PETE YA MFALME WA EDEN SEHEMU YA 1

 


SEHEMU YA 01


       Asubuhi ya saa mbili kijana Amour alikurupuka kutoka kitandani, alipotazama saa yake ya mkononi ambayo aliiweka karibu na mto alipolala kwa lengo la kumuamsha kwa kutegesha alamu, lakini ajabu siku hiyo hakuweza kusikia muito wa saa ile ikimuamsha jambo lililomfanya haraka anyanyuke na kuanza kuvaa nguo zake za shule haraka haraka.

“yaani leo nachezea stiki za boss Khamis, na u timekeeper niliopewa ndio mimi nimekuwa mchelewaji, Mungu wangu leo mh“ alisema kijana Amour akiwa anavaa viatu vyake haraka bila ya soksi, alipohakikisha yupo sawa alinawa uso wake kisha akachukua begi lake na kuanza safari ya kuelekea shuleni ambapo ni mbali kidogo kutoka kwao Magogoni ambapo ndipo anaishi kijana huyo na alipopita njiani akakata kipande cha tawi la muarobaini na kutengeneza mswaki wa kijiti huku safari ikiendelea kuelekea shule. Ilimchukua dakika 35 za kukimbia tu hadi kufika mazingira ya shuleni hapo huku akionekana kuhema sana kwa kuchoka na jasho likimmiminika kiasi cha kurowesha nguo zake. Alisogea mbele kidogo akaanza kunyata na kwa mbali alisikia bakora zikitua mwilini kwa mtu hali iliyomfanya ajibanze kwanza mahali. Alipotazama kwa makini mbele alipata kushuhudia rafiki yake wa darasani Masoud akiwa amelala chini akichapwa bakora kwenye makalio.

“duh hata jamaa leo kachelewa? Mungu wangu nisaidie" alisema Amour na kuanza kutafuta njama ya kuingia darasani bila kuonekana maana wanafunzi wote walikuwa washaingia darasani wakichungulia tu kuona watu walio chelewa wakipata adhabu ya viboko kutoka kwa Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya NYERERE SECONDARY. Alipotazama pembeni akaona kuna wanafunzi watano wanatembea wakielekea kwenye bustani hivyo akaona njia pekee ya yeye kuepuka bakora ni kujichanganya kwa wale wanafunzi apate kupenya hadi kuingia darasani. Taratibu akanyata kwa ustadi wa hali ya juu hadi kufanikiwa kuzama kwenye lile kundi ambalo walipomuona Amour walicheka tu na kuendelea na kazi zao za pale kwenye bustani huku naye akishirikiana nao huku akipanga njama ya kuingia darasana ambapo ni karibu na bustani hiyo waliyopo. Alipo piga ramani na kuona Mwalimu mkuu yule amezubaa akakimbia haraka hadi darasani kwao akaingia na kukimbia kukaa kwenye kiti chake huku baadhi ya wenzake wakianza kucheka maana walishamuona tangu anafanya ujanja wake. Dakika moja mbele akaja kijana mmoja pale karibu yake.

“mwanangu sio kama umesevu ulivyoingia humu.. Boss anakuja huku kashatuhesabu tuliowahi ana namba zake na tuliopo humu ni 36 tu.“ alisema kijana huyo na kumfanya Amour ashtuke kusikia vile. Akaona ni msala wa yeye kuendelea kuwa pale darasani bora atoke tu, na alipotaka kufanya hivyo gafla tu aliona mlango unafunguliwa na kuingia Mwalimu mkuu akiwa ameshika bakora zake tatu huku sura yake ikionesha kuwa na hasira. Alipiga macho darasa zima huku akihesabu watu waliopo mule ndani, akajikuta akirudia tena na tena.

“hesabu zangu zinakataa, kuna mtu amezidi humu“ alisema Mkuu huyo na baadhi ya wanafunzi wakaanza kumtazama Amour aliye onekana kutetemeka mwili huku akijitahidi asionekane hali ile akawa anatoa vitabu vyake kwenye begi na kuanza kuvipanga.

“simameni wote“ alitoa amri hiyo mkuu na wote wanafunzi wa darasa hilo la Form 4 wasimame.

