akiwa kama mama sasa, kauli yake ilimliza hata Mfalme na kuona kama anaombwa na raia wake wa kawaida na sio Malkia wala mkewe, hii ina maanisha kwamba ufalme wala umalkia si kitu mbele ya damu yao bora wakubali tu kuupoteza uongozi wao ili mtoto wao apone.
Mfalme alijitahidi sana kukubaliana na mkewe lakini moyo unakataa kabisa na kujikuta akishikilia msimamo wake kama Mfalme, alimuacha tu mule ndani mkewe akatoka zake nje kutafuta namna ya kufanya.
Kesho yake asubuhi Malkia Rayat baada ya kutafakari kwa kina zaidi na kuona huenda akampoteza mwanaye bora ajiongeze kama mama, maana yeye ndio mwenye uchungu zaidi, aliamua kutoka ndani ya falme akiwa na mpambe wake mmoja bila Mfalme kujua akamfuata yule mzee aliyewapasha habari kuhusu Dalfa, mzee huyo alipomuona ni Malkia ilibidi ampe heshima yake naye Malkia akapokea na wakakaa kuongea.
“Sikai sana hapa nimekuja nina jambo moja tu nahitaji kutoka kwako, nataka unielekeze wapi nitampata Dalfa." alisema Malkia na kumfanya yule Mzee ashtuke baada ya kujua huenda ndio anataka kwenda kuweka makubaliano na Dalfa.
“Mh lakini Malkia hilo swa...“
“Nimekwambia unielekeze wapi anapopatikana Dalfa.!" alisimama kwenye msimamo wake Malkia na kumtia mkwara yule Mzee ikabidi akubali tu, akamuelekeza japo kwa shingo upande akijua sasa Eden inaenda kuuzwa.
“Haya nitaenda huko kuonana naye na naomba uwe kimya nisisikie lolote ukilifikisha kwa Mfalme juu ya tulichoongea, nikutakie siku njema.” alisema Malkia na kuondoka zake baada ya kupata maelekezo ya kina zaidi anapopatikana Dalfa, akaondoka na yule mpambe wake kurudi kwenye falme.
Aliandaa farasi maalumu kwaajili ya safari ya kuelekea Mashariki ya mbali lengo ni kukutana na huyo Dalfa wapate muafaka, alimuaga mumewe kuwa anaelekea zake kuzunguka huko mipakani na kurejea hapo baadae Mfalme akamruhusu bila ya kujua kuwa mkewe anaenda safari ya mbali. Malkia aliondoka zake na mpambe wake safari ikaanza kuelekea huko.
Siku hiyo jioni Amour alikuwa zake nyumbani kwao ambapo anakaa na kaka yake na shemeji yake ambaye yumjamzito, muda mwingi anatumia kusaidia kazi za pale ndani kutokana na hali ya shemeji yake. Siku hiyo aliamua kupika huku shemeji yake akimtazama tu na kubaki kutabasamu.
“Nakwambia huyo mwanamke utakayempata atafaidi kwakweli." alisema Shemeji mtu na kumfanya Amour atabasamu.
“Sio kufaidi tu na kunenepa kabisa maana atakula mapochopocho hata yeye hakuwahi kupika." alisema Amour akiendelea kupika. Shemeji katika hali ya kumuangalia Amour akipika alipata kuiona ile pete ikiwa inang'aa.
“Kumbe ushavalishwa na pete kabisa mumewangu huko, mlete basi mke mwenzangu anisalimie.” alisema shemeji mtu na kumfanya Amour azuge tu.
“Hii ni ya urembo tu bwana shemeji wala sio yenyewe, ila akipatikana namleta wala usijali utakuwa unakaa kama hivyo anakusaidia kupika wewe si mke mkubwa bwana." alisema Amour na kumfanya shemeji yake atabasamu tu na kuendelea na maongezi mengine.
Hata chakula kilipokuwa tayari waliandaa na kula wawili hao na baadae kila mmoja akajipumzisha.
Amour aliingia chumbani kwake na kutulia kitandani akiitazama ile pete.
“sasa kila mtu anaiona hii pete siku broo akija kuiona si ndio itakuwa balaa atakaponiambia niivue na kitu kimegoma kutoka hiki." alisema Amour huku akiitazama ile pete, kwa mbali aliona kitu fulani kwenye ile pete ilibidi asogeze kidole kile karibu na macho yake.
Alipata kuona tukio ambalo linaendelea, wanawake wawili wakiwa kwenye farasi wakiwa spidi wanaelekea sehemu fulani, alishindwa kuelewa ni wakina nani wale na kubaki kuangalia tu wakizidi kwenda.
“hawa ni akina nani tena?” alijiuliza mwenyewe pale huku akitazama pete ile kile anachokiona.
