PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 2

 

SEHEMU YA 02


ILIPOISHIA....... 


 “hadi sasa ana nguvu za ajabu ambazo zitawasaidia wakati wote japo yeye hafahamu kama anazo, nitakuonesha mahala anapo patikana uende kumshawishi ili uje naye huku mfanye ile kazi kwa pamoja, ukirejea nyumbani utapata kujua mahali hapo anapopatikana, sitawaona tena hadi mambo yatakapo kwenda sawa, niwatakie kazi njema.” ilisema ile sauti ya mzee kisha kile kimbunga kikapotea gafla na kumfanya Nadhra atambue maneno aliyoambiwa.


ENDELEA NAYO....... 


Muda huo huo aliweka mikono yake chini na kutamka maneno fulani akapotea pale alipo gafla na kutokea nyumbani kwao, haraka akaelekea kwenye chumba kimoja na kufungua mlango akaenda kwenye kabati akatoa beseni dogo kisha akaliweka mezani na kulijaza maji kiasi chake, akaanza kuyazungusha yale maji huku akitamka maneno fulani ya kichawi na ghafla ndani ya maji ikaonekana tukio ambalo linapata kuendelea shuleni NYERERE ambapo Amour alionekana kupiga magoti chini huku Mwalimu mkuu akiongea mbele ya wanafunzi wote. 

Kitendo kile kilimstaajabisha sana Nadhra baada ya kuona ni kitu kigeni katika macho yake. Ni nchi ambayo hakuweza kuitambua kabisa wala mazingira ambayo anayaona pale, kitu pekee alichokibaini ni pete ambayo alimuona kijana Amour ameivaa na kujua ndio ile pete aliyoirusha juu angani. Hapo ndipo akabaini huenda huyu ndiye kijana aliyeambiwa na baba yake kuwa atakuwa naye muda wote kuikamilisha kazi fulani, aliisogeza ile picha ya Amour akiwa pale chini amepiga magoti na kuanza kumchambua kujua kila kitu.

“anaitwa Amour.. ana miaka 20... ni mtanzania... ni mpiga kengele wa shule... anaishi na kaka yake... anaadhibiwa kwa kosa la kuchelewa hadi kuharibu ratiba ya vipindi vya shule...ana nyota kali iliyozimwa na ndugu zake kutofanikiwa katika maisha...anapenda lakini hapendwi....mmh” yote hayo aliyaona Nadhra kupitia kwenye yale maji huku akimtazama kijana huyo akiwa kwenye ile adhabu.


Alitabasamu baada ya kumfahamu kuwa ndiye mtu pekee ambaye atakuwa naye katika harakati nzima ya kufanya kazi ambayo baba yake anahitaji iwe.

“muda si mrefu nitakuwa na wewe Eden, naamini tutashirikiana vyema.” alisema Nadhra huku akimtazama kijana Amour ambaye alionekana akilala chini ili aadhibiwe bakora, alichokifanya Nadhra ni kuishika tu ile bakora kwa kuingiza mkono wake kwenye yale maji. Bakora ambayo Mkuu wa shule hiyo aliinyanyuka ipasavyo kumchapa Amour matakoni, na kweli kila mtu alishuhudia bakora ile ikitua matakoni mwa Amour ambaye alikunja sura kuona inashuka lakini ajabu hakuona maumivu yeyote yale katika mwili wake na kubaki kumtazama mwalimu huyo aliyekuwa akishusha bakora akijua zinamkolea kijana huyo hadi zilipofika sita akaacha na kumtaka anyanyuke kijana huyo huku baadhi ya wanafunzi wakishangaa kuona leo mwenzao hakuweza hata kutetereka kwa fimbo zile.


“hii nakupa onyo kwa mara ya mwisho, tena nimejikuta nakusamehe bure uendelee na kitengo chako utakaporudia tena basi nampa mtu mwengine uongozi huo, leo umetufanya tunapoteza ratiba ya vipindi kwaajili yako maana watu walikuwa wanasubiri kengele kugonjwa wakafanye usafi lakini wapi watu wanaongea tu na kuweka vigenge vya umbea na muda wa masomo umefika, kwa mara ya mwisho mbele ya wanafunzi wenzako utakapo chelewa tena aisee utachimbua visiki vitano vya nguvu peke yako.., haya rudi huko” alisema Mr. Khamis na kumfanya Amour arudi na kuungana na viongozi wenzake waliokuwa nyuma ya wanafunzi.