“namba moja apite mbele“ alisema Mkuu na mwanafunzi mwenye namba hiyo akapita mbele, hali hiyo ikazidi kumfanya Amour akose amani na kukumbuka ule usemi KIFO CHA NYANI MITI YOTE HUTELEZA, hakukuwa na ujanja wowote ikabidi asubiri tu kukamatwa. Namba ziliendelea hadi kufika 34 na kubaki wanafunzi watatu waliosimama akiwemo Amour ambaye alijikuta akiomba Mungu tu kwa woga uliomjaa.

“eh Mungu wangu nishushie muujiza huyu mzee hata akinikamata asiniadhibu hata bakora moja, unajua nilivyo mbovu katika kuvumilia bakora mimi mja wako, doh saa imeniponza leo“ alijisemea moyoni Jafari huku tumbo likinguruma kwa woga akabaki ameinamisha tu kichwa chini huku wenzake wawili waliobaki wamesimama naye wakasogea mbele baada ya kutajwa namba zao akabaki yeye tu. Hapo ndipo akasikia vicheko vya wenzake wakicheka baada ya kumuona amebaki yeye tu kwenye viti.

“wewe ndio ulikuwa unanisumbua muda wote hapa hebu kuja huku, nyie rudini mkakae wewe kima njoo hapa alaah.“ alisema Mkuu na wanafunzi wakarudi kwenye viti vyao huku Amour akisogea pale mbele na kushikwa mkono na Mwalim Khamis.

“wewe una makosa mawili, kwanza wewe ni TIME KEEPER ulipaswa uwahi kugonga kengele ndio watu wahesabu namba saa moja kamili, leo kengele nimegonga mimi mwenyewe saa moja na dakika 15 hivyo umeharibu ratiba nzima ya shule leo mpaka sasa vipindi havijaanza, utabeba adhabu hii peke yako lazima uwajibike, twende huku." alisema Mkuu akitoka nje na kijana Amour aliyeshikwa mkono. Watu wakawa wanatazama tu madirishani wakitaka kushuhudia adhabu gani atakayopatiwa.


                *****


Upande wa pili katika nchi ya  kifalme  kunaonekana kuna mkusanyiko wa watu katika uwanja mmoja nje ya jengo la kifalme. Kwenye jukwaa ambalo ni maalumu kwaajili ya kutoa hukumu anaonekana babu mmoja akiwa amefungwa kamba kwenye nguzo ya mti mrefu huku mwili wake ukiharibika kwa kupigwa sana na askari wa kifalme. Alichoka mwili mzima akisubiri hukumu yake tu ambayo ilisadikika mzee huyo ni mchawi na baya zaidi ameweza kumroga mpaka binti wa kifalme ambaye hadi sasa bado yu taabani kitandani hanyanyuki. Mzee huyo alipokamatwa na kubinywa ili aweze kueleza dawa ya kumtibu binti huyo alikataa katakata na kusema hawezi kusaidia falme haramu inayoongozwa na Mfalme Siddik hivyo ilibidi Mfalme Siddik atoe amri ya kumnyonga mzee huyo kwa kumkashifu Mfalme kisha waangalie namna nyengine ya kumsaidia binti wake maana hakukuwa na jinsi maana mzee yule aliapa kutomponesha binti huyo. Basi siku hiyo ya hukumu watu walifurika sana akiwemo hata binti wa mzee huyo aliyeitwa Nadhra. Yeye alikuwa mstari wa mbele kabisa akiwa mwenye huzuni sana akimtazama baba yake huyo akiwa amening’inizwa kwenye nguzo kubwa akisubiri hukumu yake ambayo kila mmoja aliifahamu hukumu ya mtu mchawi, ni kunyongwa mpaka kufa.

Mzee huyo akiwa pale juu huku damu zikimtiririka alipata kumuona mwanaye pale mbele akiwa analia tu, alitabasamu baada ya kumuona mwanaye.

“Nadhra...usilie binti yangu, ukifanya hivyo utanifanya huko niendako niwe na huzuni kuwa nimemuacha binti muoga, simama kwenye msimamo nilio kwambia na hiyo pete kaitupe sehemu yeyote ya kengele kabla ya hukumu yangu kama unataka niwe nawe kiroho siku zote“ alisema Mzee huyo moyoni mwake lakini kwa uwezo alio nao Nadhra alipata kusikia yote aliyosema baba yake.