“Ni Malkia wa Eden, Rayat yupo na Mfanyakazi wake wakielekea Mashariki ya mbali kukutana na Dalfa ambaye ni mtu mwenye uwezo wa kumponyesha mtoto wa Mfalme aitwaye Maya” ilisikika sauti kutoka kwenye pete ile ikiongea, Amour alishangaa kusikia vile akawa anaigeuza geuza ile pete kuona wapi inapotokea sauti ile.
Alivyorudisha kidole kama awali aliona yule Malkia na mfanyakazi wake wametolewa na kuona mtu mwengine tena akiwa amelala kitandani. Alipojua kuwa kumbe pete ile ni zaidi ya zawadi kwake ilibidi aizoee tu na kujikuta akiitumia tena kuuliza.
“na huyu je ni nani?“
“anaitwa Maya Siddik, ndio Binti wa Mfalme Siddik, yupo hapo kitandani siku ya nane sasa hakuweza kuamka kwa maradhi, ndio mama yake pamoja na yule mfanyakazi wameenda Mashariki ya mbali kutafuta msaada kwa huyo Dalfa.” ilisema ile pete na kumfanya Amour aisogeze ile pete vizuri amtazame huyo binti wa kifalme hammadi..... alipomuangalia vizuri sura yake ni vile vile kama alivyo msichana aliyempenda sana shuleni kwao lakini yeye hapendwi, Aziza.
“hee, anaitwa nani umesema?“
“anaitwa Maya Siddik, ni binti wa Mfalme Siddik” ilisema ile pete na kumfanya Amour acheke.
“hapana bwana huyu ni mwanamke ambae nasoma naye shule moja anaitwa Aziza bwana na sio Maya.” alisema Amour akiwa anatabasamu baada ya kumuona Maya akiwa yupo vilevile kama alivyo Aziza msichana aliyemkataa Amour.
“ni ufanano wa sura tu, ila matendo, tabia na nchi ni tofauti.” ilisema ile pete.
“nitaamini vipi sasa kama sio Aziza ninayemjua mimi wakati sura yake naifahamu kabisa kuwa ndiye.” alisema Amour.
“fumba macho yako” ilisema ile pete na kumfanya Amour ameze mate kwa woga, ikabidi afumbe maana amesema mwenyewe.
“haya fumbua.” ilisema ile pete na kumfanya Amour aanze kufumbua jicho taratibu kama anachungulia kitu huku akitazama huku na kule, aliona yupo mahala tofauti kabisa ikabidi afumbue macho yake kabisa. Alishangaa kuona hayupo tena pale chumbani kwake na kujikuta yupo kwenye chumba tofauti kabisa.
Chumba kilichopambwa na maua na picha mbalimbali ukutani, alipo zitazama picha zile sasa akaona wazi sura na umbo la binti wa Mfalme, Maya akiwa kwenye tabasamu na mavazi tofauti tofauti ya heshima. Utofauti aliouona ni kuwa Maya anaonekana mwenye nywele refu zenye kung'aa zikifika mgongoni, hapo ndipo Amour akaamini kweli wamefanana sura tu na Aziza. Basi alitazama vitu vingine na kuzidi kuangaza huku na kule na mwishowe akapata kumuona mhusika mwenyewe akiwa amelala kitandani. Amour alibaki kumtazama tu mrembo huyo na kuanza kupiga hatua taratibu kusogea pale kitandani na kumuona Maya kwa macho yake kabisa.
“Ma..ya" aliita Amour kwa sauti ya chini baada ya kumuona mrembo Maya, hakika ni vilevile alivyo Aziza ambaye anampenda sana lakini upendo wake si chochote kwa binti yule.
Alinyanyua mkono wake na kushika nywele zake laini na kujikuta akitabasamu tu.
Ghafla akarudishwa chumbani kwake kule kama awali.
“ah sasa mbona umenirudisha tena huku?” alilalamika Amour maana alitamani kumshika zaidi binti yule.
“nilikupeleka Eden mara moja tu ukaone utofauti wa Maya na Aziza unaemzungumzia, nadhani umeshaona utofauti wao” ilisema ile pete.
“sawa nishaona, naomba nirudi basi tena nimuone vizuri Maya.” alisema Amour baada ya kunogewa na mahali pale.
“unapaswa ukaribishwe rasmi Eden, awali Nadhra alikupeleka na kukukaribisha ukakataa na kutaka urudishwe darasani uendelee na masomo yako nae akakurudisha haraka, vipi leo upo tayari akukaribishe Eden?” ilisema pete ile, na bila kipingamizi Amour akaridhia mwenyewe.
“nipo tayari sasa” alisema Amour na kujiongeza mwenyewe akafumba macho sekunde tatu tu kufumbua akajikuta yupo kwenye kiti akiwa na Mrembo Nadhra akiwa amejaa tabasamu usoni mwake.
“Amour, karibu sana Eden..” alisema Nadhra na kumfanya Amour atabasamu baada kuanza kuzoea sasa hali ile.
“asante sana” alisema Amour.
ITAENDELEA..........
GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA NNE (4)