Muda wote huo alikuwa akizuga kuumia makalio lakini moyoni alikuwa na maswali mengi juu ya jambo lile imekuwaje hadi imetokea vile. Alitazama pembeni yake na kugongana na macho ya msichana Aziza ambaye alitokea kumhusudu sana, alijikuta akijenga tu tabasamu usoni mwake baada ya kutazamwa na mrembo huyo ambaye kwa aibu alitazama mbele kumsikiliza Mkuu akiendelea kuongea.

“kengele imegongwa kwa jambo moja tu, baada ya Break Fast kutakuwa na kikao baina ya walimu na wanafunzi wa kidato cha nne wote, hivyo basi kengele ya saa nne ya kunywa chai ikigongwa muende mkirudi mkae darasa moja watakuja walimu kuna mambo tunahitaji kuyaweka sawa, baada ya kusema hayo wote rudini madarasani kwenu” alisema Mwalimu huyo na kuwafanya wanafunzi wote warudi madarasani na yeye akaelekea zake ofisini mwake.


Amour aligeuka na kuelekea zake darasani na muda huo huo akatokea msichana mmoja aliyefahamika kwa jina la Elizabeth ambaye ni rafiki sana wa karibu na kijana huyo.

“baba leo umezichezea sita za Mkuu, pole sana aisee maana tukawa tunaskia tu mlio wa bakora PAAH...PAAH... yule mzee kiboko kama anaua nyoka.” alisema Eliza akiwa amemshika mkono Amour.

“mh ina maana mlikuwa mnasikia sauti ya bakora zikitua?” aliuliza Amour maana hakusikia sauti wala maumivu yeyote yale ya fimbo zile.

“eh baba ndio kusema stiki zilikuzidi ukawa husikii au?” alisema Eliza na kumfanya Amour awe njia panda, haelewi hili swala linakuwaje tena.

“eh naona Aziza amekuvisha Pete aisee, mambo ni mukidee aisee duu.” alisema Eliza baada ya kuiona ile pete mkononi mwa Amour ambaye baada ya kusikia vile ndipo akakumbuka kumbe alikuwa na zoezi la kuutazama mkono wake pale alipokuwa akigonga kengele na kuhisi maumivu makali sana hadi kuumia.


Aliunyanyua ule mkono wake na kuutazama akaona upo kawaida ile michubuko ikiwa imepotea na kuwa sawa tu. Alishika kile kidole chenye pete ambayo ilikuwa na maneno madogo madogo ya lugha isiyo eleweka.

Alichokifanya ni kuivua maana hakufahamu ilimpataje hadi ikawa kwenye kidole chake lakini kila akiivua inashindikana kana kwamba imegandia pale kidoleni.

“Eliza.. unajua mimi sielewi hii pete imefikaje hapa kidoleni.. na nashangaa haitoki sijui nini tena hii jamani eh” alisema Amour akiendelea kujaribu kuivua ile pete.

“acha kuleta muvi za kibongo wewe... wewe sema bwana mzigo kanivalisha Wifi yako tu basi sasa unanificha nini, mimi kuna kitu niliwahi kukuficha Amour? acha zako bwana..ngoja nielekee msalani kabisa nikiingia darasani ni kupiga msuli tu.” alisema Eliza na kuelekea zake chooni akijua mwenzake anatania, akamwacha Amour akiendelea zake kupambana na ile pete itoke kidoleni kwake.

“Mungu wangu haya mabalaa gani tena jamani eh..!” alikasirika sana kuona inashindikana kutoa ile pete hadi alipoona mwalimu wa somo la Kiswahili anaingia darasani kwao naye akaamua aende kwanza darasani zoezi la pete atalifanya akitoka darasani.


Basi alielekea mahali pake na kukaa kisha akatoa daftari na kuendelea kumsikiliza mwalimu huyo wa Kiswahili aitwae Madam Asha. Alichukua chaki na kuandika somo analofundisha kisha akaandika mada ya siku hiyo na kuwageukia wanafunzi wake.