“mimi naamini nguvu zako baba sio za kudhuru mtu, wana kuhukumu bure tu hawa watu wa kifalme." alisema Nadhra moyoni mwake akiwa anawasiliana na baba yake aliyekuwa juu ya nguzo.

“hilo sio la kuliongelea kwasasa, fanya kile nilichokueleza hapo awali haraka." alisema Mzee yule na binti yake akamuelewa.


Waliangalina kwa mara ya mwisho mtu na mwanaye kila mtu akitokwa na machozi kisha Nadhra akageuka na kuondoka zake akipita katikati ya halaiki ya watu waliofurika kushuhudia hukumu hiyo.

“PISHA NJIA MFALME ANAPITA...” ilisikika sauti ya maaskari na kuwafanya watu waache njia kubwa ya msafara wa Kifalme ukiwasili sehemu ile. Nadhra alipata kuutazama tu msafara ule ukimpita akiwa naye amesimama pembeni hadi Mfalme Siddik alipopita akiwa juu ya farasi na wafuasi wake na kufika kwenye jukwaa lile alilopo baba wa Nadhra. Kiliandaliwa kitanzi maalumu kwaajili ya kukamilisha hukumu hiyo na hapo ndipo Nadhra akapata akili kumbe aliagizwa kufanya jambo. Haraka akaanza kukimbia sasa kwenda kutafuta mahala popote pale palipo kengele ili apate kuitupa pete aliyo agizwa na baba yake upate kusikika mlio kutoka kwenye kengele kwa imani yao ndio itakuwa afadhali ya baba yake atakuwa amejitoa kiroho katika mwili ambao utanyongwa hivyo ataendelea kuishi kama kawaida lakini hataweza kuonekana kama awali. Na asipofanikiwa Nadhra ni kwamba baba yake atakufa kabisa pindi atakapo nyongwa.


Muda huo baada ya kitanzi kuwa tayari yule Mzee alishushwa taratibu na kusogezwa kwenye kitanzi akaingizwa kichwa chake na askari mmoja akisubiri tu amri kutoka kwa Mfalme.


Mfalme alipanda kwenya lile jukwaa na kusimama kuwatazama wananchi wake.

“kwa kawaida na sheria za Eden atakapo bainika mtu yetote anatumia uchawi basi kunyongwa mpaka kufa ni adhabu yake pindi atakapobainika, huyu mzee ni adui wa falme yangu ametumia uchawi  kumdhuru binti wa kifalme hali yake ni mbaya sana, amethubutu kuutukana ufalme mzima na hata kunitukana mimi.. hivyo hukumu yake nii......“alisema Mfalme Siddik.


“K I F O O O” walisema wananchi kwa sauti kubwa sana wakijibu, jibu ambalo lilimfanya Nadhra kule alipo asikie na kugeuka kuangalia sauti ilipotokea, Akajua sasa baba yake anakwenda kunyongwa kweli, kila akiangalia pembeni ya kila sehemu hakuna mahala palipo na kengele apate kuitupa ile pete, Alijikuta akilia kwa sauti kama kuchanganyikiwa akiwa anakimbia huku na kule.


Muda huo huo kule shuleni Amour alikuwa akiongozana na Mwalimu mkuu aliyejawa na hasira sana.

“wewe nakuadhibu mbele ya shule nzima na kuanzia leo nakuvua UTIME KEEPER nampa mtu mwengine, kagonge kengele kwa mara ya mwisho watu waje paredi haraka” alisema Mkuu na kumfanya Amour anyong'onyee kusikia ndio anafutwa cheo chake cha kugonga kengele. Alitembea taratibu hadi kuifikia kengele ile na kuchukua kile kichuma akikiangalia sana na kuona ndio mara yake ya mwisho kukishika chuma kile kama akifutwa cheo hicho. Alikasirika sana na alichokifanya ni kuigonga kengele kwa hasira zote tena mfululizo bila kusimama. Kitendo cha kugonga kengele ile kwa nguvu zote sauti iliyotoka pale ilisikika hadi Eden na kwa mbali alipata kuisikia Nadhra ambaye alitega sikio kusikiliza sauti ile inatoka wapi ili awahi kutupa ile pete lakini kila akiweka umakini wa masikio yake sauti anaona inatokea juu angani tu na sio kusini wala kaskazini wala Mashariki wala Magharibi hali iliyomfanya azidi kuchanganyikiwa na kujikuta akiitoa ile pete na kuishika mkoni.