“haya naomba tuendelee leo, nakumbuka jana tuliishia katika kuchambua mifano ya Hadithi, Riwaya na shairi. Na tulishamaliza kuelezea namna ya Hadithi na Riwaya zinavyokuwa na mifano yake nikawapa, ila kwenye Simulizi ya kubuni nilielezea na nikatoa mfano kidogo wa ile simulizi ya NDOTO YA AJABU jinsi ilivyokuwa si ndio.?” aliuliza Madam Asha.


“ndiooo...“walijibu wanafunzi na mmoja wapo akasimama.

“ila Madam ile simulizi hukuimalizia aisee tamu sana ile tungeomba leo umalizie mfano wako” alisema kijana mmoja aliyeitwa Ayubu, Madam alitabasamu huku akiwaangalia wanafunzi wake waliokuwa wakimuunga mkono kijana Ayubu.

“jamani ile ni ya kubuni tu na haina ukweli wowote..ila sawa wacha nisimulie kidogo maana tupo kwenye kipindi chake, niliishia wapi?” aliuliza Madam na kijana Amour akasimama na kusema.

“pale ambapo Mfalme Saleh na Malkia Samira walipokuwa wakitoka kule Pangoni halafu nje Sabiha na Malik walikuwa wamejificha wakiwasubiri wawamalize” alisema na kukaa chini.


“duh mpo makini kweli maana nilishasahau, haya basi bwana Mfalme na Malkia Samira walitoka mule pangoni wakiwa na furaha sana maana washafungishwa ndoa na Mfalme wa mwanzo wa taifa la Eden na pia wakapewa zawadi ya tufe lile na kila mmoja akakabidhiwa pete ambayo ni zaidi ya ulinzi kwao.” alisema Madam na kumfanya Amour akumbuke ile pete alionayo kidoleni, aliitazama na kuanza kujenga hisia kama ni yeye ndiye Mfalme amevaa ile pete ambayo ni zaidi ya ulinzi kwake.


Alijikuta akijilaza kwenye dawati akiitazama ile pete kwa umakini sana huku akiyapitia maneno yaliyoandikwa kwenye pete hiyo ambayo hakuweza kuyatambua. Alisikia akiguswa bega lake na kumfanya ainuke pale alipoegemea kwenye dawati.

Alishangaa kumuona msichana ambaye hakuweza kumfahamu kwa sura, uzuri wake uliochangiwa na macho makubwa yaliong'aa yalimfanya Amour amtazame kwa muda bila kuchoka, yule msichana aliachia tabasamu la aibu huku akimtazama Amour.

“Karibu Eden...” alisema msichana yule na kumfanya Amour amshangae, lilipotajwa jina la Eden akakumbuka ni nchi ambayo ni ya kifalme na aliisikia kutoka kwa Madam Asha aliyewasimulia Simulizi ya NDOTO YA AJABU.


Ndipo akili zikamjia kuwa alikuwa darasani muda huo, akajikuta akitazama mbele ili kumuona Madam aliyekuwa akiwasimulia Simulizi darasani, ajabu ni kwamba hakukuwa na Madam wala ubao kwa  mbele, alipotazama pembeni kuangalia wanafunzi wenzake hakuona hata mmoja na kujikuta akiona vitabu vingi vikiwa ndani ya chumba hicho. Alijitazama pale alipokaa na kukuta amekaa kwenye kiti ambacho ni tofauti na dawati la shule ya Nyerere. Ilimbidi asimame ghafla kwa kuogopa akawa anatazama huku na kule na kuona hali ambayo ni tofauti kabisa na mazingira ya darasani alipokuwepo.

“huna haja ya kuogopa Amour, upo Eden kwasasa, na mimi ndio mwenyeji wako kuanzia sasa, naitwa Nadhra.” alisema mrembo yule akijitambulisha kwa Amour ambaye bado hakuweza kuelewa.


“wewe...wewe... kama ushirikina wenu pelekeni huko, mimi nilikuwa darasani nasoma naomba nirudishe uliponikuta samahani sana sikujui hunijui na sitaki kukujua kwanza, nirudishe darasani niendelee kusoma.” alisema Amour akiwa haelewi mazingira ambayo amejikuta yupo ghafla.

“sawa nitafanya hivyo ukitaka, ila nimekuleta Eden ufahamu mazingira ya huku mara moja kabla hatujaanza kufanya kazi pamoja.”

“wewe ndio uliniweka hii pete kidoleni!? "aliuliza Amour akiwa anamtazama Nadhra.


“sijakuweka mimi ila ilikufuata yenyewe, hiyo ni kama zawadi kwako na huenda ikakusaidia kwenye maisha yako.” alisema Nadhra na kumfanya Amour aitazame ile pete, alikumbuka lile tukio la kuchapwa bakora na Mwalimu mkuu lakini ajabu hakuweza kusikia maumivu yeyote na kuhisi huenda ni kwaajili ya pete hiyo. Akiwa kwenye tukio la kuitazama pete ile ghafla akasikia sauti tu ikimuita.


“we Jafari...” alistuka na kutazama mbele yake.

“jana hukulala kwenu? Hebu amka kanawe uso nje kwanza ndio urudi darasani nahisi hata tulicho kijadili hapa hukusikia nenda nje kwanza kanawe” ilikuwa ni sauti ya Madam Asha aliyekuwa mbele ya darasa, Amour alibaki kutazama darasa zima akiona anaangaliwa na wenzake. Alishangaa baada ya kuzidi kuona maajabu maana sekunde chache tu alikuwa akiongea na Nadhra ajabu saivi anajiona yupo tena darasani. Hakutaka kuonesha utofauti wowote akanyanyuka na kutoka nje moja kwa moja akaelekea kwenye bomba la maji na kufungulia akaweka kichwa chake maji yakaanza kutiririka.


Aliona ni kama ndoto huenda akawa anaota baada ya kuambiwa na Madam kuwa alikuwa amelala darasani.

“itakuwa ndoto tu hii..” alijisemea mwenyewe akikataa kuamini ukweli wa mambo, lakini kitu pekee kilichomfanya achanganyikiwe ni ile pete ambayo bado ipo kidoleni kwake, aliitazama kwa umakini bila kuelewa. Alikumbuka maneno yale ya Nadhra kuwa huenda ikawa ni zawadi kwake ya maisha,  alipokumbuka tena tukio la kuchapwa alianza kuhisi huenda ikawa sio ndoto tena bali ni ukweli.


Taratibu akajikuta akianza kuamini mambo yale japo moyo unakuwa mzito kukubali.

Aliitazama tena ile pete kwa umakini.

“ina maana haya mambo yapo kweli? Nilikuwa nahisi ni Simulizi tu za kubuni kumbe yaweza kuwa kweli, sasa kwanini mimi? Hakuonekana mtu mwengine zaidi yangu mimi tu.?” alijiuliza sana Amour bila kupata jibu kamili, aliamua kunyanyuka zake na kurejea tu darasani huku moyo wake taratibu ukianza kuamini matendo yaliyomtokea siku hiyo. Alipokaa kwenye dawati lake na Madam yule akawa anaandika ubaoni kazi ya kufanya wanafunzi.

“hii kazi nitaikusanya Ijumaa, leo Jumatano hadi siku hiyo mtakuwa mmemaliza, nahitaji kila mmoja wenu atunge kisa cha kuvutia ambacho hata mtu akisoma asisimke au kama ni kisa cha kutisha aogope kabisa, na nitoe tu ahadi kwa atakayefanya nikavutiwa na simulizi yake nampa ofa ya kula chakula na sisi walimu kwa wiki nzima atapumzika kula mapure (makande) ya shule na wenzake.” alisema Madam kwa tabasamu na kuwafanya wanafunzi wote wafurahi kusikia hivyo maana chakula wanachokula walimu ni tofauti na chakula cha wanafunzi. Kila mtu alitamani nafasi hiyo aipate yeye endapo akiandika simulizi itakayomvutia Madam Asha.


Baada ya kuondoka mwalimu huyo darasa likabaki na maongezi kuhusu kazi hiyo waliyopewa, kwa Amour yeye hakuwa mwenye kufuatilia kazi hiyo waliyopewa yeye alikuwa akijadili tu na nafsi yake namna itakavyokuwa baada ya kufahamu kuwa ile pete iliyopo kidoleni kamwe haiwezi kutoka , aliona ni vyema akaonana na yule msichana Nadhra ili amuelezee kwa kina zaidi juu ya swala hilo.