Alichokifanya ni kucheza mchezo wa bahati nasibu tu liwalo na liwe, alifumba macho na kuomba kwa imani yao kisha akairusha juu angani ile pete akiweka dhamira ifike kwenye kengele aliyoisikia. Kitendo cha kuirusha tu pete ile alisikia watu wakishangiria kuonesha tayari baba yake kashanyongwa, alienda chini kama mzigo kwa kupiga magoti.

“naamini nimeifanya kazi yako baba japo sina hakika kwa nilichokifanya, ni kuomba na kusubiri matokeo ya kilichofanyika.” alisema Nadhra huku chozi likimtiririka haelewi kama jambo alilo lifanya limefanikiwa au ndio laa kashampoteza baba yake?..


Upande wa pili Amour akiwa mwenye hasira zake pale kwenye kengele akizidi kuigonga mfululizo alimfanya hata Mkuu wa Shule acheke baada ya kuona kweli kijana anagonja kengele kwa mara ya mwisho kama alivyomuambia na kweli hakuwa mwenye kutania. Alipanga kumtoa Amour kwenye uongozi wa kuangalia muda wa vipindi kutokana na uchelewaji wa kijana huyo.

Wanafunzi madarasani walianza kutoka kuelejea paredi lakini ajabu Amour aliendelea tu na kuipiga kengele ile bila kusimama. 


Ghafla tu zile kelele za kengele zikaanza kubadilika na kuwa miungurumo ya radi na ni yeye pekee ndiye aliyekuwa anasikia hivyo ikabidi atazame wenzake na kuona hawana habari wanaelekea paredi. Alishangaa kuona kile chuma kinakuwa cha moto sana hali iliyomfanya akitupe chini. Alipotazama mkononi  aliona umebadilika na kuwa mwekundu kama ameungua na cha ajabu ni kuona Pete kwenye kidole huku akisikia maumivu taratibu kwenye mkono huo.

“haya mazingaombwe gani tena jamani hivi? hii pete imetokea wapi tena? Na kugonga kengele hivi ndio nipate maumivu haya jamani hadi kubabuka mikono?” alisema mwenyewe Amour akiwa anautazama mkono wake. Akasikia anaitwa Paredi na haraka akaelekea kutii wito huo.


Kule kwa Nadhra akiwa amekaa pale aliona upepo mkali ukivuma na kutengeneza kitu kama kimbunga kilichosogea karibu yake.

“Ni mtu mmoja pekee ndiye aliyenifanya niwe hivi kuliko kuuliwa na falme ya Siddik, huyu mtu yupo nchi ya mbali sana na ni wajibu wako umtafute muwe wote kuna kazi kubwa ya kufanya, yeye ndio atakuwa badala yangu hivyo mtakuwa pamoja muda wote.” ilisikika ile sauti ikitokea kwenye kile kimbuka kikali Nadhra akawa anakinga macho yake vumbi lisije kuingia, aliifahamu kuwa ni sauti ya baba yake mzazi ambaye muda mchache alikuwa kwenye adhabu ya kunyongwa.

“huyo kiumbe anatokea wapi? Na ana uwezo mkubwa kama sisi?" aliuliza Nadhra.

“hadi sasa ana nguvu za ajabu ambazo zitawasaidia wakati wote japo yeye hafahamu kama anazo, nitakuonesha mahala anapo patikana uende kumshawishi ili uje naye huku mfanye ile kazi kwa pamoja, ukirejea nyumbani utapata kujua mahali hapo anapopatikana, sitawaona tena hadi mambo yatakapo kwenda sawa, niwatakie kazi njema.” ilisema ile sauti ya mzee kisha kile kimbunga kikapotea gafla na kumfanya Nadhra atambue maneno aliyoambiwa.


ITAENDELEA..... 

Je! Nini kitakachoendelea kwa kijana Amour baada ya kujiona akiwa na mabadiliko mbele ya paredi?  Na atahitajika kwenda Eden kutokana na maneno ya baba yake Nadhra. Tukutane sehemu ya pili tujue kilichojiri.

GUSA HAPA KUSOMA SEHEMU YA PILI (2)





Chapisha Maoni

Join Our
Whatsapp Group