Masaa yalizidi kwenda na muda wa mapumziko ulipofika Amour kama kawaida yake alielekea kwenye kengele apate kugonga, alipoikaribia akawa na woga baada ya kuona ndio sehemu alipoipata ile pete, akajipa moyo na kukamata kile kichuma akagonga kengele kama kawaida na wanafunzi baada ya kusikia wakaanza kutoka madarasani kwenda kupata kifungua kinywa kwenye mikahawa iliyopo pembeni na shule yao.

 


Muda huo akapita msichana Aziza na Amour alipo muona ilibidi amfuate.

“Aziza...” aliita Amour na kumfanya Msichana huyu asimame na kugeuka, alipomuona Amour alibinua mdomo na kuangalia mbele.

“mambo vipi” alisalimia Amour baada ya kumkaribia Aziza.

“poa tu..“

“si unaelekea kunywa tea.. tuongozane basi.” alisema Amour na kupiga hatua kuongoza njia.

“we mwanaume mbona unanifuatilia sana? Si nilishakwambia lakini sitaki mazoea na wewe au husikii mwenzetu!” alisema Aziza kwa sauti na baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakipita pembeni waliwatazama na kuendelea na safari yao.

“jamani taratibu basi tusiwafaidishe watu, mimi nimeongea kwa wema tu jamani sina nia mbaya lakini”

“awe Wema awe Diamond mimi hainihusu, sitaki kuongozana na wewe na narudia tena kukwambia sihitaji mazoea na mlugaluga sawa, hebu nipishe uko..” alisema Aziza na kumpushi Amour akaendelea na safari yake. Jafari alibaki kumtazama tu mrembo huyo aliyejaaliwa uzuri na ndio sababu iliyomfanya Kijana huyo ajaribu bahati yake mara kwa mara kwa mrembo huyo bila mafanikio.

“dah mimi sijui nina kizizi gani yarabbi...haya bana..” alisema Amour na kuchanganya mwendo naye akaenda zake kupata chai akashangaa kuona ameshikwa mkono akiwa anatembea na alipotazama akamuona ni Eliza best wake na ni mtani wake pia.


“unajua nilikuwa nakukimbilia ila nilipokuona umesimama na wifi ikabidi nisimame tu niwaache mmalizane kwanza wapendanao.” alisema Eliza akiwa mwenye tabadamu usoni. Jafari alimtazama msichana huyo akiwa na hasira zake mwenyewe za kukataliwa.

‘Eliza unapoelekea sasa nakutia kofi unikasirikie.“

“ah mimi mbona kupigwa nishazoea mwenzio, ipite siku bila kupigwa sisikii raha yani we nipige tu Amour, ila aka mwenzangu kama mmegombana wenyewe mkamalizane wenyewe mimi hainihusu.” alisema Eliza.

“hivi lini niliwahi kukwambia Aziza amenikubalia tukawa wapenzi mbona unakuza mambo we boya.?” alisema Amour akionesha kukasirika.

‘acha ujinga Amour... ina maana tangu siku ile bado tu unaimbisha haelewi?” aliuliza Eliza na kumfanya Amour akose jibu la kumpa.

“dah Amour unazingua, mimi najua mambo fresh yule ndo wifi ndio maana nakutania sana kumbe dah...aisee nisamehe bure sikujua, ila nini tatizo, wapi umekwama naweza kukusaidia.” alisema Eliza na kumfanya Amour amtazame tena.

“hanitaki ndio alivyoniambia, na kila siku ninavyomsumbua kumuelewesha ndio anaona namsumbua, nahisi leo ndio amenitapika kabisa na kuniambia nikome kumfuatilia.” alisema Amour akiwa amesimama na Eliza karibu na mkahawa.

“ah achana nae basi utaumia bure ukipenda kwa mtu asiyekupenda, wanawake wapo wengi mbona unachagua tu wewe, hata hivyo nilisikia ticha Saidi anamfukuzia pia sasa sielewi kama ndio kashampata hadi Aziza anakukatalia wewe ama vipi, ila hiyo nimeisikia sina uhakika kama ni kweli.” alisema Eliza na kuzidi kumchanganya Amour.


Wakaamua waache kwanza mada hizo watafute chai maana baadae wana kikao na walimu wao.


ITAENDELEA

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA TATU (3)

Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group